Polepole asema dada yake alitekwa na kuachiwa, polisi wachunguza

Chanzo cha picha, Pole pole
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Pole Pole amesema kuwa anapinga masuala ya utekeaji na kuwa dada yake ametekwa na kuumizwa.
Alizungumzia pia kutoridhishwa na mwenendo wa mambo mbalimbali nchini Tanzania.
"Watu wanataka uwabembeleze, uwaombe, uwabembeleze, uwaombe, lakini wao wakiwa na shida watakutafuta" alisema Polepole
Balozi huyo alijiuzuru siku ya Jumatatu akidai hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi.
Usiku wa kuamkia leo, Polepole alitoa taarifa katika mtandao wake wa Instagram kwamba dada yake alivamiwa na watu wasiojulikana walioingia nyumbani kwake kwa kuruka ukuta
Hata hivyo kamanda wa kanda maalum Dar es salaam Jumanne Muliro amesema kuwa walifuatilia tukio hilo, na kuwa uchunguzi unaendelea.
Kada huyo wa CCM alidai kitendo hicho kililenga kumtisha asizungumze alichopanga kuzungumza leo na kuapa kufanya hivyo hata ikiwa familia yake yote itatekwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika hotuba yake aliyoifanya leo kupitia mtandao wa Facebook, Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan na Dr Emmanuel Nchimbi kama wagombea wa Urais na Makamu katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba Mwaka huu.
"Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara" alisema Polepole.
BBC inaendelea na jitihada za kupata maoni ya chama cha mapinduzi CCM.
Hata hivyo Polepole anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.
Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaji kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.
Anajulikana pia kwa kauli tata au ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwahi kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa.
Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa.
Linalongojewa sasa ni kuona mustakabali wake kisiasa baada ya kujiuzuru ubalozi na nafasi nyingine za umma.















