Tunayofahamu kuhusu sheria ya ardhi ya Afrika Kusini inayomkera Trump

Muda wa kusoma: Dakika 7

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa yuko katikati ya dhoruba ya kisiasa baada ya kuidhinisha sheria ambayo inaipa serikali mamlaka ya kuchua baadhi ya ardhi inayomilikiwa na watu binafsi bila kuwafidia.

Sheria hiyo, ambayo bado haijatekelezwa, imemuudhi Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye anaiona kama hatua ya kuwabagua wakulima wazungu.

Vyama vya siasa vya mrengo wa kulia na vikundi vyenye ushawishi nchini Afrika Kusini pia vimepinga, wakisema watapinga Sheria ya Unyang'anyi - kama sheria inavyoitwa - mahakamani kwa misingi kwamba inatishia haki za mali.

Serikali ya Ramaphosa inasema sheria hiyo inatoa fidia kulipwa katika visa vingi - na mabadiliko yanahitajika ili kuongeza umiliki wa ardhi ya watu weusi.

Mashamba mengi ya kibinafsi bado yanamilikiwa na wazungu.

Wakati Nelson Mandela alipoingia madarakani zaidi ya miaka 30 iliyopita, akimaliza mfumo wa ubaguzi wa ubaguzi wa rangi, iliahidiwa kwamba sheria hii itarekebishwa kupitia mpango wa mageuzi ya ardhi ya mnunuzi wa hiari, muuzaji wa hiari - lakini wakosoaji wanasema mpango huu unaonekana kuwa ni wa polepole sana na wagharama kubwa sana.

Unaweza pia kusoma:

Je ni nini hasa kinachoweza kunyakuliwa bila fidia?

Katika hali nadra itakuwa ni ardhi ambayo inahitajika kwa "maslahi ya umma", wataalam wa sheria waliiambia BBC.

Kulingana na kampuni ya mawakili ya Afrika Kusini ya Werksmans Attorneys, hii inapendekeza ingetokea hasa, au labda tu, kuhusiana na mpango wa mageuzi ya ardhi.

Ingawa inaweza pia kutumika kupata maliasili kama vile madini na maji, kampuni hiyo iliongeza, katika maoni yaliyoandikwa na wataalam wake katika suala hilo, Bulelwa Mabasa na Thomas Karberg.

Mabasa na Karberg waliiambia BBC kwamba kwa maoni yao, ardhi ya kilimo yenye tija haiwezi kunyakuliwa bila fidia.

Walisema unyakuzi wowote bila fidia - unaojulikana kama EWC - unaweza kufanyika katika hali chache tu:

  • Kwa mfano, wakati mmiliki hakuwa akitumia ardhi na alikuwa akiishikilia kwa "madhumuni ya kubahatisha"
  • Au wakati mmiliki "aliacha ardhi kwa kushindwa kuidhibiti licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo".

Wamiliki labda bado wangepata fidia kwa majengo yaliyopo kwenye ardhi na maliasili, mawakili walisema.

Mabasa na Karberg waliongeza kuwa EWC "haikulenga ardhi ya vijijini au mashamba, na inaweza kujumuisha ardhi katika maeneo ya mijini".

Hata hivyo, katika hali ambapo fidia hulipwa, sheria zinaweza kubadilika, na wamiliki wanaweza kupata pesa kidogo.

Kwanini pesa kidogo hulipwa kama fidia?

Mpango ni kwa wamiliki kupokea fidia "ya haki na ya usawa" – ili kuepuka "thamani ya soko" ya juu ambayo wamekuwa wakipata hadi sasa, Mabasa na Karberg walisema.

Serikali imekuwa ikilipa fidia ya thamani ya soko licha ya ukweli kwamba hii ni "kinyume" na katiba, iliyopitishwa baada ya utawala wa wazungu walio wachache kumalizika mnamo 1994, waliongeza.

Mawakili wanasema kuwa unyakuzi wote una "mahitaji makubwa ya haki ya kiutaratibu", pamoja na haki ya mmiliki kwenda mahakamani ikiwa hatafurahia.

Wakati ardhi inaponyakuliwa kwa ''madhumuni ya umma'' kama kujenga shule za serikali au reli, fidia ya thamani ya soko la ardhi pia hutumika.

Hili halijakuwa hoja kuu ya utata, labda kwasababu "sio dhana ya riwaya" - hoja iliyotolewa na JURISTnews, wavuti wa kisheria unaoendeshwa na wanafunzi wa sheria kutoka kote ulimwenguni.

"Katiba ya Marekani, kwa mfano, inasema kwamba serikali inaweza kukamata mali ya kibinafsi kwa matumizi ya umma mradi tu 'fidia' itolewe," iliongeza.

Je, itatakuwa rahisi kwa serikali kupata ardhi?

Serikali inatumai hivyo.

Mtaalam wa ardhi wa Chuo Kikuu cha Western Cape Prof Ruth Hall aliiambia BBC kwamba zaidi ya madai 80,000 ya ardhi bado hayajatatuliwa.

Katika mikoa ya mashariki mwa Afrika Kusini, watu wengi weusi hufanya kazi kwenye mashamba bila malipo - ili wanaruhusiwa kuishi huko na kufuga mifugo yao kwenye sehemu ya ardhi ya wamiliki, alisema.

Serikali inataka kuhamisha umiliki wa ardhi hii kwa wafanyikazi, na haikuwa "haki" kutarajia ilipe thamani ya soko la ardhi, Profesa Hall aliongeza.

Katika miongo mitatu iliyopita, serikali imetumia mamlaka yaliyopo kunyakua mali - na fidia ya chini ya thamani ya soko - katika visa chini ya 20, alisema.

Sheria hiyo mpya ililenga kurahisisha nafuu kurejesha ardhi kwa watu weusi na kwa bei ambao "walinyang'anywa" wakati wa utawala wa wazungu walio wachache au waliolazimishwa kuwa "wapangaji wa muda mrefu" kwani hawakuweza kumiliki ardhi, Profesa Hall aliongeza.

"Ni njia ya kujadiliana," alisema.

Lakini ana shaka kuwa serikali itaendelea na utekelezaji wa sheria hiyo katika siku zijazo kwani "gharama ya kisiasa" imekuwa kubwa sana.

Msomi huyo alikuwa akimaanisha ukweli kwamba Trump amepinga sheria hiyo, akisema inabagua wakulima wazungu na ardhi yao ilikuwa "ikichukuliwa" - shtaka ambalo serikali inalikanusha.

Mnamo Februari, Trump alikata misaada kwa Afrika Kusini, na mnamo Aprili alitangaza ushuru wa 30% kwa bidhaa nyingine na bidhaa za kilimo za Afrika Kusini, ingawa hii ilisitishwa baadaye kwa siku 90.

Hii ilifuatiwa na pambano maarufu la mwezi uliopita la Ofisi ya Oval wakati Trump alimuonyesha ghafla Ramaphosa video na machapisho ya hadithi zinazodai wazungu walikuwa wakiteswa - sehemu kubwa ya ripoti yake imepuuzwa.

Je, hatua hii imejibiwa vipi nchini Afrika Kusini?

Sawa na Trump, chama cha pili kwa ukubwa katika serikali ya muungano ya Ramaphosa, Democratic Alliance (DA), kinapinga sheria hiyo.

Katika taarifa yake mnamo Mei 26, chama hicho kilisema kuwa baraza lake kuu la uongozi limekataa dhana ya "fidia yoyote".

Hata hivyo, imekubaliana na dhana ya fidia ya haki na usawa badala ya fidia ya thamani ya soko, na kuongeza kuwa inapaswa "kuamuliwa na mahakama ya sheria".

La kushangaza, Jaco Kleynhans kutoka Vuguvugu la Mshikamano, kikundi chenye ushawishi mkubwa wa Wazungu, alisema kuwa ingawa sheria mpya inaweza "kuharibu" biashara zingine na alikuwa akiipinga, hakuamini kuwa ingesababisha "unyakuzi mkubwa wa mashamba".

"Sioni ndani ya maneno ya maandishi haya kwamba hilo litatokea," alisema katika majadiliano ya hivi karibuni ya jopo katika maonyesho ya kilimo yaliyofanyika katika mkoa wa Free State nchini Afrika Kusini - ambapo idadi kubwa ya wakulima wa kihafidhina wa Kizungu wanaishi.

Chama cha Wamiliki wa Mali cha Afrika Kusini kilisema "haina mantiki" kutoa "fidia yoyote" kwa mmiliki ambaye alikuwa na ardhi kwa madhumuni ya kubahatisha kuimiliki.

"Kuna wamiliki wengi wa ardhi ambao kusudi lao pekee la biashara ni kubashiri ardhi. Hawapati ardhi bila malipo na wana gharama kubwa za kushikilia," chama hicho kilisema, na kuongeza kuwa hakina shaka kuwa sheria "itachunguzwa sana" mahakamani.

Mabasa na Karberg walisema maoni moja ni kwamba dhana ya EWC ni "upuuzi wa kisheria" kwasababu "asili katika ufafanuzi wa kisheria wa unyakuzi, ni hitaji la fidia kulipwa".

Hata hivyo, mawakili walisema maoni mbadala ni kwamba katiba ya Afrika Kusini "inatambua kabisa kwamba katika hali fulani itakuwa ya haki na sawa kutokuwepo kwa fidia".

Serikali inasema nini?

Waziri wa Kazi za Umma wa Afrika Kusini Dean Macpherson ameitetea sheria hiyo, akikiuka msimamo wa chama chake, DA.

Kusema kweli yeye ndiye anayesimamia uhalalishaji mpya wa utekelezaji wa sheria na, kwenye jopo la majadiliano, alielezea kuwa ingawa ana wasiwasi juu ya sheria, ana imani ilikuwa "uboreshaji mkubwa" juu ya Sheria ya awali ya Unyang'anyi, na ulinzi mkubwa kwa wamiliki wa ardhi.

Alisema sheria hiyo pia inaweza kusaidia kukomesha madai ya unyang'anyi kwa serikali, na wakati mwingine "fidia yoyote" inaweza kuhesabiwa kwa haki.

Alitoa mfano wa matatizo yanayokabili shirika la umeme linalomilikiwa na serikali la Eskom.

Inapanga kusambaza mtandao wa usambazaji kwenye takriban kilomita 4,500 (maili 28,000) ili kuongeza usambazaji wa umeme ili kumaliza shida ya umeme nchini.

Kabla ya kusambazwa, baadhi ya watu walishirikiana na maafisa wa Eskom kununua ardhi kwa rand 1m ($56,000; £41,000), na kisha kudai fidia ya R20m , alisema.

"Je, ni haki na usawa kuwapa kile wanachotaka? Sidhani kama hiyo ni kwa maslahi ya jamii pana au serikali," Macpherson alisema.

Akitoa mfano mwingine, Macpherson alisema kuwa baadhi ya miji ya ndani ya Afrika Kusini iko katika hali "mbaya". Baada ya wamiliki kuondoka, majengo "yalizidiwa" na "kutekwa nyara" kwa uvamizi haramu. Gharama kwa serikali kuyajenga upya zinaweza kuzidi thamani yake, na katika hali kama hizo mahakama zinaweza kuamua kwamba mmiliki ana haki ya "kupata fidia", alisema.

Meya wa Johannesburg Dada Morero aliliambia gazeti la Mail & Guardian la Afrika Kusini kwamba alitaka kutumia majengo hayo kwa "faida ya umma", kama vile kuwapatia makazi karibu watu 300,000 kwenye orodha ya wanaosubiri makazi.

Aliongeza kusema kuwa wamiliki wa karibu majengo 100 hawakuweza kupatikana.

"Wameacha majengo hayo," alisema, akiongeza kuwa baadhi ya wamiliki walikuwa ni kutoka Uingereza na Ujerumani.

Lakini Mabasa na Karberg waliiambia BBC kwamba katika hali kama hizo fidia bado italazimika kulipwa kwa majengo hayo, ingawa sio ardhi.

Nini kinafuata?

Sheria hiyo iko mashakani, kwani karibu miezi minne baada ya kuiidhinisha rais Ramaphosa bado hajaweka tarehe ya utekelezaji wake.

Wala hawezi kufanya hivyo hivi karibuni, kwani hangetaka kumpinga zaidi Trump wakati Afrika Kusini inajaribu kujadili makubaliano ya biashara na marekani.

Na kwa upande wa ndani, chama cha DA kinazidisha upinzani dhidi ya sheria hiyo. Kilisema kinataka "mapitio ya mahakama" ya sheria hiyo, huku kikisonga mbele na hatua za mahakama kupinga uhalali wa sheria hiyo.

Dai gumu la DA ni tofauti na lile la Macpherson, ambaye, wiki chache zilizopita, alionya kwamba ikiwa sheria itafuatwa kwa ukamilifu: "Sijui nini kitatokea baada ya hapo.

"Katika siasa, wakati mwingine lazima uwe muangalifu na unachotaka kwasababu mara nyingi unaweza kukipata," alisema.

Maoni yake yanaangazia mpasuko mkubwa katika siasa za Afrika Kusini, huku baadhi ya vyama, kama vile Julius cha Malema cha Economic Freedom Fighters (EFF), wakiamini kuwa sheria hiyo haikwenda mbali vya kutosha kukabiliana na ukosefu wa usawa wa rangi katika umiliki wa ardhi.

Pamoja na ardhi kuwa suala tata, hakuna suluhisho rahisi kwa mzozo huo na kuna uwezekano wa kuendelea kusababisha mvutano ndani ya Afrika Kusini, na pia na rais wa Marekani.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi