Daktari mwenye shahuku ya uandishi wa habari azindua gazeti la kwanza la sayansi kwa Kiswahili Tanzania

Chanzo cha picha, Buguzi
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Swahili
Ikiwa lugha ya Kiswahili imepitishwa na kutambulika kuwa lugha rasmi kwenye mikutano ya umoja wa Afrika, sasa tunaona inaendelea kupaa zaidi kwenye masuala ya uandishi ya habari ambapo machapisho ya kiutalaamu yaliyozoeleka kuandikwa lugha ya Kiingereza kuanza kupatikana kwa lugha ya Kiswahili.
Nchini Tanzania Gazeti jipya la mtandaoni linalofahamika kama "MwanaSayansi" limezinduliwa rasmi hivi karibuni likiwa limesheheni habari za sayansi na teknolojia, likiwa ni gazeti la kwanza kwa Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa ujumla.
Syriyacus Buguzi ndiye mwanzilishi wa gazeti hilo, anasema 'ndoto yake imetimia'.
Ndoto ya Buguzi kuwa mwanahabari ilimea akiwa bado anasoma sekondari katika Seminari ya Katoke huko Biharamuro na baadaye alipomaliza kidato cha nne alipenda kusoma masomo ya Sanaa lakini alichaguliwa kwenye masomo ya sayansi.
"Tangu zamani nilikuwa na matumaini kwamba ipo siku nitamiliki gazeti langu na niliwaambia wazazi kuwa ningependa kusoma masuala ya lugha na historia lakini walinigomea baada ya kufaulu na kupata shule ya vipaji maalumu ya Iliboru."
Ikiwa bado roho yake inasononeka juu ya maamuzi ya kwenda kusomea masomo ya sayansi tumaini jipya lilijengwa baada ya baba yake kumwambia kuwa inawezekana kuandika masuala ya kisayansi.
Alipomaliza kidato cha sita akapata nafasi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, kusomea shahada ya awali ya udaktari wa binadamu ikiwa ni mwaka 2007, katikati ya masomo alipata taarifa ya mafunzo ya uandishi wa habari kwa ngazi ya cheti yaliyokuwa yanatolewa na gazeti la "The African".
"Bado nilikuwa na hamu zaidi ya kufanya uandishi wa habari nimeenda nayo kipindi nasomea udaktari katikati humo ndimo nikaanza kusoma pia na uandishi wa habari"
"Mwaka 2009 kulikuwa na programu ya uandishi wa habari kwa ngazi ya cheti, watu wengi walikuwa wakijiuliza maswali kwamba uandishi na udaktari wapi na wapi."
Alisita kumtaarifu baba yake kuhusu tasnia ya habari

Chanzo cha picha, Buguzi
Ili aweze kusomea uandishi wa habari ilimbidi alipe ada ndipo alipochukua jukumu la kumjulisha baba yake lakini ilimchukua muda kufikia uamuzi wa kumshirikisha mzazi. Bahati nzuri hakuwa na mtazamo tofauti na aliendelea kuamini kuwa mapenzi yake na uandishi bado hayakupotea.
"Kuna wakati nilimuomba anisaidie fedha kwa kuwa nataka kuanza masomo ya ngazi ya cheti ya uandishi kwani niliona kama kuna fursa hakusita, alinisaidia basi nikasonga kusoma kwani yeye alifahamu muda mrefu kuwa nina ndoto hiyo."
Lakini alipomaliza chuo kikuu na kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya kitabibu katika hospitali ta rufaa ya mkoa ya Mwananyamala Dar es Salaam, hakuendelea na masuala ya tiba na badala yake alijikita kwenye uandishi wa Habari, baada ya kuajiriwa rasmi kwenye gazeti la "The Citizen" alipokuwa akijitolea hapo mwanzo kama mwandishi. Maamuzi haya yalianza baada ya kujitafakari ni kitu gani hasa anachokipenda zaidi kitaaluma.
"Ikanibidi kukaa kuamua huku nikiangalia miaka kumi ijayo nitakua wapi ndipo ikabidi niwe nimeusimamia ukweli bila kumwambia baba yangu kuwa nimeamua kufanya kazi katika chombo cha habari."anasema Buguzi.
Ilikuwa ni fursa pekee aliyokuwa anaisubiri kwa muda mrefu, ya kuunganisha sayansi na uandishi wa habari, mwanzoni kabisa alikuwa mshika bendera wa kuanzishwa jarida la afya kwenye gazeti la "The Citizen"

Chanzo cha picha, Buguzi
"Ulikuwa mwanzo mzuri wa ndoto yangu ya kuwa mwandishi." Anaeleza Buguzi.
Nilipokuwa kwenye gazeti nilipenda kuandika sana ilinibidi nitoke nje kuhoji watu na wahariri waliona kuwa ninaweza kufanya aina mbalimbali za uandishi wa habari. Kuna wakati nilitumwa Bungeni kuandika habari.
Ilifika hatua wakanipandisha cheo na kuwa mhariri msaidizi wa gazeti la The Citizen, kusimamia shughuli nzima mpaka gazeti litoke. Mwanzoni niliona kama wananipotezea dira yangu nikidhani kuwa kuna baadhi ya mambo sikuweza kufanya ila baadaye nikagundua wananijengea uwezo na ujuzi wa uongozi ndani ya chumba cha habari.
"Baada ya kutoka hapo nikapata fursa ya kuunganisha sayansi na uandishi wa habari, ndipo nikaenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi na mawasiliano (Science Communication) katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza. Hii ilinifungua zaidi kuweza kufahamu namna ya kuwasilisha sayansi kwa lugha ya kiuandishi, nakumbuka nilikuwa naongea na Profesa aliyekuwa ananisimamia utafiti wangu na mambo ambayo yalijitokeza zaidi kwenye kuchunguza matatizo yanayowakumba wanasayansi ni katika kuandika maandiko ya kitaaluma kwa jamii katika lugha za asili".
Kwenye darasa nililokuwemo nilikuwa daktari pekee aliyekaa na kufanya kazi katika chombo cha habari, wengine wengi walikuwa wametoka moja kwa moja kwenye kazi zao za kitaaluma ya sayansi, nilikuwa ni nafasi muhimu sana na wakati nasoma mengi niliyafahamu.
Uzuri huko wakati nasoma wanakiboresha kilekile ambacho unakiweza, nilijikita zaidi kwenye kujua kwanini watu wasipate taarifa za kisayansi katika lugha zao ya asili, walinitafutia msimamizi wa kitaaluma ambaye alijikita zaidi kwenye masuala ya kilimo na habari kwenye lugha za asili.
Matamanio ya kuwa na gazeti la sayansi kwa lugha ya Kiswahili yalipata nguvu zaidi kuanzia hapo, hata jina la MwanaSayansi nikaona ndiyo gazeti lenyewe. Nikaanza taratibu zote za kuanzisha kampuni. Baadaye nililisajili gazeti baada ya kupata maelekezo ya mamlaka ya mawasiliano Tanzania(TCRA).
Mwanasayansi ni Gazeti la aina gani?

Chanzo cha picha, Buguzi
Gazeti la MwanaSayansi ni gazeti la kwanza la Kiswahili kujikita katika nyanja za kisayansi, mara nyingi imezoeleka sayansi ni masuala ya afya tu lakini sio hivyo tu sayansi ina uwanja mpana sana na mtambuka kama vile mazingira, kilimo, sayansi kwa watoto na nyingine nyingi.
Kwenye sayansi kwa watoto nilipata nafasi ya kuzungumza na Dr Lwidiko ambaye pia ni mwandishi katika gazeti hili jipya. Wakati tunasoma chuo kikuu, Muhimbili sote tuliuwa nan do zinazoendana ila yeye amejikita katika kufundisha watoto sayansi.
Kwahiyo ni gazeti linalotoa habari kuhusu tafiti za kisayansi za Tanzania na tunataka hizo tafiti ziweze kuwepo kwenye vyombo vya habari mbalimbali.
Ugumu uko wapi?
Watafiti wanaandika kwenye lugha ngumu sana hasa zile zilizopo kwenye lugha ya Kiingereza, sasa mpaka lugha hizo zivuke kwenye vikwazo viwili kwenye lugha ya kiutaalamu na iingie kwenye lugha ya Kiingereza halafu baadaye kwenda kwenye Kiswahili, huu mchakato ni mgumu hasa kwa watu ambao hawajajikita kwenye masuala ya kisayansi. Waandishi wa habari wengi inawawia vigumu kufahamu habari iko wapi katika utafiti kwa kukosa umahiri wa lugha za kisayansi lakini kwetu sisi wanasayansi inakuwa rahisi.

Chanzo cha picha, Buguzi
Kwenye habari ya mbele ya gazeti letu imeandikwa na daktari na nyingine na muhitimu wa masuala ya habari aliyemaliza katika chuo kikuu cha Dar es salaam. Timu yetu ni mchanganyiko wa wanasayansi na waandishi wa habari.
Hii changamoto ya ugumu wa tafiti za kisayansi kuwekwa katika habari inakuwa imepata suluhu na itasaidia vyombo vingine vya habari kuongeza habari za kisayansi.
"Vyombo vya habari mara nyingi huwa vinasita kuajiri wabobezi kwenye taaluma mbalimbali hasa kwenye sayansi, vyombo vya habari vinapaswa kuajiri wataalamu na kuwapa ujuzi wa kiuandishi ili kufanya taarifa mbalimbali kuwa rahisi kuandikwa."
Kwanini gazeti la mtandaoni?
Tumeamua kuanzia hapo mitandaoni kutokana na uwezo wa kiuchumi, lakini huko mbeleni huenda tukaweza kubadilisha na kulichapisha kwenda kwenye jamii. Uzuri wa gazeti hili ni bure ndio uzuri wake ili kusaidia watu wapate habari za kiundani.













