Roman Abramovich: Rabi achunguzwa juu ya uraia wa Ureno aliotoa kwa Abramovich

Rabi ambaye alimsaidia bilionea wa Urusi Roman Abramovich kupata uraia wa Ureno ameambiwa hawezi kuondoka Ureno na lazima ajitokeze kwa mamlaka inapohitajika.

Daniel Litvak alikamatwa siku ya Alhamisi kama sehemu ya uchunguzi kuhusu namna uraia ulivyotolewa.

Mchakato wa uraia wa watu kadhaa wa Kiyahudi unachunguzwa.

Siku ya Ijumaa, Bw Abramovich aliwekewa vikwazo na Uingereza kutokana na hatua ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Bw Abramovich, 55, ndiye mmiliki wa Chelsea FC na ni mmoja wa viongozi saba waliowekewa vikwazo vipya, ikiwa ni pamoja na kuzuiawa kwa mali zao na marufuku ya kusafiri.

Ligi ya Primia imemnyima sifa ya kuwa mkurugenzi wa klabu hiyo.

Mengi zaidi unayoweza kusoma

Bw Abramovich alipewa uraia wa Ureno mnamo Aprili mwaka 2021 chini ya sheria ambayo ilitoa uraia kwa wazawa wa Wayahudi wa Sephardic, ambao walifukuzwa kutoka peninsula ya Iberia zaidi ya miaka 400 iliyopita.

Waombaji wa uraia wa Ureno kupitia njia hii hutathminiwa na wataalamu katika mojawapo ya jumuiya za Kiyahudi za Ureno huko Lisbon au Porto. Bw Litvak ndiye rabi wa jumuiya ya Porto (kaskazini mwa Ureno) na alikuwa na jukumu la kutathmini ombi la Bw Abramovich.

Bw Litvak alikamatwa na mamlaka alipokuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Israel. Aliombwa kukabidhi hati yake ya kusafiria na itabidi ajisalimishe mara kwa mara kwa mamlaka.

Polisi wa Mahakama ya Ureno na mwendesha mashtaka wa umma walisema Ijumaa kwamba kulikuwa na tuhuma za utapeli wa pesa, ufisadi, ulaghai na kughushi hati katika mchakato wa kutoa uraia kwa vizazi vya Wayahudi wa Sephardic.

Jumuiya ya Wayahudi ya Porto imekanusha kufanya makosa yoyote na kusema ilikuwa lengo la kampeni chafu. Waliongeza kuwa Bw Litvak alisimamia idara inayotoa uthibitisho wa urithi wa Kiyahudi wa Sephardic na vigezo vinavyotumiwa kumpa mtu uraia wa Ureno "vimekubaliwa na serikali zilizofuata".