Uhusiano kati ya vyakula vilivyosindikwa na kifo cha mapema

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Angela Henshall
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kula kiasi kikubwa cha keki, biskuti, milo iliyo tayari au vyakula kama hivyo kunaweza kuongeza hatari yako ya kifo cha mapema, kulingana na mapitio ya utafiti katika nchi nane.
Data kuhusu vyakula vilivyosindikwa zaidi (UPF) kutoka Colombia, Chile, Mexico, Brazil, Australia, Canada, Uingereza na Marekani ilichambuliwa na timu ya Dk Eduardo Nilson katika Wakfu wa Oswaldo Cruz nchini Brazil (FIOCRUZ).
Utafiti huo uliochapishwa siku ya Jumatatu katika Jarida la Marekani la Preventive Medicine linajumuisha wito kwa serikali kutoa mapendekezo ya lishe yenye lengo la kupunguza matumizi ya UPF.
Nusu ya watu wazima nchini Brazil wana uzito uliopitiliza na mmoja kati ya wanne ana unene uliokithiri kulingana na data ya 2022 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO). FIOCRUZ imekuwa ikiongoza kazi ya wizara ya afya ya nchi hiyo katika kukabiliana na mzozo wa kiafya unaokua.
Utafiti huo uligundua vifo vya mapema vinavyotokana na UPF vilivyoanzia 4% ya vifo vya mapema katika nchi zinazotumia kwa kiwango cha chini, kama vile Colombia, hadi 14% ya vifo vya mapema nchini Uingereza na Marekani, kulingana na modeli zao za hesabu.
Walihesabu hii kulingana na UPF inayounda 53% ya ulaji wa nishati kwa watu wazima nchini Uingereza ya pili ikiifuata Marekani.
Watafiti walisema kuwa mnamo 2018-19, vifo vya mapema 17,781 nchini Uingereza vilihusishwa na UPF.
"Takwimu zinaongezeka. Sidhani kama ongezeko la hatari ya vifo vinavyohusiana na UPF ni jambo la kushangaza kwangu," anasema Dk Megan Rossi, mtafiti mwenza katika idara ya sayansi ya lishe katika Chuo Kikuu cha King's London.
"Tumejua kwa muda mrefu sana kwamba baadhi ya vyakula, ambavyo vina phytochemicals na nyuzinyuzi hulinda seli zetu kutokana na oxidation na kuwashwa. Vyakula hivyo ni muhimu na kinga ya juu dhidi ya magonjwa, na tunajua ikiwa tutakata, tunapoteza ulinzi huo," aliiambia BBC.
Anaelezea athari mbaya ni mbili: ikiwa unakula vyakula vya kusindika, basi hupati vyakula hivyo vyote vya antioxidant kama vile matunda na mboga. Na pili, kwa vile UPF vyakula hivi vimeundwa kufyonzwa haraka na kwa urahisi na miili yetu anasema usindikaji umezifanya kuwa za kupendeza sana, hazikushibi kwa muda mrefu, maana yake unakula zaidi na zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ingawa wanasayansi wanakubali ushahidi unaongezeka kwamba UPF ni mbaya kwa afya yako, changamoto ni kuwa na uhakika wa 100%.
Tafiti nyingi zimegundua muundo kati ya UPF na afya mbaya, lakini haziwezi kuthibitisha kuwa moja husababisha nyingine, kwani hakuna ushahidi wa uhakika bado.
Ni kweli hata hivyo kwamba watafiti wamepata uwiano thabiti kati ya UPF na hali nyingi za afya.
Utafiti wa karibu watu milioni 10 wanaokula UPF uliochapishwa mwaka jana katika Jarida la Matibabu la Uingereza uligundua kuwa walikuwa na hatari kubwa ya kifo kutokana na magonjwa ya moyo na mishipa, unene uliokithiri, kisukari cha aina ya 2, wasiwasi na unyogovu.
Hatahivyo, hata kwa utafiti huu, ni ngumu kubaini ikiwa ni usindikaji wa chakula uliosababisha magonjwa, au ukweli kwamba wengi wao wana mafuta mengi, sukari na chumvi. Hizi ni sababu zinazojulikana za kuongezeka kwa uzito na baadhi ya saratani.
Hatahivyo, wanasayansi kadhaa wa lishe huashiria mapungufu na utafiti ulioongozwa na Dk Nilson.
Stephen Burgess, mwanatakwimu katika Kitengo cha Takwimu za Biolojia cha MRC katika Chuo Kikuu cha Cambridge, alisema utafiti huo ulikuwa wa uchunguzi na hauwezi kuthibitisha sababu.
"Aina hii ya utafiti haiwezi kuthibitisha kuwa ulaji wa vyakula vilivyosindikwa zaidi ni hatari, lakini unatoa ushahidi unaohusisha matumizi na matokeo duni ya kiafya," alisema.
"Inawezekana kwamba sababu halisi ya hatari sio vyakula vilivyochakatwa zaidi, lakini sababu ya hatari inayohusiana nayo kama vile utimamu wa mwili.''
Unajuaje ikiwa unakula zaidi chakula kilichosindikwa?
Uzalishaji wa chakula umebadilika sana katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
UPF hufafanuliwa na michakato mingapi ya kiviwanda ambayo vyakula vimepitia na idadi ya viambato, mara nyingi visivyoweza kutamkwa, kwenye vifungashio vyake.
Vingi vina mafuta mengi, sukari au chumvi; wengi ungeita chakula cha haraka.
Aina ya chini kabisa katika orodha hiyo ni vyakula kama vile matunda na mboga mboga, ambavyo havijachakatwa kabisa, ilhali vyakula vilivyochakatwa vimebadilishwa ili kuvifanya vidumu kwa muda mrefu au kuwa na ladha nzuri zaidi, kwa ujumla kwa kutumia chumvi, mafuta, sukari au uchachushaji.
Mifano ya UPF ni pamoja na aiskrimu, nyama iliyochakatwa, krisps, mkate uliozalishwa kwa wingi, baadhi ya nafaka za kifungua kinywa, biskuti na vinywaji viyenye gesi.
Tunakula sana bidhaa hizi kwa sababu nyingi zina mapishi yaliyoundwa ili kuwa na ladha nyingi, ni nafuu, yanafaa na yanatangazwa sana, hasa kwa watoto.
Moja ya sababu za hii ni kwamba watu waliokula vyakula vilivyosindikwa zaidi pia walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na tabia nyingine zisizofaa, kama vile kuvuta sigara na kufanya mazoezi kidogo, Dkt.Rossi alidokeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ishara za hatari ni;
- Viungo ambavyo huwezi kutamka.
- Zaidi ya viambato vitano vilivyoorodheshwa kwenye pakiti.
- Chochote ambacho bibi yako hangetambua kama chakula.
Viambata fulani vinaweza kuashiria chakula au kinywaji kimechakatwa zaidi:
- Viboreshaji kama vile wanga uliorekebishwa (xanthan gum, guar gum)
- vimiminarishaji (kama vile lecithin ya soya na carrageenan)
- Mbadala wa sukari (kama aspartame na stevia) rangi za chakula za sanisi ambazo hazitoki kwenye mimea
- Ladha bandia na viambato vingine ambavyo hutavipata kwenye kabati za jikoni nyumbani au hata kwenye maduka makubwa.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












