Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni kweli Trump amesaidia kumaliza vita saba kama anavyodai?
- Author, Jake Horton & Nick Beake
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakati Rais Donald Trump akijaribu kumaliza vita vya Urusi na Ukraine, amekuwa akizungumzia rekodi yake juu ya amani tangu kuanza muhula wake wa pili madarakani.
Akizungumza katika Ikulu ya White House tarehe 18 Agosti, akiwa na viongozi wa Ulaya wakati wa kusaka kusitishwa mapigano kati ya Urusi na Ukraine, alidai: "Nimemaliza vita sita ... mikataba yote hii ya amani nilifanya bila hata kutaja neno 'kusitisha mapigano'."
Siku iliyofuata idadi aliyotaja iliongezeka hadi "vita saba."
Utawala wa Trump unasema Tuzo ya Amani ya Nobel "imepita mtu."
BBC Verify inaangazia kwa undani migogoro hii na ni kiasi gani rais huyo anaweza kuwa amehusika katika kuimaliza.
Israel na Iran
Mzozo wa siku 12 ulianza pale Israeli ilipoishambulia Iran tarehe 13 Juni. Trump alithibitisha alipewa taarifa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kabla ya mashambulizi hayo.
Marekani ilifanya mashambulizi katika maeneo ya nyuklia ya Iran - hatua inayoonekana na wengi kama njia ya kuumaliza mzozo huo. Tarehe 23 Juni, Trump alichapisha taarifa ya usitishaji wa vita kati ya Iran na Israel.
Baada ya mapigano kumalizika, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisisitiza kuwa nchi yake imepata "ushindi wa uhakika" na hakutaja usitishaji vita.
Tangu wakati huo Israel imeeleza kuwa inaweza kuishambulia tena Iran ili kukabiliana na vitisho vipya.
"Hakuna makubaliano juu ya amani ya kudumu au jinsi ya kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran," anasema Michael O'Hanlon, mtafiti katika Taasisi ya Brookings.
"Kwa hiyo tulichonacho ni usitishaji vita na sio kumalizika kwa vita, lakini nitampa pongezi, kwani kudhoofika kwa Iran kuliko fanywa na Israel - kwa msaada wa Marekani - ni muhimu kimkakati."
Pakistan na India
Mvutano kati ya nchi hizi mbili zenye silaha za nyuklia umekuwepo kwa miaka mingi, lakini mwezi Mei uhasama ulizuka kufuatia shambulio huko Kashmir, katika eneo linalodhibitiwa na India.
Baada ya siku nne za mashambulizi, Trump alichapisha taarifa kwamba India na Pakistan zimekubaliana "kusitisha mapigano.”
Alisema hayo ni matokeo ya "usiku mrefu wa mazungumzo yaliyopatanishwa na Marekani."
Pakistan ilimshukuru Trump na baadaye ikapendekeza kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, kwa "uingiliaji kati wake wa kidiplomasia".
India, hata hivyo, haikutaja mazungumzo ya kuhusika kwa Marekani: "Mazungumzo kuhusu kusitisha vita yalifanyika moja kwa moja kati ya India na Pakistan," Waziri wa Mambo ya Nje wa India Vikram Misri alisema.
Rwanda na DR Congo
Uhasama wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili ulipamba moto baada ya kundi la waasi la M23 kuteka eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DR Congo mapema mwaka huu.
Mwezi Juni, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya amani jijini Washington yenye lengo la kumaliza miongo kadhaa ya migogoro. Trump alisema makubaliano hayo yatasaidia kuongeza biashara kati yao na Marekani.
Makubaliano hayo yanataka "kuheshimiwa kwa usitishaji mapigano" kati ya Rwanda na DRC yaliyoafikiwa mwezi Agosti 2024.
Tangu makubaliano hayo, pande zote mbili zimeshutumiana kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi wa M23 - ambao Uingereza na Marekani wanasema wanasaidiwa na Rwanda - wametishia kujiondoa kwenye mazungumzo ya amani.
"Bado kuna mapigano kati ya Congo na Rwanda - hivyo usitishaji mapigano haujafanikiwa," anasema Margaret MacMillan, profesa wa historia aliyefundisha katika Chuo Kikuu cha Oxford.
Thailand na Cambodia
Tarehe 26 Julai, Trump alichapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, akisema: "Nitampigia simu Kaimu Waziri Mkuu wa Thailand hivi sasa, kuomba kusitishwa kwa mapigano, na kukomesha vita, ambavyo vinapamba moto kwa sasa."
Siku chache baadaye, nchi hizo mbili zilikubaliana "kusitisha mapigano mara moja na bila masharti" baada ya mapigano ya chini ya wiki moja kwenye mpaka.
Malaysia ilisimamia mazungumzo ya amani, lakini Rais Trump alitishia kusitisha mazungumzo ya kupunguza ushuru na Marekani, ikiwa Thailand na Kambodia hazitaacha kupigana.
Nchi zote mbili zinategemea sana mauzo ya nje kwenda Marekani.
Tarehe 7 Agosti, Thailand na Cambodia zilifikia makubaliano yenye lengo la kupunguza mvutano kwenye mpaka wao wa pamoja.
Armenia na Azerbaijan
Viongozi wa nchi zote mbili walisema Trump anapaswa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel kwa juhudi zake za kuleta makubaliano ya amani, ambayo yalitangazwa katika Ikulu ya White House tarehe 8 Agosti.
"Naamini katika mzozo huu anafaa kusifiwa, alizisukuma pande hizo kufikia makubaliano ya amani," anasema Bw O'Hanlon.
Mwezi Machi, serikali hizo mbili zilisema ziko tayari kumaliza mzozo wao wa karibu miaka 40 kuhusu hadhi ya eneo la Nagorno-Karabakh.
Vita vya hivi karibuni zaidi vilizuka mwezi Septemba 2023, pale Azabajani ilipolishikilia eneo hilo (ambalo Waarmenia wengi waliishi).
Misri na Ethiopia
Hakukuwa na vita, lakini kumekuwa na mvutano wa muda mrefu juu ya bwawa kwenye Mto Nile. Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance la Ethiopia lilikamilishwa msimu huu wa kiangazi huku Misri ikihoji kuwa maji inayopata kutoka Mto Nile yanaweza kupungua.
Baada ya miaka 12 ya mvutano, waziri wa mambo ya nje wa Misri alisema tarehe 29 Juni kwamba mazungumzo na Ethiopia yamesita.
Trump alisema: "Kama ningekuwa Misri, ningetaka maji kutoka Mto Nile." Aliahidi Marekani itatatua suala hilo haraka sana.
Misri ilikaribisha maneno ya Trump, lakini maafisa wa Ethiopia walisema yana hatari ya kuzidisha mvutano.
Hakuna makubaliano rasmi ambayo yamefikiwa kati ya Misri na Ethiopia kutatua tofauti zao.
Serbia na Kosovo
Tarehe 27 Juni, Trump alidai kuzuia kuzuka kwa vita kati ya nchi hizo, akisema: "Serbia, Kosovo zilikuwa zinakwenda vitani, vita vikubwa. Nilisema mukiingia vitani, hakuna biashara na Marekani. Walisema, sawa, labda hatutoingia vitani."
Nchi hizo mbili zimekuwa katika mzozo wa muda mrefu - urithi wa vita vya Balkan vya miaka ya 1990 - huku mvutano ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
"Serbia na Kosovo hazijapigana au kurushiana mabomu kwa muda mrefu, kwa hivyo hakuna vita vya kumaliza," anasema Prof MacMillan.
Nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kufanya biashara katika Ofisi ya Marekani chini ya rais Trump mwaka 2020, lakini hazikuwa kwenye vita wakati huo.