Lishe bora kwa watu wembamba wanaotaka kuongeza miili

wsqxa

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

"Wewe ni mwembamba sana, unaweza kuvaa suti yoyote ya kuogelea." Liliana Carvajal aliambiwa maneno hayo katika duka moja huko Miami, Marekani.

Katika mazingira ambayo kila mtu anataka kuwa mwembamba, ni vigumu kufikiria kwamba wapo wanaodhani wembamba ni tatizo au hata chanzo cha shida.

Lishe yenye afya

Kikawaida wembamba sio tatizo la kiafya, isipokuwa ikiwa umekuwa mwembamba kwa sababu ya ugonjwa au matatizo ya kutokula vizuri.

Hata hivyo, zipo sababu kwa baadhi ya watu kutaka kunenepa, kama vile kuongeza misuli, ushindani katika michezo fulani, kufidia ukosefu wa hamu ya kula, au kuwa na mwonekano mzuri zaidi.

Utawezaje kuongeza mwili? Wataalamu hawashauri uongeze mwili kwa kuanza kula mifuko ya chips, vyakula visivyo na mafuta, vyakula vya viwandani, vyakula vyenye mafuta mengi, keki au kunywa soda za sukari nyingi.

Ingawa watu wembamba wana uhuru zaidi kuliko wengine linapokuja suala la sukari nyingi, lakini lishe bora ni muhimu kwao pia. Wataalamu wa lishe wanapendekeza kuongeza uzito hatua kwa hatua hadi ufikie uzito wenye afya kuendana na urefu na umri wako.

Profesa wa lishe katika Chuo Kikuu cha Florida, Linda Bobrof, anaiambia BBC - inashauriwa kula angalau milo mitatu kwa siku, pamoja na vitafunio siku nzima.

"Vyakula vyenye kalori na virutubisho, pia vina mafuta mengi, lakini jambo muhimu ni kuchagua aina sahihi ya mafuta," anasema.

Karanga, korosho, mbegu, siagi ya karanga, parachichi na mboji ni vyanzo bora vya mafuta ya mimea yenye afya, na vina virutubisho na kalori.

Mafuta ya nyama hutoa virutubisho na kiasi sawa cha kalori kama mafuta ya mimea, lakini pia nyama ina mafuta mengi ambayo yanaweza kuongeza kalori mbaya mwilini.

Lengo ni kuchagua vyakula vilivyo na vitamini, madini, virutubisho na kalori, ili kila ulacho kiwe na virutubisho.

Kuongeza misuli

a\

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Chagua vyakula vyenye virutubishi vingi

Sababu nyingine ya kutaka kupata uzito ni hitaji la kuongeza misuli. Wanariadha na wafanya mazoezi ambao wanataka kupata misuli, wanapaswa kula kalori za kutosha na kufanya mazoezi ili kuhakikisha wanapata uzito katika sehemu sahihi za mwili.

Kulingana na mtaalamu wa lishe za michezo, Gavin Allinson, vyakula bora vya kujenga misuli ni vile vyenye protini, kama vile kuku na samaki weupe.

"Unapaswa kuchanganya milo hii na vyakula vya wanga, kama vile wali na ugali, katika mlo wa baada ya mazoezi," anaelezea.

Watu wanaofanya mazoezi sana lakini hawataki kuongeza misuli, wao wanapaswa kula mara kwa mara vyakula vyenye afya, ili kuongeza shughuli zao za kimwili na kudumisha au kupata uzito.

Kujithamini

Katika ulimwengu ambamo zaidi ya nusu ya watu wa nchi za Magharibi ni wazito kupita kiasi, watu wembamba mara nyingi huangaliwa tofauti.

Michelle Salem wa Miami Beach, anasema kutojiamini kutokana na kuwa mwembamba sana kulimpelekea kutotaka kuvaa aina fulani ya nguo.

"Si rahisi kwangu kupata nguo zinazonifaa bila kwenda sehemu ya watoto au vijana, na wakati mwingine madaktari hunishutumu sipendi kula," anasema.

Liliana Carvajal naye anaeleza kwamba mara nyingi watu humuhisi ni mgonjwa au mraibu wa madawa ya kulevya kutokana na wembamba wake.

"Ni jambo la kawaida sana kuitwa mgonjwa, kudhaniwa unatumia dawa za kulevya au kuambiwa huli, watu wanakuita mwembamba kana kwamba ni pongezi, wakati hawajui nimeridhika na uzito wangu.’’

Namna ya kupata uzito

uyjh

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wataalamu hawashauri uongeze mwili kwa kuanza kula mifuko ya chips

Kula mara mara kwa mara.

Chagua vyakula vyenye virutubishi vingi.

Kunywa juisi za matunda, mtindi na maziwa.

Pendelea vyakula vilivyotengenezwa kwa maziwa.

Pika michuzi na supu kwa maziwa badala ya maji.

Epuka msongo wa mawazo.

Fanya mazoezi.