Ukosefu wa usalama: Jinsi ambavyo DRC imekuwa tegemezi kwa uingiliaji kati wa majeshi ya kigeni

Na Armand Mouko Boudombo

BBC Africa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikikumbwa na mizozo kwa zaidi ya nusu karne, ambayo imesababisha uingiliaji kati wa majeshi ya kigeni, baadhi yakiunga mkono serikali ya Kinshasa, huku mengine yakikabiliana nayo.

Mnamo Aprili 19, 2024, ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) ulikabidhi kambi ya Bunyakiri kwa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC).

Kaimu kamanda wa kikosi cha MONUSCO, Meja Jenerali Khar Diouf, alielezea uhamisho wa kambi hii ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa iliyopo Bunyakiri mwaka wa 2004 kama hatua ya "kihistoria".

Hii ni kambi ya pili ambayo MONUSCO iliikomboa nchini humo, baada ya kujiondoa, kwa wanajeshi ambao walikuwa wamekaa katika kituo cha Kamanyola Februari 28, 2000 katika jimbo hilo la mashariki mwa DRC la Kivu Kusini.

Baada ya kuondoka, polisi wa Congo walikabidhiwa kambi hiyo.

Makabidhiano haya mawili ya kwanza yanaashiria kuanza kwa operesheni ambayo itapelekea, kuondoka kwa walinda amani, kabla ya Desemba 31, 2024 wote 13,500 wa Umoja wa Mataifa waliokuwepo nchini humo tangu mwaka 1999.

Kuondoka kabisa kwa sehemu ya kilosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa, kama ilivyoafikiwa Novemba mwaka jana kati ya mamlaka ya Congo na Umoja wa Mataifa, itakuwa hatua muhimu katika historia ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayojulikana na kiasi cha msaada wa kijeshi wa kigeni.

Katika makala haya, tunakuletea sehemu kubwa ya operesheni za kijeshi za kigeni ambazo zimefanyika nchini DRC, tangu nchi hii ipate uhuru wake.

Uhuru wa jeshi la Congo na ONUC kwa ajili ya ukombozi (1960-1964)

Ilikuwa kama hadithi ya ukosefu wa mawasiliano mema uliyochochea uhasama. Miezi michache kabla ya uhuru wa nchi hiyo, tarehe 30, 1960, askari wa Congo walionyesha kiasi fulani cha uchovu na hasira na hali iliyokuwepo.

Ndani ya jeshi, kulikuwa na wanajeshi elfu 25, wakiwemo maafisa 1000 wa Ubelgiji na maafisa wasio na vibali na hapakuwa na maofisa Wacongo .

Kwa miezi kadhaa, walikuwa wakiongeza walinzi na kuimarisha operesheni za kulinda amani nchini humo, wakiwa na matumaini ya kubadilisha vyeo mara tu baada ya kupatikana kwa uhuru , ndipo watoe vyeo vya maofisa kwa wengine.

Siku nne baada ya uhuru, uasi wa kwanza ulizuka katika kambi kubwa ya kijeshi ya Léopold, inayofahamika sasa kama kambi ya Kokolo, mjini Kinshasa. Wanajeshi 500 wa Congo waanza safari.

Kauli mbiu yao ilikuwa : "Sisi pia tunataka uhuru wetu". Kiongozi wao pia alikamatwa haraka na kuwekwa gerezani.

Jenerali wa Ubelgiji Emile Janssens, ambaye alitaka kutuliza hali hiyo, aliwahutubia wanajeshi, akiwaambia kwamba vyeo vyao havibadiliki, akiandika kwenye ubao "Kabla ya uhuru = baada ya uhuru".

Ghafla kusanyiko la wanajeshi 500 liligeuka kuwa maandamano, kisha ghasia. Wanaume hawa walitaka kuchukua udhibiti wa ghala la silaha, askari polisi wakajaribu kuwarudisha nyuma, lakini bado wanafanikiwa.

Siku iliyofuata, waasi hao waliondoka kambini na kuwashambulia wazungu wa Ubelgiji, ambao walikuwa maili 110 hivi nchini Congo.

Waziri Mkuu wakati huo Patrice Lumumba alijaribu kutuliza hali hiyo kwa kutangaza kupandishwa ngazi moja ya cheo kwa kila askari, lakini hakufanikiwa kutuliza ghasia. Viongozi wa jeshi la Ubelgiji walifanya operesheni ya nguvu kuwatawanya wanajeshi na walimuarifu Patrice Lumumba tu mwishoni mwa operesheni hiyo.

Vurugu hizo zilisababisha kufukuzwa kwa kamanda Mbelgiji wa jeshi la Congo, Emile Jansens, Wabelgiji wakituhumiwa kwa kuandaa mapinduzi dhidi yake.

Wakidai kuwa wamekuja kuwahamisha kwa ndege watu wao, viongozi wa Ubelgiji walitua DRC, bila kushauriana na mamlaka ya Congo, ndege ikiwa na askari elfu 10 wa ziada wa Ubelgiji, kusaidia wenzao.

Baada ya siku kadhaa za machafuko na mkanganyiko, miji kadhaa iliteketezwa kwa moto katika maeneo kadhaa ya nchi.

Jimbo la kimkakati na lenye wenye utajiri wa madini la Katanga liliishia kujitengwa, na kufungua mlango wa ukarabati wake kwa jeshi la Ubelgiji, lililoshirikiana na kiongozi wa jimbo, Joseph Tchombe, katika eneo hilo. "Vita vya ukoloni" vikawa wazi.

Walipokuwa ziarani nchini humo iliyolenga kuhamasisha raia kurejesha utulivu, Rais Kasa-Vubu na Waziri Mkuu Lumumba, walituma ujumbe watelegramu kwa Umoja wa Mataifa mnamo Julai 12, 1960.

Walishutumu kile walichoita "kitendo cha uchokozi dhidi ya nchi yetu, kwa kutuma askari wa Ubelgiji kinyume na mkataba wa urafiki uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili", na kuishutumu "serikali ya Ubelgiji kwa kuandaa kwa makini kujitenga kwa Katanga", kisha wakaomba "msaada wa kijeshi." kutoka Umoja wa Mataifa".

Mmno tarehe 14 Julai, walitangaza kwa serikali ya Ubelgiji, kwa njia ya telegram, kukatizwa kwa mahusiano ya kidiplomasia. Siku hiyo hiyo, Umoja wa Mataifa uliamua kuingilia kati nchini Kongo, na kupeleka wanajeshi wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kwenye ardhi ya Kongo siku mbili baadaye.

Azimio la Umoja wa Mataifa liliidhinishwa lililoitaka Ubelgiji kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo. Brussels ilijaribu kurudisha nyuma tarehe ya mwisho ya kuondoka jimboni humo na kuichelewesha iwezekanavyo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojumuisha wanaume 20,000, ambao ulidumu kwa muda wa miaka saba katika eneo la Congo, ambao haukuwa na mamlaka ya halisi ya kuingilia kati katika masuala ya ndani ya nchi. Ujumbe huo ulikuwa na jukumu la kutafuta suluhu la kisiasa.

Ujumbe huo ulitatizwa na kuendelea kwa "vita vya dunia", na kambi ya viongozi iligawanyika mwezi Agosti. Rais Kasa-Vubu akaamua kumfukuza kazi Waziri Mkuu Lumumba, ambaye alianzisha utaratibu wa kumshtaki rais.

Kufuatia mpasuko huo wa kisiasa Kanali Mobutu Sese Seko, alifanya mapinduzi ya kijeshi Septemba 14 mwaka huo huo. Hatimaye mgogoro huo uligharimu maisha ya Patrice Lumumba ambaye aliuawa mnamo tarehe 17 Januari, 1961.

Kulingana na mwanaharakati wa mashirika ya kiraia wa Congo, Omar Kavota, ONUC ilirekodi matokeo mchanganyiko kwa sababu ya "maslahi ya mataifa makubwa ambayo maslahi yao yanakinzana katika udhibiti wa utajiri wa Congo."

Vita Baridi, na hatua ya USSR (Julai - Agosti 1960).

Wito wa Umoja wa Mataifa uliotolewa na Lumumba na Rais Kaza-vubu mnamo Julai 12, 1960 uliambatana na mwingine kwa Rais wa Sovieti Nikita Khrushchev, akimjulisha kwamba anaweza kuomba msaada wake wa kuingilia kati mgogoro huo.

Mgogoro huu wa kwanza baada ya uhuru wa Congo, dhidi ya mkoloni wa zamani Ubelgiji, uliipata katikati ya Vita Baridi, ambapo kambi mbili, moja ya Magharibi na nyingine Mashariki, zilipigana.

Katika mazingira haya, Marekani ilihofia uingiliaji kati wa kijeshi kutoka kwa mpinzani wa Usovieti. Waziri Mkuu Patrice Lumumba alialikwa kwenye vikao vya Washington na New York. Wakati huo, ujasusi wa Marekani uliielezea hali nchini Congo kama hatua ya kawaida ya kikomunisti.

Huku Waziri Mkuu wa Congo, akiwa amechoshwa na majaribio haya ya kidiplomasia kuelekea Magharibi, hatimaye alipata msaada wa usafiri wa anga kusafirisha vifaa na hivyo kuzuia mpango wa kujitenga kwa eneo la Kasai Kusini, kuanzia katikati ya mwezi Agosti. Jimbo hilo pia liliamua kujitenga baada ya Katanga.

Zawadi ya Muungano wa Usovieti ambayo ilisikika kama hukumu ya kifo dhidi ya Lumumba.

Kushindwa kwa Che Guevara (mwaka 1965)

Muargentina mwenye itikadi za Kimarxist-Leninist na kimataifa, ambaye pia mwanasiasa wa Amerika ya Kusini, Ernesto Che Guevara, anajulikana kuwa mwanamapinduzi.

Mwaka 1959, alishirikiana na Fidel Castro, katika kumpindua kiongozi wa Cuba Fulgencio Batista.

Makubaliano hayo yalifikia kikomo na mshirika wake, Fidel Castro, ambaye alikuta misimamo yake ikiwa ni ya kiliberali mno na kumtimua katika serikali yake mwanzoni mwa mwaka 1965.

Kisha Che Guevara aliondoka Cuba, ambako alikuwa ni uraia, na kuelekea Congo, ambako alitua Aprili mwaka huo huo, na wanaume wachache. Lengo lake ni kuuza nje mapinduzi yake, ili kuzuia ubeberu kwenye ardhi ya Afrika.

Nia yake hiyo haitazaa matunda. Che alifika katika eneo lenye migodi ya madini na makundi mengi yenye silaha, katika vita vilivyochochewa na uporaji wa rasilimali za madini na mapambano ya Wamarekani na Wasovieti waliopigana vita visivyo na huruma.

Aidha, harakati za kizalendo zinazomuunga mkono Lumumba ambazo alikusudia kujiunga nazo ttayari zilikuwa zimevunjika na Lumumba alikuwa amebaki na udhibiti wa maeneo madogo ya ardhi.

Hatimaye Che aligundua ukosefu wa utaratibu wa wanajeshi, ukosefu wa ujuzi wa mbinu za vita vya msituni , uhasama baina ya wababe wa kivita , na kwa hiyo , Congo ilikuwa sio mahala pa kutekeleza mapinduzi, ameandika mwandishi wa wasifu wake.

Baada ya miezi 7 ya kujaribu "kuiangamiza Congo", aliondoka Congo, akielekea Bolivia ambako alifariki miaka miwili baadaye.

Watu "wabaya" kwa na dhidi ya Mobutu (1961-1967, kisha 1996)

Tangu ipate uhuru wake mwaka 1960, Congo ya zamani ya enzi ya utawala wa Ubelgiji imekuwa, kama wataalam wanasemavyo, maabara ya mazoea mapya. Hivi ndivyo ilivyo kwa mamluki.

Neno hili linaonekana katika historia ya kijeshi ya Congo, mwanzoni mwa uhuru wa koloni hili- Ubelgiji.

Jimbo tajiri la Katanga lilionyesha dalili za kujitenga mapema sana, kabla ya kuchukua hatua. Uamuzi huo usiokubalika kwa Jimbo la kati, ambalo lilinzisha mashambulizi ya kuwarudisha watu waliokaidi - jimbo hili lenye utajiri wa madini, na lile la Bas Congo.

Mamlaka ilikusanya jeshi la kitaifa na kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa kukabiliana hili. Muungano huo ulikabiliwa na uasi wa ndani, ambao mara nyingi uliungwa mkono na Ubelgiji..

Hili ni kundi la mamluki wa mataifa na jamii kadhaa, waliokuwa katika vitengo vitatu, wakiongozwa na majina matatu mashuhuri. Mike Hoare, mwanajeshi wa zamani wa Uingereza, alishiriki katika Vita vya Pili vya Dunia, kabla ya kuanza kazi kama mhasibu, kabla ya kuajiriwa mnamo 1961 kama mamluki na rais wa mkoa wa Katanga Moïse Tshombe.

Hoare aliongoza kitengo cha mamluki nchini Congo, ambacho alikipa jina la utani "the wild geese" ["bukini mwitu".]

Karibu na kitengo hiki, kulikuwa na kitengo cha Jean Schramme, al maarufu Black Jack ambaye alikuwa nahodha wa jeshi la Ubelgiji. Baada ya utumishi wake wa kijeshi nchini Kongo mwaka 1954, alianza kazi kama mkulima baada ya kununua shamba katika nchi hiyo hiyo, kabla ya kufukuzwa huko na jeshi la Congo ambalo lilikuwa limepata uhuru.

Alikimbilia Katanga, na kuanza safari yake na Moïse Tshombe mwaka 1961.

Na aliyekuwa kiongozi maarufu zaidi ya viongozi watatu wa mamluki, alikuwa ni Bob Denard. Alisajiriwa katika jeshi la majini akiwa na umri wa miaka 18, ambako alipanda ngazi hadi cheo cha kamanda wa mafunzo katika makomandoo wa bunduki, anajulikana kwa kupigana katika Vita vya Indochina [India na China], na kushiriki katika misheni kadhaa za siri za Ufaransa.

Denard alichukua madaraka ya Congo mwaka 1961, ambapo alifanya kazi kama mkono wa siri wa Ufaransa kulingana na mwanahistoria wa Ufaransa Walter Bruyère-Ostells.

Viongozi hao watatu wanatajwa katika jumbe kadhaa za ujasusi na kukabiliana na shutuma za uhalifu, na kupindua serikali za bara.

Mamluki hao walikuwa chini ya utawala wa Jenerali Mobutu, wakati huo akiwa mkuu wa jeshi la Kongo, ambapo Juni 1964, Moise Tsombe aliamua kujiunga na serikali kuu ya Rais Kasavubu, ambaye alikuwa waziri mkuu.

Jeshi la Taifa la Congo, ANC, liliungana , kwa msaada wa Denard, ambaye aliweza kujitofautisha na washindani wake wengine wawili ardhini.

Akiwa madarakani baada ya mapinduzi ya mwaka 1965 dhidi ya Rais Kasavubu, Mobutu alikataa wazo la kuunda kikosi cha mamluki na ANC, na pia alikusudia kujitenga na mamluki ambao bado wanaitwa "wageni wa kujitolea". Waliasi chini ya uongozi wa Bob Denard.

Mnamo Julai 5, 1967, Jenerali Mobutu mwenyewe alitangaza, katika ujumbe wa redio, kwamba alikuwa ameanzisha hali ya kuzingirwa, baada ya "makomando wa kigeni kutua kutoka kwenye ndege mbili zisizojulikana kwa miavuli na kuchukua uwanja wa ndege wa Kisangani (zamani ukiitwa Stanleyville).

Wakati huo huo, raia wa kigeni waliotajwa kuwa wanamgambo walishambulia vikosi vya jeshi la taifa la Congo huko Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu, ambako mapigano yanaendelea.

Kabla ya vyombo vya habari vya ndani kutangaza siku tatu baadaye, mwisho wa uhasama, kusherehekea "ushindi mkubwa wa jeshi la Congo dhidi ya majeshi ya uovu". Lilitolewa tangazo nchini Rhodesia (Zimbabwe ya sasa) kwamba Bob Denard, pamoja na baadhi ya watu wake wamejeruhiwa.

Lakini mamluki hao waliitwa tena nchini Zaire mwaka 1996, kujaribu kumuokoa Jenerali Mobutu kutoka kwa kundi la AFDL linaloongozwa na Laurent-Désiré Kabila. Katika vita hivi mamluki walishindwa tena.

Vita Kuu ya Dunia ya Congo miaka ya 1990

Moja ya sehemu muhimu zaidi ya historia ya uingiliaji wa kijeshi wa kigeni nchini DRC ulifanyika katika nusu ya kwanza ya miaka ya 1990.

Nchi jirani ya Rwanda ndiyo kwanza ilikuwa imepitia kipindi kibaya zaidi, cha mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambayo yaligharimu maisha ya watu wapatao 800,000 ya Watutsi walio wachache katika kipindi cha takriban siku mia moja.

Athari za mzozo huo ziliufikia upande wa pili wa mpaka, na kuvuka, kulingana na Umoja wa Mataifa, kuna Wahutu wapatao milioni 1.2, ambao wanaishi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako ni makao ya Watutsi wengi.

"Wengi wa wakimbizi hao ni Wahutu, wakiwa wameandamana na wa jeshi wa jeshi la zamani la serikali ya Rwanda (FAR), na wanamgambo wa Interahamwe ambao walikuwa na jukumu kubwa katika mauaji ya halaiki," anasema mtaalamu wa sayansi ya siasa nchini Ubelgiji, Filip Reyntjens.

Ni kutoka sehemu hii ya nchi ambapo uasi ulianza mwaka 1996, ambao ulihusisha Chama cha kikosi vya kidemokrasia cha ukombozi wa Congo (AFDL) kilichoongozwa na Joseph Désiré Kabila dhidi ya jeshi la kawaida la Rais Mobutu Sese Seko.

Tarehe 17 Mei, 1997, waasi wa AFDL, wakati huo wakiungwa mkono na Rwanda na Uganda, walifanikiwa kuupindua utawala wa Rais Mobutu, aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1965, na kumweka Laurent Désiré Kabila madarakani.

Unyakuzi huu wa utawala mikononi mwa Mzee Mobutu haukutuliza baina ya washirika wa zamani katika vita vya kumpindua Mobutu.

Baadhi ya wanajeshi wa AFDL waliasi na kuunda vuguvugu la waasi la Rassemblement congolais pour la democratie (RCD).

Vuguvugu hilo liliungwa mkono na Rwanda, Uganda na Burundi. Viongozi wa vuguvugu hilo walimshutumu Laurent Désiré Kabila, miongoni mwa mambo mengine kutoheshimu mpango wa kisiasa unaozingatia mabadiliko ya utawala mjini Kinshasa.

Akikabiliwa na nguvu hii ya moto, Kabila alitafuta washirika wapya- Angola, Namibia, Chad na Zimbabwe, nchi ambazo zilitoa msaada kwa wapiganaji wa ardhini.

Waasi hao walifanikiwa kwa haraka kuiteka miji mikubwa zaidi ya mashariki mwa DRC.

Mgogoro huo ulikuwa wa ghasia sana kiasi kwamba ulisababisha vifo vya "zaidi ya Wacongo milioni moja, wakimbizi wa ndani milioni 1.6 na kuwalazimisha karibu watu nusu milioni kutafuta hifadhi katika nchi jirani," kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Migogoro.

Mgogoro huo ulichanganya maslahi ya kikabila, kiuchumi na hata kimkakati. Uganda, Rwanda na Burundi, ambazo zinatajwa kuwa ni wafuasi wakuu wa waasi wa RCD, zilisema kuwa wanajeshi wao wako DRC kulinda usalama wao wa taifa, hasa kudhibiti na kuondoa makundi ya waasi yanayotumia mashariki mwa Congo kama msingi wa kuanzisha mashambulizi dhidi ya serikali zao.

Rais Kabila aliwataka wanajeshi wote wa kigeni kufunga virago na kuondoka mashariki mwa eneo lake, lakini hakuna kilichofanyika. Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ilianzisha mpango ambao ulisababisha makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyojulikana kama makubaliano ya Lusaka.

Hatua za SADC (tangu mwaka 1998)

Katika historia ya kijeshi ya DRC, vipindi vinaonekana kujirudia. Hii ndiyo ndio hali uingiliaji kati wa wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC.

Kipindi cha mwisho kilikuwa chini ya miezi mitatu iliyopita. Februari 2, helikopta ya Oryx kutoka jeshi la Afrika Kusini ilipaa katika mazingira ya Goma, ambapo M23 imekuwa ikifufua mapigano kwa miezi kadhaa.

Ndege hiyo ililengwa na shambulio la ardhini na kuharibiwa, na kuwajeruhi baadhi ya wafanyakazi. Helikopta hiyo ilikuwa ikishiriki katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa.

Tukio hilo linaambatana na kutumwa hivi karibuni kwa ujumbe wa SADC katika kanda hiyo, hasa karibu na mji wa Sake, ambao hivi karibuni uliangukia mikononi mwa waasi.

Kwa kikosi hiki kinachoundwa na wanajeshi wa Afrika Kusini, Tanzania na Malawi, hii ni mara ya tatu kwa SADC kurudi DRC katika kipindi kisichozidi miongo mitatu.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998, kundi la Kusini mwa Afrika liliomba ulinzi wa pamoja ili kuidhinisha kuingilia kati kwa Angola, Namibia na Zimbabwe kupambana na uvamizi wa Rwanda na Uganda ambao ulikuwa umefika hadi Kinshasa.

Ilipoondoka mwaka 2003, SADC iliacha kikosi cha mabaki ili kusaidia ulinzi wa nchi na kuunda sekta ya usalama ya DRC baada ya vita.

Kisha mwaka 2013 SADC ilipeleka kikosi cha uingiliaji kati, kilichoundwa na wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania, kusaidia kukabiliana na uvamizi wa kwanza kabisa wa waasi wa M23 mashariki mwa DRC.

Kutoka Monuc hadi Monusco (kuanzia mwaka 1999)

Utawala wa Laurent Désiré Kabila (Mei 1997-Januari 2001) haukuwa wa amani kwani makubaliano ya Lusaka hayakumaliza uhasama uliokuwa ukiendelea mashinani.

Kwa ombi lake, Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio mnamo Novemba 30, 1999, ambalo liliunda Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUC), na kuukabidhi jukumu la kuandaa mipango ya kusimamia usitishaji vita wa Lusaka uliotiwa saini mwaka huo.

Julai 1999 kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na mataifa matano ya kikanda (Angola, Namibia, Uganda, Rwanda na Zimbabwe), yalipewa jukumu la kufanya kazi ya kuondoa majeshi, na kudumisha mawasiliano na pande zote kwenye makubaliano.

Mamlaka ya MONUC yalibadilika , kulingana na maazimio ya Baraza la Usalama, na kuanzisha majukumu mengine kwa ujumbe huu wa Umoja wa Mataifa.

Tunazungumzia hasa kuhusu kuhakikisha usalama na uhuru wa kutembea kwa watu wake, shirika lazima pia llilihusishwa katika kuwapokonya silaha, kuwaondoa, kuwarejesha makwao na kuwajumuisha tena wajumbe wa vikundi vyenye silaha na kufuatilia mchakato wa amani.

Pia MONUC ilipewa jukumu la kukagua shehena ya ndege na chombo chochote cha usafiri kwa kutumia bandari, viwanja vya ndege, vituo vya kijeshi na vituo vya mpakani katika jimbo la Kivu Kaskazini na Kusini na Ituri, bila taarifa, inapoona ni muhimu kufanya hivyo.

Jukumu hili la ziada ililokabidhiwa mwaka 2004 unaambatana na lingine ambalo lilijumuisha kukamata au kukusanya silaha na nyenzo zozote zinazohusiana ambazo uwepo wake katika eneo la DRCutaonekana kukiuka kanuni.

MONUC ilipobadilisha jina lake na kuwa Monusco mwaka wa 2010, baraza la usalama liliidhinisha kuundwa kikosi kwa kikosi cha kuingilia kati. Kikosi hiki kiliundwa mnamo 2013, mwaka mmoja baada ya kuibuka kwa vuguvugu la M23, ambalo lilikuwa na upinzani mkali kwa Wanajeshi wa Congo.

Kikiwa na jumla ya wanajeshi 1,981 (idadi hiyo ilitofautiana kulingana na maazimio), MONUSCO inaundwa na vitengo 6, vikiwemo vikosi vitatu vya askari wa miguu, kikosi cha mizinga, kikosi maalum na kikosi cha upelelezi.

Madhumuni ya kikosi hiki ni kupunguza makundi yenye silaha nakililenga kuchangia kupunguza tishio la makundi yenye silaha kwa mamlaka ya serikali na usalama wa raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuandaa mazingira ya utulivu, kulingana na azimio 2098 ambalo liliiunda kikosi hicho.

"Ingawa kikosi cha kuingilia kati kina ujumbe wa kukera, ukweli kwamba Umoja wa Mataifa hauna jeshi lake wenyewe inaweza kuelezea ukosefu huu wa matokeo chanya kutoka kwa misheni yake nchini DRC," anasema Omar Kavota, mwanaharakati wa asasi ya kiraia ya Congo, ambayo inasimamia shughuli ya upokonyaji Silaha wa makundi ya waasi.

Ukosefu wa matokeo na kuanza kwa maandamano ya idadi ya watu dhidi ya MONUSCO hatimaye uliilazimisha mamlaka kuomba kuondoka kwa MONUSCO, angalau sehemu yake yenye silaha.

Ufaransa na Operesheni ya Artemis (Mei-Juni 2003)

Katikati ya Mei mwaka 2003, wakati DRC ilikuwa bado inakabiliwa na wakati mgumu wa kile kilichoelezewa kama "vita vya kwanza vya dunia vya Congo", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Attah Annan alizindua wito wa "kukomesha ukatili huo dhidi ya raia katika jimbo la Ituri”.

Ufaransa iliongoza operesheni hii ambayo ina jina la msimbo "Mamba", ambalo lilipendekezwa kwa washirika wake wa Ulaya, kabla ya kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Dhamira yake ni "kuchangia katika kurejesha hali ya usalama na uboreshaji wa hali ya kibinadamu katika mji wa Bunia, mji mkuu wa Ituri".

Operesheni hiyo iliyokusanya wanajeshi 1,500 ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha udhibiti wa hali hiyo huku kukisubiriwa juhudi za kuimarishwa kwa mamlaka na nguvu za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MONUC).

Kwa hivyo operesheni hiyo ilitarajiwa kuwa fupi na hudumu miezi miwili na nusu tu, kati ya Juni 16 na Septemba 1, 2003.

Kulingana na wataalamu, matokeo ya operesheni hii yanaonekana. Wanakubali kwamba ilikuwa fursa kwa Ufaransa kujiweka upya katika Afrika ya Kati na Ukanda wa Maziwa Makuu, "katika hali ambayo ilikuwa imejiondoa hatua kwa hatua tangu kumalizika kwa Operesheni ya Turquoise nchini Rwanda, kuondolewa kwa kikosi cha Ufaransa kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), baada uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo karibu kutoweka", anachambua Nyagalé Bagayoko, Mtaalamu wa mageuzi ya mifumo ya usalama (RSS) katika mataifa ya Afrika yanayozungumza lugha ya Kifaransa.

Mamluki wapya nchini DRC?

Imekuwa ni ripoti ambayo ilikaribia kunyamazishwa Ni ripoti ambayo karibu, lakini ambayo inautia wasiwasi Umoja wa Mataifa. Iliandikwa na kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa na kuwekwa wazi mwezi Disemba mwaka jana, na inaripoti mazungumzo kati ya mamlaka ya Congo na mamluki kwa ajili ya kuanzishwa kwa harakati zao mashariki mwa nchi.

Ni mamlaka hizi, kulingana na ripoti, ambazo zilianzisha mazungumzo, kuhusu makubaliano na Erik Prince, mwanzilishi wa kampuni ya mamluki ya Blackwater, yaliyofanyika kati ya mwisho wa mwezi Juni na katikati mwezi wa Julai 2023,

Mtu huyo tayari anatajwa kutoa msaada wake kwa watu na silaha kwa Marshal Khalifa Haftar, mtu mwenye nguvu wa mashariki mwa Libya, ambaye ni mpinzani wa serikali kuu.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, makubaliano hayo yanaruhusu kutumwa katika Kivu Kaskazini wanpiganaji 2,500, walioajiriwa nchini Colombia, Mexico na Argentina, wakiwa na majukumu mawili : kusimamisha kusonga mbele kwa M23 na kulinda maeneo ya uchimbaji madini.

Kwa sasa, ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema mpango huo umesitishwa, lakini wanafahamu kuwa majengo yalikuwa yakijengwa karibu na Sake, ili kuchukua wakandarasi 250 wa kwanza ambao walitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwei Julai mwaka 2023. Kontena zenye vifaa tayari zilikuwa zimefika kwenye eneo mnamo Julai 2023, tena kulingana na UN.

Wataalamu wana wasiwasi kwamba kuondoka kwa MONUSCO, ambayo inazidi kuwa wazi, na kupunguza vikwazo vya silaha nchini DRC, kutahimiza kuenea kwa vurugu katika eneo hilo.

Jaribio lisilokamilika la EAC (2022-2023

Tarehe 20 Juni, 2022, mkutano wa kilele wa viongozi 7 wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki ulifanyika mjini Nairobi, Kenya.

Katika ajenda ya majadiliano, ilikuwa ni pamoja na hali nchini DRC, na kuzuka upya kwa mashambulizi ya kundi la waasi la M23.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ilityaka kukomesha ukatili huo, na iliamua kutumwa kwa askari kutoka nchi hizi, isipokuwa Rwanda iliyo katika mgogoro na DRC na Tanzania, ambayo haikutaka kuongeza wanajeshi kwenye ardhi.

Maeneo yalitengwa kwa kila kikosi, ambacho kilianza kutua kwenye eneo hilo mnamo Novemba mwaka 2022.

Waganda walichukua udhibiti katika mji wa Kiwanja, katika kijiji cha Mabenga, na kituo cha mpaka cha Bunagana.

Warundi wwakachukua eneo la nyanda za juu za Kivu Kusini, mji wa Kitshanga, kijiji cha Kilolirwe na eneo la Sake.

Wakenya hao walikuwa katika vijiji vya Bwiza, Tongo na Kishishe. Na kikosi cha Sudan Kusini kilikalia kambi ya kijeshi ya Rumangabo.

Lakini, ujumbe wa Afrika Mashariki haukudumu muda mrefu katika eneo hilo kama ilivyotarajiwa. Mwaka mmoja tu, baada ya kuhudumu Kinshasa utawala wa Kinshasa uliomba kuondoka kwa ujumbe huo.

"Kikosi hiki kimeshindwa kusuluhisha tatizo ambalo kilitumwa kulitatua, hasa kutokana na kuendelea kwa shughuli za M23, ambayo haiheshimu mchakato wa kurudisha nyuma wapiganaji wake," alisema msemaji wa serikali Patrick Muyaya.

Kwa Onesphore Sematumba, mtafiti wa Kikundi cha Kimataifa cha Migogoro cha eneo la Maziwa Makuu, sababu ya kutofaulu ni rahisi, "jeshi la kikanda liligeuka kuwa nguvu ya kuingilia kati kwa kuanzisha aina za maeneo ya yasio ya mapigano ambayo hakuna mtu alieyetaka ".

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi