Waridi wa BBC: 'Niliambiwa siwezi kuwa daktari lakini sasa ndoto yangu imetimia'

    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC News Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Safari ya Zaituni kuwa Daktari ilianza alipokuwa na umri wa miaka minne wakati alipovunjika mguu na kuanza kupata hamasa kubwa ya kutamani siku moja na yeye kuwa daktari.

"Tangu nikiwa darasa la tano nilikuwa ninajitambulisha kila mahali kuwa, mimi ni daktari…" , anasema Daktari Zaituni.

Ndoto yake ya utotoni hatimaye ikatimia na sasa yeye ni Daktari bingwa mbobezi kwa takribani miaka 20 na pia ni rais wa madaktari wanawake nchini Tanzania.

Daktari Zaituni anakumbuka jinsi daktari aliyekuwa anamhudumia mguu, alivyokuwa anapenda kuvaa uhusika wake nyakati za utoto wake ili aweze naye kuonekana kama Daktari huyo.

Lakini pamoja na kuwa na hamasa hiyo, Dkt. Zaituni anasema katika mazingira aliyokulia kila kitu ambacho alikuwa anataka kufanya aliambiwa hawezi, isipokuwa mama yake tu ndiyo mtu pekee aliyekuwa anamuunga mkono.

Anasema alipomaliza kidato cha nne na kutaka kusoma masomo ya sayansi, aliambiwa hawezi hayo ni masomo ya kiume, lakini pamoja na ushauri hasi aliopewa na wengi, mama yake tu ndiye mtu pekee aliyeendelea kumtia moyo na kumwambia utakuwa daktari mzuri sana.

Anasema alipomaliza shahada yake ya kwanza, alipangiwa kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo katika idara tatu," idara ya kwanza ilinishtua maana ilikuwa ni wakati ambao kulikuwa na vifo vingi vya walioathirika na Ukimwi na magonjwa mengine ya kawaida kama TB, Nimonia na mengineyo.

Ila mafunzo yangu ya pili, nilienda kuwatibu Watoto, jambo ambalo nilifurahia sana.

Na mafunzo kwa vitendo ya mwisho ilikuwa ni upasuaji ambayo hayo yalinifanya nifanye uamuzi kuwa ninaenda kuwa daktari bingwa mbobezi wa upasuaji."

Dkt, Zaituni anasema kuna siku alikuwa zamu na mtoto aliletwa akiwa mahututi sana kwa tatizo la kidole tumbo, jambo ambalo lilimpa uoga na hofu kwa kuwa msimamizi wake hakuwepo ila alimhudumia na kupona jambo ambalo lilimpa motisha zaidi.

Na msimamizi wake alimwambia atakuwa daktari mzuri sana wa upasuaji.

Na alipoanza kazi rasmi mwaka 2005, alipangiwa kitengo cha Watoto na baada ya hapo alienda kusomea upasuaji Misri na baadaye Urusi.

Safari ya kuwa daktari mwanamke bingwa mbobezi wa upasuaji ilikuwaje?

Dkt.Zaituni anajivunia kuwa mwanamke ambaye ana majukumu mengi ikiwa ni pamoja na mke, daktari bingwa mbobezi, rais wa chama cha wanawake madaktari, mama,dada na majukumu mengine mengi.

Mpaka leo hii, anakumbuka jambo ambalo huwa linamuumiza sana, kuna mmoja wa mkuu wake wa kitengo wakati wa mafunzo kwa vitendo, alimvunja moyo sana kuwa wanamke si watu wa kuwategemea katika kazi hii kwasababu mara atajifungua aende likizo, mara hiki hawezi na hakuwa anaona mchango wake kama mtu mwenye taaluma jambo ambalo si sahihi.

Kwa upande wake yeye kama rais wa madaktari wanawake anaona wanawake wanafanya kazi nzuri sana katika tasnia hiyo, kikubwa katika kazi ni juhudi tu.

Dkt.Zaituni anasema juhudi za kupata matokeo mazuri, ndio jambo linampa furaha katika kazi na maisha yake kwa ujumla .

Mfano, Mgonjwa anaweza kuja katika hatua za mwisho ila ni mwiko kwa daktari kumkatia tamaa ni lazima kupambana ili kumtibu,anasema Daktari Zaituni.

Kwa sasa kuna maendeleo makubwa baada ya watu kupata elimu ya kutosha, madaktari wanapata ujuzi kutoka kwa madaktari wengi wanaokuja kutembelea hapa.

Kwa sasa Dkt.Zaituni ana mradi wa kutibu Watoto waliozaliwa na matatizo ya utumbo nje, ambapo anazunguka mikoa mbalimbali kutoa elimu kwa madaktari wengine.

Wakati ambapo tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa miaka ya nyuma, Watoto waliozaliwa na utumbo wazi katika mataifa ya Afrika na jangwa la sahara walikuwa wanakufa kwa asilimia 100 wakati mataifa yaliyoendelea ilikuwa ni asilimia nne tu.

Daktari bingwa wa upasuaji nchini Tanzania, Zaituni Bokhary ambaye alishinda safari iliyokuwa na viunzi vingi vya kuwa mwanamke hawezi kuwa Daktari ambavyo alianza kukumbata navyo tangu akiwa mtoto.

Lakini ndoto yake ya Daktari Zainabu imemfanya kupiga hatua kubwa kwa kuweza kufika mikoa mbalimbali kutoa mafunzo kwa madaktari wengine na mpaka sasa wameweza kuokoa Watoto kwa asilimia arobaini kwa kutumia tiba ya mfuko laini kusaidia kuokoa maisha ya watoto wenye tatizo hilo.

Ni mradi wa miaka mitatu na mpaka sasa amemaliza miaka miwili akiwa na matokeo chanya ya watoto wenye tatizo hilo, vifo vimepungua na sasa wamefika asilimia 40.

Daktari Zaituni anashirikiana na Wajerumani ambao wanamsaidia mifuko laini ambayo ni rafiki kwa ngozi ya mtoto

Mpaka sasa tayari wametoa mafunzo mkoani Mbeya, Arusha, Dar es salaam, Kigoma na Mwanza.

Anafurahi kuwa Daktari bingwa wa tiba hii kwa watoto

Lakini pamoja na kuwa na changamoto na mafanikio mengi ya kazini, Daktari Zaituni ni mama wa Watoto watatu.

Hata hivyo hali ya watoto wake wawili ambapo mmoja aliaga dunia wamekuwa wana maradhi adimu ambayo pia kila anapotibu watoto wengine anakumbuka hali ya watoto wake na hiyo inampatia hamasa zaidi ya kujitolea kwa watoto wengine.

Vilevile, kwa upande wake kila mtoto anayemhudumia katika upasuaji huwa anavaa kuwa yeye ni mama na mtoto ni muhimu kupona.

Imehaririwa na Leonard Mubali