DR Congo yakasirishwa na uteuzi uliofanywa na serikali ya Kenya huko Goma
Congo inachukulia uteuzi huo kama kuhalalisha kile ilichoelezea kuwa kukaliwa kwa eneo kinyume cha sheria na waasi wa M23.
Muhtasari
- DR Congo yakasirishwa na uteuzi uliofanywa na serikali ya Kenya huko Goma
- Amnesty International yataka Kenya kuchunguza biashara ya ngono ya watoto iliofichuliwa na BBC
- Mafuriko ya ghafla yaua zaidi ya watu 300 Pakistan na Kashmir
- Rapa Sean Kingston ahukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa udanganyifu
- Trump kukutana na Zelensky Jumatatu huku akisema njia bora ya kumaliza vita ni kupitia mkataba wa amani
- Israel inafanya mazungumzo kuhamisha Wapalestina hadi Sudani Kusini, vyanzo vinasema
- Makumi ya watu wafariki dunia katika sherehe ya Waislamu Senegal
- 'Hakuna makubaliano lakini tumepiga hatua kubwa' - Trump
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Trump abadili msimamo wake kuhusu usitishaji mapigano Ukraine baada ya kukutana na Putin

Chanzo cha picha, Getty Images
Saa chache baada ya Donald Trump na Vladimir Putin kushindwa kuafikiana makubaliano ya kukomesha vita vya Ukraine, waandishi wa habari wa BBC wamekuwa wakichambua mkutano wa viongozi hao huko Alaska.
Huu hapa ni ukumbusho wa uchanganuzi na ripoti za hivi punde za BBC:
Washindi na walioshindwa
Rais wa Urusi alikaribishwa kwa zulia jekundu na shangwe za rais. Trump, kwa upande wake, hakupata chochote cha kuwasilisha kama mafanikio yanayoonekana – hii ikiwa sawa na ushindi wa wazi kwa Putin, ameandika Tom Bateman kutoka Alaska.
Je, ushindi kwa Putin unamaanisha hasara kwa Ukraine na washirika wake wa Ulaya?
Mwandishi wetu wa Ukraine James Waterhouse anasema licha ya shinikizo la Trump kabla ya mkutano huo, tangazo kwamba ataachana na mpango wa usitishaji mapigano wa awali "ni pigo kwa umoja huo na Kyiv, kwa sababu lilikuwa moja ya ombi lao kuu".
Kubadilika kwa Trump?
Mwandishi wa habari wa ulimwengu Joe Inwood anasema kubadilika kwa Trump hadi makubaliano ya amani kama "njia bora" ya kumaliza vita vya Ukraine, badala ya kusitisha mapigano, ni hatua muhimu.
Kyiv
Takriban maili 5,000 kutoka Anchorage, mwandishi wetu huko Kyiv Joel Gunter amezungumza na wakaazi ambao wanasema "wameishiwa nguvu" na kile walichokiona jana usiku.
Kwa kumpa Putin makaribisho ya zulia jekundu "ulimwengu wenye busara ulifanya kitendo kisichostahili", mwanamke mmoja amesema, lakini kuna ahueni kwamba hakuna masharti yaliyowekewa Ukraine.
Soma zaidi:
DR Congo yakasirishwa na uteuzi uliofanywa na serikali ya Kenya huko Goma

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imekosoa uamuzi wa Kenya kuteua afisa kwa wadhifa wa kidiplomasia katika mji wa Goma unaoshikiliwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Wizara ya mambo ya nje ya Congo ilisema itakuwa vibaya kuhalalisha kile ilichoelezea kama kukaliwa kwa eneo kinyume cha sheria na waasi wa kundi la M23.
Orodha ya wanadiplomasia ilioteuliwa na Rais wa Kenya William Ruto inataja mabalozi wapya wa Ethiopia, Saudi Arabia na kamishna mkuu wa Uingereza.
Pia inajumuisha uteuzi wa nafasi ya Ubalozi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Goma mashariki mwa Congo.
Nafasi hiyo sio mpya lakini wakati ambao tangazo la uteuzi huo limetolewa limekasirisha serikali ya Kinshasa.
DR Congo ilipoteza udhibiti wa Goma na maeneo mengine ya madini ya mashariki mwa Congo wakati eneo hilo lilipotekwa na waasi wa M23.
Mzozo huo umeongeza mvutano katika eneo hilo na ingawa pande zote zinazohusika katika mzozo zinasema wamejitolea kusitisha mapigano, bado yanaendelea.
Soma zaidi:
Amnesty International yataka Kenya kuchunguza biashara ya ngono ya watoto iliofichuliwa na BBC

Amnesty International yataka Kenya kuchunguza biashara ya ngono ya watoto iliofichuliwa na BBC
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International nchini Kenya limeonyesha wasiwasi wake juu ya matamshi ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen kwa kupuuzilia mbali makala ya kipindi cha BBC Africa Eye iliofanywa na Shirika la Utangazaji la BBC.
Bwana Murkomen alisema makala ya BBC iliyoangazia biashara ya ngono ya watoto ni ya uwongo, matamshi ambayo Amnesty International inasema sio tu yanapunguza uzito wa kile ambacho waathirika walipitia lakini pia yanachochea wanaohusika na vitendo vya biashara ya ngono ya watoto na kwamba ni jaribio la kunyamazisha vyombo vya habari.
‘’Maoni ya Waziri ni pigo kwa kanuni za haki za binadamu na yanajitokeza kupunguza tu uzito wa mateso ambayo watoto walionusurika walipitia. Taarifa kama hizo zinatuma ujumbe wa kutisha kwa vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu, na kupendekeza kuwa kazi yao ya upekuzi na utafuaji wa taarifa za unyanyasaji zitapuuzwa,’’ Amnesty International ilisema.
Shirika hilo limetoa wito kwa Huduma ya Taifa ya Polisi Kenya kuchunguza kikamilifu uhalifu uliogunduliwa na shirika la BBC, waliohusika kuwajibishwa na kuhakikisha haki inatendeka.
Maelezo ya video, Uchunguzi wa siri wafichua 'wanawake' wanaojihusisha na biashara ya ngono ya watoto Kenya Soma zaidi:
Mafuriko ya ghafla yaua zaidi ya watu 300 Pakistan na Kashmir

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko makubwa ya monsuni na maporomoko ya ardhi nchini Pakistan na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan inaendelea kuongezeka kwa kasi, huku takriban watu 307 wakithibitishwa kufariki.
Vifo vingi vilirekodiwa na mamlaka inayosimamia maafa katika mkoa wa milima wa Khyber Pakhtunkhwa kaskazini-magharibi mwa Pakistan.
Takriban nyumba 74 zimeharibiwa, huku helikopta ya uokoaji ikianguka wakati wa operesheni na kuwauwa wafanyakazi wake watano.
Tisa waliuawa katika jimbo la Kashmir linalotawaliwa na Pakistan, huku wengine watano wakifariki katika eneo la kaskazini la Gilgit-Baltistan, mamlaka ilisema.
Watabiri wa serikali walisema mvua kubwa inatarajiwa kunyesha hadi tarehe 21 Agosti kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, ambapo maeneo kadhaa yametangazwa kuwa hatari.
Rapa Sean Kingston ahukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa udanganyifu

Chanzo cha picha, Getty Images
Rapa Sean Kingston amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu jela kwa utapeli wa mamilioni wa dola.
Rapa huyo aliyeimba wimbo wa "Beautiful Girls" alipatikana na hatia mapema mwaka huu, pamoja na mamake, katika mpango wa ulaghai ambapo waliiba vitu vya kifahari ikiwa ni pamoja na saa, runinga ya inchi 232 ya LED, na gari aina ya Cadillac Escalade na samani za zaidi ya $1m (£738,000).
Waendesha mashtaka walisema Kingston - ambaye jina lake halisi ni Kisean Anderson - na mama yake walitumia hadhi ya rapa huyo ili wauziwe vitu na waathirika na wakati wa kufanya malipo ulipofika waliwalaghai na kisha kuwatumia risiti bandia.
Mwimbaji huyo aliomba msamaha kwa mahakama kabla ya kuhukumiwa na kusema kuwa amejifunza kutokana na matendo yake, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Trump kukutana na Zelensky Jumatatu huku akisema njia bora ya kumaliza vita ni kupitia mkataba wa amani

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufuatia mkutano wa Trump na Putin na kuwapigia simu viongozi wa Nato - ikiwa ni pamoja na Zelensky wa Ukraine - Rais wa Marekani Donald Trump amesema "iliamuliwa na wote kwamba njia bora ya kumaliza vita vya kutisha kati ya Urusi na Ukraine ni kwenda moja kwa moja kwenye Mkataba wa Amani".
Katika ujumbe kwenye jukwaa lake la Truth Social platform, Trump amesema hii ingemaliza vita na kuwa na uzito zaidi kuliko "Makubaliano ya kusimamisha vita" ya vivi hivi tu.
Rais wa Marekani ameongeza kwamba "mazungumzo yao yalikuwa yenye tija huko Alaska".
Trump pia amethibitisha - kama alivyosema Zelensky - kwamba rais wa Ukraine atasafiri kwenda Washington DC kwa mazungumzo katika Ikulu ya Marekani siku ya Jumatatu.
"Kama yote yatafanyika hivyo, basi tutapanga mkutano na Rais Putin. Kuna uwezekano mkubwa maisha ya mamilioni ya watu yataokolewa," alisema.
Zelensky kukutana na Trump huko Washington siku ya Jumatatu
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa atakutana na Trump kwa mazungumzo huko Washington DC siku ya Jumatatu.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegraph alisema "anashukuru kwa mwaliko".
Zelensky alisema raia wa Ukraine hawakufurahishwa sana na kuachwa nje ya mkutano wa kilele huko Alaska, na kusisitiza katika taarifa hiyo kwamba viongozi wote watatu wanapaswa kuwepo kwa duru inayofuata ya mazungumzo.
Pia alisisitiza umuhimu wa viongozi wa Ulaya kuwepo "katika kila hatua ili kuhakikisha usalama pamoja na Marekani".
Uwepo wa viongozi wa Ulaya unaonekana na Waukraine wengi kama ngome dhidi ya uwezekano wa Trump - ambaye anajulikana kuwa rahisi kuegemea upande mmoja- kushinikizwa na Putin.
Israel inafanya mazungumzo kuhamisha Wapalestina hadi Sudani Kusini, vyanzo vinasema

Chanzo cha picha, Reuters
Sudan Kusini na Israel zinajadili mpango wa kuwapatia makazi Wapalestina kutoka Gaza, vyanzo vitatu viliiambia Reuters - mpango uliopuuzwa haraka kuwa haukubaliki na viongozi wa Palestina.
Vyanzo hivyo vya habari ambavyo vina ufahamu wa suala hilo lakini havikutaka kutajwa, vilisema kwamba hakuna makubaliano yaliofikiwa lakini mazungumzo kati ya Sudan Kusini na Israel yanaendelea.
Mpango huo, ikiwa utaendelezwa zaidi, utahusisha kuhamisha watu kutoka eneo lililoharibiwa na vita na Israel hadi taifa lililo katikati mwa Afrika lililokumbwa na ghasia za kisiasa na kikabila.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na wizara ya mambo ya nje ya Israel hazikujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema, "hatuzungumzi juu ya mazungumzo ya kibinafsi ya kidiplomasia," alipoulizwa kuhusu mpango huo na ikiwa Marekani inaunga mkono wazo hilo.
Netanyahu alisema mwezi huu kuwa, anakusudia kuongeza udhibiti wa kijeshi huko Gaza, na wiki hii alirudia mapendekezo kwamba Wapalestina wanapaswa kuondoka kwa hiari katika eneo hilo.
Viongozi wa nchi za kiarabu na dunia wamekataa wazo la kuwahamisha wakazi wa Gaza hadi nchi yoyote.
Soma zaidi:
Makumi ya watu wafariki dunia katika sherehe ya Waislamu Senegal

Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban watu 30 wamefariki dunia na zaidi ya 1000 kujeruhiwa katika ajali za barabarani zilizohusishwa na sherehe kubwa ya Magal ya 131 ya Touba, moja ya hafla muhimu zaidi ya kidini nchini humo.
Kulingana na Kamanda Yatma Dièye, mkuu wa Idara ya Habari na masuala ya umma wa Brigade ya zimamoto wa Kitaifa, jumla ya ajali 270 za trafiki zilirekodiwa tangu Jumatatu, Agosti 12, magari mengi yakihusishwa na kusafiri kwenda au kutoka Touba.
Mnamo 2024, karibu watu 700 walikufa katika ajali za barabarani huko Senegal, na 90% ya ajali mbaya zilitokana na makosa ya kibinadamu.
Siku ya Ijumaa, Agosti 15, viongozi wa Senegal walitoa wito wa haraka wa kufuata sheria za trafiki. "Hali hii inahitaji kufuatwa kikamilifu kwa kanuni za trafiki," Kamanda Dièye alisisitiza, akisema kuna hitaji la haraka la uhamasishaji wa pamoja na uwajibikaji barabarani huku serikali ya Senegal ikisisitiza lengo lake la kupunguza ajali za barabarani kwa 50% ifikapo mwaka 2030.
Zaidi ya watu milioni sita walikusanyika Touba - karibu km 150 kaskazini mwa mji mkuu, Dakar - mapema wiki hii.
Hafla kubwa ya Magal ya Touba inaadhimishwa kila mwaka na ‘Mouride brotherhood’, madhehebu la Kiisilamu la Sufi, kwa heshima ya mafundisho na urithi wa mwanzilishi wake, Shaykh Ahmadou Bamba.
Hafla hiyo inaadhimisha kukamatwa kwake na kufukuzwa kwake na viongozi wa kikoloni wa Ufaransa kwenda Gabon mnamo Agosti 12, 1895.
Trump asema hakuna makubaliano lakini 'wamepiga hatua kubwa' baada ya mazungumzo na Putin

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald Trump wa Marekani amesema yeye na Putin wamekuwa na mkutano wenye tija na kwamba wamepiga "hatua kubwa".
Trump na Putin walizungumza kwa pamoja jukwaani kwa takriban dakika 10. Wote wawili walionyesha ishara ya mazungumzo mema waliokuwa nayo wakati wa mkutano wao wa faragha, ingawa ulimalizika bila makubaliano madhubuti.
Putin alisema "ana nia ya dhati" katika kukomesha mzozo huo, ambao alielezea kuwa "janga".
Lakini alisema Urusi inahitaji "sababu za msingi" za mzozo huo zitatuliwe kwanza - na akaonya Ukraine na Ulaya hazipaswi "kuhujumu" mazungumzo hayo.
Putin, pia alielezea mkutano huo kama "mahali pa kuanzia kwa utatuzi" wa mzozo huku akisema uhusiano wake na Trump ni "imara" - na kukubaliana na madai ya mara kwa mara ya rais wa Marekani kwamba vita haingeanza ikiwa angesalia madarakani baada ya uchaguzi wa 2020.
Kwa upande wake, Trump alisema bado kuna mambo ambayo hawajakubaliana na "hakuna makubaliano hadi maafikiano yawepo" na kuongeza kuwa "hatukufikia" tulipotaka ila tumepiga hatua kubwa.
Trump alisema "wamekubaliana mambo mengi" lakini "machache" bado yamesalia, akiongeza kuwa "moja ni muhimu zaidi" bila kutaja hasa ni nini.
Trump alimalizia kwa kusema "kuna uwezekano mkubwa" ataonana tena na kiongozi wa Urusi hivi karibuni huku Putin akijibu kuwa: "Wakati ujao itakuwa Moscow"
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubasahara, tarehe ni 16/08/2025, mimi ni Asha Juma.

