Mvutano wa Rwanda na DRC: Kupigwa kombora kwa ndege yetu ni shambulio la kivita-Kinshasa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kwamba hatua ya Rwanda kuipiga risasi moja ya ndege zake za kivita kama "kitendo cha vita", huku kukiwa na hali ya wasiwasi inayozidi kuongezeka.

Serikali ya Rwanda ilisema ilichukua "hatua za kujilinda" dhidi ya ndege ambayo ilikiuka anga yake - madai ambayo yamekanushwa na DR Congo.

Hili ni ongezeko kubwa kufuatia miezi kadhaa ya mzozo mashariki mwa DR Congo, ambao umewalazimu takriban watu 400,000 kukimbia makazi yao.

DR Congo, Marekani na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23.

Rwanda imekanusha hili na inailaumu serikali ya Congo kwa mzozo huo.

Katika miaka ya 1990, Rwanda ilituma wanajeshi mara mbili kwa jirani yake mkubwa zaidi, na kusababisha mzozo mkubwa uliohusisha angalau nchi tisa na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu.

Nchi kadhaa za Afrika Mashariki zimetuma wanajeshi wake DR Congo kusaidia kupambana na waasi wa M23, huku pia zikijaribu kutafuta suluhu la kidiplomasia kwa mgogoro huo.

Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo bado hazijathibitishwa na BBC, zinaonyesha ndege aina ya Sukhoi-25 ikipigwa risasi ilipokuwa ikiruka kwenye mwinuko wa chini kati ya miji ya Goma nchini DR Congo na Gisenyi nchini Rwanda, ambayo ipo katika mpaka wao wa pamoja.

Picha nyingine zinaonyesha maji yakitumika kuzima moto kwenye ubavu wa kulia wa ndege hiyo baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Goma. DR Congo inasema ndege hiyo haikupata "uharibifu mkubwa ".

Katika taarifa yake serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliishutumu Rwanda kwa "kuhujumu" utekelezaji wa makubaliano ya hivi karibuni ya amani kati ya nchi hizo mbili.

Wizara ya Habari iliendelea kusema kwamba DR Congo "inahifadhi haki ya kutetea eneo lake la kitaifa na haitatishwa".

"Serikali inachukulia shambulio hili la kumi na moja la Rwanda kama hatua ya makusudi," wizara ilisema.

Hata hivyo, Rwanda ilisema hili ni tukio la tatu linalohusisha ndege ya kivita ya Congo kwenye anga yake na kumtaka jirani yake "kukomesha uchokozi huu".

Novemba mwaka jana, ndege nyingine ya Congo aina ya Sukhoi-25 ilitua kwa muda katika uwanja wa ndege wa Gisenyi nchini Rwanda. Kinshasa ilisema ndege ya kivita "ilitua kimakosa" hapo.