Kundi la kigaidi la ISIL tishio linalokua Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jumamoja lililopita, Jumapili alfajiri, tarehe 27 Julai 2025, wanamgambo wenye vinasaba na kundi la ISIL walivamia kanisa la Katoliki mjini Komanda, Mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kuwaua waumini 43 waliokuwa wakihudhuria ibada ya usiku.
Miongoni mwa waliouawa ni watoto. Wengine kadhaa walijeruhiwa vibaya au kuchukuliwa mateka. Mabomu pia yalilipuliwa katika nyumba na maduka yaliyokuwa jirani na Kanisa hilo.
Kundi la Allied Democratic Forces (ADF), ambalo limejiunga na ISIL na sasa linajulikana kama ISIL–Central Africa Province (IS–CAP), lilidai kuhusika na shambulio hilo kupitia ujumbe wa Telegram.
Taarifa hiyo ilifuatiwa na kilio kikubwa kutoka kwa familia za waathirika, mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), na taasisi za kidini ikiwemo Vatican.
Kwa mujibu wa ripoti iliyoandikwa na Aljazeera, Mashambulizi zaidi kutoka kundi hili na ukubwa wa kundi la ISIL, ni hatua inayokuja na vitisho Afrika Mashariki.
Kuibuka kwa ISIL–CAP, historia na uhusiano ulioko
Shambulio la Komanda lilitokea wakati serikali ya DRC, Rwanda na kundi la waasi wa M23 walikuwa wameingia makubaliano ya awali ya amani, yaliyosimamiwa na Marekani. Wataalamu wa usalama wanaamini kuwa ADF inafanya mashambulio ya aina hii ili kupinga au kuharibu juhudi za kisiasa na kidiplomasia zinazolenga kuleta utulivu katika ukanda huo.
Kwa kutumia mashambulio ya kikatili, ADF inajaribu kuonyesha kwamba bado ina nguvu licha ya juhudi za pamoja za kijeshi dhidi yao. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) ulisema mashambulio dhidi ya maeneo ya ibada ni uhalifu wa kivita unaokiuka sheria za kimataifa.
Kundi hili la ADF lilianzishwa Uganda miaka ya 1990 na lilihamishwa hadi mashariki mwa DRC baada ya kushindwa kijeshi. Mwaka 2019, kiongozi wake Musa Baluku aliapa utii kwa ISIL, na kuifanya ADF kuwa tawi la ISIL barani Afrika, chini ya jina la ISIL–Central Africa Province (IS–CAP).
Tangu hapo, kundi hili limekuwa likijipanga upya, likitumia misingi ya kigaidi ya ISIL kwa propaganda, itikadi kali na mashambulio dhidi ya raia. CIA inakadiria kwamba IS–CAP lina wanamgambo kati ya 1,500 na 2,000 mashariki mwa DRC.
Kwa nini ISIL inalenga Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo Februari 2025, wanamgambo wa ADF walivamia kijiji cha Mayba na kuwachukua mateka Wakristo 70 waliokuwa wakihudhuria ibada. Baadaye, waliwaua wote ndani ya kanisa huko Kasanga, mkoani Kivu Kaskazini. Miili ya waathirika ilipatikana tarehe 14 Februari. Vatican ilithibitisha tukio hilo huku Umoja wa Mataifa ukikosa taarifa rasmi ya uthibitisho.
Hii ni mfululizo wa mashambulio yaliyolenga makanisa, hospitali na masoko, yakionesha kwamba kundi hilo linajaribu kuibua hofu na mgawanyiko wa kijamii, huku likikiuka misingi ya kibinadamu kwa kushambulia raia wasio na hatia.
Mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini imeathirika sana na mashambulio ya ADF, M23 na makundi mengine yenye silaha. Council on Foreign Relations (CFR) inaripoti kuwa zaidi ya watu milioni 7 wameachwa bila makazi ndani ya DRC. Mashambulio dhidi ya wanawake, watoto, na watu wa imani mbalimbali yamekuwa ya kawaida.
Wataalamu wa usalama wanasema mashambulio haya ni mkakati wa ISIL kueneza ushawishi wake barani Afrika baada ya kupoteza nguvu katika Mashariki ya Kati. Maeneo kama DRC yaliyo na mapungufu ya udhibiti wa Serikali, umaskini mkubwa, na ukosefu wa elimu ni mazingira yanayofaa kwa ISIL kueneza itikadi zake kali.
IS–CAP hutumia mitandao ya kijamii kushawishi vijana, kutoa fedha, na kuandaa mashambulio kupitia mitandao ya ndani. Wanatumia vurugu sio tu kwa madhumuni ya kijeshi, bali pia kama silaha ya kisiasa na kiitikadi.
Tishio linaloendelea kukua na vipi wanalikabili?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuzuia ukuaji wa ISIL na matawi yake kama IS–CAP kunahitaji juhudi pana zaidi ya operesheni za kijeshi. Mchanganyiko wa mikakati unahitajika. Wachambuzi wa siasa za Afrika Mashariki wanataja ushirikiano wa kiusalama wa kikanda baina ya DRC, Uganda, Rwanda na nchi jirani na uwepo wa mikakati ya kuzuia msimamo mkali, hasa kwa vijana, kupitia elimu na ajira.
Masuala mengine ni uwekezaji wa kijamii na maendeleo katika maeneo yaliyoathirika pamoja na msaada wa dharura kwa wakimbizi wa ndani, waliopoteza makazi kutokana na vurugu hizi.
Mashirika kama Umoja wa Mataifa wanakubaliana na aina ya mikakati, mbali na juhudi za kukabiliana nao kwa silaha, ili kupounguza nguvu ya ISIL, kwa kuanza na IS–CAP.
IS–CAP ni mfano wa jinsi ISIL inavyojaribu kuhamia maeneo yenye udhaifu barani Afrika. Ikiwa juhudi za pamoja hazitachukuliwa haraka, kuna hatari ya mashambulio haya kuongezeka, na kuenea hadi maeneo mengine ya Afrika Mashariki kama Uganda, Rwanda, Kenya na hata Tanzania.
Mashambulio dhidi ya makanisa, masoko, na raia wa kawaida yanaweza kusababisha migawanyiko ya kijamii, chuki za kidini, na kukwamisha juhudi za muda mrefu za kujenga amani mashariki mwa Kongo.
Imetayarishwa na Yusuph Mazimu, kupitia msingi wa Aljazeera












