Uingereza yatoa onyo kwa raia wake wanaosafiri kuelekea Tanzania kuhusu Ebola

Chanzo cha picha, SNS
Serikali ya Uingereza imetoa tahadhari kwa raia wa nchi hiyo wanaosafiri kuelekea nchini Tanzania juu ya ''uwezekano'' wa kuwepo Ebola katika taifa hilo la mashariki mwa Afrika
Kulingana na taarifa tahadhari hiyo ya Uingereza mtu mmoja alifariki dunia nchini Tanzania mwezi wa Septemba 2019. Imeongeza kuwa inaonekana kuwa huenda kifo chake kilikuwa huenda kina uhusiano na Ebola. Serikali ya Uingereza kupitia wavuti wake pia imewaarifu raia wake kuwa shirika la afya duniani WHO clinaendelea kuchunguza na limetoa taarifa.
''Ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam inawasiliana na maafisa wa Tanzania na mashirika ya afya ya kimataifa, tahadhari hii itafanyiwa marekebisho pale taarifa mpya zitakapopatikana. ''Mnapaswa kufuatilia taarifa mpya kuhusu mabadiliko yoyote kwenye Mtandao wa Afya kuhusu safari na kituo na mitandao ya WHO'', imeongeza taarifa hiyo.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Tahadha hii ya Uingereza imekuja baada ya taifa la Marekani pia mwishoni mwa juma kuwaonya raia wake kuchukua tahadhari ya kiwango cha juu wakati wanapozuru nchini Tanzania kufuatia wasiwasi wa ugonjwa wa ebola, ikiitaka nchi hiyo ya Afrika mashariki kutoa habari kuhusu visa vya ebola nchini humo kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
''Wanaozuru Tanzania wanapaswa kuwa waangalifu sana'' , idara ya maswala ya kigeni ilisema siku ya Ijumaa katika tahadhari yao ya usafiri kufuatia kifo kinachohusishwa na ugonjwa huo mjini Dar es salaam.
Tanzania ilikana ripoti hiyo ikisema kuwa hakuna visa vya ebola vilivyoripotiwa, lakini kwa sasa serikali hiyo ipo katika shinikizo kali kutoa ufafanuzi kulingana na chombo cha habari cha Reuters.
Chini ya kanuni za Afya za Kimataifa, makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama, nchi zinalazimika kuiarifu WHO mara tu zitakapokuwa na milipuko ya magonjwa makubwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kuwa hatari kwa majirani zao na ulimwengu mpana.
Serikali za Afrika mashariki pamoja na zile za Afrika ya kati zimekuwa katika tahadhari ya kiwango cha juu kutokana na uwezekano wa maambukikizi ya ugonjwa huo kutoka DR Congo ambapo takriban watu 2,100 wamefariki kufuatia mlipuko wa ebola.

Mataifa ya Tanzania na DR Congo yanapakana na mto ulioyatenga.
Katika hatua isio ya kawaida, Shirika la Afya Duniani (WHO) wiki iliyopita lilisema kwamba, kinyume na kanuni za afya za kimataifa, Tanzania ilikuwa ikikataa kutoa maelezo ya watuhumiwa.
Siku chache mapema, mkuu wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa alisafiri kwenda Tanzania kwa agizo la waziri wa Afya wa Marekani Alex Azar, ambaye pia alikuwa amekosoa nchi hiyo kwa kutotoa habari.
WHO ilisema kwamba, licha ya kwamba ina wasiwasi kuhusu ukosefu wa uwazi, haina ushahidi wa kuwepo kwa Ebola nchini Tanzania, lakini ilikatiza hatua za adhabu na kusisitiza kwamba ilitoa ushauri wa kutosafiri nchini humo mbali na vikwazo vya kibiashara.
Siku ya Jumanne Tanzania ilifanya mazungumzo na mwakilishi wa ndani wa shirika la afya duniani WHO kuhusu madai yake.
Katikati ya mwezi Septemba, waziri wa afya alisema serikali ilichunguza kesi mbili za ugonjwa usiojulikana , lakini hawakupata ugonjwa huo.
WHO ilisema nini?
Shirika la afya duniani lililalamikia ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa serikali ya Tanzania katika utoaji taarifa kuhusu visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola nchini.
Katika taarifa yake ya malalamiko, shiriki hilo limeeleza kwamba uwazi na kasi katika kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo hatari ni muhimu katika kudhibiti mlipuko ambao tayari umetajwa kuwa janga la afya duniani.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa WHO limeeleza kwamba kufuatia taarifa zisizokuwa rasmi kuhusu visa vya ugonjwa na jitihada zake kupata taarifa kutoka kwa idara husika Tanzania kuhusu hali nchini humo, mpaka sasa hawajapokea data za kliniki, matokeo ya uchunguzi, mawasiliano na watu husika na hata matokeo ya uchunguzi wa maabara waliofanyiwa wagonjwa hao wanaoshukiwa.
WHO lilituma kundi la wataalamu kuchunguza kisa cha ugonjwa usiojulikana na ubalozi wa Marekani ulifuatilia hatua hiyo kwa kutoa tahadhari.
Hatua hiyo ilisababisha uvumi katika mitandao ya kijamii kwamba ugonjwa huo hatari umeingia nchini Tanzania.

Chanzo cha picha, @UMWALIMU
Serikali ya Tanzania imesema ilisema nini?
Serikali ya Tanzania ilifutilia mbali uvumi kwamba kuna visa vya ugonjwa wa Ebola nchini humo.
Waziri wa afya nchini humo bi Ummy Mwalimu aliambia mkutano na wanahabari kwamba hakuna kisa hata kimoja cha ebola katika taifa hilo.
Alisema kwamba taifa hilo limejiandaa kukabiliana na mlipuko wowote wa ugonjwa na tayari limefanya majarabio ili kujua jinsi ilivyojiandaa huku ikiweka tayari vituo vya kuwatenga waathiriwa.
Shirika hilo la Umoja wa mataifa limeendelea kueleza katika taarifa yake kwamba lilifahamishwa mnamo Septemba 10 kuhusu kifo cha mgonjwa kilichotokea mjinia dar es salaam, na kuarifiwa kwa njia isiyo rasmi siku ya pili kwamba mgonjwa huyo alipatikana kuwa na Ebola baada ya kufanyiwa vipimo.
Kadhalika WHO linaeleza kwamba liliarifiwa kuhusu visa vingine viwili vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa wa Ebola nchini humo.
Mmoja kati yao, alikutikana kutokuwa na Ebola baada ya vipimo na hapakuwa na taarifa zozote kuhusu mgonjwa wa pili, imeeleza taarifa hiyo.

Chanzo cha picha, Wizara ya Afya Tanzania
'Nataka kuwahakikishia kwamba idara ya afya ilichukua sampuli na matokeo yake ni kwamba wawili hao hawakuwa na ugonjwa wa Ebola. Hakuna Ebola Tanzania na watu hawafai kuwa na wasiwasi'', alisema waziri wa afya Tanzania Ummy Mwalimu wiki iliyopita kuhusu uvumi wa visa hivyo.
Kufanya vipimo tena vya homa ya Ebola katika maabara inashauriwa sana ili kuthibitisha matokeo ya vipimo na hivyo kubaini aina ya virusi Ebola . WHO linasema kuwa limewapatia maafisa wa Tanzania ushauri huu.
Mgonjwa huyo ambaye inaarifiwa ni mwanamke alifariki tarehe 8 Septemba kwa mujibu wa WHO.
Msururu wa matukio ya mgonjwa aliyeshukiwa kuwa na Ebola
Tarehe 10 Septemba 2019, Shrika la Afya duniani WHO lilipokea ripoti ya taarifa ya kisa cha mambukizi ya Ebola mjini Dar es Salaam, Tanzania.
Kisa hicho kinachoshukiwa kilimhusu mwanamke mwenye umri wa miaka 34 ambaye alikuwa akisomea nchini Uganda.
Aliwasili nchini Uganda akitokea nchini Tanzania tarehe 08 Agosti 2019.
Taarifa hiyo inasema kwa kuanzia tarehe 08 hadi 22 Agosti, alikuwa katika eneo la kati la Uganda, akiishi katika hosteli ya kibinafsi karibu na mji mkuu Kampala.
Ebola ni nini?

Chanzo cha picha, BSIP/Getty Images
Ebola ni kirusi ambacho mwanzo husababisha joto la mwili na kudhoofisha misuli na uvimbe kooni.
Kisha mgojwa huanza kutapika, kuharisha na kuvuja damu ndani na hata nje ya mwili.
Watu huambukizwa wanapogusana moja kwa moja kupitia michubuko ya mwili, au mdomo na pua, huku damu, matapishi, kinyesi au kugusa majimaji ya mwili ya mgonjwawa Ebola
Wagonjwa huwa wanakufa kutokana na ukosefu wa maji mwilini na kuharibika kwa viungo vya ndani vya mwili.
Tazama pia:














