Tunachojua kuhusu operesheni iliyomuua 'El Mencho' aliyekuwa akisakwa zaidi na Mexico na Marekani?

    • Author, Darío Brooks
    • Nafasi, BBC News Mundo
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Arubaini za Nemesio Oseguera Cervantes, mlanguzi wa dawa za kulevya aliyekuwa akisakwa zaidi na mamlaka za Mexico na Marekani na ambaye alikuwa amekwepa kukamatwa kwa zaidi ya muongo mmoja, zilitimia Jumapili.

"El Mencho", kama alivyofahamika kwa jina la utani, aliuawa akiwa na umri wa miaka 59 wakati wa operesheni iliyofanywa na jeshi la Mexico katika milima ya jimbo la Jalisco.

Baada ya kifo chake, genge lake lilijibu kwa mashambulizi katika eneo la Jalisco na majimbo mengine, hali iliyosababisha vifo vya takribani maafisa 25 wa usalama pamoja na watu 30 wanaoshukiwa kuwa wahalifu.

El Mencho alikuwa mwanzilishi wa genge la Jalisco New Generation Cartel (CJNG), ambalo tangu mwaka 2010 limeenea kote nchini na kuwa mojawapo ya magenge yenye nguvu na ukatili mkubwa, likilinganishwa na genge la Sinaloa.

Serikali ya Marekani ilikuwa imetangaza zawadi ya dola milioni 15 kwa atakayetoa taarifa za kumkamata, huku Mexico ikitoa zawadi ya dola milioni 1.75 kiasi kikubwa zaidi katika mpango wake wa zawadi.

Hivi karibuni, utawala wa Rais Donald Trump uliitaja CJNG kama shirika la kigaidi, ukilitaja kuwa genge katili linalohusika na usafirishaji wa fentanyl, methamphetamine, kokeini na dawa nyingine haramu kwenda Marekani.

Mamlaka za Mexico hivi majuzi zilifichua baadhi ya maelezo ya operesheni ambapo "El Mencho" aliuawa, operesheni iliyofanywa kwa ushirikiano na serikali ya Marekani.

Ni kitu gani kilichotokea katika operesheni?

Kwa miaka mingi ilijulikana kuwa Oseguera Cervantes alikuwa akilindwa na mtandao wa watu wa kumkinga katika maeneo ya vijijini na mijini ya Jalisco, jambo lililomwezesha kujificha na kukwepa misako ya mara kwa mara.

Hata hivyo, jeshi la Mexico lilifanikiwa kumtambua akiwa katika manispaa ya Tapalpa, eneo la milimani takribani kilomita 130 kusini mwa Guadalajara.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Mexico, Jenerali Ricardo Trevilla Trejo, kikosi cha ujasusi wa kijeshi kilimfuatilia tarehe 20 Februari mshirika wa mwanamke aliyekuwa na uhusiano na El Mencho. Mshirika huyo alimpeleka mwanamke huyo Tapalpa kwa ajili ya kukutana na kiongozi huyo wa CJNG.

Baada ya mwanamke huyo kuondoka siku iliyofuata, wanajeshi walibaini kuwa El Mencho alikuwa akikaa katika nyumba ya mapumziko (chalet) katika eneo hilo la kitalii lenye misitu.

Jeshi lilipanga operesheni maalum ya ardhini na angani, ikihusisha vikosi maalum na helikopta sita.

Kikosi cha ardhini kilipofika kumkamata, walinzi wake walianza kufyatua risasi mara moja. Jeshi liliwaua wanachama wanane wa CJNG katika mapambano hayo.

El Mencho na baadhi ya watu wake walijaribu kukimbilia msituni, lakini walifuatiliwa na kukutwa. Katika mapigano yaliyofuata, alipigwa risasi pamoja na walinzi wake wawili. Walipelekwa kwa helikopta katika kambi ya kijeshi lakini walifariki njiani.

Katika eneo alikokuwa amejificha, jeshi liligundua bunduki, risasi na makombora mawili ya kurushia roketi (RPG ya Urusi na Blindicide). Helikopta moja ilipigwa kwa roketi lakini iliweza kutua salama.

Katika operesheni nyingine siku hiyo, Hugo "H" maarufu kama "El Tuli", mkono wa kulia na mfadhili wa El Mencho, pia aliuawa.

"Aliratibu vizuizi vya barabarani, milipuko ya magari, mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi, Walinzi wa Taifa, biashara, majengo ya serikali n.k. Pia alitoa peso 20,000 (645,824 FCFA) kwa kila askari ambaye aliwaondoa wanachama wote wa kundi hili la uhalifu," alifafanua Jenerali Trevilla.

Kwa jumla, wanajeshi watatu walijeruhiwa moja kwa moja Tapalpa, huku maafisa 25 wa vyombo vya usalama wakipoteza maisha katika mashambulizi ya kulipiza kisasi katika majimbo mbalimbali.

"Nachukua fursa hii kutoa rambirambi zangu kwa familia za wenzetu walioanguka kwenye uwanja wa heshima," Jenerali Trevilla Trejo, akiongea kwa hisia.

"Pia napenda kupongeza kazi ya wanajeshi wetu waliofanikisha operesheni hii, inaweza kutafsiriwa kwa njia tofauti, lakini ni wazi kwamba walitimiza dhamira yao," aliongeza.

Ushiriki wa Marekani

Wizara ya Ulinzi ya Mexico ilisema operesheni hiyo ilinufaika na taarifa za kijasusi kutoka serikali ya Marekani chini ya ushirikiano wa pande mbili.

Ikulu ya Marekani ilithibitisha kuwa ilitoa msaada wa taarifa za kijasusi kusaidia operesheni hiyo, lakini ikasisitiza kuwa utekelezaji ulikuwa wa jeshi la Mexico pekee.

Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, alisisitiza kuwa operesheni zote hufanywa na vikosi vya Mexico, huku kukiwa na ushirikiano wa kubadilishana taarifa bila kuingiliwa moja kwa moja na majeshi ya Marekani.

"Marekani ilitoa usaidizi wa kijasusi kwa serikali ya Mexico kusaidia katika operesheni (...) ambayo Nemesio "El Mencho" Oseguera Cervantes aliuawa," aliandika katika X.

"Utawala wa Trump pia unapongeza na kushukuru jeshi la Mexico kwa ushirikiano wake na mafanikio ya operesheni hii," aliongeza.

Hakuna maelezo mahususi yaliyotolewa kuhusiana na aina ya taarifa za kijasusi zilizotolewa na serikali ya Marekani, ambayo tangu Donald Trump arejee Ikulu ya Marekani mwaka mmoja uliopita, imeishinikiza Mexico kuzidisha vita dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya na imependekeza uingiliaji kati wa moja kwa moja.

"Ushirikiano na serikali ya Marekani umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu. Chini ya utawala huu, ushirikiano na Kamandi ya Kaskazini ya Marekani imeimarishwa kwa kiasi kikubwa, na kumekuwa na ubadilishanaji wa habari muhimu sana. Hivyo ndivyo tulivyofikia kesi hii maalum," Jenerali Trevilla Trejo alisisitiza.

Vyanzo vya Pentagon viliiambia CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba Kikosi Kazi cha Pamoja cha Interagency Cartel, ambacho hushirikiana mara kwa mara na jeshi la Mexico kupitia Kamandi ya Kaskazini ya Marekani, kimetoa msaada.

Hata hivyo, afisa wa kijeshi wa Marekani alisema kuwa "hii ilikuwa operesheni ya kijeshi ya Mexico, hivyo mafanikio ni yao."

Rais Sheinbaum alitoa shukurani kwa Jeshi la Mexico, Walinzi wa Kitaifa, Wanajeshi na baraza la mawaziri la ulinzi na usalama kwa mchango wao katika operesheni hiyo, lakini hakutaja ushiriki wa Marekani.

Tangu aingie madarakani Oktoba 2024, Sheinbaum ameshikilia kuwa hataruhusu ushiriki wa moja kwa moja wa vikosi vya Marekani nchini Mexico, lakini amesema kuwa "uratibu bila ya kuwa chini" na Washington juu ya usalama na masuala mengine unakaribishwa.

Kitengo maalum cha Marekani cha kupambana na magenge ya dawa za kulevya (JITF-CC), ni kikosi kipya cha kijeshi cha Marekani kinachobobea katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kijasusi kuhusu magenge ya dawa za kulevya.

Maafisa wa Marekani waliiambia Reuters kuwa mashirika kadhaa ya serikali ya Marekani yanashiriki katika kikosi hicho kwa lengo la kufuatilia na kuchora ramani ya mitandao ya usafirishaji wa dawa za kulevya nchini Marekani na Mexico.

Afisa mmoja aliiambia Reuters kwamba Marekani ilikuwa imeandaa jalada la kina la taarifa za kumlenga "El Mencho" na kulikabidhi kwa serikali ya Mexico kwa ajili ya operesheni ya Jumapili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa operesheni hiyo ilitekelezwa kikamilifu na vikosi vya Mexico.

JITF-CC inaongozwa na Brigedia Jenerali wa Marekani, Maurizio Calabrese, ambaye aliiambia Reuters mwezi uliopita kwamba jeshi la Marekani linatumia uzoefu wake wa kukabiliana na makundi kama al-Qaeda na Islamic State (IS) katika kuwasaka viongozi wa magenge ya dawa za kulevya.

"Magenge ya dawa za kulevya yanafanya kazi kwa namna tofauti na al-Qaeda au Islamic State, yakiwa na malengo tofauti. Hii ndiyo sababu ni muhimu kwetu kubaini mitandao yao ili kuizuia na kuisambaratisha," alieleza.

Calabrese alisema kuna uwezekano wa kuwepo mamia ya viongozi wa magenge ya dawa za kulevya, na pia kati ya watu 200,000 hadi 250,000 wanaofanya kazi kwa njia mbalimbali kusafirisha dawa hizo haramu.

Kwa mujibu wa maafisa wa Pentagon, JITF-CC pia imeshiriki katika operesheni katika eneo la Karibiani zilizohusisha mashambulizi dhidi ya meli na kusababisha vifo vya watu kadhaa, operesheni ambazo Washington inazitaja kama sehemu ya vita dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

Kuzuka kwa vurugu za kulipiza kisasi

Baada ya operesheni hiyo, makundi yanayohusishwa na CJNG yaliweka vizuizi barabarani katika majimbo 20 ya Mexico, yakichoma magari na kufanya mashambulizi.

Jimbo la Jalisco liliathirika zaidi, huku barabara kuu katika miji ya Guadalajara na Puerto Vallarta zikifungwa kwa magari yaliyochomwa moto.

Gavana wa Jalisco alitangaza hali ya tahadhari na kuwataka wananchi kubaki majumbani.

Katika ripoti iliyochapishwa Jumapili jioni, Katibu wa usalama wa serikali ya Marekani alisema kuwa vizuizi 252 vya barabarani viliripotiwa katika majimbo 20 ya Mexico siku hiyo.

Saa 2:00 usiku kwa saa za eneo hilo (2:00 asubuhi GMT), mamlaka zilitangaza kuwa takribani asilimia 90 (229) ya vizuizi hivyo vilikuwa vimeondolewa. Video na picha nyingi zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha magari yakiteketea kwa moto na moshi mzito ukifuka katika maeneo mbalimbali.

Vivyo hivyo, baadhi ya abiria katika viwanja vya ndege walieleza hofu yao juu ya uwezekano wa mashambulizi.

Katika mji wa Puerto Vallarta, maarufu kimataifa kwa utalii, mashirika kadhaa ya ndege ya Mexico na ya kigeni yalielekeza safari zao kwingine au kufuta baadhi ya safari kutokana na hali ya sintofahamu.

Angalau safari kadhaa za ndege kutoka Marekani, Canada na maeneo mengine zilifutwa Jumapili usiku na kuendelea kufutwa Jumatatu.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa pia katika uwanja wa ndege wa Guadalajara.

Hata hivyo, Wakala wa Shirikisho wa Usafiri wa Anga wa Mexico ulisema kuwa viwanja vya ndege vya Puerto Vallarta, Guadalajara na Tepic vilirejea katika shughuli za kawaida kufikia Jumapili mchana.

Majimbo mengine yenye uwepo wa genge la CJNG, hususan Michoacán, Guanajuato na Tamaulipas, pia yaliathiriwa na vizuizi hivyo.

Rais Claudia Sheinbaum aliandika kwenye mtandao wa X kwamba "shughuli zinaendelea kama kawaida katika sehemu kubwa ya nchi," na akahakikishia kuwa serikali ilikuwa inaratibu hatua zake pamoja na majimbo yaliyoathirika. "Ni lazima tuendelee kupata taarifa sahihi na kubaki watulivu," alisisitiza.

Aidha, Waziri wa Usalama wa Mexico, Omar García Harfuch, alithibitisha kuondolewa kwa vizuizi vyote vilivyowekwa Jumapili katika maeneo muhimu ya nchi.

Wizara ya Ulinzi wa Taifa (Sedena) ilitangaza kupelekwa kwa wanajeshi wa ziada ili kuimarisha usalama katika jimbo la Jalisco.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi