Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini jeshi la Kenya linajiunga na mzozo wa DRC
Na Richard Kagoe
BBC Nairobi
Zaidi ya watu 100,000 wamekimbia makazi yao na makumi ya wengine wameuawa baada ya mapigano kuzuka kati ya wanajeshi wa Jamhuriya Kidemokrasia yaCongo na kundi la waasi wa M23, katika moja ya migogoro mirefu na mbaya zaidi duniani.
Sasa, vikosi vya Kenya vinajiunga na vita kusaidia jeshi la Congo, kwa lengo la kuleta amani katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini ambayo inapiganiwa na makundi tofauti yenye silaha.
Mapigano yanahusu nini?
Mzozo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yalizuka miongo mitatu iliyopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni sita huku wengine milioni 4.5 wakilazimika kutoroka makwao.
Katika mwaka uliopita, ghasia zimeongezeka kwa mara nyingine huku vikosi vya usalama vikipambana dhidi ya zaidi ya makundi 100 yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo, licha ya kuwepo kwa operesheni kubwa ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.
Wanamgambo wa M23 na jeshi la Congo wameshutumiana kwa kuanzisha mapigano yaliyosababisha mgogoro wa sasa.
Hali imekuwa mbaya hadi siku ya Alhamisi Rais Félix Tshisekedi akatoa wito wa mapigano na kuwomba vijana wa nchi hiyo "kujipanga katika makundi" kusaidia jeshi.
Mzozo huo haujaathiri DR Congo pekee, lakini pia umedhoofisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Rwanda, ambayo inashutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na matokeo yake ikaishia kufurushwa kwa balozi wa Rwanda wiki iliyopita.
Rwanda inakanusha madai hayo.
Kundi la M23, ambalo liliundwa miaka 10 iliyopita, linadai kutetea maslahi ya jamii ya Watutsi wanaoishi nchini DRC dhidi ya wanamgambo wa Kihutu.
Rais wa Rwanda Paul Kagame aliingia madarakani akiongoza jeshi la waasi la Watutsi wanaopigana na Wahutu wenye itikadi kali ambao waliwaua maelfu ya Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994.
Wengi wa waliohusika na mauaji hayo wanadaiwa kukimbilia DR Congo baada ya majeshi ya Bw Kagame kuchukua madaraka nchini Rwanda, na ndiposa mzozo huo ukavuka mpaka na kuingia nchi jirani.
Ni wanajeshi wangapi wataenda DRC?
Idadi kamili wanajeshi watakaopelekwa haijatolewa. Tunachojua hadi sasa ni nchi nne tu Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Burundi ndizo zinawapeleka wanajeshi wao.
Wanajeshi elfu moja wa Kenya wataungana na wenzao wa Burundi waliowasili DR Congo mapema mwezi Agosti kwa oparesheni ya pamoja dhidi ya waasi.
Haijabainika iwapo Tanzania itapeleka wanajeshi.
Maafisa wa kijeshi wamekataa kufichua idadi ya wanajeshi waliohusika, wakitaja sababu za kiusalama na za kimkakati.
Wanajeshi wa Burundi kwa sasa wako Luberezi karibu na Bukavu huko Kivu Kusini.
Kikosi cha Kenya kitapiga kambi karibu na Goma huko Kivu Kaskazini na kitaongoza Kikosi cha Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rwanda pia ni mwanachama wa EAC lakini iliamuliwa kwamba isichangie jeshi la kikanda.
Je jeshi la Afrika Mashariki litaleta tofauti gani?
Waasi wa M23 wameteka miji kadhaa mashariki mwa DR Congo na wamepata nguvu zaidi katika wiki za hivi karibuni lakini sio kundi pekee ambalo jeshi la Afrika Mashariki litakuwa likikabiliana nalo katika majimbo matatu yenye machafuko zaidi - Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.
Vikosi tofauti vitakuwa na oparesheni tofauti. Wanajeshi wa Kenya wataangazia waasi katika eneo la Kivu Kaskazini ambako baadhi ya wenzao tayari wamejikita katika kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi wa Uganda watakabiliana na kundi la Allied Democratic Forces (ADF)Nambao wana uhusiano na Islamic State huko Kivu Kaskazini na Ituri, na wamefanya mashambulizi nchini Uganda.
Wanajeshi wa Burundi watakusanyika Kivu Kusini, ambapo watapambana na wanamgambo wa Tabara. Vikosi vya Sudan Kusini vitapambana na waasi wa Lord Resistance's Army waliobakia.
Je, jeshi la Afrika Mashariki lina tofauti gani na ujumbe wa Umoja wa Mataifa?
Jukumu la jeshi la kanda ya Afrika Mashariki limewekwa wazi na ni kupambana na makundi yenye silaha.
Umoja wa Mataifa umekuwa na ujumbe wa kulinda amani nchini DR Congo tangu mwaka 2000 na hapo awali ulikuwa na mipaka ya kulinda raia na kusaidia operesheni za jeshi la Congo.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa baadaye uliidhinisha kuundwa kwa kikosi cha kijeshi chenye mamlaka ya kufanya mashambulizi maalum ili kutuliza makundi yenye silaha katika eneo hilo.
Vikosi vya kikanda vinajumuisha wanajeshi kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi.
Raia wa Congo wamekuwa wanaukosoa vikali ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kwa jina la Monusco, wakishutumu wanajeshi wake 13,000 kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya waasi.
Mapema mwaka huu, kulikuwa na maandamano mabaya dhidi ya Umoja wa Mataifa na haya yameanza tena katika siku za hivi karibuni huku kundi la M23 likiendelea kusonga mbele.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema jeshi la Afrika Mashariki na Monusco watahitaji kushirikiana kwa ukaribu ikiwa wanataka kuwa na ufanisi.
Je, Kenya ina maslahi gani nchini DR Congo?
Kenya imekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kufanikisha makubaliano ya amani ya kudumu kati ya DR Congo na waasi.
Mnamo Julai, Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta - ambaye alikuwa na jukumu muhimu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na EAC mwezi Machi - aliteuliwa kuwezesha mazungumzo ya amani na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya amani ambayo pande hizo mbili zilikubaliana mjini Nairobi.
Wachambuzi wa masuala ya ulinzi na usalama wanasema kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikishawishi mrithi wa Bw Kenyatta, William Ruto, kuhusu mpango wa amani na kutumwa kwa kikosi cha kikanda.
Kama nchi iliyoendelea zaidi katika uchumi wa Afrika Mashariki, Kenya imekuwa na nia ya kuendeleza uhusiano wake wa kibiashara kote kanda hiyo kupitia biashara na uwekezaji