Trump amshutumu Xi kwa kula njama dhidi ya Marekani pamoja na Putin na Kim
Maoni ya Trump yamekuja wakati Uchina ikiwa mwenyeji wa viongozi wa ulimwengu katika gwaride kubwa zaidi la Siku ya Ushindi huko Beijing Jumatano - onyesho la nguvu za kijeshi za Uchina.
Muhtasari
- Zelensky aliahidi kujadili vikwazo dhidi ya Urusi na Trump katika siku za usoni
- Makundi ya kutetea haki za binadamu yalaani sheria dhidi ya LGBTQ+
- Mafuriko yaua 30 na kuzamisha vijiji 1,400 katika jimbo la India
- Israel yaanza kuwahamasisha askari wa akiba kabla ya shambulio la Gaza
- Trump anamshutumu Xi kwa kula njama dhidi ya Marekani pamoja na Putin na Kim
- Sarafu ya kidigitali ya familia ya Trump yazinduliwa, na kuongeza mali yake hadi karibu dola bilioni 5.
- Putin amshukuru Kim kwa mapigano ya Korea Kaskazini nchini Ukraine
- Jopo la Bunge la Marekani latoa nyaraka nyingi za faili za Epstein
- Mahakama yamuondolea Cardi B mashtaka ya kumshambulia mlinzi huko Los Angeles
- Video: Tazama China ikionesha uwezo wake wa kijeshi katika gwaride
- Ahukumiwa kifo kwa kumchoma moto mkewe akiwa hai kwa rangi yake
- Maelfu ya wanajeshi wa akiba wa Israel waripoti kazini kabla ya kushambulia mji wa Gaza
- Marekani yashambulia meli iliyobeba dawa za kulevya
- Xi apongeza 'China isioweza kuzuilika' na kuzindua silaha mpya kuonyesha nguvu yake
Moja kwa moja
Na Asha Juma na Dinah Gahamanyi
Zelensky aliahidi kujadili vikwazo dhidi ya Urusi na Trump katika siku za usoni

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Zelensky anashiriki katika mkutano huo na nchi za Baltic na Kaskazini mwa Ulaya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema hivi karibuni kuwa atajadiliana na Donald Trump uwezekano wa kuanzishwa kwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi, huku Trump akiendelea kukataa mkutano wa kilele wa Urusi na Ukraine.
Zelensky alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen alipofanya ziara nchini humo.
"Tunaposema, ikiwa hakuna mkutano [kati ya Zelensky na Vladimir Putin ], basi toa msaada kwa njia ya misaada, kwa namna ya vikwazo," rais wa Ukraine alisema akinukuliwa na shirika la Interfax-Ukraine :"Tuliwasilisha ishara hizi kwa rais wa Marekani, alisema wiki chache zilizopita kwamba atatoa aina fulani ya jibu, alisema kuwa katika wiki chache...inaweza kuwa wiki mbili au tatu. Tutazungumza na rais wa Marekani leo au siku chache zijazo na kufafanua suala hili."
Trump alisema hatua inayofuata kuelekea kumaliza vita nchini Ukraine inapaswa kuwa mkutano wa kibinafsi kati ya Putin na Zelensky.Rais huyo wa Marekani pia aliahidi kuchukua hatua mpya dhidi ya Urusi ikiwa mkutano huo hautafanyika.
Siku ya Jumatano, mkutano wa "muungano wa walio tayari" (au "muungano wa walioazimia"), kikundi cha washirika wa Ukraine walio tayari kutoa dhamana ya usalama, utafanyika Paris.
Washiriki wameelezea uwezekano wa kumpigia simu Trump wakati wa mkutano.
Unaweza kusoma:
Makundi ya kutetea haki za binadamu yalaani sheria za Burkina Faso dhidi ya LGBTQ+

Chanzo cha picha, AFP
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Amnesty International na Huma Rights Watch, yamelaani sheria mpya ya serikali inayotawala Burkina Faso, na kuharamisha mapenzi ya jinsi moja.
Nchi hiyo ya Sahel ilijiunga na orodha inayokua ya nchi za Afrika zinazosukuma sera za kupinga mapenzi ya jinsi moja na LGBTQ+ kwa ujumla kote barani Afrika.
Siku ya Jumatatu, bunge la mpito ambalo halijachaguliwa nchini humo lilipitisha muswada wa kupiga marufuku vitendo vya mapenzi ya jinsi moja, zaidi ya mwaka mmoja baada ya rasimu hiyo kupitishwa na baraza la mawaziri.
Maafisa wa serikali wanaielezea sheria hiyo kama muhimu katika kulinda maadili ya jadi, huku serikali ikisema inakusudiwa kudumisha kanuni za ndoa na familia.
Amnesty International iliita "kurudi nyuma kwa kutisha," na kuitaka serikali ya kijeshi kufikiria upya sheria hiyo na majukumu ya kimataifa ya Burkina Faso chini ya mikataba ya kikanda na kimataifa ya haki za binadamu.
Marceau Sivieude, Mkurugenzi wa kanda wa Amnesty International wa Afrika Magharibi na Kati, alisema kuwa sheria hiyo, "inaleta ubaguzi na inakiuka haki ya usawa mbele ya sheria." Alisema kuwa ni kinyume na kkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu na mkataba wakimataifa wa haki za kiraia na kisiasa, yote iliyoidhinishwa na Burkina Faso.
Human Rights Watch pia ilisema kuwa, wanachama wa jamii ya LGBT walikuwa tayari wanaishi kwa hofu. Larissa Kojoue, mtafiti wa Haki za LGBT barani Afrika wa Human Rights Watch, aliiambia BBC kwamba hofu hiyo ilianza miaka miwili iliyopita na imefikia hatua kwamba wengi wa jumuiya ya LGBTQ+ hawawezi hata kuondoka majumbani mwao.
"Ninawasiliana na shirika la haki za kiasi, Mtandao wa Vijana wa Kiafrika wa Queer, ambao wana makao yao huko Ouagadougou. Na imekuwa miezi minne au mitano bila kwenda ofisini kwao, kwasababu wameona kuwa anwani yao imeshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii na watu walikuwa wakitishia kuwavamia," Bi Kojoue alisema.
Alieleza kuwa baadhi ya watu wanaojulikana kama wanaharakati wa LGBT wanaondoka nchini - wakiacha kila kitu nyuma ili kulazimika kwenda uhamishoni kwa kuhofia kukamatwa.
Kulingana na yeye, watu ambao walikuwa wakipinga na walikuwa wakijaribu wawezavyo kukaa nchini kufanya kazi zao watapata shida kukaa kwasababu ya sheria kwani wengi wao sasa wanahofia maisha yao. Wangeweza kupelekwa jela.
Mwaka jana, nchi jirani ya Mali, mshirika wa Burkina Faso na pia inayotawaliwa na jjeshi , ilipitisha sheria ya kuhalalisha ushoga.
Kumekuwa na upinzani mkubwa na ukosoaji dhidi ya nchi ambazo zimeimarisha msimamo wao wa kupinga mampenzi ya jinsi moja katika miaka ya hivi karibuni.
Ghana, Nigeria, na Uganda ni miongoni mwa nchi barani ambazo zimetunga sheria zinazopiga marufuku mapenzi ya jinsi moja na LGBTQ+ kwa ujumla.
Kati ya nchi zote, Uganda ilipitisha vifungu vikali zaidi, na kufanya 'mapenzi ya jinsi moja ' kunaweza kuwa kosa la kifo na kuweka vifungo vya maisha kwa mahusiano ya jinsi moja.
Unaweza pia kusoma:
Mafuriko yaua 30 na kuzamisha vijiji 1,400 katika jimbo la India

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 350,000 wameathiriwa na mvua hiyo iliyokithiri Takriban watu 30 wamekufa na zaidi ya 354,000 wameathiriwa na mvua kubwa na mafuriko katika jimbo la kaskazini la India la Punjab.
Mamlaka imetangaza kuwa wilaya zote 23 za jimbo hilo zimekumbwa na mafuriko, baada ya mito na hifadhi kuongezeka hadi kufikia viwango vya hatari.
Takriban watu 20,000 wamehamishwa kutoka maeneo ya mabondeni na yaliyoathiriwa na mafuriko, huku mamia ya kambi za misaada zikianzishwa ili kutoa makazi na vifaa muhimu kwa familia zilizoathiriwa.
Akitoa wito kwa nchi "kusimama karibu na serikali", Waziri Mkuu wa Punjab Bhagwant Mann alisema haya ndio mafuriko mabaya zaidi ambayo jimbo hilo limewahi kuona tangu 1988.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Timu nyingi za kukabiliana na maafa, pamoja na jeshi, wanasaidia shughuli za uokoaji Timu nyingi za kukabiliana na maafa, pamoja na jeshi, wanasaidia shughuli za uokoaji
Punjab mara nyingi hujulikana kama "kikapu cha chakula" cha India na ni chanzo kikuu cha uzalishaji wa kilimo, hasa wa vyakula vikuu kama ngano na mchele.
Serikali inasema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazao katika baadhi ya hekta 148,000 za ardhi ya kilimo, ambayo imezamishwa chini ya maji.
Robo ya watu milioni 30 wa Punjab wanategemea kilimo, na hivyo kuzua wasiwasi wa haraka kuhusu maisha ya vijijini.
Israel yaanza kuwahamasisha askari wa akiba kabla ya shambulio la Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Makumi kwa maelfu ya askari wa akiba wa Israel wameanza kuripoti kwa jeshi, kabla ya mashambulizi mapya katika mji wa Gaza ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anataka kuyaanza haraka licha ya onyo kutoka kwa maafisa wakuu.
Redio ya Jeshi la Israel ilisema kuwa takriban wanajeshi 40,000 wa akiba wataripoti kazini siku ya Jumanne kwa shambulio katika mji wa Gaza.
Jeshi lilitangaza kuwa linajiandaa kivifaa kuwachukua wanajeshi wa akiba kabla ya shambulio hilo.
Baraza la mawaziri la usalama likiongozwa na Netanyahu, liliidhinisha mpango wa kupanua kampeni katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kuudhibiti mji wa Gaza, ambapo vikosi vya Israel vilipambana na Hamas katika hatua za mwanzo za vita.
Israel kwa sasa inadhibiti takriban asilimia 75 ya Ukanda wa Gaza, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Soma zaidi:
Trump amshutumu Xi kwa kula njama dhidi ya Marekani pamoja na Putin na Kim

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Maelezo ya picha, Donald Trump na Xi Jinping wakisalimiana kwa mikono wakati wa mkutano wa waandishi wa habari huko Beijing mnamo 2017. Rais wa Marekani Donald Trump amemshutumu mwenzake wa China Xi Jinping kwa kula njama dhidi ya Marekani na viongozi wa Urusi na Korea Kaskazini.
Maoni ya Trump yalikuja wakati Uchina ikiwa mwenyeji wa viongozi wa ulimwengu katika gwaride kubwa zaidi la Siku ya Ushindi huko Beijing Jumatano - onyesho la nguvu za kijeshi za Uchina.
Katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump aliandika: "Tafadhali fikisha salamu zangu za dhati kwa Vladimir Putin na Kim Jong Un unapopanga njama dhidi ya Marekani."
Hapo awali Trump alikataa maoni kwamba kuongezeka kwa joto kwa uhusiano kati ya China, Urusi na mataifa mengine kunaleta changamoto kwa Marekani katika hatua ya kimataifa.
Katika mitandao ya kijamii, rais wa Marekani pia alitaja "msaada mkubwa na 'damu'" ambayo Marekani ilitoa kwa China wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Gwaride la China linaadhimisha miaka 80 ya Japan kujisalimisha katika vita na ushindi wa China dhidi ya jeshi linaloikalia kwa mabavu.
"Wamarekani wengi walikufa katika jitihada za Uchina za kile kinachoitwa Ushindi na Utukufu. Natumaini kwamba wanaheshimiwa na kukumbukwa kwa ushujaa na kujitolea kwao!"
Xi alijumuika katika gwaride hilo na wakuu 26 wa nchi, akiwemo Kim na Putin - wanaotazamwa na baadhi ya waangalizi kama wajumbe wanaoepukwa na Magharibi.
Uchina imejaribu kujiweka kama taifa lenye uwezekano wa kukabiliana na Marekani tangu ushuru wa Trump ulipotikisa utaratibu wa kiuchumi na kisiasa duniani.
Trump ameutaja ushuru wake kama muhimu kwa kulinda masilahi ya Marekani. Inaonekana kwamba gharama yoyote ya kidiplomasia ni kitu ambacho yuko tayari kulipa.
Alipoulizwa na BBC kama anaamini Beijing na washirika wake walikuwa wakijaribu kuunda muungano wa kimataifa kupinga Marekani, Trump alisema: "Hapana. Hapana. China inatuhitaji."
Aliongeza: "Nina uhusiano mzuri sana na Rais Xi, kama unavyojua. Lakini China inatuhitaji zaidi ya tunavyowahitaji. Sioni hilo hata kidogo.
Soma zaidi:
Sarafu ya kidigitali ya familia ya Trump yazinduliwa, na kuongeza mali yake hadi karibu dola bilioni 5.

Chanzo cha picha, Bloomberg/Getty
Maelezo ya picha, Familia ya Trump ilizindua kampuni ya cryptocurrency World Liberty Financial wakati wa kampeni ya urais ya Trump mwaka jana Sarafu ya kidijitali (cryptocurrency) inayoungwa mkono na familia ya Trump, World Liberty Financial, imeanza biashara ya umma, na hivyo kuongeza thamani ya mali inayoshikiliwa na Rais wa Marekani Donald Trump na watoto wake hadi takriban dola bilioni 5.
Familia ya Trump ilizindua kampuni ya World Liberty Financial, kampuni ya fedha taslimu, wakati wa kampeni ya urais ya Trump mwaka jana, na kuibua maswali kuhusu mgongano wa kimaslahi unaoweza kutokea wakati Rais Trump alipokuwa mshirika katika tasnia aliyopanga kudhibiti.
Kampuni hiyo ilichangisha pesa kwa kuuza sarafu yake ya siri isiyojulikana kwa wawekezaji ambao hapo awali walikuwa chini ya marufuku ya kuuza sarafu hizi.
Lakini wawekezaji walipiga kura Julai iliyopita kuwaruhusu wanunuzi wa mapema kuuza hadi asilimia 20 ya mali zao, inayojulikana kama WLFI. Uamuzi huo uliwatenga waanzilishi kama familia ya Trump, ambao hawangeweza kuuza hisa yoyote.
Kufikia Jumanne, WLFI ilikuwa ikifanya biashara kwa $0.22 kwa kubadilishana kama Binance na Coinbase, baada ya kushuka kwa bei kwa takriban asilimia 50 tangu kuanza kwa biashara Jumatatu.
Unaweza pia usoma:
Putin amshukuru Kim kwa mapigano ya Korea Kaskazini nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Urusi Vladimir Putin wa Urusi amemshukuru Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kwa ujasiri wa wanajeshi wake ambao wamekuwa wakipigana nchini Ukraine upande wa Urusi.
Viongozi hao wawili walikutana Jumatano mjini Beijing wakati Uchina ilipokuwa ikifanya moja ya gwaride kubwa zaidi kuwahi kutokea la kijeshi, ambalo linaadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia barani Asia.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa viongozi wa dunia. Yeye huondoka Korea Kaskazini mara chache, na kwa kawaida hukutana na viongozi mmoja-mmoja.
Putin, ambaye alianzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022, alisema uhusiano wa nchi mbili kati ya Urusi na Korea Kaskazini ni wa kirafiki na kwamba jeshi la Pyongyang lilisaidia kulikomboa eneo la Kursk.
"Askari wako walipigana kwa ujasiri na kwa ushujaa," Putin alimwambia Kim wakati wa mazungumzo ya Jumatano.
"Ningependa kutambua kwamba hatutasahau kamwe kujitolea kwa majeshi yako na familia namna wanajeshi wako walivyotesema."
Kim alitoa shukrani zake kwa kiongozi huyo wa Urusi kwa kuwashukuru wanajeshi wa Korea Kaskazini na kusema uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo mbili umekuwa "ukiendelea katika maeneo yote" - akimaanisha kuhusika kwa Pyongyang katika "mapambano ya pamoja" na Urusi huko Ukraine.
"Ikiwa kuna njia yoyote tunaweza kuisaidia Urusi, bila shaka tutafanya kama jukumu la kidugu."
Kulingana na Korea Kusini, Kaskazini imetuma wanajeshi 15,000 kuisaidia Urusi katika uvamizi wake , pamoja na makombora na silaha za masafa marefu. Inaaminika kwa upande mwingine Korea Kaskazini ilipokea chakula, pesa na usaidizi wa kiufundi kutoka Urusi.
Soma zaidi:
Jopo la Bunge la Marekani latoa nyaraka nyingi za faili za Epstein

Chanzo cha picha, Department of Justice
Jopo la bunge la Marekani limetoa nyaraka nyingi zinazohusiana na uchunguzi unaondeshwa na serikali juu ya kashfa ya ngono inayomuhusu bilionea marehemu Jeffyer Epstein.
Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi ilichapisha kurasa 33,295, zikiwemo kumbukumbu za safari za ndege, video ya uchunguzi wa jela, faili za mahakama, rekodi za sauti na barua pepe.
Lakini Republicasn na Democrats walisema faili hizo zilikuwa na taarifa finyu sana na haijulikani ikiwa idara ya haki inashikilia rekodi zingine za Epstein.
Shinikizo limekuwa likiongezeka kutoka kwa wafuasi wa Rais Donald Trump mwenyewe wakitaka uwazi zaidi juu ya uchunguzi wa kesi hiyo baada ya idara ya haki kusema mnamo mwezi Julai kuwa hakuna "orodha ya wateja" wa Epstein.
Soma zaidi:
Mahakama yamuondolea Cardi B mashtaka ya kumshambulia mlinzi huko Los Angeles

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki nyota wa muziki wa Pop, Cardi B amepata ushindi mahakamani dhidi ya mlinzi aliyewasilisha kesi ya dola milioni 24 akimtuhumu mwimbaji huyo ambaye alikuwa mjamzito wakati huo kwa kumpiga kimwili nje ya ofisi ya daktari wa masuala ya uzazi huko Beverly Hills mwaka 2018.
Majaji 12 wa Mahakama ya Juu ya Los Angeles walijadili kwa chini ya saa moja kabla ya kufikia uamuzi wa pamoja uliomuunga mkono msanii huyo mwenye umri wa miaka 32, aliyeshinda tuzo ya Grammy, ambaye nyimbo zake zilizovuma ni pamoja na "Taki Taki" na "I Like It."
Majaji waligundua kuwa mlinzi huyo wa zamani Emani Ellis, alishindwa kuthibitisha kwa uthabiti madai kwamba Cardi B alimshambulia kimwili na kumkwaruzwa usoni kwa kucha, akamtemea mate na kumrushia maneno makali ya ubaguzi wa rangi. Wanawake wote wawili ni Weusi.
Ellis alitoa ushahidi wakati wa kesi hiyo kwamba alimtaka Cardi B kuondoka kwenye maeneo ya jengo hilo la matibabu kwa sababu "alisababisha usumbufu."
Akitoa shahidi katika utetezi wake mwenyewe, Cardi B alieleza kuwa Ellis ndiye mchokozi katika kile mwimbaji huyo alichoita "mabishano ya maneno" ambayo yalianza wakati Ellis, ambaye wakati huo alikuwa kazini akiwa amevaa sare yake, alipoanza "kuingilia faragha yangu."
Kulingana na Cardi B, Ellis alianza kumfuata na kujaribu kumchukua video mwimbaji huyo alipokuwa akienda kwa daktari wa masuala ya uzazi alipokuwa mjamzito lakini alikuwa bado mwenyewe hajatangaza hadharani ujauzito huo.
Video: Tazama China ikionesha uwezo wake wa kijeshi katika gwaride
Maelezo ya video, Uwezo wa kijeshi wa China Rais Xi Jinping alionesha uwezo wa kijeshi wa China na kuzindua silaha mpya wakati wa gwaride mjini Beijing, kuadhimisha miaka 80 tangu Japan kujisalimisha katika Vita vya Pili vya Dunia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dunia akiwemo rais wa Urusi Vladimir Putin kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Ahukumiwa kifo kwa kumchoma moto mkewe akiwa hai kwa rangi yake

Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo yanaweza kuwa ya kuhuzunisha.
Mahakama nchini India imetoa hukumu ya kifo kwa mwanamume mmoja kwa kumchoma moto mkewe akiwa hai kwa sababu ya ubaguzi wa rangi.
Katika taarifa zake kabla ya kifo chake, Lakshmi alisema kwamba mumewe Kishandas "mara kwa mara alimdhihaki kwa kuwa na ngozi nyeusi".
Jaji wa Wilaya Rahul Choudhary katika mji wa kaskazini wa Udaipur alielezea hukumu ya kifo akisema mauaji yaliyotekelezwa ni "nadra sana" na "ni uhalifu dhidi ya binadamu".
Wakili wa Kishandas aliambia BBC kuwa mteja wake hana hatia na kwamba watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Mauaji ya Lakshmi miaka minane nyuma na hukumu iliyotolewa mwishoni mwa juma, yamegonga vichwa vya habari katika nchi ambayo inashuhudia visa vingi vya ubaguzi wa rangi.
Shambulizi hilo dhidi ya Lakshmi lilifanyika usiku wa tarehe 24 Juni 2017, kulingana na amri ya mahakama iliyoonekana na BBC.
Hukumu hiyo inanukuu taarifa ambazo mwanamke huyo alizitoa kabla ya kifo chake kwa polisi, madaktari na hakimu mtendaji.
Lakshmi alisema mumewe mara nyingi alimwita "kali" au ngozi nyeusi na kumwaibisha tangu walipofunga ndoa yao mnamo 2016.
Pia unaweza kusoma:
Maelfu ya wanajeshi wa akiba wa Israel wafika kazini kabla ya kushambulia mji wa Gaza

Chanzo cha picha, EPA
Maelfu ya wanajeshi wa akiba wameanza kuripoti kazini huku jeshi la Israel likiendelea na mikakati yake kufanya mashambulizi ya kuuteka mji wa Gaza.
Vikosi vya ardhini tayari vinasonga mbele katika viunga vya eneo kubwa zaidi la mjini Gaza, ambalo jeshi limesema ni ngome ya Hamas.
Mji huo pia unakabiliwa na mashambulizi makubwa ya anga na mizinga ya Israel, huku hospitali za eneo hilo zikisema kuwa zaidi ya Wapalestina 50 wameuawa tangu usiku wa manane.
Jeshi limewaamuru wakaazi kuhama na kuelekea kusini mara moja. Umoja wa Mataifa unasema takriban 20,000 wamefanya hivyo katika muda wa wiki mbili zilizopita, lakini karibu milioni wamesalia.
Marekani yashambulia meli iliyobeba dawa za kulevya

Chanzo cha picha, Donald Trump/Truth Social
Rais Donald Trump anasema Marekani imeshambulia meli ya kubeba dawa za kulevya kusini mwa Karibea, na kuwauwa "mabwanyenye 11 wa ulanguzi wa dawa za kulevya ".
Alichapisha kwenye mitandao ya kijamii kwamba operesheni ya kijeshi ya Marekani Jumanne iliwalenga wanachama wa genge la Venezuela la Tren de Aragua.

Chanzo cha picha, Getty Images
Trump alisema meli hiyo ilikuwa katika maji ya kimataifa ikisafirisha mihadarati iliyokuwa ikielekea Marekani.
Utawala wa Trump umeongeza shinikizo za kijeshi na kisiasa dhidi ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kutoa zawadi ya $50m (£37m) kwa atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwake kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya.
Maduro ameapa Venezuela itapambana na jaribio lolote la kuingilia kijeshi la Marekani.
Soma zaidi:
Xi apongeza 'China isioweza kuzuilika' na kuzindua silaha mpya kuonyesha nguvu yake

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa China Xi Jinping ameonya kwamba ulimwengu unakabiliwa na chaguo kati ya amani au vita wakati akifanya gwaride kubwa zaidi la kijeshi nchini mwake Jumatano, akiwa na Vladimir Putin wa Urusi na Kim Jong Un wa Korea Kaskazini.
"Leo, binadamu anakabiliwa na chaguo la amani au vita, mazungumzo au mzozo, ushindi kwa pande zote mbili au upande mmoja," Xi aliambia umati wa watazamaji zaidi ya 50,000 huko Tiananmen Square, na kuongeza kuwa watu wa China "wanasimama upande stahiki wa historia".
Wakati wa gwaride hilo China imeonyesha silaha ikiwa ni pamoja na ya laser ya LY-1 ambayo iliwekwa juu ya lori la kivita la Wheeler Hz-155.
Silaha hii ya laser inasemekana kuwa na nguvu sana na inaweza kulemaza au kuchoma vifaa vya kielektroniki, au hata kuziba marubani, alisema mchambuzi wa utetezi Alexander Neill.
Tukio hilo la kifahari la kuadhimisha miaka 80 tangu kushindwa kwa Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia limeepukwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa Magharibi, kutokana na vita vya Ukraine na msimamo wa Kim juu ya silaha za nyuklia.
Ni mara ya kwanza viongozi watatu wote kuonekana pamoja hadharani huku wengine zaidi wakijiunga nao.
Soma zaidi:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 03/09/2025.

