Wapalestina watoroka mashambulizi ya Israel kwenye jiji la Gaza

Jeshi la Israel limesema litaanza kuruhusu mahema kuletwa Gaza na mashirika ya misaada tena wakati inapanga kuwahamisha kwa nguvu watu milioni moja kutoka mji wa Gaza na kuwapeleka katika kambi kusini mwa nchi hiyo.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. CHAN 2024: Harambee Stars yaionyesha kivumbi Zambia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Timu ya Harambee Stars ya Kenya imepata ushindi ambao utasalia kwenye kumbukumbu za mashabki wake baada yakuichabanga Chipolopolo katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi A kwenye michuano ya CHAN 2024, huku mashabiki wao wakishindwa kujizuia kwa fuaraha waliokuwa nayo.

    Ingawa timu hiyo tayari ilikuwa imefuzu kwa Robo-fainali, ushindi dhidi ya Zambia ulikuwa muhimu ili kuongoza kundi hilo na kujinoa vizuri katika hatua inayofuata ya muondoano.

    Kenya ilitawala mchezo muda mwingi lakini ilikuwa na wakati mgumu kupenya katika safu ya ulinzi ya Zambia.

    Bao lao la ushindi lilipatikana katika dakika ya 75 pale Ryan Ogam alipouwahi mpira na taratibu kabisa akaupiga hadi ukampita mlinda lango wa Zambia, Kalumba, baada ya pasi safi kutoka kwa Boniface Muchiri.

    Katika dakika ya 83, mlinda lango wa Harambee Stars, Faruk Shikalo aliokoa pasi dhidi ya Kelvin Kampamba, na kuifanya Kenya kudhibiti mechi hiyo.

    Zambia, ambayo tayari imeondolewa kwenye michuano hiyo.

    Kenya sasa itamenyana na Madagascar katika raundi inayofuata, mchezo utakaochezwa nyumbani.

  3. Hamas yapinga mpango wa Israel wa kuhamisha Wapalestina kutoka mji wa Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kundi la Hamas limesema Jumapili kwamba mpango wa Israel wa kuwahamisha wakaazi kutoka mji wa Gaza unajumuisha "wimbi jipya la mauaji ya halaiki na kufurushwa" kwa mamia ya maelfu ya wakaazi katika eneo hilo.

    Kundi hilo lilisema mpango wa Israel wa kupeleka mahema na vifaa vingine vya makazi kusini mwa Gaza ni "udanganyifu wa wazi".

    Jeshi la Israel limesema linajiandaa kutoa mahema na vifaa vingine kuanzia Jumapili kabla ya mpango wake wa kuwahamisha wakaazi kutoka maeneo ya mapigano kuelekea kusini mwa eneo hilo "ili kuhakikisha usalama wao".

    Hamas ilisema katika taarifa yake kwamba kupelekwa kwa mahema kwa madai kuwa ni msaada wa kibinadamu ni udanganyifu wa wazi unaonuiwa "kuziba uhalifu wa kikatili ambao vikosi vya uvamizi vinajiandaa kutekeleza".

    Israel ilisema mapema mwezi huu kwamba ina nia ya kuanzisha mashambulizi mapya ya kutwaa udhibiti wa kaskazini mwa Gaza.

    Mpango huo umeibua wasiwasi kimataifa kuhusu hatima ya ukanda huo ulioharibiwa, ambao ni makazi ya watu wapatao milioni 2.2.

  4. Kuwait yawakamata watu 67 kwa utengenezaji wa pombe haramu huku 23 wakifariki

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya Kuwait imewakamata watu 67 wanaotuhumiwa kwa kutengeneza na kusambaza vileo vinavyotengenezwa nchini humo ambavyo vimewauwa watu 23 katika siku za hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema.

    Kuwait inapiga marufuku uagizaji au uzalishaji wa ndani wa vileo, lakini vingine vinatengenezwa kinyume cha sheria katika maeneo ya siri ambayo hayana uangalizi au viwango vya usalama, na kuwaweka watumiaji katika hatari ya kiafya.

    Wizara hiyo ilisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, kwamba imekamata viwanda sita na vingine vinne ambavyo bado havikuwa vimeanza kufanya kazi katika maeneo ya makazi na viwandani.

    Wizara ya afya ilisema siku ya Alhamisi kwamba visa vya sumu ya methanoli vinavyohusishwa na vinywaji ambavyo sio salama vimeongezeka hadi 160, na vifo 23, haswa kati ya raia wa Asia, kutoka vifo 13 vilivyoripotiwa hapo awali.

    Mkuu wa "mtandao wa uhalifu", raia wa Bangladesh, alikamatwa, huku mmoja wa washukiwa, raia wa Nepal, akielezea jinsi methanol ilivyotayarishwa na kuuzwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Jeshi la Israel lashambulia kituo cha nishati huko Yemen

    .

    Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA

    Jeshi la Israel limethibitisha kwamba lilishambulia kituo cha nishati kinachotumiwa na Wahouthi nchini Yemen, siku chache baada ya kuzuia kombora lililorushwa kutoka Yemen.

    Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee alisema jeshi "lilishambulia maeneo ya kigaidi ndani ya Yemen... likilenga miundombinu ya nishati" ya Wahouthi katika eneo la mji mkuu, Sanaa, ambalo wanalidhibiti, bila kutaja eneo halisi.

    Kwa upande wake, chombo cha habari cha Al Masirah chenye kuhusishwa na kundi la Houthi kiliripoti kikitaja Ulinzi wa Raia, kwamba "uchokozi wa Wamarekani na Wazayuni ulilenga kituo cha nguvu za umeme cha Haiz katika wilaya ya Sanhan, kusini mwa mji mkuu, Sanaa."

    Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti milipuko mikubwa katika eneo hilo, na kusababisha jenereta kuacha kufanya kazi.

    Hii ni mara ya pili kwa jeshi la wanamaji la Israel kufanya uvamizi nchini Yemen, kufuatia shambulio katika bandari ya Hodeidah inayodhibitiwa na Wahouthi mnamo mwezi Juni.

    Al Masirah iliongeza, ikinukuu chanzo cha Ulinzi wa Raia, kwamba timu zake zinafanya kazi ya kuzima moto uliotokana na ajali hiyo.

    Wakaazi walisema takriban milipuko miwili ilisikika mapema hii leo mjini Sanaa.

    Soma zaidi:

  6. Marekani yasitisha viza kwa ajili ya matibabu kwa wanaotoka Gaza

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kusitisha viza zote za wageni wanaotoka Gaza.

    Hatua hiyo imechukuliwa ili kufanya "uhakiki kamili na wa kina wa mchakato na taratibu zinazotumiwa kutoa idadi ndogo ya viza za muda za matibabu katika siku za hivi karibuni," Wizara hiyo ilisema kwenye mtandao wa X.

    Uamuzi huo umesababisha shutuma kutoka kwa baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Wapalestina.

    Shirika la Palestina la Children's Relief Fund lenye kuangazia matibabu na mgogoro wa kibinadamu limesema katika taarifa kwamba uamuzi huo "utakuwa na athari mbaya ambazo hazitaweza kurekebishika katika suala la kuleta watoto waliojeruhiwa na wagonjwa mahututi kutoka Gaza hadi Marekani kwa matibabu ya kuokoa maisha".

    Mabadiliko ya sera ya Wizara ya Mambo ya Nje yanakuja baada ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia Laura Loomer kuandika msururu wa ujumbe kwenye mtandao wa X akikosoa mpango wa viza na kuutaka utawala wa Trump kuachana na "vitendo vya chuki."

    Shirika la Children's Relief Fund lilisema kuwa limehamisha watoto 169 kutoka Gaza mwaka 2024 kama sehemu ya mpango wake wa matibabu nje ya nchi, na kuwaleta Mashariki ya Kati, Ulaya, Afrika Kusini na Marekani kwa ajili ya matunzo.

    Soma zaidi:

  7. Wapalestina watoroka mashambulizi ya Israel kwenye jiji la Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelfu ya wakaazi wamekimbia kitongoji cha Zeitoun kusini mwa mji wa Gaza, ambapo mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel yamesababisha hali ya "janga", manispaa ya mji huo inayoongozwa na Hamas imeambia BBC.

    Takriban watu 40 waliuawa na mashambulizi ya Israel katika eneo lote siku ya Jumamosi, shirika la ulinzi wa raia wa Gaza lilisema.

    Jeshi la Israel limesema litaanza kuruhusu mahema kuletwa Gaza na mashirika ya misaada tena wakati inapanga kuwahamisha kwa nguvu watu milioni moja kutoka mji wa Gaza na kuwapeleka katika kambi kusini mwa nchi hiyo.

    Nchini Israel, maandamano ya siku moja yanatarajiwa kufanyika leo Jumapili kupinga mpango wa serikali kuuteka mji wa Gaza.

    Maandamano hayo yaliitishwa na familia za mateka na wengine ambao wanasema kuongezeka kwa vita kunaweka maisha ya Waisraeli wanaoshikiliwa na Hamas katika hatari zaidi.

    Hilo linatokea wiki moja baada ya baraza la mawaziri la vita la Israel kupiga kura ya kuuteka kwa mabavu mji wa Gaza, ambao ndio mkubwa zaidi eneo hilo, na kuwaondoa wakazi wake hatua iliyolaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

    "Kama sehemu ya maandalizi ya kuhamisha idadi ya watu kutoka maeneo ya mapigano hadi kusini mwa Ukanda wa Gaza kwa ulinzi wao, usambazaji wa mahema na vifaa vya makazi huko Gaza utaanza tena," shirika la kijeshi la Israeli lilisema.

    Msemaji wa manispaa ya mji wa Gaza alisema kuwa watu wengi tayari wamehama makazi yao huko Zeitoun baada ya siku sita za mashambulizi ya anga ya Israel, mashambulizi ya makombora na ubomoaji.

    Vita hivyo vilichochewa na shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel, ambalo liliua takriban watu 1,200 huku wengine 251 wakichukuliwa mateka.

    Mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya Wapalestina 61,000, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, ambayo Umoja wa Mataifa unaiona kuwa ya kuaminika.

    Soma zaidi:

  8. CHAN 2024: Kocha wa Kenya asema lazima waigaragaze Zambia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kocha wa Timu ya Taifa ya Kenya Benni McCarthy amezungumza juu ya ni kwa nini lazima waicharaze Zambia katika mechi yao ya mwisho ya Kundi A leo Jumapili kwenye michuano ya CHAN 2024.

    "Tulijiwekea malengo mwanzoni mwa mashindano, lakini kila mtu aliamini kuwa hatuwezi. Tuliambiwa tuko kwenye "Kundi la Kufa", lakini baada ya michezo mitatu, tumejikuta tukiongoza kundi. Tunataka kufurahiya kucheza mpira wetu, na kumaliza mechi za makundi tukiwa juu,"

    "Jumapili, ni mchezo ambao ni lazima tushinde, hatuzingatii kufuzu kwa sababu tayari tumefuzu, ni katika hali tu ya kumaliza kampeni nzuri ambayo tayari tumekuwa nayo na ninawaambia wachezaji ili wawe bora zaidi, unahitaji kushinda walio wazuri zaidi, na nadhani tayari tumethibitisha hilo katika hatua zote za mechi ya makundi na Dr Congo, Angola na Morocco."

    Kenya alianza kampeni yao kwa mtindo wa aina yake, ikishinda Dr Congo bao 1-0 kwenye mechi ya ufunguzi kabla ya kupambana kweli kweli na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Angola kwenye mechi ya pili ya makundi.

    Katika mechi yao ya tatu, waliishangaza Morocco kwa ushindi wa 1-0, na kuwa kifua mbele katika Kundi A wakiwa na pointi saba.

    Soma zaidi:

  9. Mwanamke wa Gaza aliye na utapiamlo afariki hospitalini Italia

    .

    Chanzo cha picha, Andrea Fasani/ EPA

    Mwanamke wa Gaza ambaye alihamishwa hadi Italia kwa matibabu akiwa amedhoofika sana amefariki akiwa hospitalini.

    Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye alitambuliwa kama Marah Abu Zuhri, alisafiri kwa ndege hadi Pisa pamoja na mamake usiku wa kuamkia Jumatano chini ya mpango ulioanzishwa na serikali ya Italia.

    Hospitali ya Chuo Kikuu cha Pisa ilisema kwamba alipatwa na mshtuko wa moyo na akafa siku ya Ijumaa, chini ya saa 48 baada ya kuwasili.

    Hospitali hiyo ilisema alikuwa amepungua sana uzito na misuli, huku mashirika ya habari ya Italia yakiripoti kwamba alikuwa na utapiamlo mbaya.

    Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kuenea kwa utapiamlo huko Gaza, huku wataalamu wanaoungwa mkono na shirika hilo wakionya mwezi uliopita katika ripoti kwamba "hali mbaya zaidi" ya njaa inajitokeza huko Gaza.

    Israel imekanusha kuwa Gaza kuna njaa na kuyashutumu mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kutochukua misaada kwenye mipaka kwa ajili ya kuisambaza.

    Zaidi ya watoto na watu wazima 180 wameletwa nchini Italia tangu kuanza kwa vita vya Israel na Gaza.

    Wagonjwa thelathini na moja wakiwa na jamaa zao waliwasili Roma, Milan, na Pisa wiki iliyopita, wote wakiwa ama na magonjwa ya kuzaliwa, majeraha au kukatwa viungo, wizara ya mambo ya nje ya Italia ilisema.

    Takriban watu 36 wameuawa katika mashambulizi ya Israel siku ya Jumamosi, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

    Wizara ya afya pia ilisema kuwa watu 11 zaidi wamekufa kutokana na utapiamlo, na kufanya idadi ya vifo vinavyotokana na njaa kufikia zaidi ya 250.

    Soma zaidi:

  10. Urusi 'inafanya iwe vigumu' vita kumalizika - Zelensky

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa hatua ya Urusi kukataa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano inatatiza juhudi za kumaliza vita.

    "Tunaona kwamba Urusi inakataa wito wa kusitishwa kwa mapigano na bado haijaamua ni lini itakomesha mauaji. Hii inafanya hali kuwa ngumu," alisema katika taarifa yake katika mtandao wa X.

    Siku ya Jumatatu, kiongozi huyo wa Ukraine ataelekea Washington DC, ambapo Rais wa Marekani Donald Trump amesema atamhimiza Zelensky kufikia makubaliano ya amani.

    Trump amesema anataka kuachana na usitishaji vita nchini Ukraine ili kuelekea moja kwa moja kwenye mkataba wa amani ya kudumu baada ya mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

    Katika mabadiliko makubwa ya msimamo wake, rais wa Marekani alisema katika mtandao wa Truth Social kufuatia mkutano wa kilele wa Ijumaa huko Alaska, kwamba hii itakuwa "njia bora ya kumaliza vita vya kutisha kati ya Urusi na Ukraine", akiongeza kwamba mara nyingi usitishaji mapigano "huwa haudumu".

    Kufuatia mazungumzo ya simu na Trump baada ya mkutano huo, Zelensky alitoa wito wa kuwepo kwa amani ya kweli na ya kudumu, huku akiongeza kuwa "mashambulizi ya risasi" na mauaji lazima yakome.

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii Zelensky alielezea mahitaji yake ya "amani endelevu na ya kudumu" na Moscow, ikiwa ni pamoja na "dhamana ya kuaminika ya usalama" na kurudishwa kwa watoto ambao anasema "walitekwa nyara kutoka maeneo yanayokaliwa" na Urusi.

    Soma zaidi:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 17/08/2025.