Mpiga picha aliyepitia madhila ya vita anayeamini atawapata wazazi wake baada ya miaka 20

- Author, Faith Sudi
- Nafasi, BBC Swahili
Patience Dositha mwanzilishi wa Abled Photography jina ambalo analitumia kwa biashara yake ya upigaji picha, anaelezea simulizi ya mkono wake wa kushoto uliokatwa alipokuwa na umri wa miezi mitatu.
Msichana huyu mwenye miaka 22 alikuwa muathirika wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) mwaka wa 1997.
Mama aliyemnusuru alimwambia Patience kwamba wakati yeye na mumewe walikuwa wakitoroka vita na kupita walikokuwa wamelala wazazi wake ambao walishambuliwa na kuachwa wakiwa hali mahututi, baba yake Patience alimvuta mguu mama huyo na kumwomba amchukue mwanawe watoroke naye kuelekea Rwanda.
Ombi ambalo aliliitikia.
Walipokuwa katika harakati za kutoroka, sauti ya kilio cha Patience kutokana na jeraha la mkono wake ilifichua maskani waliokuwa wamejificha na kusababisha wao kupatikana na wapiganaji.
Lakini mumewe akaamua kuwanusuru na kumuamuru mkewe atoroke na Patience na yeye akasalia nyuma kuwazubaisha wapiganaji.
Hadi kufikia leo, hawajawahi kumuona tena.
"Alinichukua kama mtoto wake na alinipenda zaidi, Mimi ndiye nilikuwa kitinda mimba," hata hivyo masaibu ya Patience yalianza sambamba na alivyokua.
Dada zake walianza kumdhulumu na kumlaumu kwa kifo cha baba yao.
"Nyumbani maisha hayakuwa rahisi. Ingawa mama alinipenda, dada zangu walikuwa wakinitesa. Kila mara walinisuta kwamba mimi si mwenzao, waliniita muuaji, kwamba mimi nilimuua baba yao."
Dhuluma zilipoendelea, ndivyo Patience aliendelea kuwa na maswali ambayo yalitaka majibu.
"Ilifika wakati nilitaka kujua ukweli. Kila mara nilimuuliza mama yangu kwa nini mimi sifanani na dada zangu? Kwa nini wanasema eti mimi nilimuua baba? Kwa nini?... Mama alinijibu kwamba nisisikilize wanayoniambia, na kuwa mimi ndiye kitinda mimba wake.''
Mama aliwaadhibu na kuwakanya.

Mwaka wa 2015, mama yake Patience aliugua kwa muda kisha akaaga dunia. Patience kama maana ya jina lake, alilazimika kuvumilia mateso kutoka kwa ndugu zake ili aweze kukamilisha masomo yake kidato cha sita.
Patience anaamini kwamba wazazi wake halisi walinusurika na anatumai kwamba siku moja atakutana nao.
"Kila mara walikuwa wakinitukana kwamba mimi ni mchawi, nimesababisha vifo vya wazazi wao. Yote niliyavumilia, na baada ya kukamilisha mtihani wangu wa mwisho, nikaondoka"
Patience alijaribu kuvuka mpaka ili kurejea katika taifa lake la kuzaliwa, DRC, lakini akazuiliwa na maafisa uhamiaji mpakani kwa kukosa stakabadhi za kuonesha kwamba yeye ni raia wa DRC.
Msichana huyu ambaye alikuwa yatima kwa mara ya pili alikata matumaini ya kurejea kwao, na hivyo aliamua kupiga kambi kwenye ufuo wa ziwa Kivu.
" Niliishi ufuoni kwa muda wa wiki mbili. Mchana ningejaribu kujitafutia chakula na kucheza majini, kisha wakati wa usiku nilichimba mchanga na kujifinika nao mwili mzima isipokuwa pua pekee. Nilifanya hivyo ili kujikinga dhidi ya baridi na kuvamiwa", anaeleza Patience huku akisitasita kwa uchungu.
"Siku moja nikiwa katika pilika pilika zangu ufuoni, nilikutana na jirani yetu ambaye huendesha lori la kupakia mizigo. Nikamuelezea kuhusu niliyoyapitia na kumuomba aje nami nchini Kenya jijini Nairobi kwa sababu nilikuwa na kiu ya kuanza maisha mapya".
Rwanda iligeuka na kuwa kama mwiba moyoni kwangu kwa sababu ya kumbukumbu niliyokuwa nayo, naye akakubali.
Safari ya kenya
Ni safari ambayo pia ilikuwa na changamoto zake. Patience alilazimika kujificha ndani ya mizigo punde walipokaribia mipaka.
Na baada ya wao kuvuka, alirudi kuketi na dereva. Baada ya siku 9, walifika nchini Kenya na akaachwa mjini Kikuyu.
"Alinipa dola tano na akaniambia kwamba hawezi kunipeleka Nairobi kwa kuwa sina stakabadhi na polisi huwakamata raia wa kigeni wasiokuwa na stakabadhi. Kwa hivyo nililazimika kuishi katika mji huo wa Kikuyu.''

Mjini Kikuyu, alilazimika kuishi mitaani na huko alikutana na jamii iliyomkubali.
Na japo hakuwa na pa kulala wala makazi, Patience alihisi upendo.
"Maisha ya mitaani hayakuwa rahisi, ijapokuwa nilikutana na ndugu walionikubali. Walinisaidia na jinsi ambavyo ningeishi mitaani kama msichana. Walininyoa nywele, na kunifunga matiti kwa vitambara. Tulifanya hivyo ili kujilinda dhidi ya kubakwa. Kwa sababu bila matiti na nywele tulionekana wavulana. Walinifunza pia kuzungumza kiswahili."
Sawa na msemo lugha hukutanisha watu, Patience alimfuata mtu mmoja baada ya kumsikia akizungumza Kinyarwanda kwenye simu.
Alimuelezea masaibu aliyokumbana nayo na jinsi alivyoanza kuishi mitaani. Baada ya simulizi yake, mtu huyo akampatia makao.
"Alikuwa anaishi chumba kimoja, mkewe na watoto wao wanane. Kupata chakula ilikuwa shida kupata, kulala pia tulifinyana lakini hapo kulikuwa bora kuliko mitaani"
Simu ilivyobadilisha maisha yangu
Baada ya kupata makao nyumbani, aliamua kuitafutia roho yake makao. Na kila siku alipokamilisha kazi za nyumba, alienda kanisani. Na hapo mwanga ukang'aa.
"Kuna siku nikiwa kanisani, moyo wangu ulikuwa unaniuma sana na nilikuwa namuuliza Mungu maswali huku nikilia sana. Kasisi akanipata nikilia na aliponiuliza nini kinanisumbua, nikamuelezea mapito yangu. Akaniambia kwamba atakuwa ananipa fedha kidogo za kunisitiri. Kuanzia siku hiyo akawa ananipa dola 2 kila siku. Fedha hiyo ilitusaidia sana kununua chakula na kukimu mahitaji mengine."
Hatimaye kasisi huyo alimnunulia Patience simu ili waweze kuwasiliana wakati aliposafiri na pia kumuwezesha kutuma fedha za matumizi kama alivyoahidi. Simu hiyo ilibadilisha maisha ya Patience.
"Nilitumia simu hiyo kutafutia mashirika yanayowasaidia wakimbizi kwenye mitandao ya kijamii, na hapo ndipo nilikutana na Shirika la kimataifa kushughulikia wakimbizi (IRC). Shirika hilo lilinichukua na kunipeleka chuoni ambapo nilisomea Sanaa ya upigaji picha"
Na kama wasemavyo wenye busara, baada ya dhiki, faraja. Patience alikamilisha masomo yake na hata kufungua studio ya kupiga picha.
" Watu wengi hushuku kama ninaweza kupiga picha kwa sababu wanaona kwamba nina mkono mmoja. Lakini ninapowashawishi na kuwapiga picha, wao hubadili msimamo na kuwa wateja wa kila siku"
"Niliamua kusomea sanaa hii kwa sababu ninaamini kwamba itanifanya kutambulika dunia nzima na hatimaye kukutana na wazazi wangu"
Patience hajakata tamaa na anaamini kwamba wazazi wake walinusurika na anatumai kwamba siku moja atakutana nao.














