Mtazamo: Maisha yakoje kwa raia Mwafrika anayeishi Marekani ?

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati maandamano yanapoendelea kutanda Marekani kwasababu ya kifo cha raia mweusi wa George Floyd akiwa mikononi mwa polisi, mwanahabari wa Kenya Larry Madowo ameandika kuhusu ubaguzi ambao ameshuhudia nchini humo.
Wiki yangu ya kwanza mji wa New York msimu uliopita, nilialikwa chakula cha jioni katika nyumba ya rafiki yangu huko Upper West Side.
Nilinunua matunda ya kumpelekea na nikafika kwenye jengo analoishi nikiwa nimebeba mfuko wa plastiki.
Wahudumu wa eneo hilo mlangoni wakanionesha njia ya nyuma ya jengo ambapo ni lazima upitie eneo la kutupa takataka ambalo lilikuwa chafu kupita kiasi.
Baada ya kumaliza kupanda ngazi, mwenyeji wangu alifungua mlango na kuonesha kuwa mwenye aibu, uso wake ulikua umebadilika rangi.

Chanzo cha picha, Larry Madowo
"Bawabu ni mbaguzi alifikiria kwamba wewe ni mhudumu wa kuwasilisha bidhaa na hivyo basi akakuruhusu kuingia kupitia mlango wa nyuma," akaelezea wakati anaomba msamaha.
Nimefanyakazi katika nchi zenye ubaguzi wa rangi wa hali ya juu kama Afrika Kusini na Uingereza na nimesafiri maeneo mbalimbali duniani lakini bado inahuzunisha kuona kwamba Mmarekani hakufikiria kuwa mzungu kama rafiki yangu na mume wake wanaweza kuwa na miadi ya chakula cha jioni na mtu mweusi.
Tukio hilo liliniandaa kwamba Marekani inaweza kuwa nchi yenye fursa kwa wengi lakini pia inaweza kunidhalilisha kiasi cha kunibagua kirangi na kuniona nisie na thamani.
Haikujalisha kama ninatoka kwenye taifa ambalo wengi wao ni watu weusi, watu wanaofanana na mimi hapa, wanahitajika kufikiria mara mbili kwa utu wao dhidi ya mfumo ambao mara nyingi unawatenga, kuwaondoa na kuwaadhibu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchini Kenya, naweza kutokomea kwenye kundi la watu wengi lakini Marekani, mara nyingi huwa ni mlengwa kwasababu ya rangi yangu nyeusi.
Siku moja baada ya kampuni ya uwekezaji kumfuta kazi Amy Cooper kwa kuita polisi kwasababu mtu mweusi alimtaka kufuata sheria za kwenye bustani na kumfunga mbwa wake, polisi mzungu alipiga magoti juu ya shingo ya George Floyd kwa kipindi kirefu na hatimaye akasababisha kifo chake.
Ilinisikitisha na kunivunja moyo mno.
Wakati maandamano yalipotokea kote nchini Marekani na kudai haki kwasababu ya mauaji ya Floyd, na watu wengine weusi ambao wameuawa na polisi, nilizuia pumzi kidogo, nikatafakari.
Nawezaje kuanza kuomboleza mtu ambaye hata sikuwa ninamfahamu?, Naweza kuwa na machungu ambayo hata sikutarajia, kama mwafrika ambaye tu ndo nilikuwa ninaaza kuishi Marekani? Nilianza kufikiria ikiwa ningeweza kumudu kama ningekuwa raia mweusi wa Marekani katika hali hiyo.
Kisha nikaona video inayoonesha waandamanaji katika ufukwe wa California, ikionesha bayana dhamira yao.
"Namna nzuri ambayo raia Waafrika nchini Marekani wanaweza kuwasaidia Wamarekani wenye asili ya Afrika ni kuwaunga mkono na kuelewa kwamba sote ni sawa," alisema mmoja ambaye alikuwa ameandamana.
Nilimuuliza Tom Gitaa - mwandishi ya gazeti la Mshale, ambalo linalenga wahamiaji wa Afrika eneo la Midwest Marekani - maoni yake kuhusiana na maandamano hayo, uharibu na uporaji wa mali ambao umetokea katika mji wa Minneapolis.
"Wengi wetu hatukukua tukiwa na ufahamu wa masuala ya haki za kiraia barani Afrika na hivyo basi wakati mwengine ufahamu wetu huwa haupo.
"Lakini kwa masuala kama mateso na unyama unaotekelezwa na polisi na unyanyapaa makazini, vinafanana na kile ambacho raia weusi wa Marekani wamekuwa wakikabiliana nacho kwa miaka kadhaa," amesema Bwana Gitaa, ambaye alihamia Marekani kutoka Afrika Mashariki miaka takriban 30 iliyopita na ambaye msichana wake, 24, raia wa Marekani amekuwa miongoni mwa wanoapaza sauti kupitia maandamano hayo barabarani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kila wakati kumekuwa na wasiwasi kati ya Waafrika na raia weusi wa Marekani.
Rafiki yangu Karen Attiah, na mimi tulizungumzia suala hili miaka miwili iliyopita katika gazeti la The Washington Post pale filamu inayomuangazia shujaa raia mweusi ya Black Panther ilipotoka.
Ni mhariri wa makala ya Global Opinions, gazeti la The Washington Post, binti ya mhamiaji mweusi - aliyezaliwa Marekani lakini ambaye ana uhusiano wa karibu sana na bara ambalo ndo chimbuko la wazazi wake.
Taarifa zaidi kuhusu kifo cha Floyd:
- Mwanamichezo, rafiki na baba - George Floyd alikuwa nani?
- Sababu 3 zinazoonesha watu weusi hubaguliwa Marekani
- Tunafahamu nini kuhusu maafisa 4 wa polisi waliohusishwa na kifo cha George Floyd?
- Maandamano yaendelea usiku kucha Marekani kufuatia kifo cha George Floyd
- Ulimwengu unasema nini kuhusu maandamano Marekani?
Karen aliniamba kwamba wazazi wake kwa sasa wanajadiliana masuala la ubaguzi wa rangi hasa kwa namna ambayo yeye na ndugu zake hawakuwahi kusikia mijadala hiyo wakati wanakua.
"Nafikiri tulikuwa tunahitajika kutokaribia na raia weusi wa Marekani kwasababu tulikuwa wahamiaji, tulikuwa tofauti," aliniambia wiki hii.
"Lakini sasa hivi tunaelewa kwamba ikiwa polisi ataona rangi ya ngozi yako, hatauliza ikiwa wewe ni umetoka Ghana, Nigeria au Zimbambwe, au Atlanta ama kusini mwa Dallas, kwao wao wameona tu mtu mweusi."
Wasani wa Afrika kama vile Lupita Nyong'o na mchekeshaji Trevor Noah wanatumia majukwaa yao yenye ushawishi kuunga mkono maandamano ya haki na kuonyesha wanafiki katika baadhi ya wanaokosoa maaandamano.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Umoja wa Afrika (AU) pia nao ulitoa taarifa isiyo ya kawaida kushtumu mauaji ya Flyod na kutaka serikali ya Marekani kuhakikisha inatokomeza aina yoyote ile ya ubaguzi.
Raia wa kwanza waliwasili Marekani kama watumwa - katika eneo la Virginia lililotawaliwa na Uingereza - miaka 401 iliyopita.

Mwaka jana, baadhi ya familia zao walirejea Afrika kuadhimisha "Mwaka wa Kurejea" pale ambapo mababu zao waliibwa karne nne zilizopita.
Moja ya matamasha lilikuwa lile la Afrochella lililofanyika nchini Ghana Desemba mwaka jana wazo la Abdul Karim Abdullah.
Nilipomuita, alikuwa ndio ana lala baada ya kutokea kwa maandamano makubwa usiku eneo analoishi la Bronx mjini New York.
"Waafrika wengi wanapuuza ukweli wa kwamba hivi pia ni vita vyao," alisema.
"Ukosefu wa haki kwa watu weusi popote pale ni ukosefu wa haki. Tunastahili kushirikiana na kupigana vita hii pamoja."
Waafrika walio nchini Marekani pia nao wameandamana pamoja na wengine katika vuguvugu la Maisha ya Watu Weusi pia ni Muhimu, wakiunga mkono maandamano dhidi ya wazungu, wakachanga pesa kwa ajili ya kupatikana kwa haki na kuandaa matukio yao wenyewe kuonesha umoja katika jamii ya watu weusi.
Waandamanaji waliokuwa wamejifunga bendera za nchi zao pia nao wametambuliwa kushiriki kwenye maandamano katika maeneo mbalimbali Marekani.
"Watu wengine, hasa raia weusi ndio ambao kwa kiwango kikubwa wanateswa, hawathaminiwi na kutoeleweka katika dunia hii," Jada Walker amesema hivyo akiwa anatiririkwa na machozi mbele ya kundi la waandamanaji katika ukumbi wa Dallas, Texas.
Alikuwa na wasiwasi kuhusu kile kinachomsubiri mpwa wake wa miaka miwili mwenye mahitaji maalum atakapokua.
Kwasababu ya historia ya kutokea kwa ghasia ambayo imekuwa ikiendelea kati ya raia weusi na wazungu, mara myingi wazazi huwa katika njia panda.
Ifrah Udgoon, mzaliwa wa Somalia mwalimu wa sayansi huko Columbus, Ohio, anaishi akiwa na hofu hiyo kwa kijana wake, 13.
"Kila siku inayopita unaona ukweli wa kwamba karibu kama haijafika tayari, ataacha kuonekana kama mzuri na mtanashati na kugeuka kuwa tishio. Aliandika katika gazeti la Mail & Guardian Afrika Kusini.
Bi Udgoon anakabiliana na vita kama wahamiaji wengine wengi: "Nikiwa hapa natarajiwa kuwa na shukrani. Lakini niliuza nafsi yangu kwa shetani?"
Bwana Abdullah anachukulia Afrochella kama jukwaa la mtandaoni la kuunganisha Waafrika weusi wanaokabiliana na vikwazo kama hivyo.
"Niliwasiliana na rafiki zangu kutoka Haiti, Benin na wale wa taifa la St Vincent and the Grenadines kwasababu ubaguzi hauna utaifa. Mfumo huu wa ubaguzi unatuathiri sote.
"Kwa kipindi kirefu, sikuweza kutambua kwamba huu ni ukosefu wa haki hadi nilipoanza kuelewa lugha yenyewe. Vita hii ni vita yangu." Bwana Abdullah amesema.
Sio kwamba ni vita tu ya raia weusi Marekani kama yeye, ni vita ya haki ya kuwa mweusi na salama nchini Marekani.
Haya hapa tena maneno ya Karen kwasababu yalikuwa na hitimisho thabiti: "Nafikiri kile kinachoonekana sasa ni kupinga maandamano ya weusi na hilo linahamasisha ufahamu wa ushirikiano katika changamoto nyingi ingawa sio sawa lakini zote zinaendana."













