Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Makamishna wanne walijaribu kulazimisha kura ya marudio - Chebukati

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati ameyataja madai yaliotolewa na makamishna wanne wa tume hiyo kama ya uwongo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Chebukati amesema kwamba makamishna hao walijaribu kulazimisha kufanyika kwa kura ya marudio kinyume na kiapo walichokula katika tume hiyo.
''Hiyo ni sawa na kupindua Katiba na mamlaka ya Wananchi wa Kenya'', alisema Chebukati akiongezea kwamba yeye kama Mwenyekiti alikataa katakata ukiukaji wa katiba na akaendelea kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Rais kama yalivyopokelewa kutoka vituo mbalimbali vya kupigia kura.
Alisema kwamba uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na uwazi wa kiwango cha juu zaidi ya chaguzi zozote zile zilizoandaliwa na tume hiyo.
Chebukati amesema kwamba mbali na kuweka matokeo hayo kwa umma, vyombo vya habari , wachunguzi na wagombea pia walikuwa na uwezo wa kuona matokeo hayo na kufanya hesabu zao kama yalivyotangazwa katika vituo vya kupigia kura.
Kuhusu hatua ya mgombea wa Muungano wa Azimio Raila Odinga kuwasilisha kesi mahakamani, Chebukati amesema kwamba kila mtu ana haki kuwasilisha malalmishi yake mahakamani na tume hiyo itakuwa na fursa ya kujibu na kuelezea kwa kina jinsi uchaguzi huo ulivyoandaliwa , matokeo kura kuhakikiwa na matokeo kutangazwa kulingana na katiba na sheria ya Kenya.
Kuhusu chaguzi za Marudio ziliotarajiwa kufanyika katika kaunti mbili za kakamenga na Mombasa mnamo tarehe 23 mwezi huu, Chebukati amesema kwamba tarehe mpya ya chaguzi hizo zitachapishwa katika gazeti ramsi la serikali hivi karibuni.
Siku ya Jumanne makamishna wanne wa tume ya uchaguzi IEBC kati ya saba walipinga matokeo yaliotolewa na mwenyekiti wao wafula Chebukati, wakidai kwamba yalikabiliwa na kiza kinene.
Makamishna hao wanadai kwamba hesabu ya matokeo iliotangazwa na Wafula Chebukati haiingiliana na jumla ya idadi ya kura ya wagombea wanne wa Urais.
Vilevile wanadai kwamba wafula Chebukati hakuwahusisha katika kuhakiki matokeo ya mwisho kabla ya kuyatangaza kwa umma.
Tayari Aliyekuwa mpinzani mkuu wa William Ruto na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ameapa kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo akisema kwamba mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alikiuka katiba kwa kuytowahusisha makamishna wake katika mchakato wote wa kutangaza matokeo hayo.














