Rais Filipe Nyusi atembelea eneo ambalo wanajeshi wanakabiliana na Islamic State Msumbiji

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ametembelea jimbo la kaskazini la Cabo Delgado eneo ambalo wanajeshi wanapigana na wanamgambo wa kiislamu.
Mapema wiki hii, iliripotiwa kuwa wanamgambo hao wameivamia bandari kuu ya Mocimboa da Praia na hadi sasa bado wanasisitiza kuwa ipo chini ya himaya yao.
Jeshi linadaiwa kuwa lililazimika kusalimu amri baada ya kuishiwa na risasi.
Bwana Nyusi anatembelea jimbo la Pemba, eneo ambalo liko umbali wa mamia ya kilomita kutoka kitovu cha mapigano.
Alisema wapiganaji ambao wanahusishwa na kundi la kigaidi la Islamic State 'IS' hawajatoa tishio lolote dhidi ya jitihada za kimataifa kuharibu gesi iliyohifadhiwa.
Ingawa waasi hao wanaonekana kuingia nchini humo kwa kasi na kufanya usalama wa taifa la Msumbiji kuwa mashakani.
Taarifa kuhusu kile kinachoendela Mocimboa da Praia ni vigumu kubaini kwani barabara, umeme na mitambo ya simu imekatwa.
Kuna ushaidi unaodai kuwa waasi hao wana silaha za uhakika na wana nia mathubuti kufanikisha lengo lao.
Wanamgambo wanaofahamika kama al-Shabab, au vijana - ambao wana ajenda ya kiislamu, lakini kwa miongo wamejengwa na ukosefu wa miundo mbinu, ukosefu wa ajira, uchaguzi usio wa haki, rushwa na migogoro.
Siku ya Jumatano Msumbiji ilisema kuwa vikosi vyake vinapigana kuchukua udhibiti wa bandari hiyo baada ya taarifa kadhaa kudai kwamba imetekwa na wanamgambo wa Islamic State Jumatano.
Mji huo uko karibu na miradi ya gesi asili yenye thamani ya dola bilioni 60.
Jeshi limesema kuwa hatua imechukuliwa kukabiliana na kundi hilo ambalo limekuwa likitumia wenyeji kama ngao yao.
Hatua hiyo inafuatia mapigano ya siku kadhaa ya kutaka kuchukua bandari hiyo yenye utajiri wa gesi eneo la kaskazini.
Msumbiji ni kituo cha wanamgambo wa IS?
Mwandishi wa BBC Africa Andrew Harding amesema kuwa kutekwa kwa bandari hiyo ni pigo kubwa kwa jeshi la Msumbiji, ambalo lina wakati mgumu kudhibiti ukuaji wa makundi ya waasi katika eneo hilo la utajiri wa mafuta la Cabo Delgado.
Bandari ya Mocimboa da Praia inatumiwa kwa uwasilishaji wa mizigo kwa miradi ya eneo la pwani takribani umbali wa kilomita 60 (maili 40), ambayo inaendelezwa na kampuni kubwa za mafuta duniani ikiwemo Total.
Wanamgambo - wenye kuhusishwa na kundi la Islamic State - wamekuwa wakitwaa miji kadhaa ya kaskazini katika miezi ya hivi karibuni, na kulazimisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao.
Hili lilikuwa moja ya mashambulizi kadhaa katika bandari ya Mocimboa da Praia mwaka huu.
Tanzania pia imesema itafanya mashambulio dhidi ya wanamgambo wa jihadi katika misitu karibu na mpaka na Msumbiji.

Chanzo cha picha, EPA
Udhaifu uliojitokeza
Uchambuzi wa Andrew Harding, Mwanahabari wa BBC Africa
Vikosi vya ulinzi vya Msumbiji vimeendelea kusisitiza kwamba mapigano ya kutaka kukomboa bandari ya Mocimboa da Praia bado yanaendelea.
Lakini matukio ya wiki zilizopita yameonesha udhaifu uliopo ndani ya jeshi na jinsi waasi wa kiislamu wanavyoendelea kujiimarisha ambako sasa kunajitokeza na kuonyesha vile kunavyoweza kuwa tishio kubwa la eneo hilo.
Taarifa mbalimbali zinaashiria kwamba vikosi vya serikali vilikuwa vimelazimika kusalimu amri baada ya kuishiwa na silaha.
Wanajeshi kadhaa inasemekana kwamba wameuawa na boti lililokuwa linashika doria likazamishwa.
Miezi ya karibuni, waasi wameteka miji kadhaa ya eneo, kiasi fulani inaonekana kuwa propaganda.
Baadhi ya kampuni kubwa duniani za nishati sasa zinataka ulinzi zaidi wakati zinajitayarisha kuanza kuzalisha mafuta katika visima vilivyo pwani ya Msumbiji.
Aidha, serikali imetafuta usaidizi kutoka kwa wanakandarasi wa usalama wa kimataifa. Lakini hadi kufikia sasa, inaonekana haiko tayari kugeukia nchi jirani kutafuta usaidizi wa kijeshi.
Mashambulio eneo la kaskazini mwa Cabo Delgado, yalianza 2017, lakini yakaongezeka mwaka huu baada ya kundi la Ahlu Sunnah Wa-Jama, Kukiri kuhusika na mashambulizi, kudai kuwa na ushirikiano na lile la IS.
Mapema wiki hii kundi la IS lilidai kwamba limetwaa kambi mbili za jeshi karibu na bandari ya Mocimboa da Praia, ambapo wanajeshi kadhaa wa Msumbiji waliuawa na silaha zao kuchukuliwa ikiwemo, bunduki za rashasha na guruneti zilizorushwa kwa makombora.












