Ziwa Victoria laongezeka ukubwa na kupoteza fukwe zake

bk
    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Swahili

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa majira ya jioni au mwishoni mwa wiki , kukuta watu wengi wakiranda barabarani pembezoni mwa ziwa.

Mizunguko ya watu hawa si kwamba wanapita kuelekea sehemu nyingine bali ndio wamefika kwa ajili ya mapumziko.

mm

Imebaki ni simulizi tu, pale ambapo mgeni unapofika katika eneo hili unaelezwa namna ambavyo ziwa lilikuwa mbali kutoka ambapo barabara ilipo.

Kauli maarufu inayotumika "Ziwa lilikuwa kule"

Utaambiwa tu zile zilikuwa bembea, pale palikuwa na mgahawa na hapo mbele hoteli na mara kwingine kulikuwa eneo fulani la burudani na sasa hamna kitu, unaona hiyo miti haikuwa ndani ya maji kila kitu kimebadilika.

Sasa zi ziwa, hakuna wageni, magari hayawezi kuegeshwa hapa.

Ni zaidi ya mwaka hali imebadilika.

Ilikuwa kawaida kwa familia kuja kutembea na kufurahi na hata kucheza michezo mbalimbali.

Kwa sasa hatuna fukwe zaidi ni kusimama katika ukuta wa barabara na kuona ziwa.

bk
bk

Bwana William Rutha ambaye ni mdau wa utalii na anamiliki eneo la burudani katika ukingo huo wa ziwa anasema kuongezeka kwa ziwa kumeathiri biashara yake kwa kiwango kikubwa tangu mwaka jana mwezi wa nne mpaka sasa.

"Shughuli za watu kuja kupumzika ufukweni zimepungua maana hakuna mchanga tena, walizoea kuwa na mchanga mweupe zaidi ya hata wa Zanzibar lakini sasa hamna ni maji tu, "William ameeleza.

Aidha ameongeza kusema kuwa utalii umedorora katika eneo hilo si kwasababu ya corona tu bali hata ziwa kuongezeka kumechangia kukosa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Ukiachilia mbali suala la corona, ongezeko la ziwa limezuia wageni kufika katika eneo hilo.

bk

Ivan Rutashobwa kutoka Bukoba anasema alikuwa anafanya biashara ambayo ilikuwa inampa kipato kikubwa, lakini sasa hivi watu hawakai sana.

Alikuwa anauza bisi lakini sasa imembidi abadili biashara maana bisi haiwezi kulipa tena hakuna watu, hakuna watoto wengi.

bk

Miongoni mwa watu waliokuwa wana hoteli hapo ni Bi. Beatrice, imebidi kusitisha biashara yake.

Anasema kusogea kwa maji kulianza tangu mwaka 2018 lakini mwaka 2020 ndio yameongezeka zaidi na sasa imembidi kuanza kutafuta eneo lingine la biashara.

Hatujui sababu zilizopelekea ziwa kuwa kubwa zaidi.

Watu wa mazingira wamesitisha watu kuendelea kufanya biashara eneo hilo.

bk

Fazal Issa ni mtaalamu wa masuala ya tabia nchi na maendeleo endelevu anasema ongezeko la maji katika Ziwa Victoria ni kutokana na ongezeka la mvua nyingi.

Hiki ni kiwango kikubwa zaidi katika rekodi ambazo zimeanza kuwekwa katika tafiti kadhaa.

Ni karibu mita 13.2 zimeongezeka ambacho ni kiwango kikubwa kupimwa tangu mwaka 1964 katika ziwa hilo baada ya kuongezeka kwa kiwango maji mwishoni mwa mwaka na mwanzoni wa mwaka katika kipindi cha mwaka mmoja.

Vilevile inahusisha kuongezeka kwa joto, na hii kwa ujumla ni athari ya mabadiliko ya tabia nchi na si kwa Tanzania tu bali hata duniani kwa ujumla.

Athari zinazojitokeza zinaathiri shughuli za kiuchumi haswa uvuvi, kukosa makazi na kusababisha hata vifo .

Ongezeko la tatizo hili katika Ziwa Victoria si kwa upande wa Tanzania pekee bali katika eneo zima ambalo ziwa hili limezunguka.