Liverpool 1-0 Napoli, Barcelona 1-1 Tottenham Hotspur: Klabu mbili za England zafuzu 16 Bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya UEFA

Meneja wa klabu ya Liverpool Jurgen Klopp amesema anaionea fahari sana klabu hiyo baada ya Mohamed Salah kufunga bao naye Alisson kuzuia bao kwa ustadi mkubwa na kuwawezesha kufuzu kwa hatua ya muondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Liverpool wamefuzu kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Napoli.

Klabu hiyo ya Anfield ilihitaji ushindi bila kufungwa au ushindi wa mabao mawili ya wazi ndipo kufika hatua ya 16 bora.

Salah alitekeleza wajibu wao kwa kumbwaga kipa David Ospina aliyekuwa analinda lango la Napoli dakika ya 34. Salah alikuwa amefunga mabao matatu katika ushindi wa Liverpool wa 4-0 wikendi Ligi ya Premia dhidi ya Bournemouth.

Ospina alifidia kwa kuwazuia Salah na Sadio Mane kufunga baadaye kwenye mechi hiyo, Virgil van Dijk naye akakosa nafasi ya wazi ya uongeza ushindi wa Liverpool.

Hali kwamba Liverpool waliondoka bila kufungwa zaidi ilichangiwa na kipa wao Alisson aliyekomboa shuti kali kutoka kwa Arkadiusz Milik katika shambulio nadra la Napoli kwenye mechi hiyo iliyochezewa Anfield.

Kipa huyo Mbrazil alijiunga na klabu hiyo ya Uingereza kutoka AS Roma mwezi Julai kwa uhamisho uliovunja rekodi kwa magolikipa, ambapo alilipiwa £66.8m.

"Ningelijua kwamba Alisson alikuwa mzuri hizi, ningelipa bei yake maradufu," alisema Klopp baada ya mechi hiyo.

"Na bao hilo la Mo - bao zuri ajabu - lakini kwa Ali (Allison) sina cha kusema kwa sasa. Alikuwa mkombozi."

Liverpool wamesonga kwa kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Paris St-Germain -mafanikio ambayo wameyapata licha ya kushindwa mechi tatu za ugenini katika kundi lao.

Klabu hiyo ya Uingereza ambayo ilishindwa na Real Madrid kwenye fainali msimu uliopita, itakutana na mshindi wa mojawapo ya makundi katka hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya droo itakapofanywa 17 Desemba.

Walishindwa 3-1 mjini Kiev katika mechi ambayo kipa wao Loris Karius alifanya makosa kadha naye Mo Salah akaumia.

Droo hiyo huenda ikawakutanisha na Real Madrid, au Barcelona, klabu ya zamani ya Klopp Borussia Dortmund na Porto ya Ureno, klabu ambazo tayari zimefuzu zikiwa zinaongoza katika makundi yao.

Matokeo ya mechi za Jumanne UEFA 11 Desemba 2018

  • Schalke 1-0 Lokomotiv Moscow
  • Galatasaray 2-3 FC Porto
  • Club Brugge 0-0 Atletico Madrid
  • Monaco0-2 Borussia Dortmund
  • Barcelona 1-1 Tottenham
  • Inter Milan 1-1 PSV Eindhoven
  • Red Star Belgrade 1-4 Paris Saint Germain
  • Liverpool 1-0 Napoli

Tottenham walitimiza kilichodhaniwa na wengi kwamba hakiwezekani, kwa kufuzu kwa hatua ya 16 bora, kwa mujibu wa meneja wao Mauricio Pochettino.

Lucas Moura alifunga bao la dakika 85 na kusawazisha dhidi ya Barcelona uwanjani Camp Nou na kuwapa alama muhimu Kundi B, baada yao kuzoa alama moja pekee kutoka kwa mechi zao tatu za kwanza.

Walikuwa wanahitaji kufikia matokeo ya Inter Milan dhidi ya PSV Eindhoven au wapate matokeo bora zaidi ya hayo. Waliondoka na ushindi wa 1-0.

Walikuwa hatarini kuondolewa baada ya Mauro Icardi kusawazisha bao la mapema la PSV nao Barca wakawa wanaongoza kwa kipindi kirefu mechi hiyo kupitia bao la Ousmane Dembele la dakika ya saba.

Lakini Moura aliwaokoa, na baadaye wakawa wanasubiri kusikia iwapo Inter walikuwa wamefunga bao la ushindi, ambalo kwa bahati yao halikutokea.

"Nina furaha sana kwa sababu ya mashabiki - huu ni ufanisi mkubwa sana, mkubwa ajabu kwa klabu hii," alisema Pochettino.

Wayne Rooney akutana na mwana wa Donald Trump

Mechi zikichezwa Ulaya, nahodha wa zamani wa England ambaye sasa huchezea DC United Wayne Rooney alikuwa White House, makao ya sasa ya Rais wa Marekani Donald Trump.

Alikuwa amealikwa kwa sherehe ya msimu wa Krismasi.

Huko, mchezaji huyo wa miaka 33 alikutana na mtoto wa Trump na Melania, Barron, mwenye miaka 12.

Mvulana huyo ni shabiki wa mchezo wa kandanda na aliichezea timu ya wachezaji chipukizi ya DC.

Rooney, anayeshikilia rekodi ya ufungaji wa mabao Manchester United alihamia Washington kutoka Everton mwezi Juni na alifungia klabu hiyo mabao 12 na kuwawezesha kufika mechi za muondoano za baada ya msimu mwezi Novemba.

Taarifa zinasema Rooney aliandamana na mkewe Coleen na wanawe wanne wa kiume, na kwamba walitembezwa White House na mwelekezi.

Kibarua Liverpool na Manchester United

Liverpool wanasubiriwa na mechi kali Ligi ya Premia watakapokuwa wenyeji wa mahasimu wao wa jadi Manchester United Jumapili.