WHO yatoa tahadhari ya dawa bandia Kenya, Uganda

Augmentin

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pichani ni dawa halisi za Augumentin, nchini Kenya na Uganda kumeripotiwa dawa feki zinazokopi jina la Augumentin.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya wananchi wa Kenya kuwa waangalifu dhidi ya dawa bandia ya kiua vijasumu (antibiotic) nchini humo.

Kiua vijasumu aina ya Augmentin, dawa ambayo hutumika dhidi ya maambukizi ya vijidudu ni moja ya dawa imeorodheshwa na WHO kama moja ya dawa za msingi na inapatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa.

Katika taarifa yake kwa umma, WHO imesema makasha ya dawa bandia ina muonekano unaokaribiana na dawa halisi inayotengenezwana kampuni ya GlaxoSmithKline (GSK).

Dawa hizo bandia zilibainika katika utafiti wa kawaida wa hali ya soko ambao hukagua ubora wa dawa ikiwemo viua vijasumu zinazouzwa kwa wagonjwa.

Vipimo kwenye maabara maalumu za kudhibiti ubora vilionesha baadhi ya dawa hizo hazikuwa na viungo muhimu vinavyohitajika na vilivyoorodheshwa kwemye makasha.

Pia kulikuwa na makosa kwenye upakiaji na maandisi ya dawa hizo.

Kampuni ya GlaxoSmithKline imekanusha vikali kuhusika na uzalishwaji wa dawa hizo bandia.

Dawa hizo bandia pia inasemekana zipo sokoni nchini Uganda.

Hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa kutokea na WHO mpaka sasa.

Tayari nambari za utambulisho za dawa hizo feki zimeshatolewa, na WHO pia imewataka wale wote watakaogundua kuwa walitumia dawa hizo kwenda kwa daktari na kisha kuripoti katika Wizara ya Afya ya Kenya au Uganda.

Hii ni mara ya pili kwa WHO kutoa tahadhari juu tembe bandia za Augmentin barani Afrika.

Tahadhari ya kwanza juu ya uwepo wa dawa hizo bandia ilitolewa Machi 2.

Viua vijsumu ni dawa muhimu katika afya na kukabiliana na magonjwa mbalimbali, lakini baadhi ya dawa hizo hutumika vibaya, kiasi cha kuzua hofu ya kutengenezeka kwa usugu wa dawa hizo kwa baadhi ya watumiaji. Hali hiyo inamaanisha kuwa wale wote watakaopata usugu hawatapa afueni ya maradhi yao hata wakizitumia kwa kiasi gani.