Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran iko tayari kwa makubaliano ya nyuklia ikiwa Marekani itatimiza matakwa yake
Iran yaonyesha utayari wa kufanya makubaliano na Marekani ili kuondoa vikwazo na kutambua haki yake ya kurutubisha urani.
Muhtasari
- EU yawawekea vikwazo watu 8 Urusi
- Sera ya ushuru ya Marekani 'haijabadilika', asema mwakilishi wa biashara wa Trump
- Jeshi la Marekani laanza kujiondoa kutoka kambi za mashariki mwa Syria
- Mwanawe Robert Mugabe ashtakiwa kwa jaribio la mauaji Afrika Kusini
- Chad yafunga mpaka na Sudan baada ya mapigano kuua wanajeshi
- Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa makombora
- Haki za binadamu zinakanyagwa, asema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
- Iran iko tayari kwa makubaliano ya nyuklia ikiwa Marekani itatimiza matakwa yake
- Mfanyakazi wa ndani raia wa Uganda anakabiliwa na adhabu ya kifo Syria
- Ghasia zazuka Mexico baada ya mlanguzi wa dawa za kulevya El Mencho kuuawa
- Wanafunzi wa Iran waandamana kwa siku ya pili katika baadhi ya vyuo vikuu
- Trump ashangaa kwa nini Iran 'haijasalimu amri'
- Greenland yakataa meli ya matibabu ya Trump
- Mwanaume mwenye silaha auawa baada ya kuingia katika makazi ya Trump
Moja kwa moja
Rashid Abdallah
EU yawawekea vikwazo watu 8 Urusi
Umoja wa Ulaya umeweka vikwazo kwa watu wanane wanaoshukiwa kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kudhoofisha utawala wa sheria nchini Urusi, Baraza lilisema Jumatatu katika taarifa.
Watu hao ni majaji wa mahakama wanaohusika na kuwahukumu wanaharakati mashuhuri wa Urusi kwa kile ambacho EU inakielezea kama mashtaka yenye msukumo wa kisiasa dhidi ya wafungwa wa kisiasa walioshikiliwa katika hali zisizo za kibinadamu na za udhalilishaji, ilisema taarifa hiyo.
Watu waliowekewa vikwazo ni pamoja na Aleksei Vasilyevich Valizer, mkuu wa kituo cha wafungwa, na Anton Vladimirovisch Rychar, mkuu wa kituo cha kizuizini cha kabla ya kesi.
Kama sehemu ya vikwazo hivyo, wamepigwa marufuku kusafiri au kupitia EU, mali zao zimezuiliwa na raia na makampuni ya EU wamepigwa marufuku kuwapa fedha, iliongeza.
Sera ya ushuru ya Marekani 'haijabadilika', asema mwakilishi wa biashara wa Trump
Sera ya ushuru ya Donald Trump "haijabadilika", mwakilishi wa biashara wa rais wa Marekani amesisitiza, licha ya Mahakama ya Juu Zaidi kutoa uamuzi siku ya Ijumaa na kusema kuwa hatua ya kisheria uliotumiwa na Trump kuweka ushuru wa juu kimataifa sio halali.
"Chombo cha kisheria cha kutekeleza hilo - hilo linaweza kubadilika, lakini sera haijabadilika," alisema Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer katika mahojiano na ABC News siku ya Jumapili.
Ushuru ni kodi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Kodi hiyo hulipwa kwa serikali na makampuni yanayoleta bidhaa za kigeni.
Mahakama ya Juu Zaidi iliamua kwamba Trump alipitiliza mamlaka yake kwa kutumia moja ya vipengelee maalum kutekeleza mpango wa kimataifa wa ushuru mnamo mwezi Aprili mwaka uliopita.
Uamuzi huo ulitumika tu kwa Trump kuidhinisha Sheria ya Dharura ya Kiuchumi ya Kimataifa ya 1977 (IEEPA), ambayo ilichangia sehemu kubwa ya ushuru aliowekwa wakati wa muhula wake wa pili katika Ikulu ya White House.
Wakati huo huo, Shirika la Forodha na Ulinzi wa Mipaka la Marekani lilisema litasimamisha ukusanyaji wa ushuru unaotozwa chini ya Sheria ya Dharura ya Kiuchumi ya Kimataifa saa 12:01 asubuhi EST (0501 GMT) siku ya Jumanne, zaidi ya siku tatu baada ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani iliyosema kuwa sio halali.
Shirika hilo lilisema katika ujumbe kwa wasafirishaji, katika Huduma yake ya Ujumbe kwa mifumo ya Mizigo (CSMS) kwamba itaondoa misimbo yote ya ushuru inayohusiana na maagizo ya awali ya Rais Donald Trump yanayohusiana na IEEPA kuanzia Jumanne.
Pia unaweza kusoma:
Jeshi la Marekani laanza kujiondoa kutoka kambi za mashariki mwa Syria
Vikosi vya Marekani vilianza kuondoka kutoka kambi yao kubwa zaidi kaskazini mashariki mwa Syria siku ya Jumatatu, vyanzo vitatu vya kijeshi na usalama vya Syria vilisema, ikiwa ni sehemu ya kuondoka kwa wanajeshi huku serikali ya washirika wa Marekani huko Damascus ikiimarisha udhibiti wake.
Makumi ya malori, baadhi yakiwa yamebeba magari ya kivita, yaliondoka kwenye kambi hiyo huko Qasrak katika jimbo la Hasakah Jumatatu asubuhi, walioshuhudia walisema.
Picha za Reuters baadaye zilionyesha malori hayo yakitembea kando ya barabara kuu nje kidogo ya jiji la Qamishli.
Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani (Centcom) haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni kupitia barua pepe.
Kujiondoa kikamilifu kutoka Qasrak bado kutaacha muungano unaoongozwa na Marekani ukiwa na kambi huko Rmelan, ambayo pia inajulikana kama Kharab al-Jir, karibu na mpaka wa Iraq.
Qasrak imekuwa kitovu kikuu cha muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani unaopigana na Islamic State nchini Syria, ambapo wanajeshi wa Marekani walitumwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, wakishirikiana na Kikosi cha Syria kinachoongozwa na Wakurdi (SDF) dhidi ya kundi la jihadi.
Sio wizara ya ulinzi ya Syria wala SDF hawakujibu maombi ya kutoa maoni.
Pia unaweza kusoma:
Mwanawe Robert Mugabe ashtakiwa kwa jaribio la mauaji Afrika Kusini
Mwana mdogo wa kiume wa marehemu Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe ameshtakiwa rasmi kwa jaribio la mauaji katika mahakama ya Afrika Kusini.
Bellarmine Mugabe, mwenye umri wa miaka 28, alikamatwa wiki iliyopita baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 23 kupigwa risasi na kujeruhiwa katika nyumba moja katika kitongoji cha kifahari cha Johannesburg.
Alikamatwa pamoja na mlinzi wake. Hakuna mwanamume yeyote aliyetoa maoni kuhusu mashtaka hayo.
Wakipekua nyumba hiyo wakati wa uchunguzi wao, polisi walipata risasi lakini hadi sasa, bunduki bado haijapatikana.
Bellarmine ndiye mtoto wa mwisho wa Robert na mkewe wa pili Grace Mugabe. Robert Mugabe, ambaye alifariki mwaka wa 2019, aliiongoza Zimbabwe kwa miaka 37 kabla ya kulazimishwa kuondoka madarakani akiwa na umri wa miaka 93 mwaka wa 2017.
Bellarmine Mugabe na mlinzi wake wanakabiliwa na mashtaka mawili ya ziada, ikiwa ni pamoja na kuzuia haki kutendeka, ambayo inahusiana na bunduki iliyopotea, waendesha mashtaka wanasema.
Mwathiriwa yuko hospitalini na yuko katika hali mbaya.
Kesi dhidi ya wanaume hao wawili iliahirishwa hadi tarehe 3 Machi ambapo ombi la dhamana litatolewa.
Pia unaweza kusoma:
Chad yafunga mpaka na Sudan baada ya vifo vya wanajeshi
Chad ilifunga mpaka wake wa mashariki na Sudan Jumatatu baada ya mapigano yaliyotokea wikendi yanayohusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan kuua wanajeshi watano wa Chad, vyanzo viwili viliiambia Reuters.
Mgogoro nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces ulioanza Aprili 2023, umekuwa ukienea mara kwa mara katika eneo la Chad, na kusababisha majeruhi na uharibifu wa mali.
Afisa mmoja wa Chad aliambia Reuters kwamba mapigano yaliyotokea Jumamosi kati ya RSF na wapiganaji wanaotii serikali ya Sudan katika mji wa Tine ulio mpakani yaliua wanajeshi watano na raia watatu na kuwajeruhi watu 12.
Afisa wa walinzi wa mpaka huko Tine alithibitisha vifo vya wanajeshi hao watano na kusema hatua za ziada za usalama zinahitajika ili kuwalinda raia upande wa Chad.
Vyanzo hivyo viwili, vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa sababu havikuruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari, vilisema wanajeshi zaidi wa Chad walikuwa wakipelekwa katika eneo hilo.
Serikali ya Chad ilisema Jumatatu kwamba mpaka huo utaendelea kufungwa hadi itakapotangazwa tena, ikitaja "mashambulizi ya mara kwa mara na ukiukwaji uliofanywa na vikosi hivyo katika mzozo wa Sudan."
Hatua hiyo "inalenga kuzuia hatari yoyote ya mzozo kuenea katika ardhi yetu, kuwalinda raia wenzetu na idadi ya wakimbizi, na kuhakikisha utulivu na uadilifu wa eneo la nchi yetu," ilisema taarifa ya serikali.
Pia unaweza kusoma:
Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa makombora
Urusi ilishambulia Ukraine kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu, ikilenga miundombinu ya nishati na kuua takriban mtu mmoja, maafisa wa jeshi la Ukraine na wa eneo hilo walisema siku ya Jumapili.
Walisema mashambulizi hayo ya usiku kucha yaliikumba Kyiv na eneo linalozunguka mji mkuu, bandari ya Odesa kwenye Bahari Nyeusi na Ukraine ya kati.
Rais Volodymyr Zelenskiy alisema kwenye X kwamba mashambulizi hayo pia yalilenga mikoa ya Dnipro, Kirovohrad, Mykolaiv, Poltava na Sumy.
Lengo kuu la shambulio hilo lilikuwa sekta ya nishati, lakini majengo ya makazi na reli pia yaliharibiwa, alibainisha.
"Moscow inaendelea kuweka nguvu nyingi zaidi katika mashambulizi kuliko diplomasia," Zelenskiy alisema, akiongeza kuwa wiki hii pekee, Urusi ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 1,300, mabomu ya angani zaidi ya 1,400 yanayoongozwa na makombora 96 dhidi ya Ukraine.
Hakukuwa na maoni ya haraka kutoka Urusi.
Soma zaidi:
Haki za binadamu zinakanyagwa, asema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Haki za binadamu zinakanyagwa kote ulimwenguni, mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema siku ya Jumatatu, akitaja ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na mateso mabaya dhidi ya raia katika migogoro nchini Sudan, Gaza, na Ukraine.
"Utawala wa sheria unazidiwa nguvu na utawala wa mabavu," amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akizungumza katika ufunguzi wa Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva.
Guterres amesema haki za binadamu zinasukumwa nyuma kimakusudi, akizitaka nchi wanachama kutoziona haki za binadamu kama orodha ya kuchagua.
Guterres ametete mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ambao uko katika changamoto kutokana na kupungua kwa ufadhili, mashambulizi dhidi ya baadhi ya wataalamu wake na kujiondoa kwa Marekani katika mifumo muhimu ya uwajibikaji juu ya haki za binadamu.
"Mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka huku ufadhili ukiporomoka," amesema.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, kama sehemu zingine za shirika hilo, inakabiliwa na mdororo wa bajeti kufuatia uamuzi wa kupunguzwa kwa ufadhili kutoka Marekani - mfadhili mkuu wa Umoja wa Mataifa - pamoja na serikali zingine.
Pia unaweza kusoma:
Iran iko tayari kwa makubaliano ya nyuklia ikiwa Marekani itatimiza matakwa yake
Iran imeonyesha kuwa iko tayari kufanya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia katika mazungumzo na Marekani ili kuondoa vikwazo na kutambua haki yake ya kurutubisha urani, huku ikijaribu kuzuia shambulio la Marekani.
Wachambuzi wanasema hatua hiyo inaonyesha kwamba Tehran inataka diplomasia ili kuzuia shambulio kubwa la Marekani.
Afisa huyo amesema Tehran itazingatia uwezekano wa kuondoa nusu ya urani yake iliyorutubishwa na kuipeleka nje ya nchi, kupunguza kiasi kilichobaki na kushiriki katika kuunda muungano wa kikanda kuhusu urani.
Iran itafanya hivi ikiwa Marekani itatambua haki ya Iran ya "kurutubisha urani kwa matumizi ya kiraia " chini ya makubaliano ambayo pia yatajumuisha kuondoa vikwazo vya kiuchumi, afisa huyo amesema.
Zaidi ya hayo, Iran imetoa fursa kwa makampuni ya Marekani kushiriki kama wakandarasi katika viwanda vikubwa vya mafuta na gesi vya Iran, afisa huyo amesema.
"Ndani ya makubaliano hayo Marekani pia imepewa fursa za uwekezaji mkubwa na maslahi yanayoonekana ya kiuchumi katika sekta ya mafuta ya Iran," amesema afisa huyo.
Ikulu ya White House bado haijatoa kauli kuhusu suala hilo.
Pia unaweza kusoma:
Mfanyakazi wa nyumbani raia wa Uganda anakabiliwa na adhabu ya kifo Syria
Serikali ya Uganda iko chini ya shinikizo la kuingilia kati kesi ya mfanyakazi wa ndani anayekabiliwa na adhabu ya kifo nchini Syria.
Shirika la habari la MMI News lenye makao yake Uingereza likinukuu shirika la Migrant Workers Voice Uganda likiwahimiza maafisa jijini Kampala kuzungumza na wenzao wa Syria ili kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya Vicky Ajok ambayo imepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii tarehe 28 Februari.
Ajok alihukumiwa kwa kumuua mwajiri wake mwenye umri wa miaka 87, Huda Shaarawi, ambaye ni mwigizaji wa tamthilia maarufu ya televisheni nchini Syria ya Bab Al Hara.
Tukio hilo lilitokea mwezi uliopita katika mji mkuu wa Syria, Damascus.
Kulingana na ripoti, Ajok alimpiga mwajiri wake kwa kitu kizito wakati wa mabishano, na kusababisha majeraha mabaya. Inasemekana alikimbia eneo la tukio lakini baadaye akakamatwa.
Katika taarifa ya kukiri ambayo ilisambazwa katika vyombo vya habari vya ndani, inasemekana alitaja unyanyasaji wa muda mrefu na mishahara isiyolipwa kama sababu zilizosababisha tukio hilo.
Video iliyochapishwa kwenye chaneli ya Uganda ya New Vision YouTube inamwonyesha Ajok akiwa katika chumba akiwa amezungukwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa Syria, akionyesha jinsi alivyofanya shambulio hilo kabla ya kulia na kuomba msamaha.
Serikali ya Uganda bado haijatoa kauli kuhusu jambo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Ghasia zazuka Mexico baada ya mlanguzi wa dawa za kulevya El Mencho kuuawa
Wimbi la vurugu limezuka nchini Mexico baada ya mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya nchini humo kuuawa katika operesheni ya kumkamata iliyohusisha idara ya ujasusi ya Marekani.
Nemesio Oseguera Cervantes, anayejulikana kama "El Mencho", alikuwa kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation (CJNG) alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya katika mapigano kati ya wafuasi wake na jeshi siku ya Jumapili.
Wafuasi wanne wa CJNG waliuawa wakati wa operesheni hiyo katika mji wa Tapalpa, katika jimbo la Jalisco, na wanajeshi watatu pia walijeruhiwa, imesema wizara ya ulinzi ya Mexico.
Kumeshuhudiwa vurugu katika majimbo kadhaa, huku CJNG ikifunga barabara kwa magari yanayoungua.
Jumapili nzima, kulikuwa na ripoti za watu wenye silaha mitaani huko Jalisco na kwingineko.
Gavana wa Jalisco, Pablo Lemus Navarro, alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Guadalajara, akisimamisha usafiri wote wa umma na kufuta matukio ya halaiki na shule kufungwa.
Watalii waliozungumza na Reuters waliuelezea mji wa mapumziko wa Puerto Vallarta, Jalisco, kama "eneo la vita."
Vizuizi vya barabarani takriban 250 viliwekwa kote nchini wakati wa machafuko, huku 65 vikiwa Jalisco.
Baraza la mawaziri linasema watu 25 wamekamatwa, 11 kwa madai ya kushiriki katika vitendo vya vurugu na 14 zaidi kwa madai ya uporaji.
Maduka yaliteketezwa kwa moto na takriban matawi 20 ya benki yalishambuliwa katika vurugu hizo.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amesema maafisa wa majimbo na shirikisho wamedhibiti vurugu hizo, akiwahimiza watu kuwa "watulivu.
Sheinbaum aliongeza kuwa "katika sehemu nyingi za nchi, shughuli zinaendelea kama kawaida".
Mashirika kadhaa ya ndege yamefuta safari za ndege kwenda Jalisco, ikiwa ni pamoja na Air Canada, United Airlines na American Airlines.
Marekani imewaonya raia wake kujificha katika majimbo matano: Jalisco, Tamaulipas, maeneo ya Michoacán, Guerrero na Nuevo Leon.
El Mencho, afisa wa zamani wa polisi mwenye umri wa miaka 59, aliendesha shirika kubwa la uhalifu linalohusika na usafirishaji wa kiasi kikubwa cha kokeini, methamphetamine na fentanyl kwenda Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliahidi zawadi ya dola milioni 15 (£11.1m) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa El Mencho.
Pia unaweza kusoma:
Wanafunzi wa Iran waandamana kwa siku ya pili katika baadhi ya vyuo vikuu
Wanafunzi wamefanya maandamano katika vyuo vikuu kadhaa vya Iran kwa siku ya pili siku ya Jumapili, kulingana na mashirika ya habari ya ndani na machapisho ya mitandao ya kijamii, huku Iran ikikabiliwa na ongezeko la uwepo wa jeshi la Marekani wakati wa mazungumzo kuhusu nyuklia.
Machafuko mapya yanafuatia maandamano ya kupinga serikali mwezi uliopita ambapo maelfu ya watu waliuawa katika machafuko mabaya zaidi tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya 1979.
Televisheni ya serikali ya Iran ilionyesha video za kile ilichosema ni watu "wanaojifanya wanafunzi" wakiwashambulia wanafunzi wanaounga mkono serikali huko Tehran ambao walikuwa wakishiriki katika maandamano ya kulaani ghasia za Januari.
Maandamano pia yalifanyika katika vyuo vikuu huko Mashhad kaskazini mashariki, kulingana na video zilizochapishwa na kundi la haki za binadamu lenye makao yake Marekani la HRANA.
Siku ya Jumamosi video inayodaiwa ya waandamanaji katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif cha Tehran inaonesha wakimlaani Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei kama "kiongozi muuaji", na wakimtaka Reza Pahlavi, mwana wa Shah aliyepinduliwa Iran, awe mfalme mpya.
Maandamano ya hivi karibuni, ambayo yalianza Desemba kuhusu ugumu wa kiuchumi, yamegeuka kuwa ya kisiasa.
Pia unaweza kusoma:
Trump ashangaa kwa nini Iran 'haijasalimu amri'
Rais wa Marekani Donald Trump anahoji kwa nini Iran bado "haijasalimu amri" licha ya ongezeko la shughuli za kijeshi la Washington huko Mashariki ya Kati, amesema mjumbe maalum wa rais wa Marekani Steve Witkoff.
Witkoff ameiambia Fox News siku ya Jumamosi kwamba Trump ana “hamu ya kujua" msimamo wa Iran baada ya kutishia kufanya shambulio dogo la kijeshi ikiwa makubaliano hayatafikiwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Marekani na washirika wake wa Ulaya wanashuku Iran inaelekea kutengeneza silaha ya nyuklia, jambo ambalo inakanusha.
Ndani ya Iran, maandamano ya kupinga serikali yalifanyika katika vyuo vikuu kadhaa mwishoni mwa juma - maandamano ya kwanza ya kiwango hicho tangu yale ya Januari, ambapo maelfu ya watu wakiuawa.
Katika mahojiano yake na Fox News, Witkoff amesema: "Sitaki kutumia neno 'kuchanganyikiwa'... kwa sababu yeye [Trump] anaelewa ana njia mbadala nyingi, lakini ana hamu ya kujua kwa nini hawajafanya hivyo... yaani kwa nini hawajasalimu amri."
"Kwa nini, chini ya shinikizo la aina hii, nguvu za majini tulizonazo, kwa nini hawajatwambia, 'Hatutaki silaha za nyukilia."
"Bado ni vigumu kuwafikisha mahali hapo," mjumbe wa Trump aliongeza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema Jumapili anaamini bado kuna uwezekano kwamba mzozo huo unaweza kutatuliwa kidiplomasia.
Katika maoni tofauti siku mbili zilizopita, Araghchi alisema Tehran ikiandaa "rasimu ya makubaliano" na itaikabidhi kwa Witkoff katika siku chache zijazo.
Maafisa wa Marekani na Iran walijadili mpango wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Geneva, Uswisi, tarehe 17 Februari. Walisema maendeleo yamepatikana.
Oman - ambaye ndiye mpatanishi wa mazungumzo hayo - alitangaza Jumapili kwamba duru inayofuata ya mazungumzo "imepangwa kufanyika Geneva Alhamisi hii."
Pia unaweza kusoma:
Greenland yakataa meli ya matibabu ya Trump
Waziri mkuu wa Greenland amemwomba Rais wa Marekani Donald Trump kuzungumza naye badala ya kutoa "matamshi katika mitandao ya kijamii," baada ya Trump kusema Marekani imetuma meli ya matibabu ili kutoa "huduma" kwa watu kisiwa hicho.
Trump aliandika kwenye Truth Social kwamba anatuma meli iliyojaa vifaa vya matibabu, akidai "watu wengi" kisiwani humo ni wagonjwa na "hawatunzwi".
Jens-Frederik Nielsen alijibu "tunakataa," na akasema Greenland hutoa huduma ya afya bila malipo kwa raia wote, tofauti na Marekani.
Trump amekuwa akikitaka kisiwa kikubwa cha arctic kwa muda mrefu - lakini alikubali mwezi Januari kwamba hatokichukua.
Pia unaweza kusoma:
Mwanaume mwenye silaha auawa baada ya kukaribia makazi ya Trump
Mwanaume mwenye silaha ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukaribia eneo la makazi ya Rais wa Marekani Donald Trump huko Mar-a-Lago, Florida, imesema Idara ya Usalama wa rais.
Mwanaume huyo alikuwa amebeba bunduki na kopo la mafuta aliposimamishwa kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa Secret Service na polisi, imesema Idara hiyo.
Tukio hilo lilitokea Jumapili asubuhi, wakati rais alipokuwa Washington DC.
Mshukiwa ametajwa kama Austin T Martin kutoka Cameron, North Carolina, kulingana na CBS.
Familia yake huko North Carolina iliripoti kupotea kwake mapema Jumapili asubuhi, Ofisi ya Polisi ya Kaunti ya Moore imesema katika taarifa kwa BBC.
Ofisi hiyo imesema haina historia yoyote ya uhalifu inayomhusu Martin.
Mwanaume huyo alipigwa risasi baada ya kukataa amri, amesema mkuu wa polisi wa kaunti ya Palm Beach, Ric Bradshaw.
"Maneno pekee tuliyomwambia yalikuwa 'acha vitu hivyo' ikimaanisha kopo na bunduki," Bradshaw aliuambia mkutano na waandishi wa habari.
"Aliweka chini kopo la gesi, akainua bunduki yake hadi mahali pa kufyatua risasi," alisema.
Maafisa walimpiga risasi.
Aliongeza kuwa maafisa hao walikuwa wamevaa kamera za mwili na hakuna maafisa waliojeruhiwa.
Usalama huko Mar-a-Lago ni mkali sana, ukiwa na uzio wa nje wa polisi wa Palm Beach na ule wa ndani unaosimamiwa na Idara ya Usalama wa rais.
Trump amekuwa shabaha na majaribio kadhaa ya mauaji.
Julai 2024, Trump alipigwa risasi sikioni alipokuwa amesimama mbele ya umati wa watu huko Butler, Pennsylvania.
Pia unaweza kusoma:
Hujamboa na karibu
Nakukaribisha katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatatu tarehe 23/2/2026