Mfahamu Marie-Olive Lembe Di Sita Kabila, Mke wa zamani wa Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila mwenye ushawishi.

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa muda mrefu Mke wa rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila amekuwa mwanamke ambaye amekuwa na muonekano ambao wengi waliuona kama wa mwanamke mpole na mwenye huruma...Hata hivyo si wote wanaomuona hivyo.

Tangu mume wake Joseph Kabila aondoke mamlakani, Bi Olive Lembe Kabila amekuwa akionekana akishiriki mara kwa mara shughuli mbali mbali za kijamii, na kutoa misaada kwa watu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na pesa.

Shuguli hizi anazozifanya Bi Olive Lembe Di Sita Kabila zimempatia umaarufu mkubwa jambo linaloibua maoni tofauti kumuhusu miongoni mwa raia wa DRC.

Akifahamika kama ''Mama wa roho'' baadhi ya Wacongo wamekuwa wakimlinganisha na Mke wa Rais wa sasa Bi Denise Nyakeru Tschisekedi, na kusema kuwa anastahili kuitwa ''Mke wa rais''

Hali hii ilimfanya wakati mmoja alazimike kujitokeza kujitakasa baada ya baadhi ya raia wa DRC kusema kuwa amechukua majukumu ya Mke wa Rais wa sasa Bi Denise Nyakeru Tshisekedi.

''Ninafanya siasa ya kijamii, sitaki kuingia siasa au kuchukua mamlaka ya Mke wa rais'' alisema Bi Olive Lembe Kabila, alipotembelea Mashariki mwa DRC, mwezi April mwaka huu na baadaye aliwaambia washirika wake ''Mniite Mke rais wa vijijini''

Si wote wanaousifu ukarimu wake

Serikali ya Rais Felix Tschisekedi haifurahishwi na kile anachokifanya Mke wa rais wa zamani wa DRC Olive Lembe Kabila.

Akizungumza na BBC Idhaa ya Kiswahili Jean Jacques Elakano, Mshauri wa Rais Tschisekedi alisema :''Sio vibaya kwa mtu kusaidia ila ambacho sisi hatukubaliani nacho ni kwamba Olive Lembe aliwahi kuwa Mke wa Rais Joseph Kabila na walifanya kazi kwa zaidi ya miaka 20, mamlakani...unajua Mke au Bwana anakuwa mshauri wa kwanza.

Aliongeza kuwa: ''Tunachoshangaa kwamba ni kwanini badala ya kwenda anatoa toa misaada, kipindi chote kile cha utawala wa Kabila kwanini hawakuboresha, bara bara, kwanini hawakuboresha umeme, kwanini hawakuboresha maisha ya wakongomani ili watu wasiwe wanawaombaomba?'', alihoji.

Akifahamika na wengi DRC kama ''Mama wa roho''kutokana na shughuli zake za kuisaidia jamii, tangu alipokuwa Mke wa rais wa DRC, Bi Olive Lembe Kabila, ni mwanamke ambaye amekuwa na muonekano wa upole, mwenye huruma na mkarimu kwa kila anayekutana naye.

Kauli ya Rais Tshisekedi iliyoibua utata

Kwa baadhi ya Wakongo wanaiona kauli ya Tschisekedi aliyoitoa katikati ya mwaka huu alipotembelea eneo la Mashariki mwa DRC, kuwa angependa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo ajaye awe mwanamke, huenda alikuwa anamlenga Bi Olive Lembe Di Sita Kabila: ''Huenda Rais Tschisekedi aliposema kuwa angependa rais ajaye awe mwanamke alikuwa anamlenga Bibi ya Kabila'', alisema mkazi wa Bukavu aliyezungumza na BBC, ambaye hakupenda jina lake, litajwe.

Aliongeza kuwa ''Huenda likawa sio jambo la kushangaza akigombea kiti cha ubunge kama mgombea binafsi na ninavyoona akigombea anaweza kupata ubunge kutokana na matendo na tabia yake...watu wanampenda kwakweli juu ya hiyo roho yake ya kusaidia watu''.

Bi Olive Kabila amekuwa akijiita ''Mke wa rais wa Kijijini'' na kusisitiza kuwa anafanya ''siasa za kijamii'' na hili linadhihirika kupitia shuguli za maendeleo na utoaji wa misaada ambazo amekuwa akizifanya katika maeno ya vijijini.

''Mama wa roho''ambaye ni mjasiriamali mkulima, amekuwa akionekana hadharani mara kwa mara akitoa misaada ya chakula kwa raia wa DRC mjini Kinshasa na maeneo mbali mbali ya nchi hususan pale anapozuru maeneo yaliyokumbwa na majanga, hospitali au ya watu masikini.

Wakati Volkano ya Mlima Nyiragongo ilipolipuka na kusababisha maafa makubwa mwezi Mei mwaka huu, Olive Lembe Kabila alitoa msaada mkubwa wa Mahema, chakula na misaada mingine mingi, jambo lililopelekea kuitwa ''First Lady'' yaani mke wa rais na baadhi ya raia wa Congo.

Na mwishoni mwa juma alitangaza kuwalipia ada ya masomo watoto walemavu 10,000 katika jimbo lenye utajiri wa madini la Katanga nchini humo.

Ni mwanamke ambaye anaonekana kuwakusanya maelfu watu na kupata ufuasi kwa kile anachotaka yeye kukifanya.

Nguvu za ushawishi wa Mke huyu wa Bw Joseph Kabila zilijidhihirisha zaidi katika siku ya wanawake tarehe 8 Machi ambapo aliwakusanya wanawake takriban 2,500 kutoka maeneo mbali mbali ya DRC, kutoka matabaka mbali mbali, wakiwemo wasomi, wanamuziki, waandishi wa habari na washawishi mbali mbali katika shamba lake la Kingakati, ngome ya mume wake Joseph Kabange Kabila.

Katika maadhimisho hayo ilifanyika mijadala mbali mbali chini ya mada ya taifa ya siku ya wanawake. Miongoni mwa washiriki wa mijadala hiyo walikuwa ni wanawake maarufu nchini Congo Kama vile Dkt Ritha Kibambe, Bi Marie Claude Kazal, Dkt Ali Risasi na dokta Professor Félix Momat afisa wa mpango wa kupambana na covid 19, uongozi wa wanawake, saratani ya matiti na mfuko wa uzazi pamoja na umama salama.

Ushawishi huu unawafanya wengi kujiuliza ni kwanini maadhimishimisho haya yaliyofanywa na Bi Olive Lembe Di Sita Kabila, hayakufanywa na Mke wa rais aliyepo madarakani Denise Nyakeru Tchisekedi.

Sawa na wanasiasa wengi katika bara la Afrika, Bi Olive Dembe Di Sita Kabila amedhamini shuguli za kibinafsi za raia na za umma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali kubwa iliyoko zaidi ya kilomita 80 kutoka mji mkuu Kinshasa inayotoa matibabu kwa garama ya chini, jambo ambalo limemfanya awe kipenzi cha wengi nchini humo.

Binafsi akiwa Mkatoliki Mwaka jana alifadhili ujenzi wa Kanisa Kuu la Katoliki mjini Goma , na kuacha alama ambayo haitasahaulika katika eneo hilo la Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

'Kipenzi cha waandishi wa habari na wasanii'

Kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi karibu naye wanamuona kama mama, kutokana na pesa na zawadi wanazopata kutoka kwake. ''Ni mama mwenye huruma na upendo mwingi kwetu sisi wanahabari tunaofanya kazi na yeye'' alisema mwandishi wa habari mjini Kinshasa aliyezungumza na makakala hii.

Kila mwaka unapoisha waandishi wa habari wanaofanya kazi ya kuandika na kutoa taarifa zinazomuhusu hasa za shuguli zake huwapatia zawadi ya dola 1000 kila mmoja , gunia la mchele na kila waandishi wa habari wanne hupewa ng'ombe mmoja mzima wagawane, alisema mwandishi huyo wa habari.

''Jumla ya waandishi wa habari 400 nchini DRC hufanya kazi kwa nyakati tofauti na Bi Olive Dembe Kabila'', anasema mwandishi wa BBC mjini Kinshasa.

Akielezea kuhusu pesa ambazo Mke wa Kabila anazitoa kwa waandishi wa habari na wasanii wa DRC, Mshauri wa Rais Tschisekedi Jean Jacques Elakano amesema: '' Waandishi wa habari wanaopewa pesa wazile ni pesa za Congo ambazo wajilimbikizia na wajue kwamba ipo siku sheria itatekelezwa na mkono wa sheria hautaacha mtu hata mmoja!'', alidai Bw Jean Jacques Elakano, ambaye alikuwa katika upinzani kwa takriban miaka 15 eneo la Mashariki mwa DRC, wakati wa utawala wa Joseph Kabila.

Vyombo Televisheni nchini DRC pamoja na vyombo vya habari nchini humo vimekuwa vikitangaza taarifa za ''Mama wa roho'' kugarimia mazishi ya watu asiowajua kwa pesa taslimu, wakati anapokutana nao barabarani wakielekea kwenye mazishi.

Olive Lembe Di Sita Kabila ni nani?

Olive Lembe Di Sita Kabila alizaliwa Julai 29, 1975 katika eneo la Kailo, mji mdogo uliopo katika Maniema, mashariki mwa DRC.

Ni binti wa Barnabé Sita Kinsumbu na Léonie Kasembe Okomba. Hatahivyo hakulelewa na baba yake mzazi (ambaye alikuwa amekwenda Kinshasa), bali mwanaume Mbelgiji kwa jina Adam Camille, aliyefanya kazi katika Société Minière du Kivu, katika Sominki ambaye alimlea pamoja na kaka zake wawili na madada zake wawili.

Bi Olive hakumfahamu baba yake mzazi ambaye alifariki mjini Kinshasa, baada ya kuondoka Maniema. Hatahivyo mwaka 2000 alikutana na familia ya baba yake.

Elimu

Baada ya masomo yake ya shule ya msingi na sekondari alitunukiwa stashahada ya ualimu mjini Goma, lakini familia yake haikuwa na uwezo wa kumsomesha chuo kikuu. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, alianza kufanya biashara ya bidhaa za kilimo hususan maharagwe na mahindi.

Kukutana na Joseph Kabila.

Biashara yake ilishamiri na alikuwa akituma bidhaa Kinshasa. Alifahamu kuwa kuuza bidhaa zake kwa jeshi kungempatia mapato mazuri. Hivyo basi aliweza kukutana na maafisa kadhaa.

Siku moja katika mwaka 1997, alikutana na Joseph Kabila, ambaye baba yake alikuwa ndio tu amempindua mamlakani Marshal Mobutu na kuingia madarakani. Wakati huo Joseph Kabila alikuwa kamanda wa vikosi vya nchi kavu wakaoana.

Wawili hao wamejaaliwa kupata watoto wawili: Sifa Kabila aliyezaliwa mwaka 2001 na Laurent Désiré aliyezaliwa mwaka 2008.

Bi Olive Lembe Di Sita ni Mkatoliki huku mumewe Joseph Kabila akiwa ni Mprotestanti. Harusi yao ilifanyika mwaka 2006 mjini Kinshasa, katika kipindi cha muhula wa kwanza wa urais wa Joseph Kabila.

Kwa walio karibu naye, Bi Olive Dembe Di Sita ni ''Mama wa roho '' aliyezaliwa na moyo wa huruma wa kuwasaidia watu, lakini kwa wakosoaji wake, Mke huyu wa rais wa zamani wa DRC, huenda anajitengenezea njia ya kisiasa ili kuweza kugombea ubunge au hata urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2023, kwani Katiba ya nchi hiyo inamruhusu kufanya hivyo.

Wachambuzi wa siasa za Congo wanaiona njia hii ya kutoa misaada mbali mbali na kunadi ufadhili wake kupitia vyombo, inaweza kumjengea pia jina mumewe Joseph Kabange Kabila wakati atakaporuhusiwa na Katiba kugombea tena urais.

Joseph Kabila ambaye kwa sasa ni Seneta wa kudumu katika bunge la Seneti la DRC , anaruhusiwa kikatiba kugombea tena urais iwapo ataamua kufanya hivyo mwaka 2028. Na kwa uzoefu wa siasa za Afrika, umri wake bado unamruhusu kuliongoza taifa hilo lenye utajiri wa raslimali nyingi.

Kwa upande mwingine iwapo Bi Olive Lembe Di Sita Kabila atagombea nafasi ya kisiasa nchini DRC au la, tusubiri uchaguzi mkuu wa DRC mwaka 2023. Lakini ukweli ni kwamba ni mwanamke mwenye ushawishi katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.