Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, ni nchi gani zinashikilia vitu vya kale vya nchi nyingine?
Nchi za Ulaya zilipojenga himaya zao za kikoloni kote ulimwenguni, zilipata vitu vingi vya thamani ambavyo sasa vinaonyeshwa kwenye makumbusho ya nchi hizo.
Hivi karibuni, baadhi ya vitu vya kale vimerejeshwa kwa wamiliki wake wa zamani, ikiwa ni pamoja na sanamu za shaba za Benin na mzinga wa Lewke. Vitu vingine, ni vazi la kichwani la mfalme wa Azteki, Moctezuma II.
Lakini si kila makumbusho iko tayari kurudisha vitu hivyo; serikali ya Uingereza imechukua hatua ya kuziweka sanamu za Kigiriki za Elgin katika milki ya Makumbusho ya Uingereza huko London.
Sanamu za Elgin ni nini?
Ni sanamu za kale zilizojengwa kwa mawe huko Ugiriki, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Kuna zaidi ya sanamu 30 za aina hiyo zimewekwa katika Jumba la Makumbusho la Uingereza.
Zilichukuliwa katika hekalu la Parthenon, Athene, Ugiriki. Ni hekalu lililojengwa na Wagiriki wa kale katika karne ya tano.
Na sanamu nyingine zilichukuliwa katika Hazina ya mfalme Atreus wa Mycenae - sanamu hizo zina zaidi ya miaka 3,000.
Zilizochukuliwa mwanzoni mwa karne ya 19 na Thomas Bruce (Earl of Elgin), mwanasiasa, mwanadiplomasia na mwanajeshi wa Uingereza, kwa idhini ya Mfalme wa Ottoman aliyetawala Athene wakati huo.
Mwaka 1816, Bunge la Uingereza liliamua kuwa limezipata sanamu hizo kihalali, na kupitisha sheria inayofanya Jumba la Makumbusho la Uingereza kuwa mmiliki wake.
Kwa nini Uingereza hairudishi sanamu za Ugiriki?
1983 Ugiriki iliomba rasmi kurejeshewa sanamu za Elgin, lakini Uingereza ilikataa. 2009 jumba la makumbusho lilijengwa karibu na kanisa la kale la Acropolis ili kuhifadhi mabaki yaliyopotea.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak alikataa kukutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis. Ni kufuatia tangazo la Mitsotakis kwamba sanamu za Elgin ziliibiwa na kutaka zirudushwe.
Uingereza inasema haina mpango wa kurejesha sanamu za Ugiriki. Watu milioni nne kote ulimwenguni hutembelea sanamu hizi kila mwkaa katika Jumba la Makumbusho la Uingereza.
Hata hivyo, wasimamizi wa jumba hilo la makumbusho wanajadiliana ili kurudisha kwa muda baadhi ya sanamu huko Athene ili kubadilishana na mabaki mengine ya kale kutoka makumbusho ya Ugiriki.
Vinyago vya Benin
Vinyago vya Benin ni maelfu ya sanamu za chuma na mapambo mengine, yaliyoundwa kati ya karne ya 15 na 19. Mwaka 1897 majeshi ya Uingereza yalipora vinyago hivyo walipovamia na kuiharibu Benin, Nigeria ya sasa.
Vingi kati vinyago hivyo viliuzwa katika minada ya London na vingine vilinunuliwa na wakusanyaji wa kazi za sanaa kutoka nchi mbali mbali.
Tume ya Kitaifa ya Makumbusho ya Nigeria imetoa maombi rasmi kwa makumbusho kote ulimwenguni kurejesha sanamu hizo za shaba.
Novemba 2022, Jumba la Makumbusho la Horniman la London lilikubali kukabidhi vitu vya kale 72, vikiwemo vinyago vya shaba vya Benin.
Mkurugenzi wa makumbusho hiyo, Nick Merriman anasema: "Hakuna ubishi kuwa viliporwa - kwa hivyo kulikuwa na hoja ya kimaadili kuvirudisha."
Mwezi uliofuata, Chuo Kikuu cha Cambridge kilikubali kurudisha vinyago 116, na Ujerumani ikarudisha vitu vya kale 22.
Kuanzia 2026, vitu vya kale vitaonyeshwa katika Makumbusho ya Edo ya Sanaa ya Afrika Magharibi katika Jiji la Benin.
Vinyago vingine vya shaba vipo katika majumba za Uingereza, likiwemo Jumba la Makumbusho la Uingereza, ambalo linahifadhi mkusanyiko mkubwa zaidi wa vitu vya kale vya Benin, takribani mia tisa.
Jumba hilo linasema Sheria ya Makumbusho ya Uingereza ya 1963 inazuia vitu hivyo kurudishwa.
Mzinga wa Lewke
Serikali ya Uholanzi ilitangaza Julai 2023 kuwa makumbusho ya Rijksmuseum ya nchi hiyo - itarejesha mzinga wa Lewke huko Sri Lanka mwezi Novemba. Uliporwa pamoja na vitu vingine vitano na askari wa Uholanzi mwaka 1765.
Vazi la Moctezuma II
Kwa miaka mingi, serikali ya Mexico imetaka kurejeshwa kwa vazi la kichwani linaloaminika kuwa la mfalme wa Azteki, Moctezuma II.
Vazi hilo lina upana wa futi tatu, limetengenezwa kwa manyoya zaidi ya 450 ya kijani na kwa sasa liko katika Jumba la Makumbusho la Anthropolojia huko Vienna, Austria.
Wengine wanaamini ilikuwa zawadi kutoka kwa Moctezuma katika karne ya 16 kwenda kwa kiongozi wa Kihispania, Hernán Cortés. Wengine wanasema ni vazi lililovaliwa na makasisi wa Waazteki wa wakati huo.
Serikali ya Austria ilikataa kulirejesha Mexico kutokana na sheria ya Mexico kwamba ikiwa litarudishwa lazima libaki nchini humo milele. Lakini 2012, Mexico ilibadilisha sheria na Austria ikakubali kulirejesha kwa muda.
Lakini wataalamu wa makumbusho walisema kusafirisha vazi hilo hadi Mexico kungeharibu manyoya yake. Ndiposa Jumba la Makumbusho la Anthropolojia likaamua kutoa ruhusa raia wote wa Mexico kutembelea jumba hilo bila malipo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah