Je, vyakula vilivyosindikwa zaidi vinaweza kuwa na madhara kwa mwanadamu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka 20 iliyopita, hakuna mtu aliyekuwa amesikia neno vyakula vilivyosindikwa zaidi yaani ultra-processed foods - UPF - lakini karibu nusu ya vitu tunavyokula sasa vinatengenezwa hivyo.
Kutoka mkate wa kahawia uliosindikwa hadi milo iliyo tayari kwenye migahawa na aiskrimu, ni kundi la vyakula vilivyotengenezwa kwa viwango tofauti - lakini mara nyingi – ni vile vinavyosindikwa viwandani.
Viungo vinavyotumika ni kama vile vihifadhi ili chakula kiweze kuishi kwa muda mrefu bila kuharibika, vitamu bandia yaani mbali na sukari na ambavyo kwa kiasi kikubwa sio rahisi vipatikane kwa mapishi ya nyumbani.
"Vyakula vilivyosindikwa zaidi ni miongoni mwa vyakula vinavyoweza kutengeneza faida kubwa zaidi kwa kampuni," anasema Prof Marion Nestle, mtaalam wa siasa za chakula na profesa wa lishe katika Chuo Kikuu cha New York.
Kadiri utumiaji wetu wa vyakula vilivyosindikwa zaidi unavyoongezeka - Uingereza ni moja ya yenye watumiaji wengi barani Ulaya - vivyo hivyo kwa viwango vya ugonjwa wa sukari na saratani.
Baadhi ya wasomi wanafikiri kuwa uhusiano huu sio wa kubahatisha.
Prof Tim Spector, ni profesa wa magonjwa katika Chuo cha King's College London, ambaye anasomea mienendo ya magonjwa.
Aliiambia BBC Panorama: "Katika muongo uliopita, ushahidi umekuwa ukiongezeka polepole kwamba chakula kilichosindikwa ni hatari kwetu kwa njia ambazo hatukufikiria.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Tunazungumza juu ya aina nyingi za saratani, magonjwa ya moyo, kiharusi na shida ya akili."
Vyakula ambavyo vimeshatayarishwa tayari hasa katika mchakato wa usindikaji, vina kemikali ambazo wadhibiti wa Uingereza wanasema ni salama, lakini Panorama inachunguza ushahidi unaojitokeza wa kisayansi wa uhusiano kati ya baadhi ya kemikali hizi na magonjwa ya saratani, kisukari na viharusi.
Mnamo Januari, moja ya tafiti za kina zaidi juu ya chakula kilichosindikwa zaidi - uliofanywa na Shule ya Afya ya Umma ya Chuo cha Imperial - ilichapishwa katika jarida la matibabu la Lancet.
Utafiti huo wa watu wazima 200,000 wa Uingereza uligundua kuwa matumizi ya juu ya vyakula vilivyosindikwa zaidi vinaweza kuhusishwa na hatari kubwa ya kupata saratani kwa ujumla, na haswa saratani ya kifuko cha uzazi na ubongo.
Na, kufikia mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) sasa linatahadharisha dhidi ya utumizi wa muda mrefu wa vitamu bandia - likitaja hatari zinazowezekana za kiafya.
Inafuata tafiti nyingi zinazohusisha ongezeko la matumizi ya UPF na hatari kubwa ya kupata magonjwa hatari.
Lakini kuthibitisha kwamba viambato mahususi husababisha madhara kwa binadamu inaweza kuwa changamoto - kuna anuwai ya mambo mengine katika mitindo yetu ya maisha ambayo yanaweza kusababisha magonjwa haya.
Kwa mfano: ukosefu wa mazoezi, kuvuta sigara au vyakula vya sukari kupita kiasi.
Vyakula vya kawaida vilivyosindikwa kupita kiasi:
- Mkate uliotengenezwa na nafaka zenye sukari nyingi au kitamu mfano wake ni asali kwa ajili ya kiamsha kinywa
- Supu za papo hapo, zilizopakiwa tayari na milo yakutengenezwa kwa wimbi mikro yaani microwave
- Maziwa ya mtindi yenye ladha ya matunda
- Nyama iliyotengenezwa upya - kama soseji
- Aiskrimu , kaukau na biskuti
- Vinywaji visivyolewesha na vileo - kama vile mvinyo
Uchunguzi wa kwanza kuhusu vifo na utumiaji wa vyakula vilivyochakatwa sana ulianza nchini Ufaransa katika Chuo Kikuu cha Sorbonne Paris Nord, kama sehemu ya utafiti unaoendelea kuhusu tabia ya kula ya watu 174,000.
"Tuna rekodi za chakula za saa 24 ambapo hutuambia vyakula vyote, vinywaji na kadhalika, wanachokula," anaeleza Dk Mathilde Touvier ambaye anaongoza utafiti huo. Utafiti unaoendelea tayari umechapisha matokeo yanayoonyesha UPF inaweza kuongeza saratani.
Kiungo Emulsifier kinachoonekana kama miujiza viwandani
Hivi majuzi zaidi, wamekuwa wakichunguza athari ya kiungo kimoja maalum - emulsifier – kiungo kinachotumika kuleta utulivu wa vyakula vilivyosindikwa – mfano wake ni kama gundi ili kushikilia kila kitu pamoja.
Kiungo hicho ni muhimu sana kwa sekta ya chakula - huboresha mwonekano na muundo wa chakula, na kusaidia kuongeza muda zaidi wa chakula kuendelea kuwa sawa kwa matumizi ya binadamu. Ikimaanisha kwamba iwapo kitakosekana basi chakula hicho kitaharibika ndani ya muda mfupi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiambato hiki kiko kila mahali, katika mayonnaise, chokoleti, siagi ya karanga, bidhaa za nyama. Ikiwa unakula hivi, kuna uwezekano wa kuwa unatumia kiungo emulsifier kama sehemu ya mlo wako.
BBC Panorama ilipewa ufikiaji wa kipekee wa matokeo ya mapema ya Dk Touvier.
Bado hayajapitiwa na wasomi wengine - hatua muhimu ya uthibitishaji kwa tafiti za kisayansi - lakini alisema bado zinasababisha maswali mengi zaidi ya majibu.
"Tuliona uhusiano mkubwa kati ya ulaji wa emulsifier na kuongezeka kwa hatari ya saratani kwa jumla - na saratani ya matiti haswa - lakini pia na magonjwa ya moyo na mishipa," anasema.
Hii ina maana kwamba mtindo umezingatiwa kati ya ulaji wa chakula kilichosindikwa zaidi na hatari ya magonjwa, lakini utafiti zaidi unahitajika.
Licha ya kuongezeka kwa ushahidi, Shirika la Viwango vya Chakula wa Uingereza (FSA) - ambao unadhibiti tasnia ya chakula nchini Uingereza, Wales na Ireland ya Kaskazini - bado haijatoa kanuni yoyote inayozuia kiungo cha emulsifier.

Panorama ilipouliza FSA kuhusu ongezeko la ushahidi kwamba viambato vya kufanya chakula kuwa salama kwa matumizi ya binadamu kwa muda mrefu zaidi vinaweza kusababisha madhara, ilisema: "Hatujawasilishwa na ushahidi wowote - na mpango huu au vinginevyo - wa kiungo maalum ambacho inaaminika kuwa hatari kwa afya.
"Lakini FSA ilisema inapanga kufanya mashauriano na umma.
Je! mashirika ya chakula yanaweza kuchukua jukumu la kuangalia tena namna ya udhibiti wa viambato vinavyoweza kuwa hatari?
Timu ya BBC Panorama ilitumia miezi minane iliyopita kuchunguza.
"Kampuni za vyakula si mashirika ya afya ya umma... kazi yao ni kuuza bidhaa," mtaalamu wa siasa za chakula Prof Nestle aliambia BBC.
Alisema tasnia ya chakula imekuwa ikijulikana kufadhili utafiti, wataalam na kupuuza tafiti zilizopo ili kuzuia udhibiti.
Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Maisha (ILSI) ni shirika linalopokea ufadhili kutoka kwa baadhi ya makampuni makubwa zaidi ya chakula duniani.
Inasema dhamira yake ni "kutoa sayansi ambayo inaboresha afya ya binadamu" - lakini hapo awali ilichapisha tafiti zinazodhoofisha udhibiti na mwongozo wa umma juu ya lishe bora.
Mnamo 2012, Shirika la Usalama wa Chakula wa Ulaya ulikuwa na wasiwasi sana juu ya migongano ya kimaslahi inayoweza kutokea, ilisisitiza mtu yeyote anayehusishwa na ILSI aidha alilazimika kujiuzulu kutoka kwa taasisi hiyo au kuacha kuwa mshirika.
Aspartame, kiungo kitamu kuliko sukari
Aspartame ni kiungo kitamu sana zaidi ya sukari kinachotumika kama utamu bandia, haswa katika bidhaa zenye kalori ya chini.
Moja ya viambata vyenye utata katika UPF ni kiungo aspartame tamu.
Tamu mara mia mbili kuliko sukari, imetangazwa kuwa mbadala mzuri wa kalori ya chini - kubadilisha vinywaji vyenye sukari visivyofaa, aiskrimu na kuwa bidhaa zinazouzwa kama vyenye "afya".
Kumekuwa na maswali kuhusu madhara yake katika miongo miwili iliyopita.
Halafu, mwezi uliopita, Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema, ingawa ushahidi hauko thabiti, ilikuwa na wasiwasi kwamba matumizi ya muda mrefu ya kiungo hiki kitamu sana kama aspartame inaweza kuongeza hatari ya "aina ya 2 ya kisukari, magonjwa ya moyo, na vifo".















