Je, Félix Tshisekedi ataleta vita au amani kwa DR Congo na Rwanda?

Félix Tshisekedi anaapishwa kwa muhula wa pili kama rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia uchaguzi uliokumbwa na machafuko na wenye utata.

Ana miaka mingine mitano ya kuboresha hali ya taifa ambapo zaidi ya asilimia 70 ya watu wanaishi katika umaskini uliokithiri na miongo kadhaa ya migogoro imekumba maisha ya mamilioni ya watu.

Je, Bw Tshisekedi anaweza kuleta amani iliyotamaniwa kwa muda mrefu nchini DR Congo? Au je, vurugu zilizokithiri na ahadi ya rais ya kuingia vitani na nchi jirani ya Rwanda imeharibu uwezekano wowote wa hilo?

Wakati wa kampeni zake zote mbili za urais, Bw Tshisekedi ameapa kukabiliana na machafuko mashariki mwa DR Congo.

Makumi ya makundi yenye silaha - ikiwa ni pamoja na kundi maarufu la M23 - vita vya kudhibiti ardhi, na madini tele katika eneo hilo, ambayo ni pamoja na dhahabu, almasi na kobalti, ambayo ni muhimu kwa betri za simu za rununu na magari ya umeme.

Mwaka jana, mzozo kati ya vikundi hivyo ulipamba moto baada ya utulivu wa miezi kadhaa na idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao ilifikia rekodi milioni 6.9, kulingana na UN.

Ili kumaliza haya yote, Bw Tshisekedi anahitaji kubadili mwelekeo wake kutoka kwa mipango ya kijeshi ya "muda mfupi" hadi suluhisho la kudumu, Richard Moncrieff, mkurugenzi wa Mradi wa Maziwa Makuu katika Kundi la Kimataifa la Migogoro (ICG), anaiambia BBC.

Rais Tshisekedi na viongozi wengine wa Afrika walikuwa wameanza mazungumzo - yanayojulikana kama mchakato wa Nairobi na Luanda - katika jaribio la kupunguza ukosefu wa usalama wa DR Congo kupitia mikakati ya kijeshi na kisiasa. Hata hivyo, mazungumzo haya yanaonekana kukwama.

Rais wa Congo hajatilia maanani sana mchakato wowote wa amani, Bw Moncrieff anasemai, akiongeza: "Anahitaji kujijenga kwa muda mrefu katika kuleta mageuzi katika sekta yake ya usalama ... na sio kuweka imani kubwa kwa suluhu za muda mfupi."

Juhudi za kijeshi zilizochukuliwa na rais katika muhula wake wa kwanza ni pamoja na kutangaza hali ya kuzingirwa katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini, mwaka wa 2021.

Alijaribu kurejesha utulivu kwa kuwateua viongozi wa kijeshi kuchukua nafasi ya utawala wa kiraia katika maeneo hayo.

Zaidi ya hayo, rais alisukuma harakati ya kuajiri ambayo ilisababisha maelfu ya vijana kujiunga na jeshi, wakati akianzisha operesheni ya kupokonya silaha iliyolenga kuwajumuisha tena wanachama wa vikundi vilivyojihami katika maisha ya kiraia.

Wakosoaji wanaeleza kuwa mipango hii imeshindwa kupunguza mapigano mashariki, ingawa Bw Tshisekedi anasisitiza kuwa imezaa matunda.

Aliwaambia wabunge mnamo Novemba kumekuwa na "kupunguzwa kwa uchimbaji madini na ulaghai wa forodha unaochochea migogoro", pamoja na kuboreshwa kwa mivutano kati ya jamii na "kuanzishwa upya kwa mamlaka ya serikali".

Rais pia amesema kuondoa kikosi cha Afrika Mashariki kilichoundwa ili kukabiliana na mzozo wa DR Congo, na badala yake kuweka cha kusini mwa Afrika, kutasaidia kupunguza ukosefu wa usalama.

Mnamo Oktoba 2023, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisema haitaongeza muda wa Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya miezi kadhaa ya Kinshasa kulalamikia kutofanya kazi kwa wanajeshi hao.

Mwezi uliopita, waziri wa mambo ya nje wa Congo alisema wanajeshi kutoka jumuiya ya kusini mwa Afrika SADC wamepewa mamlaka "ya kuunga mkono jeshi la Congo katika kupigana na kuangamiza kundi la M23 na makundi mengine yenye silaha ambayo yanaendelea kuvuruga amani na usalama".

Inabakia kuonekana kama SADC inaweza kudhibiti wingi wa wanamgambo wa DR Congo, ambayo majeshi yaliyoko mbele yao, wakiwemo walinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao wamekuwa nchini humo tangu 1999, wameshindwa kufanya hivyo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama Monusco, unatazamiwa kukamilisha kujiondoa kutoka DR Congo mwishoni mwa mwaka huu - baada ya serikali ya Rais Tshisekedi kuona kuwa haufanyi kazi.

Sambamba na kukata uhusiano na vikosi vya Umoja wa Mataifa na EAC, Rais Tshisekedi ametishia kuingia vitani na Rwanda.

"Ikiwa utanichagua tena na Rwanda itaendelea... nitaomba bunge na Congress kuidhinisha kutangazwa kwa vita. Tutaandamana kuelekea Kigali," alisema mwezi Desemba, katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni.

Anaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23. Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilitoa angalizo sawa katika ripoti ya 2023, huku Marekani ikiunga mkono matokeo yake.

Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo na kumshutumu jirani yake kwa kuwaunga mkono waasi wa Kihutu wanaofanya mashambulizi nchini Rwanda.

Rais Tshisekedi ametishia kuishambulia Rwanda mara kadhaa kabla, lakini bado hajafanya hivyo. Wengi wanaamini kwamba ahadi hizi zilikuwa ni jitihada tu za kutafuta kura kwa watu wenye misimamo mikali.

Kufuatia ahadi ya hivi majuzi zaidi ya Bw Tshisekedi, Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema yeyote anayetaka kuangamizwa kwa nchi yake "atashuhudia yake ikiangamia".

Maneno ya Bw Kagame yanaashiria Rwanda itajibu kwa nguvu "mashambulio yoyote ya Kigali" na Rais Tshisekedi hangeshindwa tu kuleta amani DR Congo, lakini angezua ghasia zaidi katika nchi yake.

Na jeshi la Rwanda ni miongoni mwa jeshi linaloheshimika zaidi barani Afrika, huku la DR Congo likijulikana kwa ufisadi na utovu wa nidhamu.

Lakini baada ya kutoa tishio hilo, Bw Tshisekedi "atapata ugumu wa kurejea nyuma kutoka kwa maneno machafu aliyotumia katika kampeni za uchaguzi," Bw Moncrieff alisema.

Nchini DR Congo, amani haimaanishi tu kushindwa kwa M23 na makundi mengine yenye silaha. Wananchi wa Congo pia watarajie rais wao kuwezesha mazungumzo ambayo yatashughulikia mizozo kati ya makabila mengi ya taifa hilo, ambayo viongozi wa zamani hawakuyashughulikia kwa mafanikio.

Ni lazima pia ashughulikie mzozo wa kisiasa unaosababishwa na chaguzi zilizozozaniwa.

Kabla kuapishwa kwakwe, viongozi watatu wa upinzani na wagombea urais ambao walishindwa na Bw Tshisekedi waliitisha maandamano wakati wa hafla hiyo.