Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Ubalozi wa Marekani Saudi Arabia washambuliwa na ndege zisizo na rubani

Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imethibitisha kwamba ubalozi wa Marekani mjini Riyadh ulishambuliwa na ndege mbili zisizo na rubani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Watanzania watahadharishwa safari za Mashariki ya Kati

    Serikali ya Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu hali ya usalama inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Serikali kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, imeshauri raia wa Tanzania wanaoishi au wanaopanga kusafiri katika eneo hilo ikiwemo Bahrain,Israel,Kuwait,Qatar na Falme za Kiarabu (UAE) kuzingatia;

    • Kuepuka safari za kwenda au kutoka Mashariki ya Kati katika kipindi hiki.
    • Kubaki katika makazi wanayoishi inapowezekana.
    • Kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka za maeneo husika na kuwa waangalifu wakati wote.
    • Kuepuka maeneo yenye shughuli za kiusalama au kijeshi katika maeneo wanayoishi.
    • Kutumia njia rasmi za mawasiliano na taarifa.
    • Kuhifadhi pasipoti na vitambulisho vya Tanzania katika sehemu salama na vitakapopatikana kwa urahisi iwapo kutakuwa na dharura.

    Taarifa ya Wizara hiyo imesema pamoja na Misheni za Kidiplomasia, itaendelea kutoa taarifa na usaidizi wa Kibalozi kadiri hali itakavyoruhusu katika maeneo husika.

  2. Rubio: Tuliishambulia Iran kwa sababu Israel ilikuwa karibu kushambulia na majeshi yetu yalikuwa hatarini

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amesema katika akaunti mpya sababu ya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

    Anasema kwamba Marekani ilipata taarifa kutoka kwa Israel kwamba ilikuwa inapanga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, .

    Washington imedai kwamba hatua hiyo ya Israel inaambatana na shambulio la mara moja la Iran dhidi ya majeshi ya Marekani, na kwa hiyo jeshi la Marekani lilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran kwa lengo la kuizuia.

    Pia aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba "dhamira" ya msingi ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ni "kuharibu uwezo wao wa makombora ya balistiki ya [Wairani] wa kuyajenga pamoja na tishio ambalo jeshi lao la majini linaleta kwa meli za kimataifa."

    Aliendelea kusema kuwa anatumai watu wa Iran wanaweza "kuiangusha" serikali hii na "kujenga mustakabali mpya wa nchi yao."

    Bw. Rubio aliongeza kuwa "tungefurahi kama hili lingewezekana," lakini akasisitiza kuwa "lengo la misheni hii ni kuharibu uwezo wao wa makombora ya balistiki na uwezo wao wa majini."

    Viongozi wa Israel nao wameeleza kuwa "kupinduliwa kwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu" ni moja ya malengo makuu ya mashambulizi yao ya pamoja na Marekani.

    Bw. Rubio, ambaye pamoja na wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Nje pia ni mshauri mkuu wa usalama wa taifa wa Donald Trump, alienda kwenye Bunge la Congress la Marekani Jumatatu ili kuwaeleza wawakilishi na maseneta wa Marekani sababu za kuanzisha vita na Iran.

  3. Rwanda yaikosoa Marekani kuhusu vikwazo dhidi ya maafisa wake wa kijeshi

    Rwanda imekosoa vikwazo vilivyowekwa na Marekani, ikiviita hatua hizo kuwa zisizo za haki na zenye upande mmoja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kuhusu mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

    Vikwazo hivyo vinalenga Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na maafisa wakuu wa jeshi kwa madai ya kuunga mkono M23, kundi lenye silaha linalofanya kazi mashariki DRC.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Kigali ilisema hatua ya Marekani "inawakilisha vibaya ukweli na kupotosha ukweli" unaozunguka mzozo huo.

    Kigali iliishutumu serikali ya DRC kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano kupitia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya ardhini.

    "Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya ardhini yanayoendelea na yasiyo na mpangilio ni ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na DRC na yanaendelea kugharimu maisha ya watu wengi," taarifa hiyo ilisema.

    Rwanda ilisisitiza kwamba lengo lake kuu ni usalama wa taifa, ikisema kwamba vitendo vya jeshi la Rwanda ni vya kujihami na vinalenga kukabiliana na makundi yenye silaha maadui wanaofanya kazi karibu na mipaka yake.

    Rwanda ilidai zaidi kwamba Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vinashirikiana na vikundi vyenye silaha vinavyoichukia Kigali, ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Kidemokrasia cha Ukombozi wa Rwanda (FDLR).

    Ingawa Washington inasisitiza kwamba vikwazo vinakusudiwa kukuza uwajibikaji na amani, Rwanda inasema kwamba utulivu wa muda mrefu unategemea kushughulikia kile inachokielezea kama chanzo kikuu,kuendelea kuwepo kwa makundi yenye silaha yanayoipinga Rwanda yanayofanya kazi ndani ya mashariki mwa Congo.

    Majjibizano ya hivi karibuni ya kidiplomasia yanaangazia hali dhaifu ya juhudi za amani na vihatarishi tata vya kijiografia vinavyozunguka mzozo wa DRC.

    Unaweza kusoma;

  4. Marekani yaweka vikwazo dhidi ya makamanda wa Rwanda wanaowaunga mkono waasi wa M23

    Marekani imeweka vikwazo vikali kwa jeshi la Rwanda na makamanda wake wanne wakuu, ikiwashutumu kwa kuchochea migogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Wizara ya Hazina inasema Jeshi la Ulinzi la Rwanda limekuwa likitoa mafunzo, kuandaa, na kupigana pamoja na kundi la waasi la M23, ambalo tayari limeidhinishwa na Washington na Umoja wa Mataifa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhama kwa wingi mashariki mwa Congo.

    Miongoni mwa wale wanaolengwa ni Vincent Nyakarundi, Mkuu wa Jeshi; Ruki Karusisi, kamanda wa Kitengo cha 5 cha ardhini, Mubarakh Muganga, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda; na Stanislas Gashugi, mkuu wa Operesheni Maalum.

    Mali zao nchini Marekani sasa zimezuiliwa, na raia wa Marekani wamezuiliwa kufanya biashara nao. Hatua hiyo inakuja siku chache tu baada ya Marais Felix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda kusaini Makubaliano ya Washington huko Washington, wakiahidi kukomesha uhasama.

    Lakini muda mfupi baadaye, M23 iliteka Uvira, mji wa kimkakati kwenye mpaka wa Congo na Burundi, na kulazimisha maelfu kukimbia.

    Marekani inasema usaidizi wa Rwanda umeruhusu M23 kuteka eneo, kushambulia vikosi vya Congo na Umoja wa Mataifa, na kupata ufikiaji wa maeneo yenye madini mengi.

    Maafisa wanaonya kwamba kuendelea kuhusika kuna hatari ya kuiingiza kanda nzima ya Maziwa Makuu vitani.

    Washington inasisitiza kwamba vikwazo hivyo havikusudiwa kuadhibu, bali kulazimisha kuzingatiwa kwa ahadi za amani. Rwanda bado haijasema chochote.

    Unaweza kusoma;

  5. Watu 52 wauawa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon

    Jeshi la Israel limesema limeshambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon, baada ya kundi la Shia linaloungwa mkono na Iran kusema kwamba lilirusha roketi na ndege zisizo na rubani katika mji wa Haifa wa Israel ili kulipiza kisasi cha mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

    Kitengo cha usimamizi wa majanga cha Lebanon kilisema watu 52 waliuawa na mashambulizi ya Israel nchini humo Jumatatu.

    Hakukuwa na ripoti za majeruhi nchini Israel kutokana na shambulizi la Hezbollah, ambalo kundi hilo lilisema ni kulipiza kisasi kwa "damu safi" ya Khamenei na mashambulizi ya Israel nchini Lebanon tangu kusitisha mapigano kati yao miezi 15 iliyopita.

    Waziri wa ulinzi wa Israel aliapa Hezbollah italipa "gharama kubwa".

    Israel Katz alisema ameagiza jeshi la Israel “kuchukua hatua kali” dhidi ya wanamgambo na chama cha kisiasa cha Hezbollah, na kwamba kiongozi wake, Naim Qassem, sasa ni “lengo lililowekewa alama ya kuondolewa.”

    Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam, alilaani hatua za Hezbollah kuwa “zisizo za kuwajibika” na kusema serikali yake inapiga marufuku mara moja shughuli za kijeshi za kundi hilo.

    Ilikuwa imetarajiwa kwa kiasi kikubwa kwamba Hezbollah, ambayo ina uhusiano wa karibu wa kifedha na kiitikadi na Iran, ingejiunga na mzozo kati ya Iran, Israel, na Marekani.

    Mzozo huo umeenea kwa kasi katika Mashariki ya Kati tangu shambulio la pamoja la Marekani na Israel dhidi ya uongozi na majeshi ya Iran siku ya Jumamosi, huku Iran ikijibu kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel na mataifa ya Kiarabu ya Ghuba yanayohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani.

    Unaweza kusoma;

  6. Watu wasiopungua 169 wauawa katika shambulio la 'kushtukiza' Sudani Kusini

    Mamlaka nchini Sudan Kusini zimesema watu wasiopungua 169, wakiwemo maafisa wakuu, waliuawa Jumapili wakati kundi la watu wasiojulikana walipoanzisha shambulio katika eneo moja kaskazini mwa nchi.

    Akielezea shambulio hilo linalodaiwa kufanywa na vijana kadhaa wenye silaha, Waziri wa Habari wa Eneo la Utawala la Ruweng, James Monyluak Mijok, alidai kwamba walitoka katika jimbo jirani la Unity na walikuwa na uhusiano na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan katika Upinzani (SPLA-IO).

    SPLA-IO imekana kuhusika kokote katika shambulio hilo, ikishutumu mamlaka ya jimbo la Unity kwa kuingilia vurugu hizo kisiasa.

    Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara kwamba nchi iko katika hatari ya kurudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    “Waliokufa ni pamoja na watoto 90, wanawake na wazee, pamoja na maafisa 79 wa vikosi vya kikanda, wakiwemo polisi,” Mijok alisema.

    Mijok aliiambia BBC kwamba washambuliaji waliingia kaunti ya Abiemnom katika eneo la Ruweng kabla ya alfajiri Jumapili, takribani saa 4:30 asubuhi kwa saa za huko (02:30 GMT), wakati watu bado walikuwa wamelala na “waliwashitukiza”.

    Alisema kuwa vikosi vya serikali vilivyokuwa eneo la tukio “vilizidiwa idadi… Washambuliaji walichoma moto nyumba na masoko wakati wa mapigano yaliyodumu kati ya saa tatu hadi nne.” Maafisa kadhaa waandamizi wa eneo hilo waliuawa, akiwemo kamishna wa kaunti na mkurugenzi mtendaji.

    Mijok alisema tangu wakati huo vikosi vya serikali vimewafurkuza washambuliaji na kwamba sasa mamlaka zina udhibiti kamili wa eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  7. Netanyahu adai kuwa ingekuwa vigumu kwa mpango wa nyuklia wa Iran kudhibitiwa

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametetea mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran, akidai kwamba ongezeko la hivi karibuni la mpango wa nyuklia wa Tehran “lisingekuwa rahisi kudhibiti ndani ya miezi michache” kabla ya hatua ya Israel.

    Licha ya mashambulizi ya pamoja ya anga ya Israel na Marekani yaliyolenga vituo vitatu vya nyuklia wakati wa vita vya siku 12 mwezi Juni, Netanyahu anasema wanajeshi na mafundi wa Iran walianza kujenga maeneo mapya, yakiwemo “ya chini ya ardhi,” ambako wangeweza kuendeleza makombora ya balistiki na mabomu ya atomiki.

    “Kama hakuna hatua ingechukuliwa sasa, basi hakuna hatua ambayo ingeweza kuchukuliwa baadaye,” Netanyahu aliiambia Fox News.

    Israel kwa muda mrefu imepinga urutubishaji wa nyuklia wa Iran, ikionya kuwa unaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia badala ya kutumika kwa madhumuni ya amani kama inavyodai serikali ya Iran.

    Unaweza kusoma;

  8. Ubalozi wa Marekani Saudi Arabia washambuliwa na ndege zisizo na rubani

    Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imethibitisha kwamba ubalozi wa Marekani mjini Riyadh ulishambuliwa na ndege mbili zisizo na rubani, kulingana na makadirio ya awali.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo ilisema hii ilisababisha "moto mdogo na uharibifu mdogo wa vifaa kwenye jengo hilo".

    Ubalozi wa Marekani umewaagiza wafanyakazi wake walioko Saudi Arabia kubaki ndani katika miji ya Jeddah, Riyadh, na Dhahran kutokana na uwezekano wa tishio la kiusalama.

    Ujumbe huo utapunguza au utaepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye vituo vya kijeshi katika eneo hilo, kama tahadhari kwa sababu za usalama.

    Donald Trump alikiambia kituo cha runinga cha NewsNation kwamba Marekani italipiza kisasi “hivi karibuni” kufuatia shambulio dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Riyadh na vifo vya wanajeshi wa Marekani.

    Wanajeshi sita wa Marekani wameuawa hadi sasa huku 18 wakiwa wamejeruhiwa, Marekani ilisema Jumatatu usiku.

    Unaweza kusoma;

  9. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo