Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mnibake mimi na sio binti zangu' - vita vya kutisha vya Sudan
- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, BBC Africa correspondent, Omdurman
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Sudan iko katika hali mbaya.
Baada ya miezi 17 ya vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoiangamiza nchi hiyo, jeshi limefanya mashambulizi makubwa katika mji mkuu Khartoum, yakilenga maeneo yaliyo mikononi mwa mpinzani wake mkali, Kikosi cha RSF
RSF iliteka sehemu kubwa ya Khartoum mwanzoni mwa mzozo, wakati jeshi linadhibiti mji pacha wa Omdurman, ng'ambo ya Mto Nile.
Lakini bado kuna mahali ambapo watu wanaweza kuvuka kati ya pande hizo mbili.
Wakati mmoja, nilikutana na kikundi cha wanawake ambao walikuwa wametembea kwa saa nne hadi sokoni katika eneo linalodhibitiwa na jeshi kwenye ukingo wa Omdurman, ambapo chakula ni cha bei nafuu.
Wanawake hao walikuwa wametoka Dar es Salaam, eneo linaloshikiliwa na RSF.
Waume zao walikuwa hawaondoki tena nyumbani, waliniambia, kwa sababu wapiganaji wa RSF waliwapiga, walichukua pesa zozote walizopata, au waliwaweka kizuizini na kudai malipo ya kuachiliwa kwao.
“Tunavumilia ugumu huu kwa sababu tunataka kuwalisha watoto wetu. Tuna njaa, tunahitaji chakula,” alisema mmoja.
Onyo: Baadhi ya maelezo katika taarifa hii yanaweza kuwa ya kukera
Na wanawake, nikauliza, walikuwa salama kuliko wanaume? Vipi kuhusu ubakaji?
Kilio cha sauti kilipungua.
Kisha mmoja ililipuka.
"Dunia iko wapi? Kwanini msitusaidie?" Alisema maneno yake yakimtoka kwa kishindo huku machozi yakimtoka.
"Kuna wanawake wengi hapa ambao wamenyanyaswa, lakini hawazungumzi. Hata hivyo ingeleta tofauti gani?"
"Wasichana wengine, RSF inawafanya walale mitaani usiku," aliendelea. "Ikiwa watachelewa kurudi kutoka soko hili, RSF inawashikilia kwa siku tano au sita."
Akiwa anaongea mama yake aliinamisha kichwa chake mkononi huku akilia. Wanawake wengine waliokuwa karibu naye pia walianza kulia.
"Wewe katika ulimwengu wako, ikiwa mtoto wako atatoka, utamwacha?" Aliuliza “Si utakwenda kumtafuta? Lakini tuambie, tunaweza kufanya nini? Hakuna kitu mikononi mwetu, hakuna anayetujali. Dunia iko wapi? Kwa nini msitusaidie!”
Sehemu ya kuvuka ilikuwa dirisha katika ulimwengu wa kukata tamaa na mahangaiko.
Wasafiri walielezea kukabiliwa na visa vya uvunjaji sheria, uporaji na ukatili katika mzozo ambao Umoja wa Mataifa unasema umewalazimu zaidi ya watu milioni 10.5 kukimbia makazi yao.
Lakini ni unyanyasaji wa kijinsia ambao umekuwa sifa kuu ya mzozo huo wa muda mrefu, ambao ulianza kama vita vya kuwania madaraka kati ya jeshi na RSF lakini tangu wakati huo umeingiliwa na makundi yenye silaha na wapiganaji kutoka nchi jirani.
Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema ubakaji unatumiwa kama "silaha ya vita".
Ujumbe wa hivi majuzi wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa uliandika matukio kadhaa ya vitisho vya ubakaji na ubakaji kutoka kwa wanajeshi, lakini uligundua kuwa unyanyasaji mkubwa wa kingono ulifanywa na RSF na wanamgambo washirika wake, na ulifikia ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Mwanamke mmoja ambaye BBC ilizungumza naye alilaumu RSF kwa kumbaka.
Tulikutana naye sokoni kwenye kivuko, kinachoitwa Souk al-Har - Soko la Joto.
Tangu vita kuanza soko limepanuka katika ardhi kame kwenye barabara ya jangwa nje ya Omdurman, na kuwavutia watu fukara zaidi kwa sababu ya bei yake ya chini ya bidhaa
Miriam, (sio jina lake halisi), alikuwa ametoroka nyumbani kwake Dar es Salaam na kwenda kukimbilia kwa kaka yake.
Sasa anafanya kazi katika duka la chai. Lakini mwanzoni mwa vita, alisema, watu wawili wenye silaha waliingia nyumbani kwake na kujaribu kuwabaka binti zake - mmoja wa miaka 17 na mwingine 10.
"Niliwaambia wangu wasichana wabaki nyuma yangu na nikawaambia RSF: 'Iwapo mnataka kumbaka mtu yeyote basi mtanibaka mimi" alisema.
“Walinipiga na kuniamuru nivue nguo. Kabla sijazitoa, niliwaambia wasichana wangu waondoke. Walichukua watoto wengine na kuruka juu ya uzio. Kisha mmoja wa wale watu akanilalia.”
RSF imewaambia wachunguzi wa kimataifa kwamba imechukua hatua zote muhimu ili kuzuia unyanyasaji wa kingono na aina nyingine za unyanyasaji ambazo zinajumuisha ukiukwaji wa haki za binadamu.
Lakini simulizi za unyanyasaji wa kijinsia ni nyingi na matokeo yake yana athari ya kudumu.
Akiwa ameketi kwenye kiti kidogo kwenye kivuli cha safu ya miti, Fatima, (si jina lake halisi) aliniambia alikuwa amekuja Omdurman kujifungua mapacha, na alipanga kubaki.
Mmoja wa majirani zake, alisema, msichana mwenye umri wa miaka 15, pia amepata ujauzito, baada ya yeye na dada yake mwenye umri wa miaka 17 kubakwa na askari wanne wa RSF.
Watu waliamshwa na mayowe na kutoka nje kuangalia kinachoendelea, alisema, lakini watu wenye silaha waliwaambia wangepigwa risasi ikiwa hawatarudi kwenye nyumba zao.
Asubuhi iliyofuata, waliwakuta wasichana wawili wakiwa na dalili za unyanyasaji kwenye miili yao, na kaka yao mkubwa amefungiwa katika moja ya vyumba.
"Wakati wa vita, tangu RSF ilipowasili, mara moja tulianza kusikia kuhusu visa vya ubakaji, hadi tukashuhudia mbele yetu kwa majirani zetu," Fatima alisema. "Hapo awali tulikuwa na mashaka [kuhusu ripoti] lakini tunajua kwamba ni RSF ambao waliwabaka wasichana."
Wanawake wengine wanakusanyika kuanza safari ya kurejea nyumbani katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF - wao ni maskini sana, wanasema, kuanza maisha mapya kama Miriam alivyofanya kwa kuondoka Dar es Salaam.
Kwa muda wote vita hivi vikiendelea, hawana budi ila kurudi kwenye maovu yake.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah