Picha za Ronaldo zinazoonyesha ustadi wake dhidi ya Uhispania

Muda wa kusoma: Dakika 2

Ronaldo alifunga mabao matatu dhidi ya Uhispania katika mechi ambayo imesifiwa kuwa bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Kombe la Dunia katika muda mrefu.

Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 3-3, mabao ya Uhispania yakifungwa na Diego Costa (mawili) na Nacho.

Hapa, kwa picha, ndivyo mechi hiyo ilivyokuwa kwa Ronaldo.

Muda mfupi baada ya mechi kuanza, aliingia eneo la hatari na kujishindia penalti...

... ambayo aliichapa upande wa kulia wa lango na kumbwaga kipa David De Gea, na kufunga dakika ya nne.

Mchezaji huyo wa miaka 33 alionekana kuchagua ni wakati gani angehusika zaidi kwenye mechi, na wakati gani wa kuhifadhi nguvu zake uwanjani.

Baadaye kipindi cha kwanza, dakika ya 44, alimkanganya kipa De Gea tena, kwa mpira ambao uliiponyoka mikono ya kipa huyo wa Uhispania kama samaki mtelezi.

Alisherehekea kwa kuteleza uwanjani, na kisha kufuatwa na wachezaji wenzake waliompongeza.

Mechi hiyo ilikuwa imesifiwa kama mechi kati ya miamba, ambao mara nyingi hucheza wakiwa timu moja Real Madrid.

Lakini hakukuwa na uhasama kati ya Ronaldo na Sergio Ramos, Ramos akionekana wakati mmoja kumsaidia kuinuka uwanjani.

Dakika ya 88, Ureno walipata frikiki.

Ronaldo aliupinda mpira juu ya ukuta wa wachezaji wa Uhispania na ukatumbukia kwenye kona ndani ya wavu...

... ambapo alinguruma uwanjani baada ya kutimiza hilo...

... na kisha, kusherehekea kwa mtindo wake wa kipekee, kuruka juu na kuirusha mikono yake.

Baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, alimkumbatia kipa wa Uhispania De Gea, ambaye alikuwa amemfunga mara tatu.

Wachezaji wa zamani walisifu uchezaji wake.

Nahodha wa zamani wa Italia Franco Baresi alikosa maneno ya kuelezea uchezaji huo.

"Twende, familia!" alisema Ronaldo, akipigwa picha pamoja na timu baada ya mechi hiyo.

Picha zote zina haki miliki.