Uchaguzi kenya 2022: Habari potofu mitandaoni kuhusu vyeti vya elimu

Peter Mwai

BBC Reality Check

Wagombea wa urais nchini Kenya wamekuwa wakifanya kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwezi ujao, na kumekuwa na madai yanayopotosha kuhusu kufuzu kwao kuwania wadhfa huo.

Tumekuwa tukichunguza madai haya na mengine kabla ya kura hiyo.

Kuhojiwa kuhusu vyeti vyao vya masomo

Sheria za uchaguzi nchini Kenya zinamtaka mgombea wa urais kumiliki shahada kutoka chuo kikuu kinachotambulika nchini Kenya.

Wagombea wawili wa urais , Raila Odinga na William Ruto wote wametakiwa kuweka wazi vyeti vyao.

Kwa bwana Odinga , ambaye alijipatia shahada yake kutoka chuo kikuu cha Ujerumani alihojiwa na wapinzani wake.

Wamekuwa wakisambaza cheti chake katika mitandao ya kijamii wanachodai kutoka chuo kikuu cha Magdeburg Ujerumani wakisema kwamba shahada hiyo ya bwana Odinga haikutoka katika taasisi hiyo.

Lakini chapisho hilo lenyewe ni bandia na kwamba cheti hicho ni halali.

Chapisho hilo bandia hapo juu halijaorodheshwa katika mtandao wa facebook wa chuo hicho ama hata mitandao mingine ya kijamii.

Hakuna hata akaunti moja yenye rangi ya buluu iliohusishwa na chuo hicho , huku ile ilio bandia ikiwa nayo.

Kuna mkanganyiko zaidi katika habari hii. Machapisho mengine yamesambazwa yakidai kwamba Saini katika cheti hicho ni ya muhadhiri ambaye angekuwa na umri mdogo sana wakati bwana Odinga alipokuwa katika chuo hicho.

Wanadai kwamba profesa Montag alikuwa na umri wa miaka mitano wakati ambapo bwana Odinga alikuwa ametuzwa cheti hicho 1969.

Hatahivyo Chuo hicho kimethibitisha uwepo wa Montag mwengine ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha uhandisi wakati ambao bwana Odinga alikuwa chuo hicho.

Kuongezea, utafiti wa data ya watu waliosoma Ujerumani umebaini kwamba Profesa Gerhad Montag ni kweli alichaguliwa kama profesa wa teknolojia na uhandisi wa mitambo katika huo kikuu cha Magdeburg 1966.

Vilevile inaonekana kwamba chapisho la mtandao wa Wikipedia la Chuo Kikuu cha Magdeburg lilibadilishwa ili kutoa dhana potofu kwamba Bw Odinga hakuwahi kusoma hapo. Tangu wakati huo limerekebishwa ili kufafanua kuwa alikuwa mwanafunzi katika taasisi hiyo.

Mpinzani mkuu wa bwana Odinga ni naibu wa rais William Ruto ambaye hata naye cheti chake cha chuo kikuu kimehojiwa.

Wakati huu , madai sio kwamba eti hakupata cheti cha shahada , lakini kwamba utendaji wake alipokuwa Chuo Kikuu cha Nairobi ulikuwa wa kiwango cha chini kuliko ilivyoelezwa.

Badala ya kupata shahada ya pili ya daraja la juu, chapisho ghushi lililosambaa mtandaoni linadai kuwa alipata shahada ya chini ya daraja la pili.

Mbunge mmoja hata alichapisha cheti chake cha shahada mtandaoni pamoja na kile cha bandia.

Uchunguzi wa tovuti ya chuo kikuu cha Nairobi ulibaini mara moja kwamba bwana Ruto alipokea matokeo hayo ya kiwango cha juu na kwamba chapisho lililokuwa likisambazwa lilikuwa bandia.

Chuo hicho kimechapisha taarifa katika mtandao wake wa Twitter kikifutilia mbali cheti hicho bandia.

Video bandia

Wakati bwana Odinga alipoandaa mkutano wa kampeni hivi majuzi, mwanablogu Dennis Itumbi anayemuunga mkono naibu wa rais William Ruto , alichapisha kanda ya vídeo ya watu waliokuwa wakitaja jina la Ruto wakati walipoulizwa wangempigia kura nani.

Swali la ni nani mutakayempigia kura linasikika katika kanda hiyo na kelele za Ruto, Ruto, Ruto zinasikika.

Sauti hiyo hatahivyo ni bandia.

Video hiyo ilichapishwa kwa mara ya kwanza na akaunti ya twitter ya TikTok ambayo pia imechapisha video nyengine bandia za wanasiasa ili kuonesha kwamba watu wanamuunga mkono bwana Ruto.

Uchunguzi wa kanda mbili za video zilizokuwa zikienda hewani moja kwa moja kutoka kwa mkutano wa bwana Odinga zilizokuwa mtandaoni , hatahivyo , zinaonesha kwamba sauti hizo za watu wakitaja jina la Ruto ziliongezwa baadaye.

Katika Video halisi, katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi nchini COTU Francis Atwoli , ambaye anamuunga mkono bwana Odinga , anasikika akiwauliza raia katika mkutano kuhusu ni nani wangemchagua . Wanajibu baba, jina la utani la bwana Odinga

Ruto hakusita kutaja ufisadi

Ufisadi umekuwa suala nyeti katika kampeni za sasa , wagombea wamejaribu kuonesha kwamba wao ndio suluhu ya jinamizi hilo na kwamba wapinzani wao hawana nia njema.

Prof Makau Mutua, msemaji wa kundi la kampeni ya bwana Odinga, alisema kwamba bwana Ruto hakutaja hata mara moja ‘neno ufisadi ‘.

‘’Kama tauni, bwana Ruto aliepuka kabisa kulitaja neno hilo’’.

Hatahivyo taarifa ya bwana Mutua sio ya kweli. Manifesto ya bwana Ruto ilitumia neno Ufisadi mara nne na kwamba ametaja jinsi atakavyokabiliana na tatizo hilo.

Msemaji wake pia alichapisha kanda za video za bwana Ruto akizungumzia ufisadi wakati wa uzinduzi wa kampeni yake.

‘’Tunataka kujenga taasisi hizi kufikia kiwango ambacho iwapo rais atakuwa mfisadi , serikali itahakikisha anakamatwa na kufungwa’’, Ruto alinukuliwa akisema katika video moja.