Kwaheri hadi kesho
Tumefikia mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tunakutakia usiku mwema.
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gavana wa Kharkiv Oleh Synehubov amesema watu 23 wamejeruhiwa katika shambulio la kombora katika mji wa Kharkiv, ambapo operesheni ya uokoaji inaendelea kwa sasa.
Na Lizzy Masinga & Rashid Abdallah
Tumefikia mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tunakutakia usiku mwema.
Mshambulizi wa Real Madrid Vinicius Jr ataukosa mchezo wa timu yake wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool baada ya kupata jeraha la misuli ya paja.
Mbrazil huyo alicheza mechi dakika 90, katika ushindi wa Real Madrid wa 3-0, katika La Liga dhidi ya Leganes siku Jumapili.
Madrid, ambayo iko katika nafasi ya 18 kwenye jedwali la Ligi ya Mabingwa lenye timu 36, watasafiri hadi Anfield, Jumatano kumenyana na Liverpool walio kileleni mwa jedwali.
Klabu hiyo ya La Liga ilitaja kikosi cha wachezaji 19 waliosafiri na hapakuwa na jina la Vinicius Jr baada ya kupata "jeraha katika mguu wake wa kushoto."
Kulingana na gazeti la Uhispania la Marca, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil anaweza kuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki tatu lakini Madrid, haijasema lolote kuhusu jeraha hilo.
Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto na Mwalimu wa zamani wa historia, Yamandú Orsi, ameshinda uchaguzi wa urais nchini Uruguay.
Orsi amemshinda Álvaro Delgado, mgombea wa muungano unaotawala wa kihafidhina, kwa zaidi ya asilimia tatu katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili.
Delgado ilikubali kushindwa na kumpongeza Orsi na muungano wake wa Broad Front, ambao sasa utarejea madarakani baada ya miaka mitano ya utawala wa kihafidhina.
Chama cha Broad Front kilikuwa madarakani nchini Uruguay kwa miaka 15 kuanzia 2005 hadi 2020 kabla ya kushindwa na Rais anayeondoka Luis Lacalle Pou.
Orsi, 57, anafananishwa na Rais wa zamani José Mujica, ambaye alivutia mioyo ya watu wengi nchini Uruguay kupitia maisha yake ya kawaida, na kuwafanya watu wengi kumwita "rais maskini zaidi duniani."
Orsi mwenyewe anatoka katika familia duni, amekulia vijijini Uruguay katika nyumba isiyo na umeme.
Alipokuwa akifanya kazi kama mwalimu wa historia katika shule, alijishughulisha na siasa za ndani, hatimaye akawa meya wa Canelones.
Wakati Orsi akiwa ofisini huko Canelones, kampuni kubwa ya teknolojia ya Google ilitangaza kuwa itaunda kituo kikubwa cha data katika mji huo.
Akiwahutubia wafuasi wake Jumapili jioni, alisisitiza kuwa anataka kuwa rais wa Warugwai wote milioni 3.4.
Rais anayemaliza muda wake Luis Lacalle Pou amesema atafanya kazi na Orsi kuhakikisha kunakuwa na mabadilishano mazuri ya madaraka kabla ya kuapishwa kwake tarehe 1 Machi mwaka ujao.
Broad Front ya Orsi pia imeshinda wingi wa kura katika Seneti ya Uruguay, lakini muungano huo haukupata wingi wa kura katika Baraza la Wawakilishi.
Urusi na Ukraine zimeshambuliana kutokea angani kwa makombora na droni, baada ya wiki moja ya maneno makali ambapo Urusi ililifanyia majaribio ya kombora jipya nchini Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema Urusi imefanya takribani mashambulizi 1,500 dhidi ya Ukraine tangu Jumapili jioni katika nusu ya mikoa ya nchi hiyo na kusababisha majeruhi kadhaa.
Gavana wa Kharkiv Oleh Synehubov amesema watu 23 wamejeruhiwa katika shambulio la kombora katika mji wa Kharkiv, ambapo operesheni ya uokoaji inaendelea kwa sasa.
Idara ya dharura ya Odesa imesema watu 10 wamejeruhiwa katika shambulio la kombora, ambalo liliharibu majengo ya makazi, shule na ukumbi wa michezo wa chuo kikuu.
Maafisa wa mkoa wanasema watu watatu walijeruhiwa katika shambulio katika mkoa wa Kherson, na mmoja katika mikoa ya Zaporizhzhya na Chernihiv.
Wakati huo huo, jeshi la Ukraine linasema limeshambulia ghala la mafuta la Kaluganefteprodukt katika mkoa wa Kaluga kusini mashariki mwa Moscow kwa kutumia droni.
Vyombo vya habari vya Ukraine vimeripoti kuwa shambulio hilo lilisababisha milipuko kadhaa na moto kwenye eneo hilo.
Jeshi la Ukraine pia limetaja mashambulizi katika mikoa ya Bryansk na Kursk, bila kubainisha ni nini walishambulia.
Lakini wanablogu wa kijeshi wa Urusi, wanasema kambi ya jeshi la anga ya Khalino katika eneo la Kursk ilishambuliwa na makombora manane ya Atacms yaliyotolewa na Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Mahakama ya Malaysia imeamuru serikali ya nchi hiyo kuzirudisha saa 172 za rangi ya upinde wa mvua - inazozishikilia tangu mwaka jana kutoka kwa kampuni ya utengenezaji saa ya Swatch.
Serikali ilisema ilizichukua saa hizo kutoka kampuni ya Switzerland kwa sababu zilikuwa na "viashiria vya mapenzi ya jinsia moja" - ambayo ni kinyume cha sheria za Malaysia, yenye Waislamu wengi na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka 20 jela.
Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa serikali haikuwa na kibali cha kutaifisha vitu hivyo na sheria ya kukataza kuuzwa vitu kama hivyo ilipitishwa baadaye, na kufanya ushikiliaji huo kuwa kinyume cha sheria.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malaysia, Saifuddin Nasution Ismail alisema timu ya wanasheria wa serikali itahitaji "kuchunguza msingi wa uamuzi huo" kabla ya kuamua kukata rufaa dhidi ya amri hiyo.
Serikali ilivamia maduka ya Swatch kote Malaysia mwezi Mei 2023, lakini amri ya kupiga marufuku uuzaji wa saa hizo haikutolewa hadi Agosti 2023.
Mahakama iliamua kuwa Swatch haikuwa imetenda kosa wakati wa kushikiliwa saa hizo.
Lakini katazo la kutouza saa hizo halijabatilishwa, hivyo saa zenye thamani ya dola za kimarekani 14,000 (£10,700), haziwezi tena kuuzwa nchini humo.
Serikali inatakiwa irejeshe saa hizo ndani ya siku 14, mwendesha mashtaka wa serikali Mohammad Sallehuddin Md Ali aliiambia Mahakama Kuu ya Kuala Lumpur leo.
Mamlaka za Misri zinasema watu 17 hawajulikani walipo na 28 wameokolewa baada ya boti ya watalii kuzama katika bahari ya Shamu.
Taarifa kuhusu uwepo wa tatizo ilipokelewa saa 11:30 alfajiri saa za ndani kutoka boti ya Sea Story, ambayo iliondoka bandarini katika mji wa Marsa Alam siku ya Jumamosi kwa safari ya siku tano ya kupiga mbizi na watalii 31 na wafanyakazi 14, kulingana na gavana wa Mkoa wa Shamu.
Meja Jenerali, Amr Hanafi alisema walionusurika walipatikana katika eneo la Wadi el-Gemal, ambalo liko kusini mwa Marsa Alam, na kwa sasa wanapokea huduma ya matibabu.
Aliongeza kuwa meli ya kivita ya Jeshi la Wanamaji la Misri El Fateh na ndege za kijeshi zinazidisha juhudi za kuwatafuta waliotoweka.
Marsa Alam kuna kivutio maarufu kwa watalii kwenye ufuo wa bahari ya Shamu kusini mwa Misri, ambako kuna eneo la kupiga mbizi, ili kutazama miamba ya matumbawe.
Hakuna taarifa kutoka kwa mmiliki na mwendeshaji wa Sea Story yenye makao yake Misri, Dive Pro Liveaboard.
Lakini tovuti yake inasema boti hiyo iliundwa 2022 na ina urefu wa mita 44 (fuit 144). Na inaweza kubeba hadi abiria 36.
Pia unaweza kusoma:
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Angela Merkel ameiambia BBC kuwa vita vya Urusi na Ukraine vingeanza mapema na huenda vingekuwa vibaya zaidi kama sio kuizuia Ukraine kujiunga na Nato mwaka 2008.
"Tungeona mzozo wa kijeshi mapema zaidi. Ilikuwa wazi kwamba Rais Putin asingekaa kimya na kutazama Ukraine ikijiunga na Nato.”
"Na wakati huo, Ukraine kama nchi bila shaka haikuwa na maandalizi kama ilivyokuwa Februari 2022," amesema Merkel mwenye umri wa miaka 70.
Akizungumza na BBC mjini Berlin katika mahojiano ya nadra tangu kuondoka madarakani yapata miaka mitatu iliyopita, Bi Merkel yuko imara katika kutetea maamuzi yake akiwa madarakani.
Lakini Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky hakubaliana na hoja za Markel.
Anasema uamuzi wa Merkel wa kuizuia kujiunga na Nato, ulioungwa mkono na Rais wa wakati huo wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, ni “kufeli kwa hesabu kulikoipa Urusi ujasiri.”
Merkel aliiongoza Ujerumani kwa miaka 16. Alikuwa ofisini wakati wa mzozo wa kifedha, mzozo wa wahamiaji wa 2015 na wakati wa uvamizi wa Urusi wa 2014 nchini Ukraine.
Pia unaweza kusoma:
Katika video iliyotumwa na shirika la habari la NBC kwenye mtandao wa X, mshambuliaji wa Liverpoo, Mohamed Salah, amezungumzia mustakabali wake baada ya msimu na kusema "huenda atakuwa nje ya Liverpool."
"Tunakaribia mwezi wa Disemba na sijapokea mkataba wa kusalia kwenye klabu hiyo, kwa hivyo huenda nikawa nje zaidi kuliko ndani."
Salah amesema, "nimekuwa katika klabu kwa miaka mingi. Kwangu hakuna klabu kama hii, lakini mwisho wake suala hilo haliko mikononi mwangu. Kama nilivyosema, ni Desemba na sijapokea chochote kuhusu mustakabali wangu."
Alipoulizwa ikiwa anakaribia kustaafu, Salah mwenye umri wa miaka 32 amesema,"sitostaafu hivi karibuni. Nautazama msimu huu na napambana kutwaa kombe la Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa pia. Nasikitika lakini tusubiri tuone.”
Julai 2017 Mohamed Salah alijiunga na Liverpool kwa kitita cha pauni milioni 36.9 akitokea klabu ya AC Roma, ya ligi ya Serie A ya Italy.
Pia unaweza kusoma:
Nchi zinazoinukia kiuchumi hazijaridhishwa na makubaliano yaliyoafikiwa katika kongamano la tabia nchi la Umoja wa Taifa (UN), kuhusu kupokea dola bilioni 300 kwa mwaka ili kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Fedha hizo zinalenga kusaidia mataifa yanayoathirika na mabadiliko ya tabia nchi, ambayo ndio yalikuwa kiini cha mazungumzo katika jiji la Baku, huko Azerbaijan.
Ingawa kitita hicho hakikufikia dola trilioni 1.3 nchi zinazoendelea walizozitaka, hawakuwa na budi ila kuzichukua kupambana na makali ya mabadiliko ya tabia nchi.
Washauri wakuu wa kundi la bara la Afrika wameeleza fedha hizo ni kidogo na zimechelewa kuja, huku wajumbe kutoka India wakizitaja pesa hizo kuwa ni “pesa kidogo.”
Katika kongamano hilo lililofanyika wiki mbili, nchi zilizoendelea - zinazoongoza kumiliki viwanda ambavyo huchafua hali ya hewa zimetakiwa ziwajibike zaidi ili kupunguza mabadiliko ya hali ya hewa.
Pia unaweza kusoma:
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imewashutumu Wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kwa kufanya matukio takribani 500 ya ubakaji dhidi ya wanawake tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilipoanza Aprili 2023.
"Kuna takribani kesi 500 za ubakaji zimerekodiwa rasmi na serikali na mashirika ya haki za binadamu, kutoka kwa wanawake waliofanyiwa vitendo hivyo katika maeneo yaliyovamiwa na wanamgambo wa [RSF]," Shirika la Habari Suna, linaloendeshwa na serikali ya Sudan liliripoti jana.
"Wanamgambo hutumia ubakaji kama silaha ya vita kuwalazimisha raia kuhama vijiji na makazi yao, ili kuwaweka mamluki wake na kuziadhibu jamii zinazokataa uwepo wao," inasema ripoti hiyo.
Wizara hiyo inaishutumu RSF kwa utekaji nyara na kuwashikilia mateka mamia ya wanawake na kuwatumikisha kingono na kazi za nyumbani za kulazimishwa.
Ripoti hiyo imekosoa kutojali kwa jumuiya ya kimataifa juu ya ukatili wa RSF dhidi ya wanawake. Na inasema ukatili wao "umezidi ule uliofanywa na Daesh [IS] na Boko Haram na Uganda Lord's Resistance Army."
Wizara hiyo imetoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya RSF na nchi zinazoiunga mkono RFS, na kuziita nchi hizo ni "washirika katika uhalifu huu."
Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu mara kwa mara yamekuwa yakiishutumu RSF kwa kufanya ukatili, ikiwa ni pamoja na ubakaji.
Kundi hilo linakanusha madai hayo.
Pia unaweza kusoma:
Mji wa kaskazini mwa India wa Sambhal uko katika hali ya tahadhari baada ya watu wanne kufariki na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mapigano makali katika msikiti wa Karne siku ya Jumapili.
Mapigano yalizuka kati ya waandamanaji na polisi wakati wa uchunguzi uliofuatiliwa na mahakama wa Shahi Jama Masjid (msikiti), mnara wa Karne ya 16 unaolindwa na serikali.
Mamlaka katika jimbo la Uttar Pradesh, ambako Sambhal iko, wamesajili kesi nne kuhusiana na ghasia hizo na wamesimamisha huduma za mtandao na kufunga shule katika eneo hilo kwa siku moja.
Uchungizi huo uliamriwa na mahakama ya eneo hilo wiki jana, saa chache baada ya ombi kudai kuwa msikiti huo ulikuwa umejengwa kwenye eneo la hekalu lililoharibiwa.
Video na picha za mapigano hayo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha makobazi, matofali na mawe yakiwa yametapakaa katika msikiti huo.
Waandamanaji wanadai kuwa wanaume wanne walipigwa risasi na polisi lakini mamlaka imekanusha hilo.
"Hakuna silaha iliyotumiwa ambayo inaweza kuchukua maisha ya mtu yeyote," Msimamizi wa Polisi Krishan Kumar aliambia gazeti la Hindu.
Mzozo katika Msikiti wa Shahi Jama ni wa hivi karibuni zaidi katika msururu wa mizozo karibu na misikiti nchini humo, ambapo makundi ya Wahindu yamedai kuwa watawala wa Mughal waliharibu mahekalu ili kuyajenga.
Kesi zinazohusu madai hayo kwa sasa zinapigwa vita na makundi ya Waislamu katika mahakama mbalimbali.
Huko Sambhal, mvutano umekuwa ukitokota tangu Jumanne, baada ya mahakama ya eneo hilo kuamuru uchunguzi uliorekodiwa kwa video kuhusu Masjid ya Jama.
Utafiti huo uliamriwa saa chache baada ya maombi kudai kuwa msikiti huo ulijengwa baada ya mtawala wa Mughal Babur kuharibu hekalu la Hari Har katika miaka ya 1520.
Mamlaka huko Uttar Pradesh, ambayo inasimamiwa na Chama cha Bharatiya Janata (BJP), walifanya uchunguzi wa awali wa msikiti siku hiyohiyo.
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya ndege ya mizigo kuanguka karibu na uwanja wa ndege wa Vilnius nchini Lithuania alfajiri ya Jumatatu.
Ndege hiyo, inayoendeshwa kwa DHL na shirika la ndege la Uhispania la Swiftair, ilianguka karibu na nyumba wakati ilikuwa inakaribia kutua, mamlaka za eneo zilisema.
Watu wote 12 wameondolewa salama kutoka kwenye maeneo karibu na eneo la ajali, polisi walisema.
Huduma za uokoaji zilisema wale wote waliokuwa kwenye ndege kutoka Leipzig, Ujerumani, wamepatikana.
Ndege hiyo iliondoka kwenye kituo cha DHL kwenye Uwanja wa Ndege wa Leipzig baada ya saa 3:00 saa za ndani (02:00 GMT) na kuanguka karibu saa moja na nusu baadaye, kulingana na data kutoka kwa tovuti ya ufuatiliaji wa ndege ya Flightradar24.
Zima moto walionekana wakikabiliana na moshi kutoka kwenye jengo lililo kilomita 1.3 (maili 0.8) kaskazini mwa barabara ya kurukia ndege, shirika la habari la Reuters liliripoti.
Chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana na mamlaka ya Lithuania imeanza uchunguzi.
Mkuu wa kitengo cha kuzima moto na huduma za dharura nchini Lithuania, Renatas Pozela, alisema ndege hiyo ilipaswa kutua katika uwanja wa ndege wa Vilnius na "ilianguka kilomita chache kutoka eneo hilo".
Mwanaume mmoja raia wa Uingereza amekamatwa na vikosi vya Urusi alipokuwa akipigania Ukraine, kulingana na ripoti.
Katika video inayosambaa mtandaoni, mwanaume aliyevalia mavazi ya kijeshi anajitambulisha kama James Scott Rhys Anderson, 22, na anasema aliwahi kuwa katika Jeshi la Uingereza.
Shirika la habari la serikali ya Urusi, Tass linanukuu chanzo cha kijeshi kikisema kwamba kile wanachokiita "mamluki wa Uingereza" "alichukuliwa mateka katika eneo la Kursk" nchini Urusi, sehemu ambayo Ukraine imekuwa ikishikiliwa tangu ilipoanzisha mashambulizi ya kushtukiza mwezi Agosti.
Wizara ya Mambo ya Nje ilisema "inaunga mkono familia ya Muingereza kufuatia ripoti za kuzuiliwa kwake".
Katika video hiyo, iliyotumwa kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la ujumbe wa Telegram, Bwana Anderson anamwambia mtu anayemhoji kutoka nyuma ya kamera kwamba alihudumu kama mtu binafsi katika Jeshi la Uingereza kutoka 2019 hadi 2023.
Anasema alijiunga na Jeshi la Kimataifa la Ukraine, kitengo cha kijeshi kinachoundwa na wanaojitolea wa kigeni, baada ya kupoteza kazi yake na kuona ripoti kwenye televisheni kuhusu vita.
Anasema alisafiri kwa ndege hadi Krakow nchini Poland kutoka Luton na kusafiri kutoka huko kwa basi hadi mpaka wa Ukraine.
Ukraine ilianzisha shambulio la kushtukiza mjini Kursk tarehe 6 Agosti, likisonga mbele hadi maili 18 (29km) na kuchukua udhibiti wa karibu kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi.
Urusi imetuma takribani wanajeshi 50,000 katika eneo hilo, na imeanza kutwaa tena maeneo hayo huku kukiwa na mapigano makali.
Unaweza kusoma;
Jeshi la Israel linasema takribani roketi 250 zimerushwa na Hezbollah kuvuka mpaka kutoka Lebanon, na kuashiria moja ya mashambulizi makali zaidi ya Israel tangu mapigano yalipozidi mwezi Septemba.
Watu kadhaa walijeruhiwa na majengo kuharibiwa kaskazini na kati mwa Israel, baadhi yao wakiwa karibu na Tel Aviv, polisi wa Israel walisema.
Mashambulizi hayo yalifuatia shambulizi la anga la Israel katikati mwa Beirut siku ya Jumamosi, ambapo wizara ya afya ya Lebanon ilisema watu 29 waliuawa.
Pia siku ya Jumapili vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwa wingi kuwa Israel na Lebanon zinaelekea kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano ili kumaliza mapigano na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, Hezbollah.
Kufuatia mashambulizi makali kutoka Lebanon, polisi wa Israel wamesema kuwa wamepokea taarifa za vifusi vya roketi kuanguka katika eneo la Tel Aviv.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema shambulio la moja kwa moja katika kitongoji kimoja limeacha "nyumba zikiteketea na magofu".
Roketi zilianguka katika Petah Tikva, karibu na Tel Aviv, na katika baadhi ya maeneo ya kaskazini: Haifa, Nahariya na Kfar Blum, vyombo vya habari vya Israeli viliripoti.
Hezbollah, ambayo hapo awali iliapa kujibu mashambulizi dhidi ya Beirut kwa kulenga Tel Aviv, ilisema kuwa ilirusha makombora ya katika maeneo mawili ya kijeshi katika mji huo na jirani.
Baadaye, IDF ilisema ilikuwa imekamilisha mashambulizi kwenye vituo 12 vya kamandi vya Hezbollah huko Dahieh, ngome ya kundi hilo katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.
Wizara ya afya ya Lebanon siku ya Jumapili iliongeza idadi ya vifo kutoka 20 hadi 29 kutokana na shambulizi kubwa la Israeli liliioanzishwa bila ya onyo katikati mwa Beirut. Ilisema jumla ya watu 84 waliuawa nchini humo siku ya Jumamosi.
Unaweza kusoma;
Takribani watu 24 wamefariki baada ya boti mbili zilizokuwa zimewabeba raia wengi wa Somalia kupinduka katika pwani ya Madagascar, mamlaka za eneo zilisema.
Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilisema juhudi zinaendelea "kuhakikisha kuwa manusura wanarejea salama".
Boti hizo mbili zilibeba jumla ya abiria 70.
Ziligunduliwa zikiwa ziko karibu na pwani ya kaskazini mwa Madagascar siku ya Jumamosi katika Bahari ya Hindi.
Inaaminika injini zao zilifeli. Afisa mkuu wa serikali ya Somalia aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa manusura waliokolewa na wavuvi.
Walionusurika wanasema walikuwa wakijaribu kufikia kisiwa cha Ufaransa cha Mayotte, njia ya kawaida lakini hatari kwa wahamiaji wa Kisomali wanaotafuta hifadhi.
Ukosefu wa ajira na umaskini katika Pembe ya Afrika unawalazimu vijana wengi kuchukua njia hatari ya kufika Ulaya kwa matumaini ya maisha bora.
Mamlaka ya Madagascar ilionya dhidi ya "hatari kali zinazohusiana na uhamiaji haramu" ikipendekeza waathiriwa wa janga hilo walikuwa wahamiaji.
Unaweza kusoma;
Mamlaka ya Pakistani inasema kuwa wameafikiana kuhusu kusitisha mapigano kwa siku saba baada ya zaidi ya watu 80 kuuawa katika ghasia za kidini zilizozuka tena kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Wengine 156 wanasemekana kujeruhiwa katika siku tatu za mapigano katika wilaya ya Kurram, karibu na mpaka wa Afghanistan.
Ghasia hizo zilianza siku ya Alhamisi, wakati watu wenye silaha waliposhambulia misafara ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakisafiri katika eneo hilo chini ya ulinzi wa polisi. Zaidi ya watu 40 walikufa katika tukio hilo, ambalo lilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni wamejihusisha katika mizozo ya kikabila na kimadhehebu kuhusu migogoro ya ardhi kwa miongo kadhaa.
Baada ya mazungumzo siku ya Jumapili, msemaji wa serikali Muhammad Ali Seif alisema kuwa viongozi wote wa Shia na Sunni wamekubali kusitisha ghasia, Reuters na mashirika ya habari ya AFP yaliripoti.
Siku ya Jumapili afisa wa utawala wa eneo hilo aliiambia AFP: "Mapigano na mashambulizi ya msafara mnamo Novemba 21, 22, na 23 yamesababisha vifo vya watu 82 na majeruhi 156." Akizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, alisema kuwa watu 16 kati ya waliofariki ni Sunni na 66 ni wa jamii ya Shia.
Waliouawa katika mashambulizi ya Alhamisi kwenye misafara ni pamoja na wanawake na watoto. Abiria Saeeda Bano alieleza kwa BBC idhaa ya Urdu jinsi alivyohofia kuuawa alipokuwa akijificha chini ya viti vya gari pamoja na watoto wake.
Mamia ya wakazi walikimbia huku kukiwa na ongezeko la ghasia Ijumaa na Jumamosi.