Je, kudhibitiwa kwa mji wa Masisi na M23 huko DR Congo kunamaanisha nini?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Uasi wa kundi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, ulichukua udhibiti wa mji wa Masisi, mji muhimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jumamosi.

"Ni kwa masikitiko makubwa kufahamu kuhusu kutekwa kwa kituo cha Masisi na M23," Alexis Bahunga, mbunge wa jimbo la Kivu Kaskazini, aliliambia shirika la habari la AFP.

"Tunaiomba serikali kuchukua hatua zinazolenga kurejesha mamlaka ya serikali katika eneo lote," aliongeza.

Masisi iko karibu kilomita 80 kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Alexis Bahunga anaelezea eneo hilo kuwa "katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu".

Kulingana na Aimé Von Businga, Mhariri Mkuu wa Kinshasa Times Online, "idadi kubwa ya watu wanatafuta makazi katika vijiji vinavyozunguka na karibu na Goma, ambayo tayari ina msongamano mkubwa wa wakimbizi wa ndani wapatao milioni nne". Anasema hali bado ni ya wasiwasi.

Mkuu wa shirika la kimataifa linalofanya kazi huko Masisi aliiambia Reuters kwamba wafanyakazi walikuwa katika mshtuko na hawakuweza kuendelea na shughuli zao kwa sababu biashara zimefungwa, na hivyo kufanya kuwa ngumu kupata vifaa.

"Hawajui jinsi ya kuondoka mjini kwa sababu tunahofia kwamba vikosi vya Congo vitaanzisha mashambulizi ya kukabiliana na hali hiyo," alisema.

Wakati huo huo, jeshi la DRC limerudi nyuma, likisema linaepuka kupoteza maisha zaidi katika mji wa Masisi.

Mkazi mmoja aliiambia AFP kwamba M23 walikuwa na mkutano na wakazi wa mji huo, wakisema "wamekuja kuikomboa nchi."

Aimé Von Businga alisema kuwa "katika miji yote iliyochukuliwa na M23, siku chache za kwanza, watu walikimbia, kisha M23 wakafanya mikutano kuwaambia watu warudi kwenye maisha yao ya kawaida na wasiogope kulipizwa kisasi."

Wengine watarudi, lakini wengi hawatarudi.

Siku ya Ijumaa, M23 waliteka mji wa karibu wa Katale.

Mamlaka za Congo bado hazijatoa maoni yoyote kuhusu upotezaji wa miji hii.

Lakini Alexis Bahunga, alisema kuwa "Serikali itachukua hatua kurejesha mamlaka ya Jimbo katika eneo lote.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya M23

Tangu Novemba 2021, waasi wa M23 (wa "Machi 23 Movement") wameteka maeneo makubwa mashariki mwa DRC, yenye utajiri wa maliasili na yaliyosambaratishwa na migogoro kwa miaka 30.

Mwishoni mwa Disemba, uasi uliendelea kuota mizizi katika sehemu ya kaskazini ya Kivu Kaskazini.

Ulifika karibu kilomita hamsini kutoka Lubero, mji mkuu wa eneo hilo, na karibu kilomita mia moja kutoka mji wa Butembo. Mwisho ni kitovu muhimu cha kibiashara katika kanda.

Mwezi Julai, Rwanda haikukanusha ripoti ya Umoja wa Mataifa ikisema ina takribanI wanajeshi 4,000 wanaopigana pamoja na M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, Iliishutumu serikali ya Congo kwa kutofanya vya kutosha kukabiliana na miongo kadhaa ya migogoro mashariki mwa nchi hiyo.

Rwanda imesema hapo awali kuwa mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walikuwa wanafanya kazi na baadhi ya wale waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Kundi la M23, kutoka kundi jingine la waasi, lilianza kufanya kazi mwaka 2012, ili kulinda idadi ya Watutsi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

Aimé Von Businga, Mhariri Mkuu wa Kinshasa Times Online anaeleza kuwa sababu hii kuu ya mzozo imebadilika na kuwa masuala ya kiuchumi na kijiografia.

"Leo hii, mwelekeo mwingine wa kiuchumi umeongezwa, kwa sababu wengi wanaamini kwamba vuguvugu hilo sasa linaungwa mkono na Rwanda, sio tu kwa sababu za ukaribu wa kikabila na Rwanda, lakini pia kwa sababu za kiuchumi," anabainisha.

Kwa mwanasayansi wa siasa Christian Moleka, kutekwa kwa Masisi kunaweza kuwa na mambo mawili makuu.

La kwanza ni kwamba wakati FARDC inaonekana kupinga kusonga mbele kwa M23, kutekwa kwa Masisi kunaimarisha utawala wa kundi hili katika maeneo ya Rutshuru na Masisi.

M23 inadhibiti maeneo mawili kati ya sita katika jimbo la Kivu Kaskazini.

"Zaidi ya kipengele hiki cha kijeshi, pia kuna suala muhimu la kiuchumi," anaongeza.

Masisi ni kituo kikubwa cha kibiashara na njia ya kimkakati ya kuunganisha Saké na Goma.

"Kwa kudhibiti Masisi, M23 inapunguza uwezo wa usambazaji katika jiji la Goma kupitia Saké, kwa sababu ni barabara muhimu, ni kituo muhimu cha biashara," anaelezea Christian Moleka.

Wakosoaji wa Rwanda wanaishutumu, kwa kuitumia M23 kupora madini kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kama vile dhahabu, cobalt na tantalum, ambayo hutumiwa kutengeneza simu za mkononi na betri za magari yanayotumia umeme.

Mwezi uliopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisema inaishitaki Apple kwa matumizi yake ya "madini ya damu," na kufanya kampuni kubwa ya teknolojia kusema kuwa imeacha kutafuta madini kutoka kwa nchi hizo mbili.

Rwanda imekanusha kuwa mshirika wa usafirishaji wa madini haramu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mazungumzo magumu ya amani

Kusonga mbele na kuendelea kwa mapigano kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano kunadhoofisha zaidi juhudi za kumaliza mzozo huo.

Mwezi Desemba, Marais wa Congo Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walipaswa kukutana kwa ajili ya mkutano ulioandaliwa mjini Luanda na mkuu wa nchi ya Angola Joao Lourenço.

Kwa bahati mbaya, mkutano ulioandaliwa na mpatanishi mteule wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro huu haukufanyika.

Hakika, makubaliano ya kurejesha amani na utulivu mashariki mwa DRC yalipaswa kuwekwa mezani lakini pande hizo mbili zilishindwa kuafikiana kuhusu masharti hayo.

Hii ilisababisha mkutano huo kuahirishwa katika dakika za mwisho.

Lakini mwezi mmoja uliopita, wenye mamlaka huko Kinsahsa walitangaza kwamba wataendelea kwenye safu ya kijeshi.

Aimé Von Businga anaamini kwamba utekaji huu mpya wa miji na M23 "unaweza kuilazimisha DRC kurejea kwenye meza ya mazungumzo".

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga