Ebola yaendelea kuua DRC

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamethibitisha watu 24 zaidi wamefariki dunia kutokana na virusi vya ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo katika kipindi cha wiki iliyopita.
Maafisa hao wa Afya wametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuchukua hatua za kujikinga dhidi ugonjwa huo hatari.
Makundi ya waasi yamekuwa yakiendeleza uhalifu mpakani mwa Rwanda na Uganda hali ambayo imefanya kuwa ngumu jitihada za kutoa huduma za kimatibabu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameonya kuwa ghasia za hivi karibuni nchini humo zinakwamisha juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo.
Mmoja miongoni mwa waadhirika ni fundi bomba ambaye anafanyakazi na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika ukanda huo, amepata maambukizo ya virusi vya Ebola alipokuwa akienda kwa mganga wa kienyeji ambaye anadaiwa kumhudumia mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo.
Mapema mwezi huu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya ziara ya dharura kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mapigano makali nchini humo ambayo yametatiza jitihada za kudhibiti kuzuka kwa virusi vya Ebola.

Mapigano makali kati ya makundi yaliyojihami katika mji wa Beni Mashariki mwa nchi yamewalenga pia wahudumu wa afya wa Umoja wa Mataifa na kupunguza kasi ya vita kuzuia kuenea kwa Ebola nchini DRC.
Shirika la afya duniani WHO, lina mpango kufanya kikao maalumu siku ya Jumatano kutathmini iwapo litangaze mlipuko wa ugonjwa huu kama janga la dharura la kiafya linalohitaji uangalizi wa Jumuia ya Kimataifa .













