Jinsi Akili Mnemba (AI) inavyosaidia kuzuia kukatika kwa umeme kwa siku zijazo

Chanzo cha picha, Aseef Raihan
Huku mahitaji ya umeme yakiongezeka, Akili Mnemba (AI) sasa inatumiwa kusaidia kuzuia kukatika kwa umeme.
"Niliamka katikati ya usiku kukiwa na baridi sana," anakumbuka Aseef Raihan. "Nilichomoa begi langu la kulalia la kijeshi, na kulala ndani yake usiku huo kwa ajili ya kupata joto. "Asubuhi niligundua kuwa hakukuwa na umeme."
Bw Raihan anaelezea kuhusu tukio lililotokea mnamo Februari 2021 alipokuwa San Antonio, Texas, alipokuwa akihudumu katika Jeshi la Wanahewa la Marekani.
Mwezi huo jimbo lilikumbwa na dhoruba ya Uri ya msimu wa baridi. Halijoto iliposhuka hadi -19C, wenyeji wa jimbo la Texas walipotaka kurejesha joto kwenye nyumba zao , mahitaji ya umeme yaliongezeka kwa kiwango cha juu.
Wakati huo huo, minara ya umeme ya Texas ikuwa imeharibika Mitambo ya upepo iliganda juu, theluji ilifunika paneli za jua, na kinu cha nishati itokanayo na nyuklia kililazimika kuondolewa nje ya mtandao kama tahadhari.
Kwa kukosa umeme wa kutosha kuzunguka, umeme ulikatika kwa zaidi ya nyumba na biashara milioni 4.5, kwanza kwa masaa, na kisha kwa siku nyingi.
"Bila nishati ya umeme, kazi hazikufanyika hata kidogo. Na haungeweza kutumia jiko la umeme au microwave kwa chakula," anakumbuka Bw Raihan.
Mwishowe ilichukua zaidi ya wiki mbili kwa milingoti ya umeme ya Texan kurudi katika hali ya kawaida.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dhoruba hiyo ilifichua udhaifu wa mifumo tunayochukulia kirahisi kutuletea umeme saa nzima.
Na ingawa si nchi zote ambazo zina majira ya baridi kali kama inavyotokea katika Amerika Kaskazini, mahitaji ya umeme yanaongezeka kote ulimwenguni.
Kuanzia kuchaji magari ya umeme, hadi viyoyozi vya nyumbani (AC) ni dhahiri kuwa tunatumia nguvu zaidi na zaidi katika maisha yetu ya kila siku.
Hii inakuja wakati nchi zinapozidi kuelekea kwenye vyanzo vya nishati mbadala. Ikiwa upepo hauingii, na jua haiangazi, basi uzalishaji wa umeme hupungua.
Haya yote yalisababisha Waziri wa Nishati wa Uingereza Claire Coutinho kuonya mwezi uliopita kwamba nchi inaweza kukabiliwa na kukatika kwa umeme katika siku zijazo iwapo hakutakuwa na vituo vipya vya nishati ya gesi vya nyongeza.
Njia nyingine ya kufanya mifumo ya nishati iwe thabiti zaidi ni kwa kuongeza betri kubwa kwenye mfumo wa umeme wa taifa.
Wazo ni kwamba wakati umeme unapodkatika kuwe na nishati ya ziada, betri zinaweza kuchaji, na kisha kutolewa umeme baadaye wakati kuna mahitaji zaidi ya nishati.
Hii ni njia ambayo imeanza kutumiwa katika jimbo la Texas nchini Marekani.
"Tangu dhoruba tulijenga zaidi ya gigawati tano za uwezo wa kuhifadhi betri huko Texas katika miaka mitatu, ambayo kwa kweli ni kasi ya ajabu," anasema Dk Michael Webber, profesa wa rasilimali za nishati katika Chuo Kikuu cha Texas huko Austin. Nishati nyingi hiyo, anasema, imetokana na "viwanda vinne vikubwa vya nguvu za nyuklia".

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini, ili betri kama hizo ziwe muhimu sana, inahitajika kujua ni wakati gani mzuri wa kuchaji, na wakati mzuri wa kuzitumia. Hiyo ina maana ya kufanya ubashiri tata kuhusu kiasi gani cha umeme kitahitajika katika siku zijazo.
"Jambo kuu linaloleta utofauti mkubwa zaidi ni hali ya hewa na mahitaji ya umeme," anasema Gavin McCormick, mwanzilishi wa WattTime ya teknolojia mpya.
Kampuni yake ya Oakland, California inatengeneza programu ya Akili Mnemba (AI) inayotabiri usambazaji na mahitaji ya umeme katika eneo fulani.
Taarifa hii inaweza kisha kueleza betri wakati wa kuchaji na kutochaji.
Taarifa hiyo hiyo pia inaweza kutumika majumbani kusaidia watu kutumia umeme kwa bei nafuu zaidi.
"Kwa hivyo ikiwa ulikuwa na gari la umeme ambalo unahitaji kuwa tayari kwa saa nane, lakini inachukua masaa mawili au matatu tu kuchaji, kinachoweza kufanyika ni kupata vipindi vya dakika tano usiku kucha ambapo kuna nishati ya ziada, au labda kuna nishati safi," Bw McCormick anasema.
"Itachaji kwa kasi ndogo wakati wote kwa ubora na bado itakuwa tayari asubuhi."
Akili Mnemba inaweza kufanya ubashiri huu kwa kuchanganua mifumo ya hali ya hewa, tarehe za likizo, ratiba za kazi, na hata wakati mpira wa miguu unachezwa. "Kila mtu huamka na kutengeneza kikombe cha chai wakati wa mapumziko," Bw McCormick anasema.
Kampuni nyingine inayotumia AI kutabiri mahitaji ya umeme ni ya kampuni ya umeme ya Denmark. Hutumia Akili Mnemba katika utabiri wa mifumo ya hali ya hewa kama vile mawingu , nguvu ya upepo, halijoto na mvua.
Taarifa hii inatumika kuelewa vyema ni kiasi gani cha umeme kitazalishwa kutoka kwa mitambo ya upepo au paneli za jua.
"Ikiwa unaweza kutabiri kwa usahihi mapema ni kiasi gani cha upepo utakuwa kwenye mfumo, unaweza kupanga mapema." Anasema Olivier Corradi, mwanzilishi wa kampuni hiyo.
"Mfano mmoja ni Google, ambapo tunawapa utabiri wa jinsi mifumo ya taifa ya umeme itakavyofanya kazi katika saa chache zijazo.
Wanaweza kuutumia katika vituo vyao vya data kubadilisha muda ambao wanatumia umeme "
Akili Mnemba pia sasa inatumiwa kulinda miundombinu halisi ambayo hupeleka umeme kwenye nyumba zetu.
Kampuni moja, Buzz Solutions, huitumia kuchanganua picha za nyaya za umeme, nguzo na vituo vidogo, kubaini dalili za uharibifu kama vile sehemu zilizovunjika au zenye kutu.
Mfumo huo pia unabainisha wakati miti na mimea mingine ya kijani inakua karibu sana na nyaya za umeme.
Sio tu kwamba hii inaweza kuzuia kukatika kwa umeme kutoka kwa njia zilizoharibika, lakini pia inaweza kupunguza hatari ya moto wa nyikani, ambao unaweza kusababishwa na kugusana kwa nyaya za umeme na miti kama ilivyotokea California katika miaka ya hivi karibuni.
Teknolojia hiyo pia inaweza kubaini na kuripoti kiotomatiki kwa wafanyakazi wa kampuni ya umeme sababu nyingine kuu ya kukatika kwa umeme - wanyamapori.
"Mara nyingi cha kushangaza, wanyama wadogo kama vile panya huingia kwenye vituo vidogo na kupigwa na umeme," anasema mwanzilishi mwenza wa Buzz Solutions Vikhyat Chaudhry.
"Kupigwa kwao na umeme wakati mwingine husababisha mlipuko mkubwa katika kituo kidogo. Akili mnemba yetu ambayo imetumwa kwenye vituo vidogo, moja ya mambo ambayo inagundua ni kuingiliwa na wanyama ikiwa ni pamoja na simbamangu na chindi."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












