Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jeshi la Sudan limetwaa madaraka kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe - Kiongozi wa Mapinduzi
Kiongozi wa mapinduzi Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, amesema jeshi liliamua kuchukua mamlaka siku ya Jumatatu ili kuzuia "vita vya wenyewe kwa wenyewe". Aliongeza kuwa Waziri Mkuu aliyeondolewa madarakani Abdalla Hamdok alishikiliwa katika nyumba ya jenerali huyo "kwa usalama wake", lakini sasa amerejea nyumbani. Maandamano yanaendelea kwa siku ya pili katika mji mkuu, Khartoum, huku barabara, madaraja na maduka yakiwa yamefungwa. Mitandao ya simu na huduma za intaneti hazipatikani.
Takriban watu 10 wanaripotiwa kuuawa tangu machafuko hayo yaanze. "Hatari tulizoshuhudia wiki iliyopita zingeweza kusababisha nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe," Jenerali Burhan aliwambia wanahabari mapema Jumanne. "Waziri mkuu alikuwa nyumbani kwake lakini tulihofia kwamba atadhurika," aliongeza. "Nilikuwa naye jana usiku ... na anaendelea na maisha yake ... atarudi nyumbani kwake wakati mgogoro umekwisha na vitisho vyote vimekwisha."
Jenerali huyo alisema ameuvunja utawala wa kiraia, amewakamata viongozi wa kisiasa na kuitisha hali ya hatari kwani makundi ya kisiasa yamekuwa yakichochea raia dhidi ya vikosi vya usalama.
Mwandishi wa BBC aliyeko Khartoum, Mohamed Osman, anasema ukweli ni kwamba Jenerali Burhan aliandaa orodha ndefu ya mawaziri, pamoja na kuahidi kutangaza uteuzi wa wakuu wa mahakama ndani ya siku mbili, na kupendekeza mipango mingi kabla ya hata mapinduzi.
Mapinduzi hayo yameibua shutuma za kimataifa. Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, ambayo Sudan ni mwanachama, zote zimetaka kuachiliwa mara moja kwa viongozi wote wa kisiasa waliokamatwa ambao ni pamoja na wajumbe wa baraza la mawaziri la Bw. Hamdok.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Sudan ni miongoni mwa "majanga ya mapinduzi" yanayoathiri Afrika na Asia, na akahimiza "madola makubwa" duniani kuungana pamoja "kuzuia ipasavyo" hatua hiyo ya Jeshi Sudan kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo, Marekani imesitisha msaada wa dola $700m (£508m) kwa Sudan huku Umoja wa Ulaya (EU) ikitishia pia kufanya hivyo. Marekani na EU zinataka kurejeshwa kwa serikali ya kiraia bila masharti. Tangu Jumatatu, wanajeshi wanaripotiwa kupita nyumba kwa nyumba mjini Khartoum wakiwakamata waandaaji wa maandamano.
Mwandishi wetu anasema maelfu zaidi ya watu wamejiunga na maandamano katika mji mkuu, haswa katika vitongoji vya makazi karibu na katikati mwa jiji. Uwanja wa ndege wa Khartoum umefungwa na safari zote za ndege zimehairishwa hadi Jumamosi. Wafanyakazi katika benki kuu ya nchi hiyo wameripotiwa kugoma, na madaktari kote Sudan wanasemekana kukataa kufanya kazi katika hospitali zinazosimamiwa na jeshi isipokuwa kama itatokea dharura.
Viongozi wa kiraia na wenzao wa kijeshi wamekuwa katika mzozo tangu mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir alipopinduliwa mwaka 2019.
Makubaliano ya kugawana madaraka kati ya viongozi wa kiraia na kijeshi yaliundwa ili kuielekeza Sudan kwenye demokrasia lakini yamethibitika kuwa tete kutokana na majaribio kadhaa ya awali ya mapinduzi, huku jaribio la mwisho likifanyika zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Jenerali Burhan, ambaye alikuwa mkuu wa baraza la kugawana madaraka, alisema Sudan inathamini na kuheshimu utawala wa kiraia, huku uchaguzi ukipangwa kufanyika Julai 2023.