Ligi kuu ya Ulaya : Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham zakubali kujiunga

Liverpool na Manchester United ni timu zilizo na mafanikio makubwa katika historia ya soka la England

Chanzo cha picha, Getty Images

Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham ni miongoni mwa vilabu 12 ambavyo vimekubali kujiunga na Ligi Kuu ya Ulaya (ESL).

Katika hatua ambayo huenda ikayumbisha soka huko Uropa, vilabu hivyo vya Ligi ya premia vitajiunga na AC Milan, Atletico Madrid, Barcelona, Inter Milan, Juventus na Real Madrid katika kuunda ligi mpya ya bara ulaya .

ESL ilisema vilabu waanzilishi vilikubaliana kuanzisha "mashindano mapya ya katikati ya wiki" na timu zinazoendelea "kushindana katika ligi zao za kitaifa".

Inasema msimu wa uzinduzi "unakusudiwa kuanza mapema iwezekanavyo" na "ilitarajia kwamba vilabu vingine vitatu vitajiunga na" ligi hiyo .

ESL inasema pia ina mpango wa kuzindua mashindano ya wanawake haraka iwezekanavyo baada ya mashindano ya wanaume kuanza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Uefa na Ligi Kuu Uingereza walilaani hatua ya kuzindua Ligi Kuu ya Ulaya wakati habari hizo zilipotolewa siku ya Jumapili.

Shirikisho la soka duniani Fifa limesema hapo awali halitatambua mashindano kama hayo na wachezaji wowote wanaohusika katika mechi hizo wanaweza kunyimwa nafasi ya kucheza kwenye Kombe la Dunia.

Uefa, shirikisho linalosimamia soka Ulaya, lilikariri onyo hiyo siku ya Jumapili wakati liliposema wachezaji wanaohusika watapigwa marufuku kutoka kwa mashindano mengine yote katika ngazi ya nyumbani, Ulaya au ulimwengu na wanaweza kuzuiwa kuwakilisha timu zao za kitaifa.

Baada ya Ligi hiyo kuu Kuu ya Ulaya kutangazwa, Fifa ilielezea "kutokubali" mashindano hayo yaliyopendekezwa na kutoa wito kwa "pande zote zinazohusika katika majadiliano kushiriki mazungumzo ya utulivu, yenye kujenga na yenye faida kwa mchezo wa soka ".

Katika taarifa, ESL ilisema: "Kwa kuendelea, vilabu vya waanzilishi vinatarajia kufanya majadiliano na Uefa na Fifa kufanya kazi pamoja kwa kushirikiana kutoa matokeo bora kwa ligi mpya na kwa soka kwa ujumla."

Kwanini ni wakati huu?

Kulikuwa na mazungumzo mnamo Oktoba, yakihusisha benki ya Wall Street JP Morgan, juu ya mashindano mapya ya pauni bilioni 4.6 ambayo yatachukua nafasi ya Ligi ya Mabingwa.

Uefa walikuwa na matumaini mipango ya Ligi ya Mabingwa ya timu 36 - na marekebisho yaliyothibitishwa Jumatatu - yatasitisha uundaji wa Super League.

Hatahivyo, pande 12 zinazohusika kwenye Super League hazifikiri marekebisho hayo yanaenda mbali.

Walisema janga la Corona kote duniani "limeongeza kasi ya kukosekana kwa utulivu katika mtindo uliopo wa uchumi wa soka barani Ulaya".

"Katika miezi ya hivi karibuni, mazungumzo ya kina yamefanyika na wadau wa mpira kuhusu muundo wa baadaye wa mashindano ya Uropa," waliongeza.

"Klabu za waanzilishi zinaamini suluhisho zilizopendekezwa kufuatia mazungumzo haya hazitatui maswala ya kimsingi, pamoja na hitaji la kutoa mechi za hali ya juu na rasilimali za ziada za kifedha kufanikisha kilele cha soka kwa jumla."

Ni muundo gani uliopendekezwa?

Ligi hiyo itakuwa na timu 20 - wanachama 12 waanzilishi pamoja na vilabu vitatu ambavyo havikutajwa majina vinavyotarajia kujiunga hivi karibuni na timu nyingine tano ambazo zinafuzu kila mwaka kulingana na mafanikio yao ya nyumbani.

Chini ya mapendekezo, kampeni ya ESL ingeanza mnamo Agosti kila mwaka, na kutakuwa na mechi za katikati mwa wiki, na vilabu vitagawanywa katika vikundi viwili vya vilabu 10, vikicheza dhidi ya kila mmoja nyumbani na ugenini.

Timu tatu za juu katika kila kundi zitafuzu kwa robo fainali, na timu za nambari nne na tano kucheza mechi ya mikondo miwili kwa sehemu mbili zilizobaki.

Kuanzia hapo na kuendelea, itakuwa na muundo sawa na ule wa ligi ya mabingwa wa mechi za mikondo miwili kablaya Fainali ya awamu moja mwezi Mei katika ngome isiokuwa ya kilabu yoyote kati ya zilizofika fainali .

ESL inasema ligi hiyo itazalisha pesa nyingi kuliko Ligi ya Mabingwa na itasababisha usambazaji mkubwa wa mapato wakati wote wa mashindano

Viongozi wa ligi ya ESL wamesema nini ?

Juventus na AC Milan zimejiunga na makubaliano ya kuunda ligi mpya kuu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Juventus na AC Milan zimejiunga na makubaliano ya kuunda ligi mpya kuu

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ndiye mwenyekiti wa kwanza wa ESL na anasema "tutasaidia soka katika kila ngazi".

"Soka ndio mchezo pekee ulimwenguni ulio na zaidi ya mashabiki bilioni nne na jukumu letu kama vilabu vikubwa ni kujibu matakwa yao," ameongeza

Mwenyekiti wa Juventus Andrea Agnelli amejiuzulu kutoka kamati kuu ya Uefa na kama mwenyekiti wa muungano wa vilabu vya Ulaya (ECA), ambayo ilikuwa imesukuma mageuzi yaliyopangwa ya Ligi ya Mabingwa.

Alisema vilabu 12 vilikuwa "vimekutana wakati huu muhimu, na kuwezesha mashindano ya Uropa kubadilishwa, na kuweka mchezo tunaopenda kwa msingi endelevu kwa siku nyingi zijazo ".

Mwenyekiti mwenza wa Manchester United Joel Glazer atakuwa makamu mwenyekiti wa Super League.

Alisema: "Kwa kukusanya pamoja vilabu na wachezaji wakubwa ulimwenguni kucheza kila msimu, Super League itafungua sura mpya kwa soka ya Uropa, kuhakikisha ushindani na vifaa vya kiwango cha ulimwengu, na kuongeza msaada wa kifedha ili kufikisha soka katika kilele chake . "

Majibu yamekuwaje?

Kimsingi, kumekuwa na shutuma na laana kutoka kwa yeyeote ambaye hayumo katika mipango ya kuanzisha ligi hiyo mpya .

Johnson alisema mipango hiyo itakuwa "mibaya sana kwa soka" na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikaribisha vilabu vya Ufaransa vinavyokataa kujiunga.

Uefa ilitoa taarifa ya pamoja na shirikisho la soka Soka Uingereza, Ligi Kuu, Shirikisho la Soka la Uhispania, La Liga na Shirikisho la Soka la Italia, pamoja na Serie A, ikisema "watabaki wamoja" kujaribu kukomesha kujitenga, wakitumia " hatua zote zinazopatikana ".

Miongoni mwa wachezaji wa zamani, kiungo wa zamani wa Liverpool na Tottenham, Danny Murphy aliiambia BBC Sport mipango hiyo "ilikuwa isiyo na roho", nahodha wa zamani wa Manchester United Gary Neville aliiambia Sky Sports "alikuwa amechukizwa kabisa", wakati mwenzake wa zamani Rio Ferdinand alisema kwenye BT Sport kwamba mapendekezo hayo yataumiza mashabiki zaidi.

Je ,huu ni Usaliti ?

Vikundi vya mashabiki vinavyohusishwa na vilabu vyote sita vya England vinapinga vikali Super League.

Kundi la wafuasi wa Liverpool la Spirit of Shankly (SOS) limesema "limeshtushwa" na uamuzi wa Fenway Sports Group, mmiliki wa kilabu hiyo wa Marekani .

Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii , SOS ilisema: "FSG imepuuza mashabiki katika harakati zao za ulafi na kusaka pesa. Mpira ni wetu, sio wao. Klabu yetu ya mpira ni yetu sio yao."

Wakfu wa Wafuasi wa Chelsea ulitaja hatua hiyo kuwa "isiyosameheka" na wakasema wanachama wao na "wafuasi wa soka ulimwenguni kote wamepata usaliti wa mwisho"

Wakfu wa Wafuasi wa Arsenal uliita makubaliano ya kilabu yao ya kujiunga kama "kifo cha Arsenal kama taasisi ya michezo".

Kudi la wafuasi wa Manchester City FC lilisema hatua hiyo ilionyesha "wale waliohusika hawaheshimu sana itikadi za mchezo" na walikuwa "wameamua kupigana dhidi ya Ligi Kuu inayopendekezwa".