Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ndani ya kikosi cha 'Makomando hatari' wa Somalia wanaozua hofu kwa al-Shabab
Ni baada saa kumi na moja asubuhi, na lori tatu za kubebea mizigo - kila moja ikitoa mlio, kama wa nungunungu, ikiwa na makumi ya askari wenye silaha nzito - zinanashika njia yenye vilima namchanga katika nyika kuelekea katikati mwa Somalia.
Dereva wa gari la katikati, akiwa ameinama juu ya gurudumu lake, anabadilisha gia ili kuruka kichaka cha miiba, kisha anatabasamu na kuangalia kioo chake cha pembeni ili kuhakikisha wenzake walioketi kwa kuning’nia miguu kando ya gari, hawajaanguka.
"Kazi yetu ni ukaguzi kwanza," anasema Luteni kijana, kwenye kiti cha abiria na kukagua eneo wanaloelekea ili kubaini dalili za uwezekano wa uvamizi, au kuwekewa mitego ya vilipuzi ambayo hutumiwa na kundi la wanamgambo, al-Shabab.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, wanajeshi hao wa ngazi ya juu wa jeshi la taifa, kikosi cha Danab kinachofadhiliwa na Marekani na kupewa mafunzo - maana yake "hatari" - kikosi cha komando, wamekuwa na jukumu kubwa katika mapambano dhidi ya al-Shabab.
Makomando hao wamewafanya wanamgambo wa al-Shabab kuondoka maeneo ya miji na vijijini katikati mwa Somalia.
Mafanikio ambayo hayakutarajiwa ya mashambulizi haya yasiyotarajiwa yamezua wimbi la matumaini kote nchini, hata wakati mamilioni ya watu wakikabiliana na ukame mbaya.
"Haya ndiyo matumaini zaidi ambayo nimekuwa nayo kwa miaka mingi. Hakuna kitu ambacho kinaweza kusimamisha operesheni hizi kwa sababu tumeonja ushindi dhidi ya al-Shabab. Tumeona kwamba wanaweza kushindwa, na watu wa Somalia hatimaye wameamka," Alisema Malik Abdalla, mbunge wa eneo hilo katika eneo la Hiran ambako mapigano mengi yametokea.
Baada ya kuendesha gari kwa bidii kwa saa tatu, msafara huo unafika viunga vya mji mdogo unaoitwa Bukure, na askari wa Kikosi cha Sita cha Danab wanashuka kutoka magari yao.
Ni wanaume wembamba, wanaojiamini, wanaoweza kumudu silaha zao na wamezoea kusafiri bila mizigo mingi.
Bila kutamka neno lolote, wanatoa ulinzi karibu nasi - timu ya waandishi wa habari watatu wa BBC waliopata fursa adimu ya kuandamana na kikosi hicho katika eneo la mashambulizi.
"Taarifa zinaenea haraka. Al-Shabab watajua tayari uko hapa. Ndio maana tulilazimika kuondoka kambini mapema sana asubuhi ya leo, ili tuingie barabarani kabla watuwekee mitego," alisema Asli Halane, afisa uhusiano wa kijeshi na raia. na mwanachama pekee wa kikosi cha siri sana aliyeidhinishwa kuzungumza nasi.
"Taarifa zinaenea haraka. Al-Shabab watajua tayari uko hapa. Ndio maana tulilazimika kuondoka kambini mapema sana asubuhi ya leo, ili tuingie barabarani kabla watuwekee mitego," alisema Asli Halane, afisa uhusiano wa kijeshi na raia. na mwanachama pekee wa kikosi cha siri sana aliyeidhinishwa kuzungumza nasi.
Wanajeshi watatu wamesalia kwenye magari hayo, macho yao yakichungulia bunduki za kutisha za DShK zilizowekwa nyuma ya kila gari, huku raia wa eneo hilo, wengi wao wakiwa wafugaji wa kuhamahama, wakijitokeza polepole kutoka maeneo ya mashambani.
"Tulifanikiwa kuwauwa wapiganaji 60 wa al-Shabab hapa," alisema Sajenti Halane, akipita nyuma ya mabaki ya maduka kadhaa madogo yaliyoteketea, huku akisimulia vita vya siku nzima vya mji huo mwezi Septemba.
Mamia kadhaa ya wanamgambo hatimaye waliondoka Bukure, lakini walifanya hivyo baada ya kuchoma moto majengo mengi, na kutumia vilipuzi kuharibu mnara wa maji wa mji huo katika kitendo kilichotafsiriwa na wenyeji kama hasira kubwa.
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Khadra Farah, alielezea jinsi mwanamgambo aliyekuwa akitoroka alivyompiga risasi baada ya kuchoma duka lake.
Wakazi waliachwa bila maji wala chakula kwa siku kadhaa, na "bado hawana mahitaji ya kimsingi. Mambo ni mabaya sana hapa," anasema Sgt Halane.
'Tulilala kwa hofu'
Na bado, hali ya Bukure, na katika sehemu nyingine za Somalia, si ile hali ya kukata tamaa iliyozoeleka na ya kutisha ambayo mtu hukutana nayo mara kwa mara katika nchi ambayo kwa miaka kadhaa imeshindwa kujinasua kutoka mikononi mwa kundi hilo lenye ufungamano al-Qaeda.
Katika hatua ambayo sio ya kawaida makumi ya raia walikubali kuzungumza na sisi, wakitangaza waziwazi chuki yao dhidi ya al-Shabab, na imani yao kwamba kitu cha msingi kilikuwa kimebadilika.
"Chini ya al-Shabab tulilala kwa hofu kila usiku," alisema Ali Dahir Warsame, 48, kiongozi wa jamii ya eneo hilo.
"Lakini sasa tunaelewa kwamba hawana uhusiano wowote na Uislamu. Wamekuwa wakiwadhuru watu wasio na hatia. Sasa tuna uhakika 100% kwamba hawatarejea hapa."
Kwa kiwango fulani ni hali ngumu ya Maisha. Ukame unaokumba Somalia kwa sasa – ni mbaya haujawahi kushuhudiwa ndani ya miongo minne na imesukuma jamii nyingi zinakodolewa macho na baa la njaa, na kuwaacha wengi wao wakihisi hawana chaguo ila uasi dhidi ya kundi la wanamgambo wenye sifa mbaya ya unyang'anyi, rushwa na kukusanya kodi za adhabu.
Lakini sababu nyingine ni hali ya maasi yenyewe ambayo yanaashiria mapinduzi ya chini kwa chini, yanaongozwa na wakulima wa ndani jamii kwa ujumla- serikali, jeshi na vikosi maalum mara nyingi hufanya jukumu la kusaidia.
"Hii ni hatua ya mabadiliko. Watu wamechoshwa na al-Shabab. Serikali ikiweza [kuchukua] fursa hii nadhani al-Shabab watatokomezwa," alisema Mohamed Moalimu, mwandishi wa habari wa zamani na mbunge ambaye amenusurika mashambulizi mengi ya wanamgambo na ametumia wiki nzima kuwatembelea wanamgambo wa ukoo wa "ma'awiisley" ambao wamefanya mapigano mengi katika eneo la Hiran.
Lakini swali linabakia - je, uasi wa umma unaweza kushinda migawanyiko kwa misingi ya koo ambayo imechangia Somalia kukumbwa na migogoro na machafuko ya miongo mitatu?
Tayari kuna dalili kwamba viongozi wenye ushawishi mkubwa katika baadhi ya maeneo wana mashaka juu ya dhamira na uwezo wa serikali kuu, na kusita kuunga mkono uasi ambao bado unaweza kuzuka na kuwaingiza tena kwenye dhiki za kutawaliwa na wanamgambo.
"Mkakati unafanya kazi," alisisitiza Hussein Sheikh-Ali, mshauri wa usalama wa kitaifa wa rais wa Somalia, akitabiri kwamba wanasiasa wanaoyumba hivi karibuni watajikuta wakilazimika kuunga mkono uasi huo.
"Kwa sababu chuki dhidi ya al-Shabab umepata umaarufu sana, wanasiasa hawatadhubutu kupinga serikali ya shirikisho," alisema Bw Sheikh-Ali.
'Watu wazuri'
Mchanganyiko wa ukame na migogoro kwa hakika umeisukuma Somalia katika eneo lisilo na uhakika na kuipatia serikali kuu fursa adimu ya kukabiliana na uvamizi wa wanamgambo hao wanaodhibiti sehemu kubwa za mashambani.
Kikosi cha Danab kinatarajiwa kukua kutoka karibu wanajeshi 1,500 hadi zaidi ya mara mbili ya ile iliyopo sasa katika miezi ijayo, huku Marekani ikitoa ufadhili zaidi, na msaada zaidi wa kijeshi.
"Marekani? Ni watu wazuri. Walitusaidia na ndege zisizo na rubani [katika vita vya Bukure]. Nimepigana zaidi ya vita sita dhidi ya al-Shabab, na sasa, wanapoona tunataka kupigana wanakimbia," alisema mmoja wa maafisa wakuu wa kikosi cha Danab, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
Lakini alitilia maanani zaidi uasi mkubwa dhidi ya wanamgambo hao, akiwa na wasiwasi kwamba bado ungeweza kusambaratika katika mzozo mbaya "kati ya koo".
Na baada ya hayo, msafara wa Danab ulianza tena kwa mwendo wake wa kawaida wa kasi, kwanza, kutuacha kwenye uwanja wa ndege wa saa nne baada ya safari ya kupitia msituni, na kisha kugeuka kusini, kuelekea Mto Shabelle na barabara kuu ya mji mkuu, Mogadishu, ambapo vita vingine dhidi ya al-Shabab tayari vilikuwa vinaendelea.