Iceland walivyomzima Messi - kwa picha

Muda wa kusoma: Dakika 3

Iceland mwanzoni mwa Kombe la Dunia walikuwa wametazamwa kama wanyonge ambao wangekabiliwa na maangamizi dhidi ya 'masihi' Lionel Messi.

Wengi walitarajia taifa hilo na watu 335,000 pekee lifungwe mabao mengi sana Jumamosi. Lakini walibadilisha hilo na badala yake wakatoka sare na Argentina.

Hapa ni yalivyotokea kwa picha.

Kabla ya mechi kuanza, mashabiki wa Iceland walipiga makofi kwa pamoja, kama kawaida yao.

Taifa lao lina watu 335,000 pekee, iwapo mashabiki walioonekana Moscow ni raia wa taifa hilo, basi ni kama taifa lote lilikuwa limesafiri.

Mashabiki wa Argentina walijaribu kuwanyamazisha, kwa bango na kumrejelea nyota wao anayechezea Barcelona Lionel Messi.

Je, angeweza kufikia kiwango kilichofikiwa na mshindani wake mkuu Cristiano Ronaldo siku iliyotanguliwa?

Angefanikiwa?

Argentina walifunga kwanza kupitia Sergio Aguero na wengi wakatarajia kichapo kikali kwa Iceland.

Lakini Iceland walikomboa kupitia Alfred Finnbogason, na kuzua shangwe na nderemo uwanjani.

Macho yote sasa yakaelekezwa kwa Messi, angefanikiwa kuupenya ukuta wa Iceland?

Ronaldo alikuwa amefunga penalti, lakini Messi alipopata fursakama hiyo, ilizuiwa na kipa Hannes Halldorsson.

Isitoshe, alishindwa kufunga frikiki dakika za mwisho tofauti na Mreno Ronaldo ambaye alikuwa amefunga kwa mpira kumponyoka kipa wa Uhispania David de Gea kwa bao lake la pili. Kombora la Messi lilielekea nje ya goli la Iceland.

Haikuwa siku nzuri kwa Messi.

Kwa timu ya taifa, messi angalau amebaki kuwa chini ya shujaa mwingine Diego Maradona ambaye alikuwa akiitazama mechi hiyo.

Maradona alieleza kusikitishwa kwake na uchezaji wa taifa hilo Urusi.

Wakati huu, wengi katika mitandao ya kijamii, Maradona ambaye hufahamika sana kwa bao lake la 'mkono wa Mungu' alionekana akiwa ameshika sigara akitazama Messi uwanjani, kinyume na sheria za Fifa kwamba uvutaji wa sigara hauruhusiwi uwanjani.

Badala yake, ilikuwa ni siku ya kipa Halldorsson ambaye ustadi wake ulisaidia Iceland kujimudu dhidi ya Argentina.

Mji mkuu wa Iceland Reykjavik kulijaa shangwe baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, licha ya mvua kubwa kunyesha.

Mashabiki wa Argentina hata hivyo walijawa na masikitiko, masihi wao Messi alikuwa ameshindwa kuvuma. Wangelazimika kusubiri wakati mwingine.

Unaweza kusoma pia:

Picha zote zina hakimiliki