Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi Wasomali wanavyokumbuka vita vya 'Black Hawk Down' miongo mitatu baadaye
Black Hawk Down', ni jina la filamu ya Hollywood, limekuwa neno maarufu kwa maafa ya kijeshi ya 1993 nchini Somalia.
Wanajeshi 18 wa Marekani walipoteza maisha katika mapigano yaliyoanza tarehe 3 Oktoba, lakini pia mamia ya Wasomali.
Wakati Netflix inazindua filamu kuhusu matukio hayo, BBC imezungumza na baadhi ya Wasomali ambao bado wana makovu kutokana na kile kilichotokea.
Licha ya kuzungukwa na vifusi vya vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea, wakazi wa Mogadishu mapema miaka ya 1990 walikumbatia nyakati za utulivu.
Mwangaza wa jua wa Jumapili na upepo baridi wa bahari ulitoa fursa nzuri kwa Binti Ali Wardhere, 24 wakati huo, kutembelea jamaa na mama yake.
"Siku hiyo ilikuwa shwari," anakumbuka.
Lakini kama watu wengine wote katika jiji hilo hakujua kuwa Wamarekani walikuwa wakijiandaa kumshambulia mbabe wa kivita Mohamed Farah Aideed - na kile kilichotokea kingebadilisha maisha yake milele.
Marekani ilikuwa imepeleka wanajeshi Somalia mwaka 1992. Walikuwepo kuunga mkono ujumbe wa Umoja wa Mataifa ambao ulitoa msaada wa kibinadamu ili kupunguza njaa - katika sehemu iliyosababishwa na kuanguka kwa serikali kuu.
Lakini baada ya Aideed kulaumiwa kwa kuhusika na mauaji ya walinda amani 24 wa Umoja wa Mataifa mnamo Juni 1993, alilengwa kijeshi.
Hii ilijumuisha uvamizi wa Marekani mwezi Julai ambapo Wasomali wasiopungua 70 walikufa, na kuashiria mabadiliko katika jinsi Wamarekani walivyotazamwa. Pia ilisababisha kutumwa kwa wanajeshi wataalamu kutoka Marekani.
Tarehe 3 Oktoba, Marekani ilipata taarifa za kijasusi kwamba Aideed atakuwa kwenye mkutano na maafisa wake wakuu kwenye hoteli. Wamarekani walianzisha operesheni ya anga ambayo ilipaswa kuchukua dakika 90 - mwishowe ilichukua masaa 17.
Kwa Binti, ishara ya kwanza ya kwamba jambo lisilo la kawaida lilikuwa likitokea ni sauti za milipuko iliyoanza baada ya saa 15:30 za huko.
Wakazi wa Mogadishu walikuwa wamezoea sauti ya mapigano, lakini kulikuwa na kitu kuhusu ukubwa wa milipuko hii na mawimbi ya mshtuko ambayo yalikuwa sio ya kawaida.
Watu walianza kukimbia kila upande.
Akiwa ameazimia kuelewa kinachoendelea, Binti alipanda juu ya paa la nyumba ya jamaa yake. Kutoka hapo, aliona kwamba mapigano yalikuwa yanafanyika katika eneo jirani.
Helikopta mbili za Marekani aina ya Black Hawk zilidunguliwa, moja saa 16:20 na nyingine saa 16:40. Kikosi kazi kilizingirwa na ndipo kazi ya uokoaji ikaanza.
Kwa kuhofia familia yake, Binti alikimbia kuelekea nyumbani.
"Hadi leo, bado naona miili imetawanyika kila mahali mitaani," anasema.
Binti alifika nyumbani kwake baada ya saa 18:00 tu na kufarijika kuona kila mtu akiwa salama.
Mapigano yalipungua kidogo, na kuleta utulivu wa muda mfupi.
Alitoa chai huku mumewe akijadili vita na jirani yake. Lakini hakupata nafasi ya kuonja chai hiyo baada ya ganda la risasi kupiga nyumba yao.
Binti alihisi mkono wake umekatika. Alianguka chini, na mwanamke mmoja akamuangukia juu yake.
"Kulikuwa na maji ya moto juu ya kichwa changu. Nilijiwazia: 'Nani alifungua bomba la maji?'
Kisha akagundua kuwa ni damu ya mtu aliyekuwa juu yake, ambaye alikuwa amekufa. Jirani yake Binti ndiye aliyekuwa amefika nyumbani kwao kwa ajili ya kujilinda.
Usiku huo, Binti pia alipoteza mumewe, Mohamed Aden, na wanawe wawili - Abdulkadir Mohamed mwenye umri wa miaka 14 na Abdurahman Mohamed mwenye umri wa miaka 13.
Watoto wake wengine wanne, pamoja na kaka yake, ambaye alikuwa akikaa nao, walijeruhiwa. Baadaye kaka yake alikufa kutokana na majeraha yake.
Ifrah, ambaye alikuwa na umri wa miaka minne tu wakati huo, alipata upofu.
Mtoto mkubwa wa Binti, ambaye sasa ni baba, anaendelea kuhangaika na masuala ya afya ya akili. Hadi leo, kuona au kusikia sauti ya ndege humfanya ajifiche.
Hakujua kuhusu hilo katika siku ya Jumapili asubuhi iliokuwatulivu, lakini mpigapicha mashuhuri Ahmed Mohamed Hassan, anayejulikana pia kama Ahmed Five, alikuwa na jukumu kubwa katika jinsi matukio yalivyoonekana.
Akiwa miaka Ishirini na tisa wakati huo, tayari alikuwa ameandika vita vya koo, njaa na matukio ya machafuko ya Mogadishu na vitongoji vyake.
Siku hiyo, hakuwa akiwaza kuhusu kazi wakati milipuko hiyo ilipotanda hewani.
Sauti ya helikopta na milio mizito ya risasi iliashiria kitu kikali zaidi ya mlio wa AK-47 ambao kwa kawaida aliusikia.
Ahmed daima alibeba kamera yake, akijua kwamba huko Mogadishu lolote linaweza kutokea wakati wowote. Alianza kuandika machafuko yaliyokuwa yakitokea na kuelekea katikati ya vita.
"Ingawa hali hii ilikuwa tofauti kabisa na zile ambazo nilifanya kazi hapo awali, bado niliamua kurekodi matukio haya na kuchukua jukumu hilo," anaambia BBC.
Tukio la karibu zaidi alilowahi kushuhudia ni uvamizi wa Julai ambao ulichochea hisia za chuki dhidi ya Marekani na kuweka mazingira ya mapambano ya Oktoba.
Katika siku ya kwanza, alirekodi baadhi ya mapigano kati ya wanajeshi wa Marekani na Wasomali.
Kisha siku ya pili, aliongozwa hadi kwenye nyumba ambayo rubani wa Marekani Michael Durant alikuwa akishikiliwa.
Bw Durant alikuwa akipeleka ndege ya pili ya Black Hawk iliyoanguka baada ya kushambuliwa na guruneti la roketi. Baada ya kuanguka, wafanyakazi wake watatu waliuawa katika mapigano hayo pamoja na wengine wawili waliokuwa wamekwenda kuwaokoa.
"Ilikuwa mapigano makubwa sana ya risasi. Wanasema kuwa Wasomali 25 waliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la pili la ajali, hivyo hiyo inakupa mwanga kuhusu ni kiasi gani cha risasi zilikuwa zikifyatuliwa," Bw Durant baadaye aliambia BBC.
Aliokolewa wakati mtu mwenye bunduki alipotambua kwamba rubani anaweza kuwa na thamani kama mfungwa.
Ahmed kisha akamrekodi yule Mmarekani mwenye jazba na aliyepigwa ambaye alikuwa na makovu kadhaa usoni mwake. Anaweza kuonekana akithibitisha utambulisho wake huku akipumua kwa nguvu na kutazama upande wa mtu anayemuhoji, ambaye haonekani katika picha.
Hadi wakati huo, sio Marekani wala Aideed waliojua kuwa Bw Durant alikuwa anashikiliwa, Ahmed anasema.
"Nilikabidhi kanda za video kwa ndege ya Umoja wa Mataifa ambayo ilikuwa ikiruka kila siku kutoka Mogadishu hadi Nairobi [katika nchi jirani ya Kenya].
"Ripoti ya kwanza ya vita vya Mogadishu kufikia ulimwengu ilikuwa kutoka kwenye picha nilizorekodi. Wakati huo, nilikuwa nikifanya kazi kama mfanyakazi huru wa CNN."
Picha zilizonaswa na Ahmed ziligonga vichwa vya habari kote ulimwenguni.
Pia walishiriki katika mjadala kuhusu sera ya mapambano ya Marekani katika bara la Afrika, ambayo ilibadilika baada ya mapigano huko Mogadishu.
"Hili ni jambo ambalo najivunia - ingawa wakati huo, sikutarajia matokeo yake," Ahmed anasema.
Ndani ya miezi sita, Marekani ilikuwa imeondoa vikosi vyake kutoka Somalia. Kushindwa kwa ujumbe wake nchini Somalia kulifanya Marekani kuwa na wasiwasi wa kuingilia kati migogoro ya Afrika iliyofuata.
Tarehe tatu ya Oktoba ilianza kama siku ya sherehe nyumbani kwa Saida Omar Mohamud kwani asubuhi hiyo alijifungua mtoto wa kike.
Ndugu, jamaa na majirani walikusanyika nyumbani kwake kwa ajili ya kumpongeza, huku familia ikijiandaa kwa sherehe za kitamaduni za kupeana majina.
Lakini mhemko ulibadilika mara tu mapigano yalipoanza.
Ghasia zilizuka wakati helikopta ya kwanza ilipoanguka mbele ya nyumba ya Saida.
Muda mfupi baadaye, anakumbuka angalau wanajeshi 10 wa Marekani waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba hiyo.
Walikusanya kila mtu sebuleni, na kuwaamuru wasisogee na wakaigeuza kuwa hospitali ya dharura.
Familia ilitazama kwa mshtuko wakati wanajeshi waliojeruhiwa walilazwa kwenye meza yao ya chakula, wakipokea matibabu ya dharura.
"Ingawa waliogopa, walitutia hofu pia. Waligeuza nyumba yetu kuwa ngome," Saida anasema.
Pamoja na kumbukumbu zake za kutisha, Saida aliacha kumbukumbu ya kudumu ya siku hiyo kwa kile alichoamua kumuita bintiye.
Kama Wasomali wanavyosema, "hakuna jina linalotolewa bila sababu" na hivyo msichana mdogo wa Saida sasa anajulikana kama Amina Rangers.
Filamu ya hali halisi ya Netflix inaangazia "hadithi mbichi, iliyo na mahojiano ya mtu wa kwanza kutoka pande zote mbili za Vita vya Mogadishu", kulingana na utangazaji. Inaangazia maovu waliyopitia Wasomali kama Binti wakati wa vita.
"Wakati huu, Wasomali walipewa fursa ya kushiriki kutoa maelezo yao ya matukio. Ni muhimu kwamba pande zote mbili za hadithi zinasimuliwa kila mara," Ahmed Five anasema.
Lakini kwa Binti Ali, kusimulia hadithi tu hakutoshi.
Alipoteza wapendwa wake katika vita. Hata hivyo anahisi uharibifu unaoletwa kwa familia za Kisomali bado haujatambuliwa.
"Wamarekani ndio walioharibu nyumba yangu, wakaua mume wangu, wanangu wawili, na kaka yangu, na kuiacha familia yangu katika taabu ya kudumu," anasema, sauti yake ikivunjika.
"Kwa ufupi, lazima wakubali walichofanya na kutufidia."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla