Kukamatwa kwa Mbowe: Zitto amtaka Rais Samia kuingilia kati

- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Tanzania
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amemtaka rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuingilia kati sakata la kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi kwa kiongozi wa chama cha upinzani Chadema Freeman Mbowe, huku akisema kuwa rais anao uwezo huo.
'Niikumbushe serikali kuwa mashtaka yasiyo na dhamana si mbinu mpya ya kudhibiti washindani wa kisiasa, ni mbinu ambayo imetumika ndani ya miaka 6 iliyopita na serikali za CCM kuwaziba midomo wote ambao hawakubaliani na nao kisiasa, ni mbinu ya kutesa watu," amesema Zitto.
Zitto ameyasema hayo mapema hii leo, katika ufunguzi wa mkutano wa kamati kuu ya chama na kuongeza kusema kuwa wakati umefika kwa wadau wa kisiasa kukaa na kukubaliana namna bora ya kufikia malengo ya kuwa na katiba mpya.

Mbowe alikamatwa kule mkoani Mwanza mwezi jana pamoja na wenzake 11, muda mfupi tu, kabla ya kuanza kwa kongamano linalodai vuguvugu ya katiba mpya.
Zitto amesema kumfungulia Mbowe shitaka la ugaidi katu hakuwavunji moyo wa kupambania Tanzania yenye usawa wa kisiasa na kuheshimu utoaji wa mawazao.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa chama hicho cha upinzani kutoa maoni yake baada ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa upinzani. Mara ya kwanza ilitoa taarifa ya pamoja na chama NCCR Mageuzi.
Tayari, wito umetolewa na watu mbalimbali yakiwemo mashirika ya kutetea haki za binadamu, wakitaka serikali iwasilishe ushahidi wa kutosha dhidi ya kesi inayomkabili Mbowe, au aachiliwe huru.
Ijumaa ijayo, Mbowe atafikishwa tena mahakamani baada ya kesi hiyo kuahirishwa mwishoni mwa juma, baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kusema, ingawa uchunguzi umekamilika, lakini taratibu za kuihamisha kesi hiyo kwenda mahakama yenye mamlaka haijakamilika.

Chanzo cha picha, AFP
Kwa upande wake, katika mkutano na waandishi wa habari, mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania- IGP Simon Siro amesema kiongozi huyo wa upinzani sio malaika, na hivyo ni vyema kuiacha mahakama kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa.
Punde tu, baada ya Rais Samia kuchukua hatamu kutoka kwa mtangulizi wake akilihutubia bunge mnamo mwezi Aprili miongoni mwa vitu alivyoahidi kuvifanya ni pamoja na kukutana na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Hata hivyo, ahadi hiyo mpaka sasa bado haijatimizwa, ingawa alipoulizwa pindi alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari, Rais Samia alisema, kipaumbele chake kwa sasa ni kujenga uchumi wa nchi.
Upinzani unaonekana kutoridhishwa na kauli hiyo, na kuhoji, kama ni hivyo, iweje rais Samia aweze kukutana na makundi mengine ikiwemo vijana, wanawake na viongozi wa dini.













