Lionel Messi: Ataongeza ukali wa safu ya ushambuliaji ya PSG na kuwa bora katika karne ya 21?

Chanzo cha picha, Getty Images
Linaweza kuwa jambo la kufikirika zaidi kwa wapenda soka, lakini ukweli ni kwamba, Lionel Messi ameondoka Barcelona na kutua PSG, uhamisho uliofahamika toka wiki iliyopita, ambapo sasa atavaa jezi za klabu nyingine tofauti na Barcelona aliyodumu nayo kwa miaka 21.
Kwa miaka mingi, Vilabu vikubwa Ulaya vimekuwa na ndoto kubwa ya kumsajili Messi, lakini suala la fedha limekuwa mtihani na kikwazo kikubwa cha kunasa saini yake. Hata bila ada ya uhamisho, ni klabu chache sana tajiri zingeweza kumsajili. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 sasa ametambulishwa rasmi kama mchezaji halali wa PSG kwa mkataba wa miaka miwili.
Messi ametua PSG, kujiunga na nyota mwenzake wa zamani wa Barcelona Neymar, pamoja na nyota anayekuja kwa kasi, Kylian Mbappe, anayetajwa kumrithi Messi kama mchezaji bora wa dunia ajaye wa soka.
Messi ataleta kitu gani kwenye kikosi cha PSG?
Kuwasili kwa Messi kutamfanya kocha wa PSG Mauricio Pochettino, kuwa na machaguo ya kutosha hasa wachezaji wanaocheza mbele. Wapo wanaojiuliza kukaa muda mrefu ndani ya PSG, kutaathiri kiwango cha Messi Barcelona?
Urafiki wake na Neymar uko wazi na unajulikana, lakini hatua ya Neymar kujiunga na PSG mwaka 2017 kunatajwa kuwa kulitokana na kukimbia kivuli cha Messi ndani ya Barcelona.
Lakini sasa uwepo wa Messi, Neymar na nyota wengine kama Angel di Maria na Mauro Icardi unaleta uwiano unaosubiriwa na wengi kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu na mashindano mengine Ulaya.
Lakini Messi amekuwa akicheza kama namba tisa ya kuvizia akiwa Barcelona kwa miaka mingi, na uwezo wake akishuka katikati ya uwanja kunatengeza nafasi kwa Neymar na Mbappe kunufaika , hivyo Pochettino anaweza kumtumia kwenye nafasi hiyo. Kwa miaka ya hivi karibuni pale Camp Nou, amekuwa akicheza upande wa kulia zaidi.
Mtu muhimu zaidi katika utatu wao ni uwepo wa Neymar. Uwepo wake na ufungaji wake wa magoli, unaonekana kushuka kwa miaka minne aliyokipiga kwenye ligi kuu ya Ufaransa (Ligue 1, akitoka kufunga magoli 19 na kutoa pasi 13 za mabao kwenye michezo 20 aliyocheza kwewnye msimu wake wa kwanza wa 2017-18 mpaka magoli 9 na pasi 5 katika michezo 18 aliyocheza kwenye ligi msimu uliopita.
Ni Mbappe anayeonekana kufanya vizuri na kuchukua mikoba ya kufunga mabao ya PSG, akifunga mabao 27 na kutoa pasi 7 za mabao, katika michezo 31 ya ligi msimu uliopita. Messi anaweza kuongeza jambo kwenye utatu wao, lakini swali litabaki kwa upande wa Neymar, ataboresha kiwango chake au atapotezwa na ujio wa Messi?.
Utatu wao unaweza kuwa bora kuwahi kutokea kwenye ulimwengu wa soka?
Kufuatia uhusiano wake na Neymar na kile ambacho kila mtu anakitarajiwa kutoka kwa Mbappe, ni rahisi kufikiria kwamba, ni hatari zaidi kwa wapinzani watu hawa watatu wakicheza pamoja.
Lakini Messi aliwahi kuchezaji pia na magwiji wengine wakali ndani ya Barcelona akiwa anachipukia na kutengeneza safu kali ya ushambuliaji inayoundwa na yeye, Ronaldinho, na mtu aliyekuwa anamsaidia sana wakati akikua kisoka, Mcameroon, Samuel Eto'o.
Walicheza pamoja, mpaka Pep Guardiola, alipowasili kukinoa kikosi hicho mwaka 2008, akafanya uamuzi wa kumuondoa kikosini Ronaldinho na kumpa nafasi zaidi Messi, akicheza pacha watatu na Eto'o na gwiji la ufaransa Thierry Henry.

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa na miaka 21 wakati huo, Messi alipachika mabao 38 katika michezo 51 aliyocheza kwenye mashindano yote, akiongeza idadi ya mabao 62 waliyofunga kwa pamoja na Henry na Eto'o, na kuisaidia Barcelona kushinda tuzo yake ya kwanza kati ya sita za Ballon d'Ors, ilikuwa mwaka 2009.
Msimu wa 2010-11 alikuwa sehemu ya utatu wa David Villa na Pedro Rodriguez, wakipewa jina la 'MVP'. Washambuliaji hao kwa pamoja walifunga mabao 98 goals, Messi pekee akifunga 53.
Pengine utatu uliokuwa na umaaarufu zaidi uliomuhusisha Messi ni ule ulioitwa 'MSN', akiwa pamoja na Luis Suarez na Neymar. Kuwasili kwa Suarez akitokea Liverpool mwaka 2014 kukaleta mabadilioko makubwa ya nafasi na uchezaji wa Messi akipelekwa upande wa kulia, ili kumruhusu Mruguay huyo kucheza kama mshambuliaji wa kati. Katika misimu mitatu waliyocheza pamoja, waliisaidia Barcelona kushinda makombe matatu katika msimu mmoja, Messi, Suarez na Neymar wakifunga jumla ya mabao 364 na kutoa pasi za mabao 174.
Safu gani kali ya ushambuliaji duniani kwa sasa?
Kwa ushindani uliopo, inaonekana safu ya ushambuliaji ya Liverpool inaweza kushindana na ya PSG.
Tangu Mohamed Salah ajiunge na klabu ya Liverpool mwaka 2017, yeye, Sadio Mane na Roberto Firmino kwa pamoja wamefunga mabao 273 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwawake wa sita wa ligi ya mabingwa Ulaya na ubingwa wa kwanz awa ligi katika kipindi cha miaka 30.

Chanzo cha picha, Getty Images
Safu ya ushambuliaji ya Bayern Munich siyo ya kubezwa pia. Ingawa Robert Lewandowski akiweka rekodi ya kufunga mabao 40 kwenye ligi ya Bundesliga msimu uliopita, aliweza kusaidiwa vyema na washambuliaji wenzake, Serge Gnabry na Thomas Muller.
Cristiano Ronaldo anakipiga pamoja na Alvaro Morata na nyota matata Federico Chiesa pale Juventus, lakini klabu za Manchester City na Manchester United, zinatarajiwa pia kuwa na safu ya kutisha baada ya kusajiliwa kwa Jack Grealish aliyetua City na Jadon Sancho aliyeelekea United.
Utatu gani mkali zaidi katika karne hii ?
Pengine Messi na klabu yake ya zamani ya Barcelona wanaweza kutajwa hapa, lakini usisahau utatu Ronaldo, Gareth Bale na Karim Benzema uliosaidia klabu yao ya Real Madrid, kushinda mataji manne ya ligi ya mabingwa Ulaya katika misimu mitano kati ya 2014 na 2018.
Inter Milan na Bayern Munich zote zimeshinda makombe matatu kati ya mwaka 2010 na 2013, huku Eto'o akiww amchezaji wa kwanz akushinda makombe matatu akiwa na vilabu tofauti
Alikuwa na washambuliaji wengine matata Diego Milito na Goran Pandev chini ya kocha Jose Mourinho, huku Arjen Robben, Franck Ribery na Mario Mandzukic wakiwa na mchango mkubwa kwa Bayern chini ya Jupp Heynckes.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sir Alex Ferguson alikuwa na nyota wakali kama Ronaldo, Wayne Rooney na Carlos Tevez, huku Dimitar Berbatov akiongeza chauchu ya safu yake ya ushambuliaji, iliyosaidia kutwaa makombe muhimu katika msimu ya 2007-08, na kutajwa kama safu bora kuwahi kutoka pale Manchester.
AC Milan ilikuwa na Rui Costa, Andriy Shevchenko na Filippo Inzaghi wakisaidia kuipatia taji la sita la ulaya mwaka 2003, kabla ya Clarence Seedorf kupelekwa mbele na kutengeneza safu nyingine kali iliyokuwa na Kaka na Inzaghi na kusaidia kutwaa taji la saba la Ulaya miaka minne baadae.
Pengine safu inayoundwa na Messi, Neymar na Mbappe inaweza kuwika zaidi kutokana na vipaji walivyonavyo. Huenda wakatawala ligi kuu ya Ufaransa miaka miwili ama mitatu ijayo, na kufanya kuogopwa ndani na nje ya Ufaransa.












