Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"El Mencho" Mlanguzi wa dawa za kulevya aliyekuwa akitafutwa sana Mexico, ni nani?
Mlanguzi wa dawa za kulevya Nemesio Oseguera Cervantes, aliuawa siku ya Jumapili, katika oparesheni moja ya kijeshi katika manispaa ya Tapalpa, kilomita 130 kusini mwa Guadalajara, mji mkuu wa Jalisco.
Kifo chake kimezua vita miongoni mwa makundi yaliyojihami katika eneo hilo.
Alikuwa akijulikana kama "El Mencho," Oseguera Cervantes mwenye umri wa miaka 59, kiongozi mkuu wa kundi la Jalisco New Generatio Cartel (CJNG), mojawapo wa makundi yenye vurugu ambayo huhusishwa na uhalifu nchini Mexico.
Kundi hilo lilitajwa na Marekani kuwa kundi la kigaidi mwaka uliopita.
Oseguera Cervantes, ni mmoja wapo wa walunguzi wa dawa za kulevya ambaye alikuwa akitafutwa sana na serikali ya Mexico na Marekani.
Idara ya kupambana na madawa ya kulevya nchini Marekani (DEA) ilikuwa imemuorodhesha "El Mencho" katika orodha ya watu wanaotafutwa sana duniani kuanzia mwaka wa 2020.
Marekani ilikuwa imeweka zawadi ya dola million 15 kwa yeyote mwenye habari kumhusu.
Serikali ya sasa ya Donald Trump ilikuwa imeiweka kundi la CJNG katika orodha ya makundi ya kigaidi ambayo Marekani inapania kuangamiza, hii ni baada ya maafisa wa usalama wa Marekani kudhibitisha kuwa kundi hilo linahatarisha usalama wa taifa hilo.
Uongozi wake katika kundi la CJNG
Baada ya Joaquin "El Chapo" Guzman kukamatwa na kupelekwa Marekani mwaka wa 2017, mmoja wa walanguzi wakuu waliokua wamesalia na kulengwa ni Oseguera Cervantes.
Pia anaitwa Nemesio Oseguera Ramos au Ruben Oseguera Cervantes, huku akiwa na majina mengine bandia kama "El Mencho" au "The Lord of the Roosters".
El Mencho anasemekana kuwa alizaliwa katika eneo la Tierra Caliente, jimbo la Michoacán,nchini Mexico karibu na mji wa Uruapan au Aguililla.
Alihamia nchini Marekani miaka ya 1980. Katika jimbo la Carlifornia alikamatwa mara kadhaa kwa makosa madogomadogo, ila akaanza kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya miaka ya 1990, na baadaye akarudishwa nchini Mexico.
Aliporejea Mexico, alijiunga ka kikosi cha polisi katika manispaa ya Jalisco, na akawa miongoni mwa wale waliojihusisha kumlinda mlanguzi wa dawa za kulevya Armando Valencia Cornelio, "El Maradona" kiongozi wa genge la Valencia au Milenio Cartel.
Kundi hilo lilikuwa na ushirikiano na kundi la Sinaloa Cartel, ila wakatengana mwaka wa 2010 baada ya kifo cha mmoja wa waanzilishi wake, Ignacio "Nacho" Coronel Pamoja na shemeji yake Abigael Gonzalez Valencia, "El Cuini".
Kuanzia hapo kundi la CJNG lilizaliwa, na kazi ya uhalifu ya "El Mencho's" ikaanza kushika kasi.
Upanuzi wa CJNG
Kundi la CJNG lilipanda ngazi kutoka kuwa genge linaloendesha oparesheni zake katika jimbo la Jalisco na Colima na kuenea karibu taifa nusu la Mexico.
Biashara yao kuu ni ilikuwa kuuza dawa aina ya amphetamine nchini Marekani na Ulaya, ila pia walikuwa wameanza kuuza dawa hizo bara Asia.
Kuna sababu tofauti kuhusu ukuaji wa kundi hilo la CJNG;
Mojawapo ni kukamatwa kwa viongozi wa makundi mengine na kusababisha kufifia kwao au kutokomea kwa makundi hayo kama kundi la Knights Templar katika jimbo la Michoacan.
CJNG lilijaza pengo la kundi hilo na wapinzani wake wengine.
Sababu nyingine ni kuwa CJNG iliwaajiri wataalam wa fedha na kemia, waliokuja na mifumo mipya ya kutengeneza dawa hizo.
Vurugu za magenge pia imechangia ukuaji wa kundi hilo. Mamlaka za Mexico ziliitaja kundi hilo la "El Mencho" kuwa hatari sana . Wachambuzi wanasema Oseguera Cervantes alipata umaarufu kwa kuangamiza makundi pinzani.
CJNG haikujihusisha na dawa za kulevya tu, bali pia kilimo,ufugaji wanaya, ujenzi katika jimbo la Jalisco ili kufungua biashara watakazotumia kutakatisha pesa za dawa za kulevya.
Kundi la CJNG pia inajulikana kwa ufisadi na kuwa na ushawishi kwa mamlaka za manispaa na ofisi za forodha. Hii imewasaidia kupata kemikali na malighafi zinazotumika kuzalisha dawa hizo kupitia bandari ya Manzanillo katika mji wa Colima na Lazaro Cardenas katika jimbo la Michoacan magharibi mwa Mexico.
Njia nyingine ya kujipatia kipato, ilikuwa kuwalazimisha wanabiashara wadogo na wastan magharibi mwa Mexico kuwalipa ushuru wa ziada.
Ila uvumi kuhusu hali yake mbaya ya afya, ulianza kuenea mwaka wa 2022. Iliripotiwa mara kadhaa kuwa alikuwa amefariki, ila mamlaka hazingeweza kudhibitisha hilo.
Wachambuzi wanasema huenda "El Mencho" wakati huu hakuwa anahusika moja kwa moja na oparesheni za CJNG.
Mmoja wa wanae, Ruben Oseguera Gonzalez, ndio alikua anashikilia nafasi ya pili katika uongozi wa kundi hilo, alikamatwa nchini Mexico na kupelekwa Marekani mwaka wa 2020, na hili lilisemekana kuwa pigo kwa kundi hilo pamoja sasa na mauaji ya Oseguera Cervantes na jeshi siku ya Jumapili.