Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mzozo wa DRC: Rwanda yaikosoa Uingereza kwa kuiekea vikwazo

Uingereza inasema imesitisha misaada kwa Rwanda kufuatia hatua yake ya kuunga mkono kundi la waasi la M23.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Yusuf Mazimu

  1. Shukran kwa kufuatilia matangazo haya ya moja kwa moja. Usiku mwema

  2. WFP yasitisha shughuli za misaada Sudan

    Programu ya Chakula Duniani ya Umoja wa Mataifa (WFP) imesitisha kwa muda shughuli zake katika kambi ya Zam Zam, iliyoko Darfur Kaskazini, kutokana na mzozo unaoendelea na vita vinavyokithiri.

    Mamlaka ya WFP imetangaza kuwa imewaondoa maafisa wake kutoka kambi hiyo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

    WFP ililazimika kusitisha misaada ya chakula katika kambi hiyo baada ya mashambulizi kutoka kwa waasi wa RSF, ambayo yalifanyika karibu na kambi na kusababisha idadi kubwa ya watu kuomba hifadhi humo.

    Waziri wa masuala ya kigeni wa serikali ya kijeshi ya Sudan ameiambia BBC kwamba ana wasiwasi kuwa suluhu ya mzozo huu huenda isiwepo, akiwataka waasi wa RSF kuachilia silaha wanazozimiliki.

    Aidha, alisema anahofia kwamba vita vinaweza kuendelea hadi mwezi wa Ramadhani, wakati ambapo waumini wa Kiislamu hufunga kula na kuepuka maasi.

    Mzozo huo umewalazimu watu milioni 12 kukimbia makazi yao. Maelfu ya raia wameuawa, huku RSF na jeshi wakituhumiwa kufanya ukatili.

    Soma pia:

  3. Wanandoa walalamikia tukio la maiti kuwekwa karibu yao katika ndege

    Wanandoa wawili raia wa Australia wamezungumza juu ya "mshtuko" walioupata baada ya mwili wa abiria aliyefariki kuwekwa karibu yao kwenye ndege ya Qatar Airways.

    Wakizungumza na Cahnnel 9, Mitchell Ring na Jennifer Colin, wanasema walikuwa wakisafiri kwenda Venice, Italy kwa mapumziko na mwanamke aliyekuwa kando yao alifariki wakati wa safari ya kutoka Melbourne kwenda Doha.

    Wanandoa hao wanasema wafanyakazi wa ndege hiyo waliiweka maiti iliyofunikwa blanketi, karibu na Ring kwa saa nne zilizosalia za safari bila ya Ring kumhamisha, licha ya kuwa kulikuwa na viti tupu.

    Qatar Airways inasema imeomba radhi kwa "usumbufu wowote ambao uliosababishwa na tukio hilo," na kuongeza kuwa iko katika harakati za kutafuta kuwasiliana na abiria hao.

    Wanandoa hao wanasema hawajatafutwa au kupewa msaada na Qatar Airways au Qantas, shirika ambalo walitumia kukata tiketi ya ndege.

    Ring ameiambia Channel 9 kwamba wafanyakazi wa ndege walikwenda haraka pale mwanamke huyo alipoanguka katika njia baina ya viti kwa ajili ya kumsaidia, lakini "kwa bahati mbaya alifariki."

    Amesema wafanyakazi hao walijaribu kuusogeza mwili wake ili kuupeleka daraja la biashara "lakini ni mwanamke mnene na hawakuweza kumpitisha kwenye njia baina ya viti."

    Ring anasema wafanyakazi walio viti vitupu kando yake na hivyo wakamuuliza: 'Je, unaweza kusogea kwenye kiti chengine, tafadhali?' na nikasema, 'Ndiyo, hakuna shida'.

    "Kisha wakamweka yule mwanamke kwenye kiti nilichokuwa nimekaa."

    Bi Colin aliweza kuhamia kiti cha karibu kilichokuwa kitupu, lakini Ring anasema hakupewa nafasi ya kuhamia kiti chingine ingawa kulikuwa na viti vitupu.

    Wanasema kunapaswa kuwepo na itifaki ya kuhakikisha abiria walio ndani ya ndege wanashughulikiwa katika hali kama hizo.

  4. Familia ya kiongozi wa waasi wa LRA yarejeshwa Uganda

    Wanafamilia wanne wa kiongozi wa waasi wa Uganda, Joseph Kony, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa uhalifu wa kivita, wamehamishwa kurudi Uganda.

    Watu hao ni mke wa zamani wa Kony, mabinti wawili, na mvulana mmoja, ambao walikuwa wameishi kwa miaka mingi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya utekaji wa kundi la waasi la Kony, Jeshi la Upinzani la Lords (LRA).

    Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, wanne hao walikimbia kutoka kambi ya LRA mwaka jana.

    Wakiwa wanakaribishwa usiku huo katika uwanja wa ndege wa Entebbe, Kenneth Omona, Waziri wa Nchi wa Uganda anayehusika na Kanda ya Kaskazini, aliwataka waasi wengine kujiinua na kujisalimisha kwa serikali ya Uganda.

    “Tunaendelea kuwasihi waliobaki msituni warudi nyumbani. Mlango bado upo wazi, na wote waliojisalimisha wamepewa msamaha, kama vile wale waliorejea leo,” alisema. Waziri Omona alieleza kuwa marais wawili, Yoweri Museveni wa Uganda na Faustin Archange wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, walifanya mazungumzo ili kusaidia kurejesha waasi hao.

    Kurudi kwao kulisaidiwa na PAX-Netherlands, shirika lisilo la kiserikali kutoka Uholanzi, ambalo limekuwa likirahisisha urejeshaji wa waasi wa zamani wa LRA na familia zao.

    Kwa takribani miongo miwili, Jeshi la Upinzani la Bwana (LRA) la Joseph Kony lilituhumiwa kutekeleza ukatili kama mauaji, ubakaji, na kuajiri watoto kama askari katika Kaskazini mwa Uganda.

    Lengo lao lilikuwa kuingilia serikali na kuanzisha utawala unaozingatia amri kumi za Biblia.

    Mnamo mwaka 2006, Jeshi la Uganda (UPDF) lililazimisha kundi hilo kutoka Kaskazini mwa Uganda.

    Tangu wakati huo, limekuwa likifanya shughuli zake katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Mwaka jana, Mahakama ya Uganda ilimkuta na hatia Thomas Kwoyelo, mmoja wa makamanda wa zamani wa LRA, kwa mashitaka 44 ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, na utekaji.

    Alikana mashitaka hayo na alitiwa kifungo cha miaka 40 gerezani.

    Joseph Kony bado anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na inadhaniwa kuwa anafanya shughuli zake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

    Kundi la LRA liliundwa nchini Uganda, lakini lilifurushwa nchini humo na vikosi vya serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Wanaharakati wa mazingira wakamatwa Uganda

    Polisi nchini Uganda wamewakamata wanaharakati kumi na mmoja wa mazingira, waliokuwa wakiandamana kupinga ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki EACOP.

    Wanaharakati hao wengi wao wakiwa wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali mjini Kampala, walikuwa wakiandama kwa kutembea hadi hadi majengo ya Muungano wa Ulaya mjini Kampala kuwasilisha malalamiko yao ya kupinga ujenzi wa bomba mafuta la EACOP.

    Luke Owoyesigyire, naibu msemaji wa polisi mjini Kampala amesema watafunguliwa mashtaka ya kuwa kero kwa umma.

    Wanafunzi hao chini ya kundi linaolojiita wanafunzi dhidi ya EACOP, wanadai mradi huo utaathiri pakubwa mazingira pamoja na maisha ya watu wa kawaida.

    Aidha wanakosoa namna watu walioathirika na mradi huo kuhusiana na ardhi yao kutwaliwa kwamba wamepunjwa haki zao wakati wa kuwafidia.

    Bomba la mafuta la Afrika Mashariki lenye urefu wa takribani kilomita 1443, litasafirisha mafuta ghafi kutoka wilaya ya Hoima magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

    Uganda inatarajiwa kuanza uzalishaji mafuta mwishoni mwa mwaka huu wa 2025.

  6. Trump azindua visa mpya kwa wanaotaka kuwa raia wa Marekani

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza uzinduzi wa Kadi ya Visa ya rangi ya dhahabu ambayo unaweza kuinunua ukitaka kuwa raia wa Marekani.

    Trump amesema kuuza visa mpya kutaleta fursa za ajira nchini Marekani, na mapato yatakayopatikana yatatumika kupunguza nakisi katika bajeti ya taifa.

    “Tutauza kadi ya visa ya rangi ya dhahabu. Una kadi ya kijani, lakini hii ni kadi ya rangi ya dhahabu. Tutaiuza kwa takribani dola milioni 5,” alisema Trump kwa waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais, kulingana na mashirika ya habari Reuters na AFP.

    “Watu wengi wanataka kuishi Marekani. Wenye kadi za dhahabu watakuwa na uwezo wa kufanya kazi hapa, kujenga kampuni na kutoa ajira.” Aliendelea kusema kuwa mauzo ya kadi hizo yataanza katika wiki mbili zijazo na kwamba wanatarajia kuuza kadi milioni moja, huku mchakato wa kisheria ukiwa umekamilika.

    Trump pia alieleza kuwa watakaotaka kununua uraia kupitia njia hiyo watachunguzwa kwa makini, na alipoulizwa kuhusu Warusi matajiri, alijibu kuwa inawezekana.

    “Najua wafanyabiashara wa asili ya Urusi ambao ni watu wazuri. Ingawa hawana utajiri kama walivyokuwa zamani, wanaweza kulipa dola milioni 5.”

    Mtu mmoja alimuuliza Trump kama kadi hiyo inaweza kuitwa “Kadi ya Dhahabu ya Trump,” na Trump alijibu, “Ikiwa itasaidia, kwa nini isiwe hivyo?”

    Haya yanajiri baada ya Trump kuagiza watu wanaoishi Marekani bila vibali halali waondoke nchini humo warejee makwao.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Jeshi la Israel lawaamuru Wapalestina kuhama kutoka kwa kambi za ukingo wa Magharibi

    Hata baada ya muda wa wanajeshi wa Israel kushinikizwa kuondoka Palestina kama kipengee kimoja cha utekelezaji wa makubaliano ya amani kutamatika wiki jana mambo bado yanazidi kutokota.

    Vyanzo vya ndani vimeripoti kuwa jeshi la Israel limeliambia familia 11 katika kambi ya Nour Shams, mashariki mwa mji wa Tulkarm, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi ulio chini ya utawala wa Israel, kuwa linakusudia kubomoa nyumba zao kuanzia leo, Jumatano, na kuwapa familia hizo masaa matatu tu kuchukua mali zao.

    Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa lengo la jeshi ni kujenga barabara kutoka uwanja wa kambi hadi eneo la “Harat Al-Manshiya.”

    Kamati ya Wazalendo katika kambi ya Nour Shams imesema kuwa jeshi la Israel “lililazimisha” familia nyingi kuhama kutoka kambi hiyo, ambayo walivamia siku 18 zilizopita, huku idadi ndogo ya familia zikibaki kwenye mipaka ya kambi hiyo.

    Vikosi vya Israel vinaendelea na operesheni zao za kijeshi katika Ukingo wa Magharibi wa kaskazini kwa wiki ya tano mfululizo, wakituma vikosi vya ziada katika mji wa Tulkarm na kambi zake mbili, huku ndege za upelelezi zikifanya doria angani.

    Kamati ya vyombo vya habari katika kambi ya Tulkarm imesema kuwa operesheni hiyo ya kijeshi katika mji huo na kambi yake imeingia mwezi wake wa pili mfululizo, ikiwaacha watu 12 wakiwa wameuawa, akiwemo mtoto mmoja na wanawake wawili, na zaidi ya watu 20 wakiwa wamejeruhiwa.

    Wahanga wamepitia madhila kama vile kupigwa risasi za moja kwa moja na vipande vya marisau ya risasi, na wengine kwa kugongwa na magari ya kijeshi, kulingana na kamati hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Ugonjwa usiojulikana wawaua watu zaidi ya 50 Congo

    Ugonjwa usiojulikana ulioanza kugundulika kwa watoto watatu waliokula popo, umeua zaidi ya watu 50 katika kanda ya kaskazini-magharibi ya Congo ndani ya kipindi cha majuma matano yaliyopita, wanasayansi wa afya wamesema.

    Dalili za ugonjwa huu, ambazo ni homa, kutapika, na kutokwa na damu ndani ya mwili, husababisha kifo katika masaa 48 kwa wengi wa wahanga, jambo linalowatia wasiwasi wataalamu wa afya.

    Serge Ngalebato, mkurugenzi wa matibabu katika Hospitali ya Bikoro, alisema, “Hicho ndicho kinachotia wasiwasi mkubwa.”

    Dalili hizi zinazofanana na homa za kutokwa na damu, ambazo kawaida huambatana na virusi vichafu kama Ebola, dengue, Marburg, na homa ya manjano, zimefanyiwa uchunguzi lakini watafiti wamekosa uwepo wa virusi hivyo baada ya kufanya majaribio kwa sampuli zaidi ya kumi na mbili zilizokusanywa hadi sasa.

    Mlipuko wa ugonjwa huu ulianza tarehe 21 Januari, ambapo kesi 419 zilirekodiwa na vifo 53.

    Mlipuko huo ulianzia katika kijiji cha Boloko baada ya watoto watatu kula popo na kufa ndani ya masaa 48, kama ilivyosema ofisi ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatatu.

    Kwa muda mrefu kumekuwa na wasiwasi kuhusu magonjwa yanayohamwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, hasa katika maeneo ambako wanyama wa porini wanaliwa kwa wingi.

    WHO ilisema kuwa idadi ya milipuko ya magonjwa haya barani Afrika imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60% katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

    Baada ya mlipuko wa pili wa ugonjwa huu kuanza katika kijiji cha Bomate tarehe 9 Februari, sampuli kutoka kwa visa 13 zilitumwa kwa uchunguzi katika Taasisi ya Utafiti wa Binaadamu ya Kitaifa mjini Kinshasa.

    Hata hivyo, Sampuli zote hazikuwa na ugonjwa wa Ebola au magonjwa mengine ya kawaida ya kutoka damu kama Marburg. Wengine walipimwa na kupatikana kuwa na malaria.

    “Sampuli kutoka kwa visa 13 zimeonyesha matokeo hasi kwa Ebola na Marburg, lakini WHO ilisema kuwa timu za afya zinaendelea kuchunguza sababu zingine zinazoweza kuwa chanzo cha ugonjwa huu,” ilisema WHO.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Ajali ya ndege ya jeshi la Sudan yawaua wanajeshi na raia

    Ndege ya Sudan iliyoanguka Oktoba 2012

    Ndege ya kijeshi ya Sudan imeanguka katika eneo la Omdurman Jumanne jioni na kuwaua abiria na wanajeshi kadhaa, kulingana na ripoti ya shirika la habari la Suna.

    Bila kutoa maelezo zaidi, msemaji huyo wa jeshi alisema kuwa ndege hiyo ilianguka ilipokuwa ikijaribu kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Wadi Seidna.

    "Tumepokea maiti na majeruhi wengi, wanajeshi na raia. Waliojeruhiwa wametibiwa, na wazima moto wamezima moto kwenye eneo la Al-Iskan," taarifa ilisema.

    Gazeti la Sudan Tribune lenye makao yake mjini Paris liliripoti kuwa takriban raia watano waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati waasi hao walipopigana karibu na nyumba za umma.

    Alinukuu vyanzo vya kijeshi ambavyo vilisema tukio hilo lilisababishwa na shida ya kiufundi, na kwamba kulikuwa na maafisa wakuu kati ya abiria.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Misaada ya Marekani katika enzi ya Trump inakuja na masharti,

    Uchambuzi

    "Hicho ndicho ninachofanya. Ninafanya mikataba," Donald Trump alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari na Rais wa Ufaransa Emanuel Macron siku ya Jumatatu. "Maisha yangu yote ni mikataba."

    Sasa, maafisa wa Ukraine wameiambia BBC kuwa rais wa Marekani ana mkataba wake wa nadra na Ukraine, na Trump amependekeza Zelensky atazuru Washington DC siku ya Ijumaa ili kutia saini mkataba huo.

    Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Ukraine, Marekani ilibidi ijiepushe na baadhi ya matakwa yake magumu zaidi kutoka kwa taifa hilo lililokumbwa na vita. Na mengi ya maelezo ya mkataba huu yatahitaji mazungumzo zaidi.

    Mwanzo, hatahivyo, umewekwa. Misaada ya Marekani katika enzi ya Trump inakuja na masharti. Misaada kwa ajili ya misaada - iwe imetolewa kwasababu za kibinadamu au za kimkakati - ni jambo la zamani.

    Hii inawakilisha upangaji upya wa kimsingi wa sera ya kigeni ya Marekani kwa zaidi ya miaka 75, kutoka siku za Mpango wa Marshall hadi Vita Baridi na msukumo wa George W Bush wa "Ajenda ya Uhuru" kukuza demokrasia duniani.

    Ukraine ni mwanzo tu. Tarajia Trump na timu yake ya sera za kigeni kutumia kanuni zao za "Amerika Kwanza" kote ulimwenguni katika kipindi cha miaka minne ijayo.

    Soma zaidi:

  11. Hamas yatangaza makubaliano ya kutolewa kwa wakati mmoja miili ya mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina

    Vuguvugu la Kiiislamu la Hamas limetangaza, makubaliano kuhusu suluhisho la tatizo la kuchelewesha kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina ambao walipaswa kuachiliwa huru katika kundi la mwisho.

    Hamas iliyasema hayo katika taarifa yake kuhusu kuachiliwa kwa wafungwa hao kwa wakati mmoja na miili ya mateka wa Israel ambao walikubaliwa kukabidhiwa wakati wa awamu ya kwanza, pamoja na wanawake na watoto sambamba wa Kipalestina.

    Israel haikuzungumzia kuhusu kauli ya Hamas.

    Wakati hayo yakijiri mjumbe wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, ameahirisha ziara yake Mashariki ya Kati kwa siku chache kutokana na "juhudi za kidiplomasia za Marekani juu ya Urusi na Ukraine," Reuters imeripoti.

    "Israel itatuma wajumbe nchini Misri au Qatar, na ikiwa mambo yatakwenda vizuri, ninaweza kwenda huko Jumapili kuhitimisha makubaliano, kuweka awamu ya pili kwenye mstari, na kuhakikisha kuwa mateka zaidi wanaachiliwa," Shirika la Utangazaji la Israel lilimnukuu Witkov akisema.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Mzozo wa DRC: Orodha ya vikwazo vilivyotangazwa na Uingereza dhidi ya Rwanda

    Uingereza imetangaza vikwazo 6 dhidi ya Rwanda kama kwa kutokana na nchi hiyo kuhusishwa na mzozo wa mashariki mwa Congo ambapo uasi wa kundi la M23 umesabisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni bila ya makazi.

    Ifuatayo ni orodha ya vikwazo hivyo kama ilivyoainishwa katika taarifa ya Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uingereza:

    • Uingereza itasitisha kuhudhuria kwa kiwango cha juu katika hafla zinazoandaliwa na Serikali ya Rwanda.
    • Itapunguza shughuli za kukuza kibiashara na Rwanda.
    • Kusitisha usaidizi wa kifedha baina ya nchi mbili moja kwa moja kwa Serikali ya Rwanda, isipokuwa msaada kwa maskini zaidi na walio hatarini zaidi.
    • Uingereza itashirikiana na washirika kuhusu uwezekano wa kuwekwa kwa vikwazo vipya dhidi ya Rwanda
    • Itasitisha usaidizi wa siku zijazo wa mafunzo ya ulinzi kwa Rwanda.
    • Itakagua leseni za mauzo ya silaha kwa jeshi la ulinzi la Rwanda

    Unaweza pia kusoma:

  13. Mzozo wa DRC: Uingereza yatangaza vikwazo kwa Rwanda huku Rwanda ikisema inalinda mipaka yake,

    Uingereza imetangaza itasitisha karibu misaada yote kwa Rwanda kutokana na nchi hiyo kuhusishwa na mzozo wa mashariki mwa Congo ambapo uasi wa kundi la M23 umesabisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni bila ya makazi.

    Hayo yanajiri huku mkutano wa pamoja wa jumuiya ya Afrika Mashariki na ya nchi za kusini mwa Afrika zikiwateua viongozi wa zamani wa Kenya, Nigeria na Ethiopia kusimamia mchakato wa kutafuta amani Congo.

    Rwanda inasema vikwazo vilivyotangazwa na Uingereza "havifanyi chochote kusaidia DRC , wala kuchangia katika kupata suluhu la kudumu la kisiasa" kwa mzozo huo.

    Rwanda imeshtumu vikali hatua hizo za kusitisha misaada ikisema inalengwa kimakosa na kwamba kile inachofanya ni kulinda mipaka yake kwa manufaa ya raia wake.

    Kwa upande wake serikali ya Congo imekuwa ikihimiza Rwanda iwekewe vikwazo zaidi wakidai nchi hiyo inaunga mkono waasi wa M23- madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakana vikali .

    M23 wamekuwa wakiteka maeneo zaidi huko mashariki ya Congo, ya hivi karibuni yakiwa Goma na Bukavu- baada ya makabiliano na jeshi la serikali, hali iliyoongeza maafa ya mauji ,majeraha na kusababisha wimbi la wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

    Vikao mbalimbali vimekuwa vikifanyika kujaribu kuutanzua mzozo huu lakini hali bado ni tete mno.

    Miongoni mwa hatua ya hivi karibuni ni mkutano wa pamoja wa viongozi kutoka mashariki na kusini mwa Afrika uliowateua wasuluhishi wapya kusimamia mchakato wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

    Waliopewa jukumu hilo zito ni Marais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, Olesegun Obasanjo wa Nigeria, na Hailemariam Desalegn wa Ethiopia.

    Miongoni mwa yanayotakiwa kupewa kipaumbele ni kuboreshwa na kuendelezwa kwa jitihada za usitishwaji wa mapigano - na vilevile kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia walioathriwa na vita hivyo.

    La msingi pia ni kuunganisha michakato ya juhudi za kutafuta makubaliano ya amani kwa kujumuisha mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika Luanda na Nairobi.

    La muhimu zaidi ni jinsi ya kushawishi makundi ya wapiganaji - hasa kundi la M23 kuweka Sihala chini - mojawapo ya mambo yanayotegemewa sana katika kuondoa uhasama kati ya serikali ya Congo/Kinshasa na jirani yake Rwanda.

    Mataifa ya Afrika pia yana mpango wa kupeleka vikosi chini ya mamlaka ya Umoja wa Afrika ili kusaidia kudhibiti maeneo ya mashariki mwa Congo.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Israel na Palestina: Israel yafanya mashambulizi kusini mwa Damascus, na kuahidi kufanya mashambulizi ya ardhini ndani ya Syria

    Ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi ya anga kusini mwa Damascus, usiku wa manane, huku kukiwa na mazungumzo ya uvamizi wa ardhini wa Israel katika maeneo mbalimbali.

    Shirika la uchunguzi wa haki za binadamu la Syria limeripoti kuwa jeshi la anga la Israel lilifanya mashambulizi kadhaa katika maeneo ya jeshi la Syria katika maeneo ya vijini ya Damascus na Daraa na kuwaua watu 4.

    Mkurugenzi wa kituo cha uchunguzi, Rami Abdel Rahman, alielezea uvamizi wa Israeli kama "mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwanzoni mwa mwaka."

    Kulikuwa na mashambulizi 4 yaliyolenga makao makuu ya kijeshi, yaliyofanywa kwa mizinga . Anasema pia kwamba milipuko ilisikika huko Azraa wakati Israeli ilipolenga Brigedi ya 112 katika maeneo ya mashambani ya Daraa, kulingana na uchunguzi.

    Kikosi cha Israel kikisaidiwa na magari ya kijeshi kilipenya kuelekea kijiji cha Al-Bakkar, magharibi mwa Daraa.

  15. Muuguzi alishtakiwa kwa kutoa video ya kujivunia kuwadhuru wagonjwa wa Israeli

    Muuguzi wa Sydney ambaye alisimamishwa kazi kutokana na video ambayo alidaiwa kutoa vitisho dhidi ya wagonjwa wa Israel amefunguliwa mashtaka na polisi.

    Sarah Abu Lebdeh, 26, anakabiliwa na mashtaka matatu: kutishia vurugu kwa kikundi, kutumia huduma ya mawasiliano kutishia kuua, na kutumia huduma ya mawasiliano kusumbua au kusababisha makosa.

    Bi Abu Lebdeh na mwanamume mwingine wote walisimamishwa kazi katika Hospitali ya Bankstown baada ya video hiyo kurekodiwa kwenye jukwaa la mtandaoni ambalo halikujulikana jina ambalo huwashirikisha watu kwa ajili ya mazungumzo - kutolewa mtandaoni.

    Mamlaka inasema hakuna "ushahidi" kwamba wawili hao waliwadhuru wagonjwa.

    Katika picha hiyo, ambayo ilionekana kurekodiwa ndani ya hospitali na kuchapishwa na mtayarishaji wa maudhui wa Israel, Bi Abu Lebdeh na Ahmad Rashad Nadir wanadaiwa kujisifu kwa kukataa kuwatibu wagonjwa wa Israel, na kuwaua, na kusema wataenda kuzimu.

    Video hiyo ilisambaa sana mtandaoni na kusababisha malalamiko ya umma, huku Waziri Mkuu Anthony Albanese akiitaja kuwa "ya kuchukiza" na "mbaya".

    Unaweza pia kusoma:

  16. Ukraine yakubaliana na Marekani kuhusu mpango wa Madini, asema afisa wa Ukraine

    Ukraine imekubali masharti ya mkataba mkuu wa madini na Marekani, afisa mkuu wa Kyiv ameiambia BBC. "Kwakweli tumekubaliana na marekebisho kadhaa mazuri na tunaona kama matokeo ni chanya," afisa huyo alisema, bila kutoa maelezo zaidi.

    Ripoti za vyombo vya habari zinasema Washington imepunguza madai ya awali ya haki ya $500bn (£395bn) katika mapato yanayoweza kutokana na kutumia maliasili lakini haijatoa hakikisho dhabiti la usalama kwa Ukraine iliyokumbwa na vita ambalo ni hitaji kuu la Ukraine.

    Bila kuthibitisha kuwa makubaliano yamefikiwa, Trump alisema Jumanne kwamba kwa malipo ya makubaliano hayo Ukraine itapata "haki ya kupigania".

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema anamtarajia mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Washington kutia saini mkataba huo wiki hii, baada ya viongozi hao wawili kurushiana maneno makali.

    "Wao ni wajasiri sana," aliwaambia waandishi wa habari, lakini "bila Marekani na pesa zake na zana zake za kijeshi, vita hivi vingekuwa vimeisha kwa muda mfupi sana".

    Alipoulizwa kama usambazaji wa vifaa vya Marekani na risasi kwa Ukraine utaendelea, alisema: "Labda hadi tutakapokuwa na mpango na Urusi... Tunahitaji kuwa na makubaliano, vinginevyo yataendelea."

    Unaweza kusoma zaidi kuhusu vita vya Ukraine:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya Jumanne ya tarehe 26.02.2025, tukikuletea taarifa za kikanda na kimataifa kadri zinavyojiri