Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afcon 2019: Tanzania yaifumua Cape Verde 2-0 na kufufua matumaini ya kufuzu
Matumaini ya Tanzania kufuzu katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 bado yangalipo baada kuichabanga Cape Verde 2-0 jijini Dar es Salaam.
Huu ulikuwa ni mchezo wa marudiano wa kundi L ambapo Tanzania ilifungwa Ijumaa iliyopita goli 3-0 na kufanya matumaini ya taifa hilo la Afrika mashariki kwenda Cameroon kwa michuono ya Afcon mwakani kufifia.
Ushindi wa leo unaifanya Tanzania kufikisha pointi 5 baada ya kucheza michezo 4. Imetoka sare michezo miwili na kufungwa mmoja.
Tanzania almaarufu kama Taifa Stars kwa sasa ipo nafasi ya pili nyuma ya vinara Uganda wenye pointi 7. Uganda na Lesotho inayoshika mkia kwa sasa kwa kuwa na pointi 2 wanashuka dimbani usiku wa leo na endapo Uganda itashinda watakuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu.
Lakini kama Lesotho watapata ushindi mambo yatakuwa magumu kwa timu zote za kundi hilo ambapo kinara Uganda atasalia na pointi 7 akifuatiwa na Tanzania na Lesotho watakaokuwa na pointi 5 kila mmoja na Cape Verde watashika mkia kwa alama zao 4.
Tanzania ilianza mchezo wa leo kwa kasi, Nahodha wa Tanzania na nyota wa klabu ya Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta aliwaacha watanzania midomo wazi kwa mshangao baada ya kukosa mkwaju wa penati katika dakika ya 21.
Samatta alirekebisha makosa yake katika dakika ya 29 kwa kutengeneza nafasi maridhawa iliyotumiwa vyema na mshambuliaji Saimon Msuva aliyeandikia Tanzania bao la kuongoza.
Tanzania ilirudi na kasi katika kipindi cha pili na nyota wao Samatta kuiandikia bao la pili katika dakika ya 58.
Baada ya kichapo cha Ijumaa nchini Cape Verde matumaini ya wengi nchini Tanzania yalififia lakini kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike hakukata tamaa.
Amunike, ambaye ni nyota wa zamani wa Nigeria alisema kuwa; "nafasi bado ipo, kundi letu bado lipo wazi, tunaweza kufanikiwa."
Maneno hayo ya Amunike yanaonekana kuwa na uhalisia sasa, lakini Taifa Stars bado wanakibarua kigumu cha kuvaana na Lesotho ugenini na Uganda nyumbani Dar es Salaam.