Wasichana na wanaume 22 wanaodaiwa kufanya biashara ya ngono na ushoga wahukumiwa

- Author, Na Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
Mahakama ya Mwanzo Nunge manispaa ya Morogoro nchini Tanzania imewahukumu watu 22 kifungo cha miezi sita jela baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la uzembe na uzururaji, limeripoti gazeti la Mwananchi nchini humo.
Baada ya hakimu Emelia Mwambagi kusoma hukumu hiyo, washtakiwa hao ambao wengi ni wanawake waliangua kilio mahakamani, kuomba kusamehewa.
Kesi hiyo ilisikilizwa jana Jumatano kwa zaidi ya saa tano dhidi ya wasichana wanaodaiwa kufanya biashara ya ngono pamoja na wanaume wanaodaiwa kujihusisha na ushoga.
Washtakiwa hao walikamatwa usiku wa Agosti 16, 2019 eneo la Kahumba manispaa ya Morogoro.
Hakimu Mwambagi aliieleza mahakama hiyo kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa washtakiwa hao na wengine wanaotumia miili yao kujidhalilisha na kuwadhalilisha wazazi, ndugu na jamaa kwenye maeneo wanayotoka.
Hakimu Mwambagi aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wote waliokamatwa ni vijana wenye uwezo wa kufanya kazi za kuwaingizia kipato halali lakini wamekuwa wakizurura na wengine wakitumia vibaya miili yao.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo hakimu Mwambagi aliwaachia huru washtakiwa sita kutokana na utetezi wao pia vielelezo walivyoviwasilisha mahakamani hapo kudhihirisha kuwa hawahusiki na shtaka hilo.
Katika utetezi wao washtakiwa hao walidai walikamatwa kwenye nyumba za kulala wageni walipokwenda kujipumzisha baada ya kutoka safari, huku wengine wakidai kukamatwa katika maeneo yao ya kazi wakidai kuwa wanajihusisha na biashara ya kuuza chakula.
Changamoto za kuzuwia biashara ya ukahaba

Chanzo cha picha, AFP
Suala la kuzuwia biashara ya ukahaba limekuwa na utata mkubwa miongoni mwa mataifa ya kiafrika kutokana na madai kwamba wengi wanaojiingiza katika biashara hii wanadai kuwa wameamua kufanya ukahaba kutokana na ugumu wa maisha. Wanadai wanauza miili yao ili kupata pesa za kujitunza na kuzitunza familia zao ambazo hazina uwezo wa kiuchumi.
Mataifa mengi ya kiafrika hayana mpango kabambe wa kukabiliana na biashara hii, hali inayosababisha idadi ya wanawake na wanaume wanaoingia mitaani kujiuza kuongezeka kila uchao.
Hivi karibuni maafisa katika mji mkuu wa Ethiopia Adis Ababa walitangaza kuwa wanapanga mkakati wa kupiga marufuku ukahaba na kuombaomba wa mitaani , ikiwa ni hatua ya hivi karibuni katika msururu wa hatua za kusafisha sura ya taifa.

Chanzo cha picha, PA
Nchi hiyo imeanda muswada unaoonyesha wa sheria ambao uko mbioni kukamilika.
Afisa habari wa Meya wa Mji wa Adis Ababa Feven Teshome, aliliambia shirika la habari la AFP alisema marufuku hiyo ni muhimu ili kupambana na "matatizo ya kijamii " katika mji huo wenye zaidi ya watu milioni moja.
Hata hivyo baadhi ya raia wa Ethiopia walilalamikia marufuku hiyo dhidi ya makahaba na ombaomba jini Adis Ababa:
''Kusema kweli marufuku marufuku ingetolewa baada ya utafiti kufanyika, hakuna sheria inayozuwia ukahaba na ombaomba...hala fu jiji la Adis Ababa halikufanya matayarisho ya kukabiliana suala hili kabla hata ya kuandaa marufuku hii... kuna sababu nyingi zinazomfanya mwanamke awe kahaba hasa matatizo ya kiuchumi, hivyo mwanamke anapaswa kuwezeshwa ili asifanye biashara ya ukahaba'' amesema wakili mjini Adis Ababa Seble Assefa.
Ukahaba ni kazi zenye malipo mazuri , jambo linazowafanya zoezi la kuwaondosha mitaani kuwa gumu katika miji na vitongoji mbali mbali vya mataifa ya Afrika.
Inadaiwa kuwa makahaba wanaweza kupata mapato ya juu zaidi kuliko mishahara ya kawaida ya wafanyakazi wa umma.

Nchini Kenya makahaba wamekuwa wakisistiza biashara ya ukahaba ihalalishwe.
Mwaka 2013 waliandamana kulalamikia kile wanachosema ni unyanyasaji wanaofanyiwa na polisi pamoja na askari wa baraza la jiji wakati wakiendesha biashara zao.
Walikusanyika katikati ya mji na kuelekea katika ofisi za baraza la jiji kuwasilisha malalamiko yao wakisema kuwa wamechoka kuhangaishwa na polisi na wanataka ulinzi.
Mwanaharakati wa maswala ya biashara ya ngono, John Mathenge aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji, alisema kuwa wengi wao wameuawa na kunyanyaswa hata na wateja wao pamoja na maafisa wa usalama.
Biashara ya ngono ni haramu nchini Kenya lakini baadhi ya watetezi wa makahaba wanasema kuwa katiba haijaeleza bayana ikiwa mtu atakayekamatwa akijihusisha na biashara hiyo achukuliwe hatua gani za kisheria.
Mathenge alielezea kuwa lazima watu wakome kuwabagua wanaofanya biashara ya ngono, kwani ni kazi kama kazi nyingine tu.
Wengi walilalamika kuwa jamii imepuuza watu wanaofanya biashara ya ngono wala haiwatetei wakati wanaponyanyaswa au kuuawa .
Ripoyi iliyotolewa mwaka jana kuhusu makahaba mjini Nairobi ilisema kuwa wanahangaiswa sana na askari wa baraza la jiji na kuwa wengi wao huachiliwa tu pindi wanapotoa rushwa.akahaba mjini Nairobi Kenya waliungana na wenzao duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga unyanyasaji dhidi yao.
Inakadiriwa kuwa kuna idadi kubwa ya makahaba nchini Tanzania, kinachosubiriwa ni kuona kuwa adhabu iliyotolewa kwa wanaume na wasichana 22 mkoani morogoro, itakuwa ni fundisho kwa makahaba wengine nchini Tanzani kama ilivyodaiwa na Hakimu Emelia Mwambagi au la.













