Ghana wapinga mpango wa kuanzishwa kwa elimu ya ngono kwa watoto

Chanzo cha picha, Getty Images
Wazazi na makundi ya kikristo nchini Ghana wamepinga mpango wa kuanzisha elimu ya lazima ya ngono katika shule za msingi na kwa watoto wenye umri wa miaka minne.
Maofisa wa sekta ya elimu nchini Ghana wamesema kuwa shirika la umoja wa mataifa linaloangazia masuala elimu, Unesco limeandaa programu itakayowawezesha watoto kuwa na taarifa sahihi kuhusu masuala ya kijinsia na afya ya uzazi.
Mkurugenzi wa sekta ya elimu anasema kuwa programu hiyo itasaidia katika malezi ya watoto na kuwa wawazi, kujiheshimu na kuwaheshimu watu wengine.
Vilevile programu hii itawasaidia watoto kuweza kutoa maamuzi ya mabaya na mazuri na kujua majukumu yaliopo endapo watajihusisha na ngono .
Lakini makundi ya wanaharakati nchini humo wanadai kuwa programu hiyo inachochea watoto kujiingiza kwenye tabia za mapenzi ya jinsia moja au kuwa wanaharakati wa watu wenye jinsia mbili.
"Ni mpango mkakati ambao uko wazi kwa mtu kuweza kuuona, " alisema Moses Foh Amoaning, kiongozi wa haki za jinsia na miiko ya kifamilia kutoka kundi linalodai kuwa mapenzi ya jinsia moja ni dhambi.
Wazazi na makundi ya kikristo wanahoji kwa nini watoto wadogo wafundishwe kuhusu ngono kabla ya kufikia umri wa kushiriki kitendo hicho.
Viongozi wa jumuiya ya walimu nchini humo wamedai kuwa hawakushirikishwa katika mpango huo na wao pia wanapinga kuanzishwa kwa somo hilo.
Mpango wa elimu hiyo utaanza mara moja baada ya kujadiliana na wadau wa elimu kutoka sekta mbalimbali.












