Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
COP 27: Mkutano wamalizika kwa makubaliano ya kihistoria, nchi zilizoathirika na hali ya hewa duniani kulipwa
Mkutano wa kilele wa COP27 umefikia makubaliano na mpango mkubwa wa kihistoria wa hali ya hewa, ambapo pamoja na mengine, kuanzisha mfuko wa fedha za kulipa mataifa masikini kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Suala la kuundwa mfuko wa kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na gharama ya uharibifu unaosababishwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa limeonekana ni suala la kihistoria.
Kilichobaki sasa ni kufuatwa kwa uratibu na vipengele ambavyo Umoja wa Mataifa unapaswa kukubaliana.
'Sauti hatimaye zimesikika - katika ardhi ya Afrika' Akaunti rasmi ya Twitter ya COP27 inapongeza mpango huo "uliosubiriwa kwa muda mrefu" wa kuzindua mfuko wa kusaidia mataifa yaliyoathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.
"Historia imeandikwa," inasema kwenye Twitter. "Katika ardhi ya Afrika, sauti ya jamii zilizoathirika sana hatimaye zimesikika."
Justin Rowlatt, mhariri wa masuala a hali ya hewa BBC, anayeripoti mkutano huo wa COP27 anasema wenyeji wa Misri katika mkutano huu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wamefanikisha kitu cha ajabu.
Wameshughulikia suala ambalo limekuwa kidonda ndugu tangu mazungumzo haya yalipoanza miaka 30 iliyopita - kuhusu nchi zilizo hatarini kusaidiwa kutokana hasara na uharibifu wa mabadiliko ya hali ya hewa ambazo tayari zinasumbua katika jamii zao.
Lakini anasema wakati huo huo hawajaibua nia ya kukabiliana na chanzo kikuu cha mabadiliko ya hali ya hewa - ambacho ni uzalishaji wa gesi chafu ambayo inaongeza joto kwenye sayari yetu.
Uchambuzi wake unaeleza kwa hakika, kwa kuanzisha aina mpya ya nishati ya inayotoa"chafu kidogo" wengi wanaamini kuwa wamerejea kile kilichokubaliwa katika mkutano uliopita wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa huko Glasgow.
Nchi za Umoja wa Ulaya zimeashiria utayari wa kufikia maelewano kuhusu ufadhili kwa nchi zilizo hatarini.
Hata hivyo zimeeleza wazi kwamba hazitosaini makubaliano ambayo yataenda kinyume na malengo ya kupunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia nyuzi 1.5 katika kipimo cha Celsius.
Mkutano huo uliokuwa umalizike Ijumaa, umelazimika kusogezwa mbele kwa siku mbili zaidi mpaka usiku wa manane ili kufikia makubaliano hayo yaliyochukua muda.
Zaidi ya nchi 200 zimeshiriki na kukubaliano mpango huo ambao, nchi nyingi za Afrika zinanufaika.
Ikiwa sasa zinasubiri utararibu rasmi wa uamuzi huo, lakini haitarajiwa kuchelewa kuchukuliwa hatua kwa kuwa mkutano ujao wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 utakaofanyika mwezi Novemba, 2023, utapokea ripoti ya hatua zilizochukuliwa.